BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

TAFAKURI YA KINA NA NDESANJO MACHA. August, 18, 2007

Filed under: Blogging,Blogs — bongocelebrity @ 2:54 PM

Tangu kuanzishwa kwa blog hii imetokea mara chache sana tukakosa maneno ya kumtambulisha celebrity yeyote ambaye tumeshawahi kufanya naye mahojiano. Leo tunaelekea kuwa na wakati mgumu kidogo. Ugumu unatokana na mtu mwenyewe, mambo ambayo ameshayafanya na anaendelea kuyafanya hususani kwa upande wa blogs za Tanzania au ki-tanzania!Ngoja tujaribu.

Issa Muhidini Michuzi anamuita “mfalme wa blogs za Tanzania”. Anapomuita mfalme anakuwa hamaanishi tu kwamba yeye ndiye aliyemuingiza au kumtambulisha katika ulimwengu wa blogs walipokutana nchini Finland (Ufini) Septemba mwaka 2005, bali kuna sababu nyingi za kustahili hadhi hiyo ya ufalme. Blog yake ya Jikomboe(wakati huo ikipatikana katika http://www.jikomboe.blogspot.com) ndio blog ya kwanza kabisa ya Kiswahili mtandaoni. Takribani blog zote zilizoanzishwa siku zile zilichochewa kwa njia moja au nyingine, achilia mbali kupata msaada wa kiufundi, na yeye.

 

Tunamuongelea Ndesanjo Macha (pichani), mwanasheria kitaaluma ambaye anasema dhamira yake kuu ni kuhakikisha lugha za kiafrika,kikiwemo Kiswahili hazibaki nyuma kunako mapinduzi yatokanayo na tekinolojia.

Katika mahojiano haya nasi, Ndesanjo Macha anajibu karibuni kila swali kuhusu ulimwengu wa blogs kuanzia ilikuwaje akaanza kublog, nini faida na hasara za blogs,blogs zinawezaje kulisaidia bara la Afrika, ukitaka kufungua blog yako na iwe yenye mafanikio ufanyeje na mengineyo mengi. Muhimu zaidi anazungumzia kwa undani mategemeo ya baadaye ya tekinolojia ya mtandao na masuala ya blogs.Fuatana nasi katika mahojiano na Ndesanjo ambayo tunaweza kuyaita kwa kiiingereza “a must read interview”.

BC: Ulianza lini masuala ya kublog na nini kilikuvutia kuanza kublog?

NM: Nilianza kufuatilia masuala ya blogu nadhani kwenye mwaka 2003. Nilianza kufuatilia kijuujuu. Wakati huo nilikuwa nasoma masuala ya uhusiano kati ya jamii na teknolojia (social informatics). Baadaye nilianzisha blogu lakini nikaiacha, wala siikumbuki tena. Nadhani niliandika mara mbili tu. Blogu hiyo ilikuwa ya Kiingereza. Baadaye mwaka 2004 niliamua rasmi kuingia kwenye masuala haya kwa nguvu zangu zote. Nikaamua kuwa blogu yangu kuu itakuwa ni ya lugha ya Kiswahili.Uamuzi huu ulikuwa una msukumo wa kiitikadi na kitamaduni. Wakati huo nilikuwa pia nikifuatilia masuala ya lugha mtandaoni ambapo ilikuwa ikionekana wazi kuwa kuna hatari ya mtandao wa Intaneti kuwa ni eneo la maarifa, ila maarifa yenyewe yakawa kwenye lugha chache tu. Unajua dunia ina lugha kama 6000 hivi, lakini mambo yote unayoyaona mtandaoni yanapatikana kwa lugha chache sana (kama lugha 12, lakini kiingereza kikiwa ndio kinatawala). Ngugi wa Thiong’o na mwandishi mwingine wa Nigeria, Chinweizu, waliwahi kuandika vitabu wakielezea suala waliloliita, “Decolonizing the Mind” na “Decolonizing African Literature.” Basi, nilipoanza kublogu nilisema kuwa ninachofanya na watakachofanya wengine watakaokuwa wakiandika kwa lugha zao ni muendelezo wa falsafa na wito wa Ngugi na Chinweizu kwa jina la “Decolonizing Cyberspace.”

Nikijibu moja kwa moja swali lako, kilichonivutia kuhusu kublogu ni uwezo wa kuwasiliana na dunia nzima katika uwanja ninaomiliki mimi bila vizingiti vyovyote, bila mhariri anayeniambia nibadili ninayoandika. Blogu kwangu naiona kama ni nyenzo inayoniwezesha kufaidi haki yangu ya kimsingi ya kikatiba na kibinadamu ya kujieleza na kusambaza mawazo yangu kwa watu wengine. Labda niseme kidogo kuwa nimekuwa nikiandika magazetini toka mwaka 1993. Toka enzi hizo kulikuwa hakuna njia yoyote ya mimi kuwa na uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja na wasomaji wangu. Ni wale watu waliokuwa wananijua ambao ndio nilikuwa nakutana nao wananiambia habari fulani niliyoandika ilikuwa nzuri, au nilikosea jambo fulani, au mada fulani sikuielezea vizuri, n.k. Mara chache wasomaji walikuwa wanaweza kuandika barua za posta (jambo ambalo lina usumbufu wake). Blogu zilipokuja, kwa mara ya kwanza nikaweza kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wasomaji wangu. Sio hilo tu, bali mawazo na fikra zangu zikaanza kusomwa na sio tu watu walioko Tanzania, bali hata walioko Brazili, India, Uswidi, Uingereza, New Zealand, China, n.k. Haya ni mabadiliko makubwa. Ni mapinduzi.

