BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

TUNAMUITA “MZEE WA MACHARANGA”! September, 12, 2007

Filed under: Kabumbu/Soka,Michezo,Soka,Tanzania/Zanzibar,Watangazaji — bongocelebrity @ 6:54 PM

Kunako miaka ya 80 mpaka 90 ushindani wa soka nchini Tanzania ulikuwa ni wa aina yake. Ilikuwa ni kama kosa la jinai kusema wewe huna timu unayoishabikia baina ya mafahari wawili wa soka enzi hizo ; Simba na Yanga. Ilikuwa ni lazima uwe Simba au Yanga ! Kipindi cha michezo radio Tanzania cha saa mbili kasorobo usiku kilikuwa ni almasi.Hakuna anayetaka kukikosa !

Ni wakati huo huo ambapo kama ulikuwa huna fedha au muda wa kwenda uwanjani, hususani Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam, bado ulikuwa na nafasi ya kupata uhondo wa kinachoendelea taifa. Watangazaji wa Radio Tanzania walikuwa wanakupeleka « live » japo kimawazo tu uwanja wa taifa. Ulikuwa unapata msisimko wa kinachoendelea uwanjani kutokana na umahiri wa watangazaji wa mpira. Msisimko ulikuwa unazidi kutokana na vionjo na madoido ya watangazaji wenyewe. Kila kona ya nchi wapenzi wa soka ambao hawakuweza kufika Uwanja wa Taifa walikuwa wameketi chini, wameizunguka radio wakisikiliza mpira kwa makini kabisa.Ole wako upige kelele bila sababu.

Charles Hilary akiwa kazini

Mmojawapo kati ya watangazaji waliokuwa wakiturushia uhondo ule kiasi kwamba bila hata kutaja jina lake, kila mmoja aliweza kumtambua kwa sauti yake tu ni CHARLES MARTIN BARNABAS HILARY NKWANGA (pichani) ambaye wengi tunamjua tu kama Charles Hillary au « Mzee wa Macharanga ». Hivi karibuni tulifanya naye mahojiano motomoto kabisa. Hapa utapata historia nzuri ya maisha yake binafsi na yale ya utangazaji, mtizamo na ushauri wake kuhusu soka la Tanzania hivi sasa nk. Lakini pia utapata kujua ni kwanini mpaka hii leo bado tunamuita « Mzee wa Macharanga » ? Angepewa fursa ya kuwaalika wageni wanne kwa chakula cha jioni angewaalika kina nani ?Anakumbuka kitu gani kuhusu enzi zake za kutangaza soka Uwanja wa Taifa na mengineyo mengi.

Hivi sasa Charles Hilary anafanya kazi BBC London ambapo pamoja na shughuli zingine za utangazaji wapenzi wa ligi ya soka ya Uingereza (Premier League) na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC London bado wanapata fursa ya kuendelea kufaidi umahiri wake katika fani ya utangazaji hususani wa soka. Unaweza pia kusikiliza Idhaa ya Kiswahili BBC mtandaoni kwa kubonyeza hapa. Mahojiano kamili haya hapa ;

BC : Ulianza lini rasmi kazi ya utangazaji? Nini kilikuvutia kuingia kwenye kazi ya utangazaji? Uliwahi kufanya kazi nyingine mbali na utangazaji?

CH : Nilianza rasmi kazi ya utangazaji mwaka 1981 ingawa nilijiunga na Radio Tanzania mwaka mmoja kabla yaani mwaka 1980.Ilibidi kwa utaratibu wa wakati ule uzoee mazingira ya kazi kwa kipindi fulani,ukiwa unapanga kadi za salamu na mambo kama hayo na baadae unasoma masomo ya utangazaji ambayo yanahusisha mambo mengi ikiwemo namna ya kutumia mikrofone,utayarishaji wa vipindi,namna na kufanya mahojiano,vipindi vya muziki na siasa ya utangazaji,si unajua tena Radio ya serikali ni lazima upigwe msasa nk.Kwa hiyo baada ya mwaka mmoja nikaanza kazi ya utangazaji rasmi hiyo ni mwaka 1981 nikiwa kijana kabisa pale Radio Tanzania,ukumbuke kuwa wakati huo radio ilikuwa ni hiyo moja tu.

