BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

UKIAMBIWA MICHUZI NI MVIVU UTAKUBALI? June, 12, 2007

Filed under: Photography/Picha — bongocelebrity @ 8:46 PM

Ukimuita Issa atakuitikia,ukimuita Muhidini hatoshangaa, ukimuita Michuzi atakuitikia kisha mtaketi chini na kuzungumza mengi. Hivyo ndivyo ilivyo kuwa hivi karibuni BongoCelebrity ilipopata nafasi adimu ya kufanya naye mahojiano.

Safari yake katika ulimwengu wa picha aliianza loooong time.Wanaomjua tangu siku hizo watakuambia hajabadilika, umaarufu haujamfanya asahau alikotoka.Bado utamkuta katikakati ya gumzo.Liwe ni kuhusu soka,bongo flava,siasa kidogo,utanzania nk,Michuzi hutomkosa.

Hivi sasa anajulikana zaidi kwa mambo mawili, ni mmiliki wa blogu yenye watembeleaji wengi kuliko sio tu blogu zingine zote za kitanzania/watanzania bali hata tovuti nyingine yoyote ile ya Tanzania. Jambo la pili ni kwamba yeye ni shabiki wa kutupwa wa klabu ya Liverpool ya kule nchini Uingereza. Fuatilia mahojiano yafuatayo;

BC: Unaweza kutuambia ulianza vipi masuala ya upigaji picha? Nini kilikuvuta katika ulimwengu wa sanaa hii ya upigaji picha? Je ulichukua mafunzo yoyote maalumu ya upigaji picha?

MICHUZI:Nakumbuka nilianza mwaka 1980 kwa kutumia kakamera ka shemeji yangu ambapo mdogo wake na mimi tulikaiba na kwenda kupigia picha zetu (mie na mdogo wa shemeji yangu) sehemu mbalimbali. Matokeo yakanivutia na kunifanya niwe na kiu ya kuwa mpiga picha.Miaka mitano baadaye rafiki yangu mmoja alinizawadia Pentax Spotmatic ambayo nilikuwa sijui hata namna ya kuitumia. Bahati wakati huo kulikuwa na masomo ya jioni ya photogrtaphy pale Goethe Institute (jengo la IPS) na mwalimu wangu wa kwanza alikuwa Tom Mwewuka wa us info. services. Masomo ya vitendo yalinifanya niwe napiga picha mitaani kama mazoezi hatimaye nikajikuta ukumbi wa YMCA ambako disko la ma DJ Kalikali, Neagre J na wengineo lililokuwa juu sana enzi hizo. Wengi hawajui siri hii kwamba picha nilizokuwa napiga zilikuwa ni kwa ajili ya pesa za kusafishia (sio faida) ili kupata mazoezi.Nilifanikiwa sana kwa hilo kwani nilifaulu vizuri masomo yangu. Baada ya masomo niliendelea pale YMCA na kisha mitaani ambako kila mtu alitaka kupigwa picha na mimi kutokana nadhani na uzuri wa picha zangu. Nakumbuka picha za ajali ya jumba lililobomoka na kuua watu wawili mtaa wa Msimbazi ambapo gazeti la Mfanyakazi walitumia nne hivi. Hizo picha zangu za kwanza gazetini.