BC: Unaweza kukumbuka ni blog ipi au ya nani iliyokuwa ya kwanza kwako kuisoma?

NM: Ni vigumu kukumbuka blogu ya kwanza. Ila naweza kukumbuka kuwa kati ya blogu zilizonipa hamasa kubwa ni blogu ya rafiki na ndugu yangu, Ethan Zuckerman. Halafu pia blogu ya Ory Okollah, Kenyan Pundit.

BC: Kila mwanablog anakuwa au anashauriwa kuwa na malengo maalumu na blog yake. Nini lengo maalumu la jikomboe?

NM: Mwanzoni nilipoanza kublogu nilikuwa nikiandika mambo mengi ambayo huwa pia yako kwenye makala zangu za magazetini. Nilikuwa nikiandika sana masuala ya siasa, utamaduni, na demokrasia. Ila baadaye niligundua kuwa zipo blogu nyingine zinajitokeza zinazungumzia masuala hayo. Ila ni blogu chache zinazozungumzia masuala ya teknolojia na kuonyesha jinsi gani ilivyo muhimu kwetu Watanzania na Waafrika kufikiria jinsi ya kutumia teknolojia hizi kama zana za kuleta maendeleo ya kijamii, kielimu, kiuchumi, n.k. Hivyo nikaanza kuandika sana kuhusu teknolojia, nikaanza kutoa taarifa mbalimbali kuonyesha ni nini kinaendelea kwenye nyanja ya teknolojia ya mawasiliano na habari.

Kwasababu ninahudhuria mikutano mingi, ninatumia blogu yangu pia kuandika habari ninazopata kwenye hiyo mikutano. Mara nyingi mikutano hii inahusu teknolojia na maendeleo. Nimekuwa pia nikitoa taarifa mbalimbali na matangazo kuhusu nafasi za kujiendelea kitaaluma na kimasomo sehemu mbalimbali duniani hasa kwa waandishi au watu wanaojihusisha na masuala ya teknolojia ya habari.

Lakini pia hutokea nikaandika jambo au habari ambayo haihusu teknolojia, siasa, au utamaduni. Huu ndio uzuri wa blogu. Ni uhuru. Jina la kitabu cha shujaa Steve Bantu Biko kinaelezea kwa ufupi ninavyochukulia malengo ya Jikomboe. Kitabu hicho kinaitwa, “I Write What I Like.”

BC: Ni blog gani au zipi unazozisoma kila siku? Kwanini?

NM: Ninasoma blogu nyingi sana kwa siku. Nikianza kuzitaja mahojiano haya hayataisha leo! Nikikutajia idadi yake unaweza hata usiamini. Kwakuwa ninatumia zana za kusomea blogu/habari) (newsreader), huwa sitembelei blogu moja moja. Akaunti yangu ya Bloglines, kwa mfano, inakusanya mambo yote mapya yanayoandikwa kwenye blogu ninazofuatilia. Hii inanipunguzia muda wa kwenda kwenye blogu moja hadi nyingine.

Blogu nyingi ninazosoma ni zile zinazoandika kuhusu Afrika, yaani blogu za Waafrika au wasio Waafrika ambao wanaandika kuhusu Afrika.

Sababu kubwa ya kusoma blogu hizi au kufuatilia blogu nyingi namna hii ni kuwa kazi yangu ya Uhariri kwenye Global Voices Online inanihitaji kufuatilia kwa karibu blogu zinazohusu Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara.

BC: Tangu uanze kublog umeshaandika mambo mengi sana. Uwezekenano ni kwamba kuna jambo ambalo uliandika likaleta gumzo au majadiliano kushinda mengine. Unakumbuka ni jambo gani na nini kilitokea?

NM: Ili nijibu kwa uhakika itabidi nitazame blogu yangu kwenye nyaraka za nyuma. Ila kwa kufikiria haraka haraka moja ya habari ilileta gumzo ni wakati ule nilipoandika kumjibu mwanablogu wa Kenya aliyeandika mambo fulani ambayo niliona kuwa hakuonyesha kutuheshimu Watanzania hata kidogo. Niliona kuwa alimtukana Rais wetu. Ingawa sikubaliana na mambo mengi anayofanya Rais, niliona kuwa mwanablogu huyu alifanya makosa. Alisema pia kuwa Watanzania sisi ni Maimuna, hatujui Kiswahili.

Niongeze kidogo: katika mjadala uliofuatia kutokana na habari hii, niligundua jambo ambalo bado naliona hadi leo. Inaelekea kuwa itachukua muda kwa watu wengi kujifunza jinsi ya kujadiliana na kubishana mtandaoni. Nadhani kwakuwa watu wengi tumezoea kubishana na kujadiliana na watu tunaowajua, watu waliotuzunguka, teknolojia ya blogu inatuletea mazingira mengine ambapo wanatokea watu usiwajua wanakupinga, wanakusahihisha, wanakukosoa, n.k., hii inaweza kuwapa tabu baadhi yetu. Ni utamaduni ambao huzaliwi nao, ni utamaduni wa kujifunza. Utamaduni wa kukubali kukosolewa, kusahihishwa, kupingwa, n.k. Na huko ndio kukua kimawazo.

BC: Unajuaje kama blog yako inaleta mabadiliko yoyote katika jamii?