Nilivutiwa na kazi ya utangazaji tangu ningali mdogo tu. Nilipokuwa shule ya sekondari wenzangu wengi walikuwa wakipenda niliwakilishe darasa letu katika debate mbalimbali kwa maelezo kuwa nilikuwa naweza kujieleza kwa ufasaha. Hiyo ikanipa changamoto ya kuweza kusimama mbele za watu na kuzungumza bila soni. Hiyo hasa ndio ilinivutia kuingia kazi ya utangazaji wa Radio.Kwa umri wangu sasa wa miaka 48 sijawahi kufanya kazi nyingine zaidi ya hii ya utangazaji wa RADIO.

BC: Unaweza kututajia sehemu mbalimbali ambazo umewahi kufanya kazi kama mtangazaji?

CH: Nimefanya kazi ya utangazaji kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1993 Radio Tanzania Dar es Salaam. Mwaka 1994 nilijiunga na Radio One ikiwa ni radio ya kwanza binafsi kuanzishwa nchini Tanzania.Wakati huo nikiwa mmoja wa waanzilishi wake pamoja na kina Mikidadi Mahmoud na Julius Nyaisangah.

Mwaka 2003 niliamua kuacha kazi Radio One na kujiunga na Radio DW Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani ambapo nilifanya kazi mjini Koln na baadae Bonn hadi mwaka 2006 nilipokatiza mkataba wangu baada ya kupata ajira Idhaa ya Kiswahili ya BBC London,ambako nilijiunga mwaka 2006 tarehe 14 mwezi wa august na nipo hapo hadi sasa.

BC: Wengi tunafahamu kwamba ulizaliwa Zanzibar mnamo mwaka 1959. Unaweza kukumbuka mambo gani ya visiwani Zanzibar wakati wa utoto wako?

CH: Kwa bahati pamoja na kuzaliwa Zanzibar lakini sikukaa sana kwani mwaka 1968 nilikwenda Dar es Salaam na kusoma huko ambako niliingia darasa la pili katika shule ya Mchikichini,Ilala Dar-es-salaam.Kwa hiyo siifahamu zaidi Zanzibar kuliko ninavyoifahamu Dar es Salaam. Hata hivyo jambo moja ninalokumbuka wakati wa utoto wangu ni lile la mwaka 1964 siku moja baada ya mapinduzi ya Zanzibar,ambako nikiwa na umri wa miaka mitano nilikoswakoswa risasi na mtu mmoja namkumbuka akiitwa Herman kwa vile alikuwa ni rafiki wa marehemu baba yangu nilikuwa napenda kumuita Baba rafiki,yeye pamoja na mzee wangu walikuwa ni askari polisi na walikuja nyumbani kwetu kule Jang’ombe na wakiwa na bunduki zao alianza kuiangalia kama ilikuwa na risasi au la na hapo wakati akiwa anafanya hivyo marehemu mama yangu akawa anamsihi aache kuchokonyoa hiyo bunduki kwani ni hatari. Basi Baba Rafiki akawa anaendelea tu na mikakati yake huku akitoa uhakikisho kuwa ile bunduki haikuwa na risasi na ghafla ulisikika mlio mkubwa kuashiria risasi ilitoka.Mimi wakati huo nilikuwa nimekaa mkekani nakunywa chai na ile risasi ikapiga hatua chache kutoka nilipokaa,kama ingenipata basi hapana shaka ingeuvuruga mguu wangu wa shoto.Kulikuwa na shimo kubwa nyumbani kwetu kutokana na hiyo risasi.Pamoja na kuwa na umri mdogo tukio lile halinitoki mawazoni.Hofu yangu kubwa ni kuwa utaalamu wakati ule wa mtu kuingiwa na risasi sijui kama ulikuwepo wa kuweza kuitoa au pengine mguu ungekatwa sijui lakini namshukuru Mungu.