Lakini kujikita katika fani ilitokea kwamba siku moja, nakumbuka mwaka 1989, Jah Kimbute na kundi lake la Roots and Culture walifanya onyesho pale YMCA na waliniomba niwapigie picha za kumbukumbu. Mmoja ya wageni waalikwa alikuwa Attilio Tagalile wa Daily News ambaye hakuja na mpiga picha. Akaniomba nimpatie picha moja na nilipompa nakumbuka kwa mara ya kwanza Daily News walitumia picha ya msanii ukurasa wa mbele. Nahisi walivutiwa jinsi nilivyomtoa Jah Kimbute huku rasta zake zikiwa zimeruka juu na uso kaukunja kwa hisia kali za kuimba. Kuanzia hapo Tagalile akanitia moyo wa kuwa mie ni mtu wa magazeti. Pia mpiga picha mkuu wa Daily News wakati huo hayati Vincent Urio aliyekuwa na studio binafsi pale YMCA iliyoitwa Studio Laura akavutiwa nami na kunichukua. Kuanzia hapo nikawa naendelea na mafunzo ya vitendo na gwiji ambaye alinifundisha sio sanaa pekee ya picha bali pia mbinu za dark room za kusafisha mikanda (black&white) na kuprint. Nilijiunga rasmi na Daily News Januari 1, 1990 na kupelekwa Berlin nchini Ujerumani mwaka 1992 kwa mafunzo zaidi. Baada ya kumaliza tu TSJ (nilisoma 1994-96) nikapelekwa Cardiff, Wales kwa mafunzo ya juu ya upigaji picha za habari za kisiasa. Sisi ndio tulikuwa wa kwanza kufundishwa Digital Photography wakati huo. Nakumbuka Canon na Kodak walishirikiana kuunda kamera ya digital ambayo walituletea chuoni nasi tukawa kama wahusika kwa uchunguzi wao wa kuendeleza digital photography.

BC: Kwa wapiga picha wengi kitendo cha kumfuata mtu(watu) usiyemjua na kumuomba kumpiga picha sio jambo rahisi. Wewe kama mpiga picha huwa unavuka vipi kizingiti hicho ?

MICHUZI: Ni sawa na kuniuliza ukiwa mwindaji unapokuwa porini nawezaje kumpiga risasi mnyama. hapo ni akili kichwani kutegemea na situation ilivyo. kuna wakati unaiba ama unavizia ama unatabasamu na kuomba. inategemea. hakuna situation ya kufanana. ila naona raha sana kupata picha kwa kutumia akili na maarifa bila mwenyewe kujua.

BC: Je unakumbuka lini ilikuwa ni mara yako ya kwanza kulipwa kama mpiga picha?

MICHUZI: Siwezi kukumbuka vizuri. Labda mwaka 1987 nilipoanza kupiga picha disko la YMCA. Pesa ya maana nadhani ilikuwa mwaka 1989 ambapo kampuni ya Inter Consult walinipa tenda kubwa ya kupiga majengo wanayojenga nchi nzima. Nililipwa milioni moja na ushee hivi.Nusura nipate uchizi kwani enzi hiyo pesa hiyo ilikuwa nyingi sana. Nakumbuka nusu nilinunua kiwanja na kiasi kingine kamera mpya na flashi.

BC: Ni lini hasa ulipogundua kwamba sasa wewe ni mpiga picha weledi (professional photographer)?

 

MICHUZI: Baada ya kazi ya Inter Consult

BC: Ni aina gani ya vifaa unavyotumia katika kazi zako za kila siku za upigaji picha? Nina maana unatumia kamera ya aina gani na vitu kama hivyo.

 

MICHUZI: Ninatumia kamera nyingi , ila kamera kubwa natumia aina ya Canon d5 na eos d30 na lens zote toka fish eye (17mm), ya kati (35-185mm) hadi long lens (100- 1000mm) pia natumia skylight (light pibk) filter ama Ultra Violet clear filter muda wote na ninazo filter zote kuanzia polarising filter hadi neutral density (ND-L & ND8-L). Pia natumia flash nne za speedlite 580EX, tripod ya canon, memory card za 2gb kama sita hivi, light meter na photo-torch moja. Kila niendapo huwa mkobani nina Sony Cybershot 7.2megapixel DSC P200.

BC: Ni maeneo gani ambayo wewe hupendelea zaidi kupiga picha? Majengo, watu, milima, bahari nk?

 

MICHUZI: Chochote cha kuvutia hisia zangu na za watu.

BC: Unaweza kutueleza ni eneo gani la kustajaabisha (spectacular) ulilowahi kutembelea?

