BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

MZEE FRANK HUMPLINK HATUNAYE TENA! August, 27, 2007

Filed under: Breaking News,Muziki — bongocelebrity @ 12:37 AM

Wakati wa harakati za kugombea uhuru wa Tanganyika kati ya mwaka 1954 mpaka 1961, jina moja lilitamba sana katika fani ya muziki. Jina hilo ni la Frank Humplink. Humplink alikuwa mwimbaji na mpiga gitaa maarufu sana wakati ule. Alikuwa akipiga muziki wake akishirikiana na dada zake wawili Maria Regina na Tecla Humplink.

Habari za kusikitisha ni kwamba Frank Humplink hatunaye tena. Mzee Humplink amefariki dunia jana tarehe 25 August 2007 huko nyumbani kwake Lushoto,mkoani Tanga. Alizaliwa tarehe 3 Aprili mwaka 1927. Amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Marehemu atakumbukwa sana kwa wimbo wake uliokuwa na mashairi yafuatayo, ‘Uganda nayo iende, Tanganyika ikichangamka, Kenya na Nyasa zitaumana’. Wimbo huo ambao ulikuwa ukiwasisimua sana wananchi, ulikuwa umesheheni ujumbe mkali wa kisiasa jambo ambalo lilikifanya chama cha TANU kuufanya kama vile wimbo wake rasmi kwani ulikuwa ukipigwa katika mikutano yake yote. Mikutano ya TANU ya siku za mwanzo ilikuwa ikifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja mbele ya Princess Hotel. Sahani ya santuri ilikuwa ikipigwa katika gramafoni kupitia kipaaza sauti.

Pamoja na kutamba sana kwa wimbo huo haikupita muda serikali ya kikoloni ikaelewa ujumbe mzito uliokuwemo katika wimbo huo ambao kimsingi ulikuwa unasema Tanganyika itakapoamka, kutakuwa vilevile na mapambano nchini Uganda, Kenya na Nyasaland.

Kilichofuata ni kupigwa marufuku kwa wimbo huo jambo ambalo inasemekana kuufanya pengine kuwa wimbo wa kwanza kupigwa marufuku katika historia ya utangazaji Tanganyika.

Enzi hizo Frank Humplink alijulikana zaidi kama “kijana wa kichaga kutoka Moshi” kwa sababu mama yake aliyejulikana kwa jina la Odilia Shayo alikuwa anatokea Kilema, Moshi mkoani Kilimanjaro. Baba yake alikuwa mzungu.

Ukiachilia mbali wimbo huo nyimbo zingine za marehemu na dada zake zilizotamba sana na zingali inapigwa mpaka leo katika sehemu mbalimbali zinapopigwa “oldies” ni pamoja na Chaupele Mpenzi, Mwalimu Shekinuru, Sisi kwa sisi, Hodi mimi mgeni, Kichupukizi, Bibi Maria Salome,Shida,Masuti Njiani, Nyoka Kabatini na kibao maarufu cha Harusi ambacho baadaye kilikarabatiwa na bendi ya Afro 70 na kuwa moja ya vibao vinavyopigwa hadi leo kwenye sherehe za harusi.

Katika ulimwengu wa muziki Marehemu Frank Humplink anasimama kwenye safu moja na Mzee Gabriel Omolo, Marehemu Fadhili William, Marehemu Fundi Konde, Marehemu Ahmed Kipande, Marehemu salum Abdallah na wengine wengi waliovuma katika miaka ya sitini. Ni hoja isiyo na ubishi kwamba majina kama hayo hapo juu ndiyo yanaweza kusemwa kuwa ni msingi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki.

Marehemu ameacha mjane, watoto sita (watatu wa kiume na watatu wa kike),wajukuu kadhaa na kilembwe mmoja. Anatarajiwa kuzikwa jumamosi ijayo huko nyumbani kwake Lushoto mkoani Tanga alipohamia tangu miaka ya 60. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Advertisements
 

9 Responses to “MZEE FRANK HUMPLINK HATUNAYE TENA!”

 1. Tedi Shangeni Says:

  Kwanza lazima nitoe pongezi kwenu bongocelebrity kwa kutambua vipaji halisi na mchango wa watu kama Humplink kwa muziki wa Tanzania.Bila watu kama huyu na wengine mliowataja muziki wa Tanzania usingesikika popote.Ingawa hivi leo tunauzika taratibu muziki wetu,bado napata ahueni nikisikia oldies kama za watu hawa.Pole kwa ndugu ,jamaa na marafiki.Pumzika pema Frank Humplink

 2. Nampesya Says:

  Poleni sana wafiwa wote.Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu.

 3. Bob Sankofa Says:

  Mzee amekwenda lakini historia alishaandika, hakunan haja ya kusikitika bali tumuenzi kwa kuendeleza mapambano. Swali kubwa la kujiuliza ni je, wanamuziki wetu wa leo hawaoni umuhimu wa kutunga mashairi ya kimapinduzi zaidi ya yale yaliyopo ambayo mengi ni ya mapenzi?