Tukio jingine ni kuondoka Zanzibar na kwenda kuishi Dar es Salaam.Nakumbuka ilikuwa tarehe 11 Machi mwaka 1968. Pamoja na kwamba wakati ule Dar kama tulivyokuwa tukiita tulikuwa tunaiona kama ulaya lakini nilihuzunika kuwaacha ndugu na hasa marafiki zangu nikiwa na umri mdogo kwenda kuanza maisha mapya ugenini.Nashukuru nilizoea haraka maisha ya Dar na sasa inaniwia vigumu kuishi Zanzibar kwa zaidi ya mwezi mmoja jinsi nilivyoizoea na kuipenda Dar.

BC: Ingawa wapo baadhi ya watanzania ambao wanaweza kusema waliufahamu muziki kutoka nchi za Latino au “macharanga” hata kabla hujautambulisha rasmi, wengi wameusikia na kujenga mapenzi na aina hiyo ya muziki kupitia kwako. Nini kilikuvutia katika aina hiyo ya muziki? Nani aliutambulisha kwako na kwanini ukauita “macharanga”?

CH: Muziki wa Latino upo kwenye damu yangu ukinikumbusha enzi za mapinduzi ya Zanzibar wakati ule Sauti ya Zanzibar ilikuwa ikizipiga sana nyimbo za Latino zikiwa katika ala tupu wakati vipindi vilipokuwa vimekatizwa kutokana na tukio la mapinduzi,basi ukawa mawazoni mwangu tangu wakati ule.Tatizo baada ya hapo sikuwahi kuzipata nyimbo zake.Nilipojiunga na Radio Tanzania nilifanya kila jitihada kuweza kuzisaka na nilipokwenda maktaba ya santuri nikazikuta na hasa za Celia Cruz na zile za Endy Montanyez. Lakini kwa bahati mbaya hakukuwa na nyimbo nyingi za aina ya Latino.Bahati nilipokuwa najiunga na Radio One na ulimwengu nao ukawa unapanuka wa miziki ya aina mbalimbali ikawa inaingia nchini kirahisi hivyo nikaamua kujikita zaidi katika miziki hii na kwa vile nilikuwa mmoja wa viongozi wa Radio ile basi sikusita kuchagiza na zinunuliwe nyimbo niyngi za Latino. Hilo lilitekelezwa na wakati wa kugawana vipindi ndio tukaamua kuanzisha kipindi cha muziki wa Mcharanga.

Charanga ni moja tu ya mitindo ya Latino ikiwemo mingine mingi kama vile Salsa,Cumbia,Chacha,Merengue nk.Kwa hiyo nilipokaa na Mikidadi Mahmoud tukaona neno Charanga linamvuto kuliko kuita majina hayo mengine,basi ndio tukaanzisha kipindi kwa jina la Muziki wa Charannga.Nashukuru ulipokelewa vizuri muziki ule na pia wapenzi wengi wa muziki ule waliokuwa kimya wakajitokeza akiwemo Brother Zenno Lukas na Brother Ghafour ama kwa jina la utani Mr.Latino na wengine wengi.

Charles Hilary (kushoto) akiwa na Mr.Mshana wa TVT hivi karibuni jijini Dar-es-salaam.

BC: Umahiri wako katika kutangaza mechi za soka ni jambo ambalo watu wengi sana wanalizungumzia pindi jina lako linapotajwa kuhusiana na soka. Unakumbuka ni mechi gani ilikuwa ya kwanza kwako kutangaza “live”? Unakumbuka ilikuwaje?