NM: Nadhani tunaweza kutazama swali hili kwa pande mbalimbali. Blogu yangu imeipa lugha ya Kiswahili nafasi fulani muhimu kwenye mtandao wa Intaneti na duniani.

Jikomboe imehamasisha watu wengi kuanza kufuatilia masuala ya blogu na hata kuanzisha blogu zao wenyewe. Unaona kama blogu ya Michuzi ambayo imesaidia sana kuwaunganisha Watanzania walioko nje ya nchi na mambo yanayoendelea Tanzania. Blogu ile naweza kusema kuwa ni moja ya mafanikio ya Jikomboe. Nisingekuwa na blogu ya Jikomboe, nisingeenda Ufini, na kama nisingeeda Ufini nisingekutana na Michuzi. Nilipokutana na Michuzi pale ndipo blogu yake murua ilipozaliwa.

 

Pichani Ndesanjo Macha akimpa mkono wa hongera na karibu Issa Muhidini Michuzi baada ya kumkaribisha rasmi kwenye ulimwengu wa blog walipokutana huko Ufini mwaka 2005

Tukiacha hiyo, blogu nyingine nyingi ambazo zimekuja kutokana na kuhamsishwa na Jikomboe zimetuletea maarifa na habari za kila aina. Habari hizi na maarifa haya ndio hujenga mitazamo na falsafa zinazoongoza maisha yetu ya kila siku.

Mabadiliko makubwa kwa mwanadamu humjia kutokana na maarifa, mafundisho, elimu, habari, n.k tunazopata toka:
1. Dini

2. Utamaduni Maarufu (filamu, habari za watu maarufu, muziki n.k.)

3. Vyombo vya habari

4. Mfumo wa Elimu

Mitazamo yetu, staili yetu ya maisha, na karibu kila kitu kinachotufanya kuwa tuwe kama tulivyo vimetokana na mambo hayo manne niliyotaja hapo juu. Jikomboe nayo inakuwa kwenye kundi hilo kwenye namba 3. Watu wananiandikia barua kusema wanaanzisha miradi fulani au wameanza kusoma vitabu fulani na mambo kama hayo kutokana na habari walizosoma kwenye Jikomboe. Mabadiliko haya yanayotokea kwa watu binafsi ndio hasa kiini cha mabadiliko kwenye jamii. Jamii hubadilika kutokana na walioko kwenye jamii kubadilika. Ndio maana watu husema, “kama kuna mabadiliko unataka kuyaona duniani, basi wewe binafsi badilika kwanza.”

Matangazo mbalimbali ya mikutano au nafasi za kujiendeleza ambayo nimekuwa nikitoa kwenye blogu ya Jikomboe yamesaidia watu mbalimbali (wale waliochukua hatua za kuomba nafasi hizo na kukubaliwa). Mfano mmoja ni mkutano wa TEDGlobal: Africa, the Next Chapter, uliofanyika Arusha mwezi wa sita mwaka huu.

Baadhi ya watu waliohudhuria toka Tanzania walipata taarifa hizo toka Jikomboe. Kuhudhuria kwao kumewajenga kitaaluma, kumewakutanisha na watu muhimu kwenye njanya mbalimbali, na pia wamefaidika kwa kupata kompyuta za mapajani za bure ambazo zimetolewa kwa wahudhuriaji wote 100 toka Afrika. Mmoja wao ni mwanafunzi wa masuala ya sayansi ya kompyuta, zawadi hii ni muhimu sana kwake kitaaluma. Mwingine ni mtengeneza filamu ambaye kompyuta hii itakuwa ni ofisi yake kuu ya kuhariri na kutengeneza filamu zake. Pengine mtu anaweza kusema kuwa watu hawa wanafaidika kama watu binafsi na sio mabadiliko ya jamii. Kumbe jamii ni mkusanyiko wa hao watu binafsi. Watu hao binafsi wanapobadilika, wanapowezeshwa, wanapokuzwa kitaaluma na kitaalamu, wanapoingia kwenye mtandao wa watu wengine kama wao duniani – wakibadilika, ndio jamii inabadilika. Kubadilika kwa jamii ni kubadilika kwa mimi, wewe, yule, na huyu, na yule. Tunapowezesha watu binafsi ndio njia mojawapo ya kuiwezesha jamii.

Nitamaliza kwa kusema kuwa Jikomboe ilikuwa ni blogu ya kwanza ya Kiswahili na pia blogu ya kwanza ya lugha ya Kiafrika. Hii imechochea mfumuko mkubwa wa blogu za Kiswahili na hivyo kukipa Kiswahili nafasi ya pekee kwenye blogu za Afrika na mtandanoni. Hili ni badiliko kubwa na linalonipa furaha kila kukicha. Tunahifadhi lugha yetu. Na kwangu mimi, lugha sio tu chombo cha kuwasiliana bali pia ni benki ya maarifa.

BC: Katika kublog unapenda kutumia zaidi nyenzo (tools) zipi?

NM: Zamani nilianza kublogu kwa kutumia Blogger ambayo iko chini ya Google. Ila siku hizi ninatumia WordPress. WordPress haimilikiwi na mtu yeyote. Ni ya kila mtu. Ni programu huria (open source). Kutokana na itikadi zangu za kisiasa na falsafa zangu, programu huria ninazipa kipaumbele. Lakini pia WordPress ninaipenda maana inanipa uhuru na vikolombwezo vingi zaidi kuliko wakati ule nikiwa kwenye Blogger.