 4. Shetui S.D Says:

  Mzee Frank Humplick alikuwa msanii hasa, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi Amina.

 5. fidelis m tungaraza Says:

  Tatizo langu siku zote ni kushindwa timiza yale ninayoyaazimia kuyatimiza. Na moja kati ya yale niliyoshindwa kuyatimiza ni kumuenzi Marehemu Frank Humplink.

  Mwezi Septemba 2006 nilikutana na Binti wa Marehemu Mzee Frank. Jambo la kwanza nililomuuliza ni juu ya Marehemu Mzee; Hali yake? Yuko wapi? Anafanya nini? Akanijibu, “..Hajambo, yupo Lushoto, amepumzika baada ya kustaafu..” Nikamuulizia kuhusu miziki ya Mzee. Akaniambia “..Sina miziki ya Baba..” Nikamuuliza “..Baba anazo santuri zake?..” Akanijibu “..Hana. Ziliazimwa na jamaa yetu mmoja ambaye hakuzirudisha tena..” Nikamuuliza “..Bado anapiga gitaa?..” Akanijibu “..Baba aliumia vidole wakati akiwa anafanya kazi Amboni..Lakini huwa anapigapiga from time to time..” Baada ya mazungumzo hayo nilijisikia uchungu sana. Nikaanza kufikiri ni namna gani nitaweza kumuenzi Mwanamuziki huyu mkongwe aliyebakia bila kujulikana kwamba yupo.

  Baada ya siku kadhaa nilikutana tena BJ ambaye ni binti wa Marehemu. Siku hiyo akanichukua kwenda Rose Garden Bar kuongea zaidi. Siku hiyo ndiyo nilipomuambia kwamba “..BJ! Kwenye maktaba yangu ya muziki nina miziki ya Mzee..” BJ alistuka sana, akaniambia “…Fidelis, Baba mwezi April Baba atatimiza miaka 80. Akipata zawadi ya miziki yake itakuwa ni zawadi kubwa sana..” Nikamwambia “..Nitakuleta hiyo miziki tena kwenye cd..”

  Siku kadhaa baada ya hapo. Nikaanza kampeni ya kuwatafuta wanasanii na wapenda sana ili kuwaeleza kwamba Mzee Frank Humplink yu hai na yupo wapi ili tumuenzi. Niliongea na Carola Kinasha na jamaa wengine wa Shada. Carola alinijibu “..Tatizo letu sisi wanamuziki ni kusuasua mpaka mwenzetu afe ndiyo tunaanza kumkumbuka. Fide, unamzungumzia Mzee Frank, David Musa ambaye amewafundisha wanamuziki kibao mmoja wao Athanas sasa anaumwalakini hatujajitokeza kumuangalia wala kumuenzi. Mambo yakiharibika ndiyo tunaanza kuhaha. Kafariki Uvuruge hapa na msururu mrefu sana wa wanamuziki wengine lakini tupo kama hakijatokea kitu..” Nikamuomba namba tya simu ya Tido Mhando. Akanipa. Nikajaribu kuipiga nikiwa Dar na Hata niliporudi Helsinki lakini haikuwahi kupokelewa.

  Niliongea pia na Abraham Kapinga na jamaa wengine wa Tanzanite. Tanzanite wana historia kuibuka na wanamuziki wakongwe. Pia nilimtambulisha Abraham kwa BJ kuhusiana na suala hili hili la kumuenzi Marehemu. Miaka ya 80 wakati wakiwa resident band Kilimanjaro Hotel, Simba grill waliwahi kuibuka na wanamuziki wakongwe kama Marehemu Fadhili William na Marehemu Fundi Konde.

  Nikaongea ana kwa ana na kwa simu na rafiki zangu wa miaka mingi Joseph Kussaga na Stewart Chiduo kuhusiana na kumuenzi Mzee Frank. Sikupata majibu.

  Hali kadhalika niliongea na kumpigia simu mara kadhaa rafiki yangu kwa miaka mingi Muhidin Michuzi ili anisaidie kutafuta njia ya kumuenzi Marehemu Mzee Frank. Kwa sababu nisizozijua sikufanikiwa.

  Jumapili tarehe 26.August.2007 saa tano asubuhi nikapokea text message toka binti wa Marehemu BJ ikisema “..Fide, Baba passed yesterday..” Kwa kweli ujumbe huu ulinistua, kunisikitisha, kunidhoofisha sana. Ilikuwa vigumu kuamini kwa sababu ujumbe wenyewe ulikuwa tata nikamuuliza tena BJ “..Una maanisha nini?..” Akanijibu “..Baba amefariki jana jioni saa kumi..”

  Baada ya kupumzika na kupata nguvu nikamtumia ujumbe Jeff Msangi, Muhidin Michuzi, na Joseph Kussaga kwamba Mzee Frank Humplink hatunaye tena. Jeff Msangi akanipigia simu mara tu alipupata ujumbe wangu na kuniambia nimtumie yale yote niyajuayo kuhusu Marehemu. Nikamtumia maelezo na picha za marehemu Mzee frank nilizokuwa nazo, bahati mbaya sikuwa na mziki yake yoyote kwa wakati huu kwa sababu niliiacha Helsinki wakati nikija Gotenborg, Sweden. Jeff, akawasiliana na BJ ili kupata maelezo zaidi. Ili kwamba awezi japo kutoa tanzia kama njia ya kumuenzi Marehemu Mzee Frank Humplink.