CH: Kwa upande wa soka mechi yangu ya kwanza kutangaza ilikuwa ni Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaa,mwaka 1982 ilikuwa mechi kati ya Yanga na Coastal Union ya Tanga,katika ligi daraja la kwanza Tanzania wakati ule kabla haijaitwa Ligi Kuu.Nilitangaza live mechi ile nikiwa na waalimu wangu Salim Mbonde na Ahmed Kipozi.Nilipelekwa kujaribiwa baada ya kufanya majaribio mengi tu yasiyo live.Kwa kujaribiwa ulikuwa unapewa dakika tano tu kutangaza na halafu unawaachia wazoefu.Basi nilipopewa dakika hizo tano nilipozimaliza nakumbuka nikawa najiandaa kumkabidhi mic Salim Mbonde lakini akawa ananiashiria niendelee tu.Huku kijasho kikiwa kinanitoka nikajitoa woga na kumaliza dakika 15 kama ilivyokuwa kawaida mnapotangaza watu wawili na nikaendelea hivyo na tangu wakati huo nikawa napangwa katika rosta ya watangazaji mpira Radio Tanzania.Hapa sina budi kuwashukuru sana Ahmed Kipozi na Sekioni Kitojo kwa jitahada zao binafsi walizokuwa wanachukua kunielekeza namna ya kutangaza vizuri zaidi mpira.Ilifika wakati mpira ukimalizika uwanja wa Taifa basi wananiambia tuelekee studio na kuanza kucheza tape ya mpira tuliotangaza na kunikosoa na kunirekebisha.Nawashukuru sana na Mungu awajaalie popote walipo.

BC: Katika kutangaza soka inasemekana wewe ndio mtu wa kwanza kutumia neno “majalo”. Neno hili lina maana gani hasa na ulilitoa wapi kwa sababu tumejaribu kulitafuta kwenye kamusi mbalimbali za Kiswahili hatulioni.

CH: Neno majalo sikumbuki kama mimi ndiye mtu wa kwanza kulitumia ila mimi nilishtukia tu tukilitumia hasa nilipokuwa natangaza mpira na Ahmed Jongo. Nadhani hapo kumbukumbu zangu zimeondoka kidogo,na nisingependa kujivika kilemba cha ukoka,ila nachoweza kusema ni kuwa nilikuwa nalitumia sana nikiwa na maana ya mipira ya cross ambayo ilikuwa ni ya hatari langoni.Kuna maneno mengi ya utangazaji wa mpira hayamo katika kamusi ya Kiswahili ni vionjo tu vinavyotoka wakati raha ya mpira inapopamba moto.Nakumbuka neno songombingo nilianza kulitumia hasa nikiwa na maana mchezaji anapojiandaa kupiga mpira basi akijichanganya miguu ndio inaitwa songombingo.

BC: Kutokana na kazi yako ya utangazaji umeshuhudia soka ya Tanzania ikipitia steji mbalimbali. Unalizingumziaje soka la Tanzania hivi sasa leo ukilinganisha na hapo zamani?

CH: Ingawa kwa muda mrefu sasa sijaziona timu za Tanzania zikicheza, kutokana na ninavyosoma kwenye magazeti ya nyumbani, soka ya sasa imeporomoka ukilinganisha ile soka ya zamani.Pamoja na kwamba vijana wa sasa wana bahati ya kupata vitu vingi tofauti na wachezaji wa zamani wameshindwa kucheza soka ya ushindani.Tukitaka Tanzania tuwe na timu nzuri ya taifa hatuna budi kuruhusu vijana wetu wadogo waende kucheza soka nje na pia kwa sasa timu ya taifa ichaguliwe kwa kuangalia vijana badala ya wachezaji waliokomaa ambao hata kufundishika inakuwa vigumu.Mwalimu wa soka wa timu ya taifa apewe uwezo wa kuzunguka kila kona ya nchi kusaka vipaji vya wachezaji vijana ili kuwa na timu nzuri ya soka.

BC : Ni tukio gani la utangazaji ambalo unalikumbuka zaidi?