 

MICHUZI: Robben Island alikofungwa Nelson Mandela

BC: Nini unakipenda zaidi katika maisha yako kama mpiga picha?

 

MICHUZI: Tabasamu la furaha na kuridhika mtu niliyempiga picha ama anayeangalia picha niliyopiga

BC: Nini usichokipenda katika maisha yako kama mpiga picha?

MICHUZI: Usingizi. Naona unanipotezea muda na opportunity zinazoweza jitokeza

BC: Ni tukio gani katika maisha yako ya upigaji picha ambalo hutolisahau kamwe?Kwanini?

MICHUZI: Siku ya matembezi ya mshikamano mwaka 1990 ambapo nilitumwa kufanya coverage. Mgeni rasmi alikuwa Mwalimu Nyerere. Hii ndiyo siku yangu ya kwanza kumpiga picha Hayati Baba wa taifa. Nyingi ziliharibika kwani nilikuwa natetemeka kwa msisimko.

BC: Je unaye mpiga picha yeyote anayekuvutia zaidi na unayeheshimu kazi zake katika sanaa nzima ya upigaji picha? Kwanini?

MICHUZI: Pete Turner. Hana mshindani kwa upigaji picha. Pia nazimia na Ansel Adams ambaye nashauri mtu anayetaka kujifunza picha atafute vitabu vyake vyoote. Nyumbani nawaheshimu wapiga picha wote hasa wale wa picha za mitaani ambao hadi leo wanatumia filamu maana anapata picha 38 zote nzuri. Tofauti na sisi wa digital ambapo tunapiga picha hamsini kwa tukio moja. lakini kueleza ubaya ama uzuri wa mpiga picha ni ngumu kwani picha ni kama ulimbwende, beauty is in the eye of the beholder.

BC: Katika kazi yako hii ya upigaji picha umeshakutana na wapiga picha wengi, maarufu, wa kujitegemea na wale wa serikali za nchi zingine. Unaweza kutuelezea umejifunza nini kutoka kwao?

MICHUZI: Be daring, passionate and always think ahead not only in getting the shot but also in getting satisfying results.

BC: Nini maoni yako kuhusiana na tekinolojia zilizopo hivi sasa katika kusafisha picha,kuzikuza, kuzibadili na hata kutengeneza picha ambazo sio za kweli (photoshoped photos)?

 

MICHUZI: Wakati ni ukuta. Huwezi kushindana nao.

BC: Sanaa ya upigaji picha ni ya muda mrefu na haina dalili ya kufikia kikomo bali kuboreshwa tu siku baada ya siku. Una ushauri gani kwa wale ambao wangependa kuongeza ujuzi wao katika masuala ya upigaji picha?

MICHUZI: Piga picha, piga picha, piga picha na zingatia mafunzo ya kinadharia na vitendo

BC: Sasa tuongelee kuhusu blog yako ambayo imetokea kupata umaarufu mkubwa sana. Unadhani watembeleaji wa blog yako huwa wanapenda zaidi kupata habari za aina gani?

 

MICHUZI: Swali gumu maana naona kila ninachoweka kinapata wasomaji wengi tu ambapo baadhi huunga mkono na baadhi hukosoa. Nahisi (na kushukuru kwa hilo) ni kutokana na kiu ya kupata habari mpya kila siku toka nyumbani na kwa wale waliopo hapa nyumbani kupata habari nyepesi nyepesi na nzito nzito kwa njia ya picha zaidi.

BC: Nitakuuliza swali hili mahususi kwa ajili ya mashabiki au watembeleaji wa blog yako.Mwenyewe unapenda kuwaita “wadau”. Unatofautishaje picha unazopiga kwa ajili ya safari kwa mfano za raisi nje na ndani ya nchi na zile unazopiga kwa ajili ya watu wa kawaida?

 

MICHUZI: Kwangu mimi picha ni picha tu. Hazina tofauti kwani wanaoziangalia ni wote wenye nafasi na uwezo wa kufanya hivyo.