  Japo huwa nina tabia ya kuchelewa kuazimisha ninayoazimia kuyafanya nadhani moja ambalo sikuchelewa kulifanya ni kurekodi miziki ya Marehemu Mzee Frank na dada Zake kutoka kwenye kanda kupeleka kwenye Cd na kumtumia BJ ili aziwakilishe kwa Marehemu Mzee Frank kama zawadi na kumbukumbu kwa Marehemu kwa hazina alizozipoteza. Nilitengeneza durufu moja tu ya CD hiyo kwenye Chuo Kikuu Cha Muziki cha Sibelius kwa msaada wa mwalimu Arnold Chiwalala. Natumaini ilimfikia Marehemu.

  Namuomba Mwenyezi Mungu Ampumzishe Marehemu kwa Aamani na aipe faraja familia, ndugu, jamaa na marafiki zake wote. Amen.

  Ni miye maridhiya,

  Fidelis M Tungaraza.

 6. Sam Says:

  Please, please kama una CD/mp3 ya wimbo huo ulioutaja kwenye obituary tafadhali sana naomba unifahamishe wapi naweka kukupata uniuzie. Ningependa sana kum-surprise mama yangu mzee kwani huwa anaumba wimbo huu

 7. BJ Humplick Says:

  Fidelis na Jeff,

  Nawashukuru sana kwa juhudi zenu za kuweka habari za Baba yangu Mpendwa Marehemu Frank Joseph Humplick katika tovuti. Jambo moja tu kwa wasomaji wote: naomba muangalie ‘spelling’ ya jina lake. Ni “HUMPLICK”, na siyo “HUMPLINK”.

  Baada ya kusema hayo, napenda niungane na mawazo ya Fide, Bi. Carola, na wengineo, kuwa juhudi za wasanii wengi waliochangia masuala mbalimbali ya kisiasa na/au kimaendeleo nchini zinapita bila kutambuliwa wakiwa wangali hai, na wengi wao kufa bila kufaidi matunda ya jasho lao hususan kutokana na kwamba sheria ya hati miliki ilichukua muda mrefu sana kutekelezwa hapa nchini kiasi kwamba kazi nyingi za wasanii hawa zimekuwa zikitumika na baadhi ya watu kwa faida yao binafsi bila kutaja “source” au “original composition” ni ya nani. Mfano hai ni ule wa Bendi ya “The Mushrooms” ya nchini Kenya iliyopiga nyimbo za Marehemu Frank Joseph Humplick na wasanii wengine wakongwe na kuziuza katika nchi za Afrika Mashariki na pengine hata nje, bila wasanii husika kuombwa ridhaa yao au hata kutambuliwa kama watunzi wa nyimbo hizo. Nashukuru kwamba tovuti hii imeufahamisha umma kuwa wimbo maarufu wa “Harusi” ulitungwa na Marehemu Mzee Frank Humplick kwani sifa za wimbo huo ambao mashairi yake yamejaa nasaha nzito uliipatia bendi ya Afro 70 sifa kubwa na watu wengi kudhani kwamba WAO ndio walioutunga. Ni muhimu kazi za wasanii (wawe wa zamani au wa sasa) ziheshimiwe na kutambuliwa hata kama hazina hati miliki.

  Mwisho, napenda kuwafahamisha wasomaji wote kuwa Mzee Frank Joseph Humplick amezikwa Jumamosi tarehe 1 Septemba 2007 nyumbani kwake Lushoto, Tanga.

  Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina!

 8. Mohamed Said Says:

  Frank Humplick alikuwa rafiki yangu na kwa mapenzi yaliyokuwa baina yetu pamoja na mkewe ambae nilimchulia kama mama yangu nilikuwa nikiingia na kutoka katika nyumba yao hapo Lushoto bila ya wasiwasi.

  Mtu aliyeniunganisha na Mzee Frank alikuwa marehemu Peter Colmore wa Nairobi ambae ndiye aliyeufanya muziki wa Frank Humplick ujulilkane Afrika ya Mashariki kwa kuwa yeye ndiye aliemshawishi Frank Humplick katika umri mdogo wa miaka 23 ahame Moshi kwenda Nairobi kupiga muziki wake.

  Nimefahamiana na Mzee Frank takriban kwa miaka kumi na katika kipindi hicho nilichota mengi kuhusu maisha yake ya muziki.

  Nimesikitika kuona kuwa hapana mtu ambae ameweza kuandika tanzia ya maana kuhusu Frank Humplick kwa ajili hii basi nimetayarisha tanzia ambayo nimeifikisha katika gazeti moja maarufu Afrika ya Mashariki nikitegemea kuwa wataichapa.

  Insha Allah baada ya kuchapwa nitaitia katika mtandao ili wengine nao waisome kwa wakati wao.


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s