CH : Tukio ninalolikumbuka katika kazi ya utangazaji ni mara ya kwanza siku nilipoanza kusoma taarifa ya habari ulikuwa mwaka 1981 lakini sikumbuki mwezi wala tarehe.Siku hiyo kwa vile kusoma taarifa ya habari wakati ule ilikuwa ni kitu cha tunu sana pale Radio Tanzania Dar es Salaam,nilijiandaa kwelikweli na radio ya nyumbani nikanunua betri mpya ili wanisikilize,nilipiga simu hata Zanzibar kwa Mzee na Mama na ndugu zangu wanisikilize ninavyosoma habari.Nikaingia studio tayari kwa taarifa ya habari ya saa saba mchana. Basi ngoma za Marehemu Mzee Nyunyusa zilipomalizika na saa kugonga zile nukta sita mtangazaji wa zamu akataja saa,ilikuwa ni saa saba kamili mchana.Ile naanza kujiandaa kusema HII NI TAARIFA YA HABARI…..umeme ukakatika.Duu nilipata hofu kubwa na haukurejea hadi saa saba na dakika ishirini.Nakumbuka wakati ule Mkuu wa Mipango Radio Tanzania alikuwa Mzee Suleiman Hegga,basi akaamuru taarifa ya habari isomwe baada ya umeme kurejea,niliisoma umeme uliporejea lakini sikuwa na mashamsham kama ambavyo ningesoma wakati ule saa saba kamili.Nakumkuka sana tukio hilo kwa kazi yangu ya utangazaji wa Radio.

BC: Unapokumbuka majina ya wachezaji wa soka wa zamani wa Tanzania ni yepi yanakujia kichwani mara moja kutokana na umahiri wao katika kusakata kabumbu?

CH: Wachezaji wa soka wa zamani Tanzania walikuwa wengi wanacheza soka safi sana lakini majina yanayonijia awali ni ya Gilbert Mahinya, Sunday Manara,Kassim Manara,Mohammed Rishard ama Adolf,Juma Pondamali,Lenny Ramadhani(marehemu),Edward Chumila(marehemu),Charles Boniface Mkwasa,Hamisi Gaga(marehemu),Julius Kalambo, Zamoyoni Mogella na marehemu Methold Mogela,Aboubakar Salum,Isihaka Hassan,Ahmed Amasha,Athumani Mambosasa(marehemu),Salhina akichezea winga Zanzibar na pia timu ya Taifa ya Muungano,Willy Mwaijibe(marehemu),Nassoro Mashoto,Rwemaho Mkama alichezea Pamba ya Mwanza huyu nasikia yupo Shinyanga siku hizi sina mawasiliano naye. Khalid Bitebo,Omari Zimbwe na Saleh Zimbwe wa Tanga hao na kulikuwa na beki mmoja wa Cosmo ya Dar akiitwa Msuba sijui yuko wapi hivi sasa.Wapo wengi sana lakini kwa ufupi hao walikuwa wakinikosha sana na usakataji wao wa kabumbu.

BC: Hivi sasa kupitia radio unayofanyia kazi , BBC, mnaweza kuwapa wasikilizaji wenu uhondo wa ligi ya soka ya Uingereza “live”. Ukiwatizama wachezaji mbalimbali kutoka Afrika wanaochezea vilabu mbalimbali vya Uingereza unadhani ni kwanini Tanzania hatuna bado wachezaji wetu katika ligi kama hiyo ya Uingereza? Kikwazo kiko wapi kwa mtizamo wako?

CH: Kikwazo kwa wachezaji wetu ni ubora wa soka ya Tanzania. Kiwango chetu kwa mujibu wa FIFA hakitufanyi tuwe kifua mbele kiasi cha wachezaji wetu kukubalika soka ya Uingereza au Ulaya kwa ujumla.Kinachotakiwa angalao tuwatoe wachezaji wetu wacheze Ulaya hata katika ligi ndogo ili watambulike.Sina uhakika ni kwa kiasi gani wachezaji wetu wameweza kutambuliwa vipi kutokana na ziara za mafunzo wa lizofanya katika nchi za Ulaya hivi karibuni. Vijana wetu wana vipaji, tatizo ni kwamba hawapati nafasi ya kucheza Ulaya badala yake wanaambulia kwenda Uarabuni ambako soka yake sio ya kutisha.

BC: Tangu uanze kazi yako ya utangazaji ni wazi kwamba umeshawahoji watu wengi. Katika watu wote uliowahi kufanya naye mahojiano yupi hutomsahau kamwe? Kwanini?