BC: Kwa siku huwa unatumia muda kiasi gani kufanya masuala yanayohusiana na blogs kwa njia moja au nyingine?

NM: Nadhani natumia muda mrefu sana tofauti na watu wengi kwakuwa masuala haya ya blogu, pamoja na sababu nyingine, yananipa ulaji. Yananiingizia mkono kinywani.

BC: Baadhi ya blogs huchuja (moderate) maoni ya wasomaji kabla hayatokea katika blog ili kila mtu ayasome. Je blog yako huwa inafanya hivyo? Nini maoni yako kuhusiana na suala zima la kuchuja maoni ya wasomaji wa blogs?

NM: Nadhani kuna raha fulani mtu anapotoa maoni kisha anayaona yamejitokeza dakika hiyo hiyo. Ila pia njia hii inatoa mwanya kwa watu wanaotaka kuharibu uwanja huu badala ya kuwa uwanja wa majadiliano na mawasiliano huku tukiheshimiana, wanaufanya unakuwa uwanja wa upuuzi na matusi. Wako watu wengine pia wanaotumia blogu zetu kuweka matangazo yao ya biashara kama maoni na hata wakati mwingine viungo vya tovuti zenye picha za ngono. Kimsingi, sioni ubaya wa kuchuja uchafu kama unataka wasomaji wako waje mahali penye heshima na utu.

BC: Dunia hivi sasa inazidi kutekwa na tekinolojia ya internet siku baada ya siku. Ukitizama miaka kumi mbeleni, unadhani tekinolojia ya internet itakuwaje? Tutarajie mabadiliko gani/ yoyote?

NM: Ni vigumu sana kusema kwa uhakika tutakuwa wapi baada ya miaka kumi. Ninavyoandika hivi sasa pengine kuna watu wamekaa chini wanabuni zana ambayo inaweza kubadili kabisa Intaneti baada ya wiki mbili. Ni mfano tu. Ona kama YouTube. Nani alijua kuwa kutakuja kitu kama YouTube na kubadili kabisa masuala ya video mtandaoni?

Suala ni kuwa tunazungumzia teknolojia ambayo inabadilika kwa haraka sana. Teknolojia ambayo haihitaji gharama kubwa sana kwa watu kuichukua, kuifanyia kazi, kuibadili, kuiboresha na hata kuja na mapya kabisa. Jambo hili ndio linafanya zama hizi kuwa tofauti kabisa na zama kama za Mapinduzi ya Viwanda. Zama zile unaona matajiri walikuwa ni watu wanaotengeneza vitu vya kushikika. Kulikuwa na akina Ford…alikuwa anatengeneza magari. Siku hizi tuna akina Bill Gates….anatengeneza nini? Huwezi kushika kitu anachotengeneza ukaniletea. Najua baadhi ya watu wanadhani Bill Gates utajiri wake ni kutengeneza kompyuta. Hapana, yeye utajiri wake ni kutengeneza mfumo unaofanya kompuyta yako kufanya kazi za aina mbalimbali. Tazama Oprah Winfrey, yeye ni tajiri…hazalishi kitu cha kushikika. Kashike anachozalisha Oprah uniletee! Tuko kwenye zama ambazo uchumi unaendeshwa, kwa lugha yao, na “service” na “content.”

Jamaa wale waliiuza YouTube kwa fedha nyingi tu. Walikuwa jamaa wa kawaida kabisa. YouTube wala haikutengenezwa kwa akili za ajabu. Hapa unaona kuwa, utabiri mmoja ninaoweza kuutoa kwa uhakika ni kuwa Intaneti itazua watu toka madongo kuinama na kuwa nafasi kubwa kwenye jamii.

Kwahiyo tutegemee mabadiliko makubwa sana ingawa ni vigumu kusema kwa uhakika mabadiliko hayo. Nami sitaki kuwa Shehe Yahya. Ila nitasema kuwa simu za mkono Afrika zitakuwa ndio uwanja mkubwa wa masuala yanayohusu Intaneti kwa Afrika. Itakuwa rahisi zaidi, siku zinavyokwenda, kwa mtu aliyeko Afrika kufanya kila kitu kinachofanywa na kompyuta kwenye Intaneti. Hii imeanza kutokea ila mabadiliko makubwa zaidi yanakuja, siku sio nyingi.

Kwa upande wa Tanzania mabadiliko ambayo yanakuja na ninayasubiri kwa hamu ni yale yanayohusu masuala ya uchumi na blogu. Nina maana kuwa mifumo itaanza kujiweka wazi kwa jinsi ambavyo wanablogu watakuwa wanaweza kuingiza kipato kwa kutumia hii teknolojia. Jambo hili limeanza kidogo ila makampuni makubwa ya biashara siku zinavyokwenda yataelewa kuwa kuna blogu ambazo zinazomwa na wateja wao zaidi hata ya magazeti. Kuna aina ya biashara ambazo ukizitangaza gazetini sio rahisi upate wateja wake kama vile ukitangaza kwa watu ambao wako mtandaoni. Eneo jingine ni biashara ambazo wateja wake ni Watanzania ila wako nje ya nchi. Maeneo makubwa ya kuwapata wateja hao wanaoishi Ughaibuni ni kwenye blogu. Tunachohitaji ni kuandika na kuonyesha jinsi gani blogu zinaweza kutumika katika kukuza biashara na pia kumfaidisha mwanablogu wakati huo huo. Hili ni eneo ambalo nimepanga kulizungumzia zaidi kupitia vyombo vya habari Tanzania.