BC: Wakati blog yako inaanza kupata umaarufu kulitokea tatizo la watoa maoni kutumia lugha ambazo hazikuwa muafaka (matusi). Baadaye tatizo lile uliliondoa kwa kila maoni kupitiwa kwanza kabla hayajaonekana kwa kila mtu (moderating comments). Unasemaje kuhusu kibarua hicho cha kupitia maoni lukuki ya watoa maoni wote?Kuna mtu anakusaidia katika hilo na je bado maoni ya matusi yanaendelea kuletwa kwako?

 

MICHUZI: Kwa vile naipenda kazi yangu na nawapenda wadau sioni tatizo la kuupanda mlima wa maoni kila siku. Kwanza nafurahia kwani angalau najua kila kilichotumwa. Sidhani kama nikimpa mtu anisaidie nitakuwa na amani kwani aidha ataweka ama atazuia kinacho/kisicho faa kwa mujibu wa utashi wangu.

BC: Unapoandika na kisha kutoa picha ya habari fulani katika blog yako; kwa mfano habari ya mheshimiwa Amina Chifupa hivi karibuni, unafanyaje ili kufikisha ujumbe kwa wasomaji wako na wakati huo huo usionekane kupendelea upande mmoja?

 

MICHUZI: Natumia busara na akili za kuzaliwa.

BC: Umekuwa photoblogger kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa kama sijakosea. Nini faida na hasara zake?

 

MICHUZI: Faida ni kujulikana dunia nzima na hasara ni kunyimwa uhuru wa kuwa huru. Kila dakika nahisi nina deni la kuwaridhisha wadau.

BC: Nini mipango yako katika miaka mitatu ijayo.Wapenzi wa blog yako watarajie nini?

 

MICHUZI: Watarajie website itayokuwa moto kama ilivyo blog.

BC: Tuje upande wa maisha yako ya kila siku. Unaweza kunipa kwa ufupi ratiba yako ya kila siku? Unaamka saa ngapi, unalala saa ngapi nk?

 

 

MICHUZI: Siku ya kawaida naamka saa 12, nafanya mazoezi (nina mkanda wa kahawia goju ryu karate) kwa lisaa limoja. Saa moja unusu nagombana na foleni hadi kazini Mtaa wa Samora. Nalala baada ya kuhakikisha nimepitia maoni yote katika blog hivyo hutegemea; Saa ingine saa 10 alfajiri ama nikiwahi sana ni saa 6 unusu.

BC: Unaweza kukumbuka sinema uliyoiona mara ya mwisho au siku za hivi karibuni?

 

MICHUZI : Spiderman 3

BC: Ukiwa ndani ya gari lako huwa unasikiliza muziki wa aina gani? Ni msanii gani wa muziki wa aina yoyote unayependelea kuzikiliza miziki yake zaidi? Kwanini?

 

MICHUZI: Nikiwa garini napenda sebene lolote. Ottis Redding na Percy Sledge ndio my idols. Sababu zinaeleweka.

BC: Je kuna chochote ambacho ungependelea wasomaji wa mahojiano haya wajue kuhusu wewe na ambacho hatujakuuliza?

 

MICHUZI: Amini usiamini hakuna mtu mvivu kama mimi. Hii kuchakarika kote huku ni kuogopa nisizame kwenye kilindi cha uvivu. Vile vile suala la watu kuniona mie ni mtu wa ‘matawi ya juu’ wakati sio na siwezi kuwa hiyo kwani ndani rohoni mie ni mpiga picha wa mitaani. Hivyo wenye kazi zao za harusi, ubatizo ama zozote zile wasisite na wala wasisikie kwa mtu wanaponihitaji. Napatikana kama zamani na nafanya kazi yoyote. Mimi najali sanaa na sio pesa. Wanaosema mie niko ghali nawahakikishia sivyo na wasitumie ‘third party’ kujua ukweli. Huwa nafanya kazi hata bila malipo, mradi nipate ujira wa tabasamu la kuridhika. Vile vile sio kweli kwamba kila picha naweka kwenye blog. Kwa mfano, ukinipa tenda ya harusi siwezi kubandika picha kwenye blog bila idhini yako. Hata nikiweka picha haitohusiana na mwenye harusi kwa vyovyote. Nathamini na nazijua work ethics.