CH: Ni kweli, mahojiano nimefanya na watu wengi ila sitomsahau Waziri wa Sheria wa Kenya Martha Karua ambaye nilifanya nae mahojiano hivi karibuni tu kuhusu sheria mpya ya wahariri wa vyombo vya habari kutakiwa kutoa vyanzo vya taarifa zao huko Kenya. Kwa kweli ni mama mkakamavu kujibu maswali ya waandishi wa habari na alinitoa jasho kweli hasa nilipombana kuwa yeye mwenyewe aliwahi kuandamwa na waandishi ndio sababu wanapitisha sheria hiyo basi katika kujibu swali hilo akaniambia MIMI NIMECHANGANYIKIWA.Nilifurahi hata hivyo kupata mhojiwa mkakamavu namna ile.

BC: Maendeleo ya kitekinolojia ya mitandao ya internet yanakusaidia kwa kiasi gani katika kazi zako za utangazaji? Kwa maoni yako nini faida au hasara ya redio za mitandaoni katika nyanja nzima ya utangazaji?

CH: Maendeleo ya teknolojia kamwe hayawezi kuepukwa katika kazi hizi za utangazaji. Hii ni kwa sababu hata sasa hapa BBC na hata kule Ujerumani kila kitu unafanya kwa kutumia kompyuta ikiwemo kuhariri story yako,kutafuta contacts za kila aina nakadhalika.Faida ya Radio za mitandaoni ni kuweza kuwafikia watu kila kona ya dunia kutokana na urahisi wake na unafuu.Hasara inaweza kuwepo iwapo radio hizo zitakuwa na waendeshaji ambao hawana ujuzi na taaluma ya utangazaji na badala yake kuzitumia kwa mtazamo usiofaa ambao unaweza kuwapotosha wasikilizaji.

BC: Je kuna mtu yeyote ambaye hujawahi kufanya naye mahojiano na ambayo ungependa siku moja kupata fursa ya kufanya hivyo?

CH: Ningependa kabla ya kufikia muda wangu wa kustaafu kazi niweze kufanya mahojiano na Nelson Mandela. Ingawa kwa sasa hivi sio jambo rahisi tena kwa sababu Mzee Mandela amekwishatangaza kujiondoa katika masuala ya hadhara, kumhoji ni jambo ambalo ningependa sana.Sauti ya Mandela hata ikisalimia tu ina mvuto mkubwa achilia mbali anachokizungumza.

Charles Hilary (wa tano kutoka kulia) akiwa na wafanyakazi wenzake wa Idhaa ya Kiswahili BBC -London hivi karibuni jijini Dar-es-salaam wakati wa kusherekea miaka 50 ya idhaa hiyo.

BC: Ni watangazaji gani nchini Tanzania na nje ya Tanzania wanaokuvutia zaidi katika utangazaji wao hivi sasa?

CH: Kwa Tanzania watangazaji wanaonivutia kwanza ni Tido Mhando ambaye hivi sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa TvT. Kaka yetu huyu fani ya utangazaji imo ndani ya damu yake na ni mtu makini sana hasa afanyapo mahojiano. Wengine ni pamoja na Julius Nyaisangah wa Radio One hasa kwa usomaji wa taarifa ya habari anasoma kitu unakielewa na kwa upole sana.Mwingine ni Maulid Kitenge wa Radio One ambaye mahojiano yake ya uchokozi kwa viongozi wa michezo yanasisimua. Huyu bado ana muda mrefu wa kuendelea na fani hii kama atazidi kujibidiisha.

Kwa nje ni mwenzangu hapa BBC Ali Saleh ambaye ingawa mwenyewe husema hapendi kujisikiliza sauti yake, ni mtangazaji mzuri sana anayeifahamu sana kazi yake na kisima kizuri cha kuchota hekima ya kazi hii kwa vijana wanaochipukia katika kazi hii hivi sasa.Labda niseme pia kwa nyumbani Tanzania zamani aliyekuwa ananivutia katika kazi ya utangazaji ni Mzee Suleiman Hegga,ambaye sasa amekwishastaafu. Bado nashangaa kwa nini hajishughulishi kutoa utaalamu wake kwa vijana wa siku hizi wanaopenda fani ya utangazaji.