BC: Watu wengi wanaoanzisha blogs wamekuwa wakizitelekeza baada ya muda mfupi wakilalamika kwamba watu hawasomi wanachokiandika na hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kublog.Unawapa ushauri gani watu kama hao?

NM: Watu wengi hudhani kuwa ili blogu yako iweze kuleta mabadiliko lazima isomwe na maelfu ya watu. Kumbe maarifa na elimu vina uhai wake. Kuna kitu nashindwa kupata tafsiri yake kinaitwa “social life of knowledge.” Naweza kutembelea blogu ya Harakati (ya Jeff Msangi). Nikasoma jambo fulani, likanielimisha. Likaniongezea uelewa na maarifa. Nikatoka hapo nikaenda kijiweni kupiga gumzo na washikaji, nikawamegea maarifa yale niliyopata toka kwenye blogu hiyo, nao wakafaidika na kuelimika (ingawa hawakutembelea blogu hiyo). Jamaa hao nao wakaenda kazini kesho yake, wakagawia wafanyakazi wenzao hayo maarifa (ambapo wafanyakazi hao nao hawakutembelea blogu hiyo ila wanafaidika kama vile waliitembelea). Wakawagawia na hata wapenzi wao. Au anaweza akaja mwalimu kwenye blogu ya Jikomboe, akasoma jambo, akafumbua macho, akaenda kufundisha wanafunzi wake. Huyo ni mtu mmoja, kachukua maarifa na kuyapeleka darasani. Wanafunzi wake wakafaidi ingawa hawakutembelea Jikomboe. Au mwandishi wa habari, akatembelea blogu akapata maarifa fulani. Akatumia maarifa hayo kuandika makala ambayo inakuja kusomwa na maelfu ambao hawakutembelea blogu hiyo.

Ukiwa na blogu ina wasomaji kumi usifikiri kuwa unaongea na watu kumi tu. Labda watu hao wawe wanaishi aina ya maisha ambayo hawachanganyiki na kuongea na watu wengine.

Jiangalie wewe mwenyewe, mambo mengi unayoongelea, mitazamo yako, n.k., hukuzaliwa navyo. Vimetokana na vitabu ulivyosoma, mazungumzo na watu, maarifa shuleni, filamu ulizotazama, n.k. Kwa mfano, kuna mambo mengi ninaandika kwenye blogu yangu ambayo yametokana na mtazamo uliojengwa na kupanuliwa na kalamu za watu niliosoma vitabu vyao. Wasomaji wangu wanaweza wakawa hawajasoma hivyo vitabu, ila wanapoelimika kutokana na elimu yangu iliyotokana na hivyo vitabu inakuwa kama vile nao wamevisoma. Ndio blogu hivyo hivyo. Ukisomwa na watu kumi wanaofaidika sio hao kumi tu.

Kama mtu anaandika masuala yakinifu, basi ajue kuwa maarifa yake yanakuwa kama muhindi. Unapanda mbegu moja, muhindi ukikua na kukomaa unakuta una mbegu zaidi ya moja.

Jambo muhimu ni kuwa mvumilivu na kuchagua masuala utakayoandika ambayo unayafahamu vyema na unajua kuwa yatavuta watu kuyasoma na kutaka kurudi tena. Hata kama sio maelfu.

BC: Kila suala la blogs linapotajwa mara nyingi jina lako limekuwa likiwa mstari wa mbele. Wengine wamekupachika jina na kukuita “raisi wa blogs”. Hii inatokana na ukweli kwamba umekuwa mstari wa mbele katika kuelezea na kutoa ushauri mzuri kuhusu blog. Je ungepewa nafasi ya kuandika fomula kuhusu jinsi ya kuandika blog yenye mafanikio unadhani ungetoa fomula gani?

NM: Kwanza asante. Ila napenda kusema kuwa marais wa blogu tuko wengi siku hizi. Sitaki kutaja maana itabidi nitaje wote. Na wengine wapya wanakuja nyuma yetu.

Tuje kwenye swali sasa. Jinsi gani ya kuandika blogu yenye mafanikio? Swali gumu lakini rahisi pia. Ni gumu kwakuwa inategemea unazungumzia blogu ya namna gani maana kunaweza kuwa na tofauti kidogo kutokana na aina ya blogu.

Ngoja nijaribu kujibu kwa kifupi na kijumla (maana kama nilivyosema jibu linaweza kuwa tofauti kutokana na blogu yenyewe ni ya nini na iko kwenye muundo gani):

1. Andika kuhusu jambo au masuala yanayokugusa na ambayo una uelewa wake.

2. Heshimu wasomaji wako (muda wao na uelewa wao [kwa mfano, usiwe unaandika jambo jipya mara moja kila baada ya miezi miwili! Watu watakuja mara ya kwanza, ya pili, na labda ya tatu kisha huwaoni tena]).

3. Andika vizuri, tumia lugha vizuri (unaweza hata kutafuta vitabu vya jinsi ya kuandika) na panga kazi kwenye blogu yako kwa namna na kupendeza na itakayorahisisha msomaji kusoma na kujua ziliko habari nyingine.

4. Tembelea blogu za wengine na ushiriki kwenye majadiliano

5. Rejea namba moja: unaweza pia kutumia ubunifu kuchagua jambo muhimu ambalo hakuna watu wengine au wanablogu wengi wanaoliandikia. Kuna blogu za namna hii ambazo zimekuja na staili na maudhui tofauti na blogu nyingine nyingi.