BC: Michuzi asante sana kwa mahojiano haya.

MICHUZI: Shukrani.

 

Advertisements
 

28 Responses to “UKIAMBIWA MICHUZI NI MVIVU UTAKUBALI?”

 1. Hamza Mwanakilala Says:

  Duh,Michuzi kumbe bwana mdogo kabisa kwangu.80’s nilikuwa nshaacha kwenda disco.Interview safi kabisa.Nimejifunza mambo mazuri kupitia hii interview

 2. Laila Says:

  Hii interview nzuri sana. Duu michuzi kumbe mzee mtu wa maana. mimi nilidhani wewe ni utani tuu. Nimeifurahia sana hii interview. kazi nzuri bongo celebrity. tuleteeni mambo. nani next?????

 3. Mahojiano mazuri!Na kazi nzuri Wazee!

 4. Haya mahojiano yametulia!.Michuzi kumbe na wewe hupendi usingizi?.Mimi huwa nafikiria mawili yanayonipotezea muda kwanza kula na kulala.

 5. octavian Says:

  Michuzi, mimi siku moja nilikuwa nawahi home, niangalie update kwenye Blog yako, ndio nilale, kesho job. Sasa ile kutoka nje ya hiyo sehemu niliyokuwa najipa raha, nikakuona. Nikashindwa kukustua kwamba mwanangu vipi kuna update yeyote? au nikifika home nilale tu. Ma celebrity hamchelewi kumtoa mtu nishai. Leo nimejua kuwa wewe kawaida tu. Nikikuona this time nitakustua. Good JOB!

 6. fadhy mtanga Says:

  heshima yako mtu mzima Michuzi. nimekuona magazetini tangu utotoni nilipojua kusoma na kuandika.
  Binafsi nimepata hamasa kubwa sana kutoka kwako hata nami nikaanzisha blog yangu http://www.fadhymtanga.blogspot.com
  napenda sana siku moja nifike hapo ulipofika wewe katika maswala ya kublog. na ikibidi nisonge hata zaidi yako.
  umekuwa mmoja ya role models wa nchi hii kwangu.
  mahojiano haya yamenisisimua zaidi, hawakukosea kukuhoji. majibu yako yannifanya nijifunze kuongeza bidii daima katika maisha.
  kila la kheri mjomba Michuzi.

 7. Erasto Mhagama Says:

  Niwape hi, bongocelebrity kwa kupata wasaa mzuri wa kuhojiana na Michuzi, sio siri nazimia kazi zake. Big Up

 8. Henry Lyimo Says:

  Nimefurahi kumfahamu zaidi Michuzi kupitia mahojiano haya. Naamini kuna mengi sana ya kujifunza kutokana na kazi zake na staili yake za maisha.

 9. Bob Sankofa Says:

  Michuzi nakupa salute kaka.

  Waandaaji wa mahojiano na web hii nao salute vilevile.

  Napenda kumuuliza Michuzi, vipi wanablog wa fotografia wanaozungumza kiswahili tukaandaa Maonyesho ya kazi zetu kwenye web hii japo mara moja kwa mwaka?

 10. Haki Blog Says:

  Michuuuu hongeraa sanaaa mkuu..
  by
  Admin
  Haki BLOG

 11. godfrey Says:

  Kaka Michuzi, binafsi nimefurahi, hasa hasa kwa kuiona na kuijua sanaa ya Picha. Nafurahia picha zako. Je hujawaongelea watu kama marehemu Mohamed Amin, Jafery, Alf Kumalo, je hao hawakugusi katika muundo wowote, hasa kwa picha za kiafrica? Anyway nahisi watakuwa wanakugusa pia ila si rahisi kuongelea mengi.