BC: Endapo ingetokea ukapewa fursa ya kuwaalika wageni wanne duniani kwa ajili ya chakula cha jioni (dinner) ungewaalika kina nani? Kwanini?

CH: Kwanza ningependa kumualika Che Guevara, mwanamapinduzi mzaliwa wa Argentina aliyeshiriki katika harakati za ukombozi katika nchi mbalimbali zikiwemo pia za Afrika. Marehemu Mama yangu Mzazi kwa vile hakuna kama mama na nilimpenda sana mama yangu(RIP).Hayati Bob Marley mwanamuziki wa zamani wa Reggae ambaye tungo zake zilikuwa zinahisia kali kwa dunia. Mwisho ni Arsene Wenger kocha wa timu ya soka ya Arsenal,huyu namuona ni profesa wa soka kwa sasa duniani kutokana na mbinu zake za ufundishaji.

BC: Asante sana Charles kwa mahojiano haya. Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.

CH: Asanteni BongoCelebrity.

Tulipompa Charles Hillary Nkwanga nafasi ya kuchagua wimbo ambao angependa uambatane na mahojiano haya hakusita kuuchagua wimbo uitwao Mario uliokarabatiwa na AFRICANDO kwa kushirikiana na Marehemu Madilu System ambaye originally ulikuwa ni wimbo wake alioutoa kwa mara ya kwanza mwaka 1986. Unapatikana katika albamu ya AFRICANDO iitwayo Ketukuba. Usikilize hapa chini na utaelewa kwanini anaitwa “Mzee wa Macharanga”.

Picha zote kwa hisani ya Issa Michuzi.

Advertisements
 

31 Responses to “TUNAMUITA “MZEE WA MACHARANGA”!”

 1. Zaynab Says:

  Kwakweli nimefurahi kumsikia mzee wa macharanga na amenichekesha sana kuhusu siku yake ya kwanza kusoma taarifa ya habari. Inaonekana alipania kwelikweli!

  Yani ana kipaji na sauti yenye mvuto, unakuwa na hamu ya kumsikiliza tu, besi flani hivi.

 2. beutness Says:

  Mahojiano mazuri sana, tunashukuru. Naomba kuuliza Charles Hilary ni mwenyeji wa wapi? namaanisha kabila lake.

 3. muddy Says:

  Leo kaka Chaaaz amenikumbusha mbali sana enzi zile za utangazaji wake namnukuu wakati mchezaji anapoanguka uwanjani hasa awe marehemu Hamisi Gaga utamsikia ‘kuna mchezaji anagaagaa pale chini sijui nani yule!ah ni Gaga gaga anagaagaa hapa! kwa kweli ilikuwa ni burudani tupu.
  Kaka Chaaaz nakutakia maisha mema na yenye baraka BC keep it up!

 4. BongoSamurai Says:

  Uncle Chazzzzzzzz nashukuru kwa mahojiano mazuri.Mimi sikuwa mpenzi wa muziki wa latino ila kwa kupitia kipindi cha muziki wa macharanga ambacho ulikuwa unakiendesha nilijikuta navutwa kwenye ulimwengu wa macharanga maana ulikuwa unatoa pia historia ya muziki huo wa latino na kupitia hapo nilijifunza mengi sana.
  Kila la kheri Mzee wa Macharanga.

 5. Editor Says:

  Kwa ruhusa kutoka kwa Charles Hilary naomba nikujibu mtoa maoni # 2 kwamba Charles ni Mpogoro na mama yake ni Mmakua.Asante.

 6. Lizzie Says:

  Nampenda sana charles hillary alikuwa mzee wa macharanga sana na mzee wangu(baba)wakijirusha enzi zao weekend enzi hizo na kumbuka tulikuwa tunakutana nae pale guyz & galz karibu na victoria kwenye suop was nice siku zile

 7. DarRu Says:

  Safi sana Chaz. Utangazaji wako wa mpira bado uko msikioni mwa wapenzi wa mpira wa siku hizo kabla luninga hazijatufikia. Swali kwako Chaz: Ni timu gani hapa Tz kati Yanga na Simba unaipenda? Na uliweza kumudu vipi kuendelea kutangaza pale timu uipendayo inapofungwa?
  Kila la kheri katika kazi zako.