BC: Masuala ya blog yamekuwa na mchango mkubwa sana katika mabadiliko ya kijamii katika nchi nyingi duniani. Unadhani Tanzania inaweza kujifunza nini kutokana na mabadiliko ambayo yameshatokea kwenye nchi zingine kama vile Misri, Marekani nk?

NM: Tunaweza kujifunza mambo kadhaa:

1. Zama za vyombo vya habari vya hotuba zinaanza kufika ukingoni. Yaani vyombo vya habari vinavyotoa habari tu bila kushirikisha wasomaji zaidi ya kutufanya tu kama wasomaji tusio na kauli.

2. Teknolojia kama blogu zinaweza kutumiwa kuimarisha demokrasia na uwazi (kwa mfano, kwenye vyama, mashirika yasiyo ya kiserikali, n.k.).

3. Mabadiliko yanayoletwa na teknolojia kama blogu hayaji kimiujiza, watu wenye kuelewa sayansi ya mabadiliko ya jamii wanakaa chini na kuamua kuitumia teknolojia hii kama zana ya mabadiliko na maendeleo.

4. Ili teknolojia ilete mabadiliko kwenye jamii, kigezo au kizingiti kikubwa sio fedha au upatikanaji wa teknolojia bali ni mtazamo na fikra sahihi.

5. Wananchi hatuwezi kusubiri tuwezeshwe na serikali au wahisani, tunaweza kujiwezesha sisi wenyewe hata kwenye mazingira magumu namna gani.

BC: Katika siku za hivi karibuni kumeanza kuibuka malalamiko kwamba wanablog nao hawana tofauti sana na wanasiasa.Nao pia wanakutana katika matamasha,wanatumia hela kibao katika mikutano na hakuna lolote la maana linalotokea.Unazungumziaje shutuma kama hizo?

NM: Hapa labda na mimi niko maana nakwenda sana kwenye mikutano. Labda niseme kuwa kuna mikutano ambayo faida zake mtu huwezi kujua hadi pale utakapohudhuria. Halafu pia mikutano mingi ya masuala ya teknolojia, tofauti na ile ya wanasiasa ambao hupewa fedha ili wahudhurie, mikutano hii unayehudhuria ndio unalipa na sio unalipwa. Mkutano kama Pop!Tech unaofanyika Camden, Maine, Marekani kila mwezi wa kumi, kiingilio chake mwaka huu ni dola 3,495 za Kimarekani. Kwahiyo ukiona mtu anatoa fedha hizo bila faida yoyote na anahudhuria kila mwaka, basi atakuwa ana tatizo. Mikutano hii inasaidia, kwanza, kujenga jumuiya. Kuna umuhimu sana hasa watu ambao tuko mtandaoni kukutana ana kwa ana na watu wanaofikiria kama wewe. Ndio maana mimi husema kuwa wakati mwingine mikutano hii faida zake sio mada zinazotolewa (maana wakati mwingine unakuta mada hizo ulishazisikia mara nyingi) bali ni mtandao wa kijamii unaojenga. Nimejenga mitandao mikubwa ambayo huwa ina faida zake kikazi, kitaaluma, na hata kibinafsiJ

Ningependa hapa unipe muda ili niweze kuandika vyema na kuweka viungo vya mambo kadhaa makubwa yanayotokea Afrika ambayo yametokana na mikutano hii ya teknolojia. Tena mojawapo linatokea Singida hivi sasa ambapo panajengwa zahanati kutokana na mkutano uliofanyika mwaka juzi. Ningependa kuelezea hili kwa upana zaidi wakati mwingine.

 

Ndesanjo Macha akichangia jambo ndani ya Global Voices Summit huko New Delhi,India mwaka jana.

BC: Pamoja na kwamba idadi ya wanablog wa Kiswahili au watanzania inazidi kukua kila siku, ni blog chache sana ambazo ziko hai(active). Unadhani kwanini hali iko hivyo?

NM: Kuna suala la muda, kukata tamaa mapema, na kuanzisha blogu bila malengo maalum. Unapoanzisha blogu tu hivi hivi unafika wakati hujui hata uandike nini!

BC: Baadhi ya wanasiasa nchini Tanzania wameshaanzisha blogs zao.Ungependa kuwapa ushauri gani? Una ujumbe gani kwa wale ambao hawajaanzisha blogs?

NM: Moja ya kazi ambazo ningependa chama chetu, JUMUWATA, ifanye ni kuandaa warsha ndogo ndogo zisizo hata na chai ili kuwaonyesha wanasiasa jinsi gani blogu zinaweza kuwasaidia katika harakati zao za kisiasa. Wakati mwingine watu mpaka uwaonyeshe. Uwasukume kidogo.

Bado ningependa kuona ubunifu zaidi kwenye matumizi ya blogu kisiasa nchini Tanzania. Kuna mambo mengi ya kufanya. Bado sijaona ubunifu na mtazamo wa mbele.

Ninachoweza kuwashauri ni kuwa wajifunze toka kwa wanasiasa na nchi nyingine na kuona mambo ambayo yanaweza kuendana na mazingira yetu.

BC: Unatoa ushauri gani kwa vijana wanaotaka kuanzisha blog zao hivi leo?