  Kaka mivifaa yoote hiyo unatumia? Du!!! haya kaka, mi na kakamera kangu tobwe nadhani ntajitahidi kama wewe siku moja. Give thanks…

 12. Michuzi Jr Says:

  yaaa interview imetulia sana kiukweli,heshima kubwa kwa wote juu ya hilo, Kiukweli nami Michuzi amenipa hamasa kubwa katika suala zima la mambo ya upigaji picha kiasi ambacho mpaka sasa nahisi kuzifuata nyayo zake kwa ukaribu mno, mbali ya hilo amenifanya nami nianzishe blog yangu michuzijr.blogspot.com.

  Heshima kubwa kwa Michuzi

 13. Rugs Says:

  kazi nzuri Bongo celebrity, mimi leo ni mara yangu ya kwanza kusoma hii blog. Sie tulioko nje ya Tanzania mnatupa habari za maana sana kwetu. Tunaendelea kuunganika na nyumbani.Asante sana.
  Kwa bwana Michuzi, nakubali kuwa yeye ni mtu simple maana namfahamu kwa hiyo simplicity anayoizungumzia..

 14. Shagi Says:

  Bongocelebrity nawapa flag sana kwa huu mchezo!
  imetulia sana.
  Pia big brother Michuzi.
  Gud interview.
  Mungu aendelee kukuneemesha kwa kazi nzuri.
  Naipenda sana kazi yako kuliko niwezavyo kutafuta maneno ya kuisemea.

 15. Nakomolwa Says:

  MICHUZI WEWE NI MORE THAN CELEBRITY,
  UNATUUNGANISHA SANA SISI TULIO NJE YA NCHI NA MAMBO YANAYOENDELEA NYUMBANI.HAKIKA WEWE UPO SIMPLE SNA NINAKUFAHAMU KWA HILO NA NAOMBA ENDELEA HIVYO,
  USHAURI WANGU KWAKO
  NAOMBA UINGIE KWENYE SIASA MAANA NAAMINI UNAWEZA KUFANYA HIVYO SAUTI YAKO INA NGUVU NA USHAWISHI UNAOKUBALIKA POPOTE WALIPO WATANZANIA,

 16. Jumbe Says:

  Michuzi safi hebu mtafuteni na huyui dogo anayemnyemelea kwa blogu ya picha Fadher Kidevu http://www.blog.co.tz/mrocky nayetupate yake.

 17. Rev.Ed A.M Says:

  Michuzi hata mimi mlokole huku kwa mzee Bush nazimia kazi zako hasa blog yako naitembelea kila siku x2. Nilikufahamu tangu huko nyuma na picha yako uliyowahi piga kifundi sana uwanja wa taifa mpira umejaa wavuni huku kipa bado hajatua chini siwezi kuisahau. Interview imenipa hamasa kusaka nyezo za uhakika.

 18. Napenda kutoa shukrani kwa muandaaji wa bongocelebrity.com kwani kama lilivyo jarida la Ebony hii blogu ni chachu ya kuhamasisha maendeleo.

  Aidha, napenda kutoa shukrani kwa wote waliotoa maoni hapa kuhusu mimi na kazi yangu ya kupiga picha na kutoa habari. Najihisi sistahili mengi yalosemwa kwani sidhani kama nafanya kikubwa zaidi ya kutekeleza wajibu wangu. Naweza kujaza ukurasa wote huu na bado nisiwe nimefikisha robo ya shukurani zangu kwenu. AHSANTENI SANA

  Rai yangu kwenu wasomaji na pia ma-celebrity mtaotokea humu na kwingineko ni kwamba msiruhusu mafanikio yoyote yaingie kichwani. Daima baki kama ulivyo na utaona faida yake

 19. mum Says:

  Hongera sana kaka Michuzi, kwakweli mimi binafsi nafurahiya sana kazi zako coz unatupa kila siku vitu vipya vinavyo endelea nyumbani. huwa nawaonyesha picture zako wenzangu huku mnaona kwetu na huwa wananiuliza leo ujafungua kumcheck michuzi, wanapenda kuangalia na huwa nafungua mara kwa mara nicheki labda tena kuna kitu kipya. big up michuzi all the best kaka

  Mum

 20. Mama wa Kichagga Says:

  Masubu (Michuzi kwa Kichagga),

  Hongera sana kaka yangu. Mie huwa napenda sana mtu anayejua kusimamia miguu yake mwenyewe.

  Yaani nakukubali sana kiutendaji na jinsi unavyojua kujipa raha! Naamini BP kwako itakuwa inapita mtaa wa pili.

  Nimefurahi sana ulikotokea , kazi zako hadi hapa ulipo – una msingi imara.

  Ndio maana mimi huwa naamini ukitaka uondokane na umaskini ni lazima ujitahidi mwenyewe kwanza! Mfano mzuri nii huu wa kwako, hivi ungekaa na kusubiri serikali ikuondolee umaskini si ungeshazeeka saa hii ama ungeshasahaulika!

  BIG UP SANA KAKA, HISTORIA YAKO IMESHAONEKANA KABLA HATA HUTAENDA MADUKANI AKHERA! NA HII NI MUHIMU SANA.

  NB: ONGEZA HABARI MOTOMOTO HASA ZA UFISADI MAANA NAONA MCHANGO WAKO WAWEZA KULIKWAMUA TAIFA

 21. luis sirikwa Says:

  Alles klar? kumbe umepata na ujuzi hapa Germany Berlin!
  nimefurahi kuona haya mahojiano yako, kumbe watu tunatoka mbali sana,mimi bado niko hapa Münich katika kupambana na maisha,sasa kwanini usitose kwenye siasa tz? na wewe sasa ni maarufu kila kona ya nchi! any way keep in touch bro.
  Best,
  LUIS.

 22. DAWSON T.MOSHY Says:

  ISSA,KWA KWELI UNACHOKIFANYA NI KIZURI SANA KWA KUWA UNATUFUNDISHA MENGI.UNATUTOA MATONGOTONGO KWA KUWA TUNAYAJUA MENGI YA WALIMWENGU.NAKUPA HI NA BIG UP

 23. DAWSON T.MOSHY Says:

  HAPANA SI KWELI KWA KUWA KAZI YAKE TUNAZIONA

 24. binti-mzuri Says:

  naona watu wana advertise blogu zao kijanja hapa..hahaha..safi sana..tunawasupport!

 25. mwahu y Says:

  haya mahojiano ya michuzi safi sana!!! nilikuwa sikufahamu kiundani mzee,lakini sasa nimekusoma mzee,kumbe wewe ni mtu mashughuri sana kutokana na kazi yako,mzee tulikuwa wote kwenye sulvan summit pale arusha.mzee hongera kwa kazi nzuri sana.

 26. reenaa Says:

  yes bro wewe ni mkala kweli umetoka mbali hii ni fundisho kwa wapiga picha wote, kaza buti babab maisha ni kufanikiwa kama wewe ulivyofika mbali

  warm regards ,

  reenaa

 27. underwood Says:

  Du kumbe Michuzi ni mshabiki wa Liverpool. Angalia sana Brother utaja pata pressure bure. Njoo MAN U.

 28. […] aliyekuwa na studio binafsi pale YMCA iliyoitwa Studio Laura akavutiwa nami na kunichukua. source; UKIAMBIWA MICHUZI NI MVIVU UTAKUBALI? BONGO CELEBRITY …Kama Mzee Vicent Urio (R.I.P) aliweza miaka hiyo kwanini michuzi asiweze? au wenye uwezo wa […]


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s