NM: Waende wakazifungue haraka sana sekunde hii kabla geti halijafungwa! Nawashauri pia wanablogu wapya kuwasiliana na wanablogu wakomavu kwa ushauri na msaada. Watu wengi hawajui, jumuiya ya wanablogu ni jumuiya inayopenda sana kusaidiana na kushauriana. Mwandikie mwanablogu yeyote, atakwambia kama ana jibu, au kama hana au hawezi kukusaidia atakwambia nenda kwa fulani.

Nawashauri pia wasifungue blogu zao kimya kimya, wazitangaze kwa kupitia kwenye blogu za wengine na pia hata kutumia barua pepe. Sio vizuri kuwa mwanablogu mkiwa.

BC: Ukiwa hufanyi mambo ya blog huwa unafanya nini?

NM: Kama sisafiri, basi kusoma, kutembea (sehemu zisizo na kelele au watu wengi), kula, kuhudhuria maonyesho ya muziki. Siku hizi natembelea sana mito na milima.

Pia ninatumia muda wangu kuandika kitabu kuhusu masuala haya ya teknolojia.

 

BC: Ungependa wasomaji wa mahojiano haya wajue nini kuhusu wewe ambacho pengine hawakijui?

NM: Nilishawahi kuwa mchunga mbuzi!

BC: Je kuna swali lolote ambalo hatujakuuliza ambalo ungefurahi kama tungeliuliza? Kama lipo tafadhali liulize na kisha lipe majibu.

NM: Naona umeuliza yote. Asante sana wana BongoCelebrity. Kazi nzuri mnafanya. Nimependa sana wazo hili la blogu kama hii. Nawatakieni mafanikio.

 

Pichani ni Ndesanjo Macha na mwanae aitwaye UKWELI.Samaki mkunje angali….

Kama unataka muongozo wa jinsi ya kuanzisha blog yako bonyeza hapa.

Advertisements
 

29 Responses to “TAFAKURI YA KINA NA NDESANJO MACHA.”

 1. michuzi Says:

  NINA FURAHA NA FAHARI KUWA MMOJA WA WATU WA AWALI KUTIA NENO JUU YA NDESANJO MACHA AMBAYE KWANGU NI MFALME WA BLOGU ZA KISWAHILI DUNIANI. HAKUNA WA KUMGUSA, SIO TU KWA UMAHIRI WAKE BALI PIA KWA UTOVU WA UCHOYO WA KUTAKA KILA MTU AFAHAMU KUBLOG. TEMBELEA www,jikomboe.com KUTHIBITIS HILO.

  HATA SIJUI NIMSHUKURU VIPI JEFF MSANGI WA HII TOVUTI YENYE LENGO LA KUFAHAMISHA ULIMWENGU WATU MUHIMU KATIKA JAMII YA KITANZANIA POPOTE ILIPO. KWA MSEMO WA KIJIWENI NAOMBA NIKIRI KWAMBA KWA NDESANJO MACHA BONGO CELEBRITY IMEGOTA IKULU NA HAPA MTU KAMA MIE SICHOMOI!!

  NAWASIHI WATANZANIA WOTE KUIPITIA HII INTAVYUU ADIMU YA NDESANJO MACHA KWA SUBIRA ILI MTU ASIRUKE MSTARI HATA MMOJA. KILA NENO LA NDESANJO NI DIRA YA KUBLOGU KWA YEYOTE ANAEONGEA KISWAHILI.

 2. Duh! Na heshima kubwa kuliko!Na haya mahojiano ni shule….

 3. Ni mahojiano elimishi, nami naungana na walionitangulia katika kuelezea kufurahishwa kwangu na juhudi za mwenzetu Ndesanjo Macha.
  /Maggid

 4. Zumba's Says:

  Kama wadau hapo juu walivyochangia, Ndesanjo ametoa elimu kwa wana blog katika haya mahojiano. Kama alivyosema katika kuanzisha blog usikurupuke bila kujua wewe mwenyewe unataka nini, matoke yake ndiyo yale ya kuanzisha blog na kuitelekeza kwa madai watu hawasomi.

  Hongera na asante sana Mr. NDESANJO

 5. Mloyi Says:

  Maelezo mazuri na kwa ufupi sana. Yanatosheleza kuelezea mwelekeo wa ndesanjo.

 6. aliko mwakanjuki Says:

  Kuna” wadau” “wawekezaji” Ndesanjo ni Muwezeshaji.safi sana bongo celeb kwa kutambua vipaji vya kweli.

 7. mwandani Says:

  Mahojiano mazuri na ya kuelimisha.

 8. Najion kama nimechelewa kuweka maoni hapa,lakini jamaa huyu ni mfano wa kuigwa.Ukikutana nae ana kwa ana ni darasa tosha lazima utoke na maarifa japo kiduchu.
  Nilikutana nae hapa Delhi kwenye GV2006 summit pamoja ni kwamba tuliongea kwa muda mchache kwa kuibia kamuda kadogo wakati wa vitafunwa lakini leo hii lile darasa la muda mfupi bado ninalo kichwani.

  Ndesanjo,hivyo hivyo spidi 120!

 9. chesi Says:

  Pongezi kwa wote wawili. maswali yalikuwa mazuri na majibu pia. yameongeza ufahamu wangu kuhusu blogu. pongezi Msangi. Pongezi Macha.

 10. Bob Sankofa Says:

  Kwangu Ndesanjo ni kaka na mwalimu, si tu wa maswala ya teknolojia bali kuhusu kujitambua utu wangu pia. Nimekutana na Ndesanjo mara ya kwanza mwaka 2001 kwa njia ya barua pepe, kipindi hicho nafanya kazi kama Graphic Designer kwa binamu yake mmoja anaitwa Charles Macha.

  Ndesanjo kwangu pia ni mzazi katika swala zima la blogu, yeye ndiye hasa mkunga mkuu wa http://www.mwenyemacho.wordpress.com, alisaidia kuzaliwa kwa mtoto huyu mnamo tarehe 5/6/2007 pale Arusha Hotel.

  Nimefurahia mahojiano haya sana sana. Kuna kitu kimoja kuhusu Ndesanjo, Jamaa hata ukimhoji mara tano kwa siku mahojiano yake yatavutia na utahitajika kusikiliza, hana jibu moja, hana uelewa mmoja, hana mtazamo mmoja. Safi sana mahojiano haya kaka Jeff.

  Mpaka wakati mwingine,

  UHURU!

 11. Kaka Poli Says:

  Kaka Macha, haya mahojiano ni elimishi kama asemavyo ndugu yangu Maggid. Mjomba Michu naye nampongeza sana tena sana maana blogu yake ni kioo kitazamwacho sana miongoni mwa Watanzania duniani kote.

  Kubwa Juu kaka

 12. mwandani Says:

  A luta continua Ndesanjo. Shukrani BongoCelebrity kwa kuweka mahojiano.

 13. Wahenga walisema;AHSANTE ni miongoni mwa maneno machache yenye HEKIMA,Nami napenda kumpa neno hilo Mfalme wa Blog;Ndesanjo Macha.
  Alisaidia sana kunitanzanga mimi binafsi nilipoamua kuanzisha blogu yangu,soma http://jikomboe.blogspot.com/2006/02/blogu-hadi-kasulu.html
  nilianzia tangia gazeti la Mwananchi kusoma makala
  AHSANTE KAKA.

 14. simbadeo Says:

  Du, katika yote nimefurahia zaidi picha zilizotundikwa humu, hasa hasa inayomwonyesha UKWELI. Ni kweli, UKWELI utakuweka huru.

  Ahsante Kaka Ndesanjo. Hili ni darasa la kutosha.

  Kila la kheri katika blogging.

 15. freddy55 Says:

  Kuna methali ya Wa-Twi toka Ghana inayosema:
  “Ni mtu mmoja tu ndiye aliyeua tembo lakini mji mzima ukafaidi ile nyama…”
  Ni fahari sana kuwa na Mtanzania kama Ndesanjo.

 16. Halil Mnzava Says:

  Mahojiano haya yamenipa mwanga zaidi,
  Ingawa nakiri kwamba pindi nisomapo makala za Ndesanjo zinaniongezea maarifa zaidi.

 17. Kwangu mie yafaa tu kusema nachelea nisijechafua yaliyonenwa na wachangiaji hapo juu. Hiki ni kichwa bwana.

 18. Inocent Peter Ras IPE Says:

  Ndesanjo Big up! we ni kichwa sometime najiuliza uwezo ulikuwa nao wa kuandika mambo umepita kikomo hongera sana???/ UNITE FOREVER

 19. Annastazia Says:

  BWANA YESU AKUANGAZIE NJIA, UKAWE KICHWA NA SIO MKIA!
  BLESS U A MILLION MILLION TIMES!

  IN JESUS NAME WE PRAY,

  AMEN

 20. Ras Twin Says:

  Amani, Heshima na Upendo kwako Kaka Ndesanjo na mheshimiwa uliyefanya mahojiano. Ni mtazamo mwema kuwa na aina hii ya watu wenye mtazamo wa namna hii kwa watu wa taifa lake.
  Tunashukuru kuwa umeweza kumpata na kufanya haya akingali anapatikana ili kila mwenye swali amsake na kama alivyosema Michuzi (naye heshima kwake kwa taarifa latest) hana uchoyo wa elimu ya blog, basi wenye nia njia ndio hiyo.
  Blessings Mankinds

 21. Dinah Says:

  Heshima yako Macha, inafurahisha kuona Mtanzania anafanya mambo kwa ajili ya watanzania wengine kujifunza au kujisaidia.

  Mungu akubariki.

 22. gladness Says:

  Mi naomba tu kuuliza, je huyu ndie yule Fred Macha aliekuwaga anaandika forum kwenye Sunday News enzi hizo?

 23. Jangala Says:

  Gladness,
  Huyu na Freddy Macha ni mtu na kaka yake.Huyu ni mdogo wake Freddy.Freddy siku hizi anaandika makala zake The Guardian.

 24. gladness Says:

  Asante sana Bwana Jangala, unaweza kunipata email adress ya yoyote kati yao tafadhali?

 25. Jangala Says:

  Gladness,unaweza kutembelea site zao;jikomboe.com au freddymacha.com.Utapata mawasiliano nao pale.

 26. gladness Says:

  hi, Jangala! asante sana bwana nimempata Freddy ni binamu bwana, asante……..!

 27. Reg... Says:

  Glad;

  Na mimi tufahamiane waweza kuwa ndugu …. hata kama n kwa Adam na Eva.

 28. Reg... Says:

  Jangala;

  Una uhusiano na Jangala mzee wetu wa Mawenzi Tabata?

 29. lightness Says:

  Wachaga tunapendana…..watanzania wote ni ndugu
  Dada Glady huyo ni ndugu yako kabisaaa
  Hata mimi nimeona


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s