 8. muoshakinywa Says:

  Good lakini bado mnahitaji improvement katika kufanya mahojiano. Personal history bado kabisa hamjui kuuliza.

 9. Seoul city Says:

  yep nimefurahi sana kumsikia mzee wa charanga akituahabirisha mambo,nyinyi watangazaji wetu wa bongo mna wajibu wa kuyafanyia kazi hayo muhimu alozungumza,kama kuhusu soka..ni muhimu kupata vijana katika timu ya taifa..ambao watadumu wka mda na kuelewa haraka yale ambayo wafundishwa na mwalimu…hongera bongocelebrity kwa kazi nzuri.

 10. Meliyo Says:

  Mahojiano safi sana.Charles mimi nazimia sana utangazaji wako..keep it up.@ Muoshakinywa hapo juu, hivi unataka mpaka waulize watu wamevaa nguo za ndani za rangi gani ndio uridhike? Kaulizwa kazaliwa wapi,kakulia wapi,kasomea wapi,kafanya kazi wapi nk.Hujatosheka?Big up bongo celebrity.Endeleeni hivyo hivyo.

 11. Max Tarimo Says:

  Nimefurahi sana kusoma mahojiano haya.Charles amesema mambo muhimu sana kuhusu soka la bongo.Ni muhimu yakazingatiwa.Bongocelebrity napenda sana utendaji wenu na watu mnaowachagua kuwahoji.Mnahifadhi historia muhimu sana za nchi yetu.Serikali yetu ingetakiwa kuwaungeni mkono kabisa kwa sababu kwa mwendo huu vizazi na vizazi vitayakumbuka majina haya.Tukumbuke kwamba kizazi cha leo ni digitalized.Hongereni sana,endeleeni kutupa vitu.

 12. Mikasi Says:

  Editor tunabishana huku, Je waweza kumuuliza Chaaz alikuwa ni mpenzi wa timu gani kati ya Yanga na Simba?

 13. Editor Says:

  DarRu na Mikasi,Tumeyafikisha maswali yenu kwa Charles.Akitujibu tutaweka majibu yake hapa.

  Muoshakinywa,asante kwa maoni yako.Ungependa tumuulize maswali gani kwa mfano?Tutumie maswali yako bongocelebrity at gmail dot com.

 14. KASINGIRIMA, Says:

  MELIYO, JAMAA ANAPOWAKOSOA HAWA WAANDISHI WEWTU KUHUSU PERSONAL HISTORY ANAMAANA;WAULIZIE KWA UNDANI JINSI WALIVYOFIKIA KUWA WATANGAZAJI,CHARLES ALIJIELEZA ALIINGIA DAR AKIA DARASA LA PILI,JE ALIFIKIA ELIMU GANI ALISOMEA WAPI ,ANA DEGREE KATIKA MAMBO GANI,ATUKUMBUSHE SHULE NA VYUO ALIVYOSOMA,HII NI KUTAKA KUJUA NAMNA GANI VIJANA WANAEZA KUWA WAANDISHI MAHIRI KAMA WATAFUATA NYAYO ZA CHARLES.
  NINAKUUNGA MKONO CHARLES,SOKA LETU LITAKUWA KAMA VIJANA WATAPEWA MAFUNZO.NINAFUATILIA KWA KARIBU MICHEZO HUKO MAREKANI JINSI WANAMICHEZO WANAVYOPATIKANA KUPITIA VYUONI.NCHI YETU INGERUDISHA MSISIMKO WA MICHEZO YA UMISETA NA UMISHUMTA AMBAYO NILISHIRIKI KIKAMILIFU,KWANZA ITAAFANYA VIJANA WAWE NA MAHUDURIO MAZURI KWANI MICHEZO NI SEHEMU YA ELIMU

 15. yesenya Says:

  nampenda sana huyu mzeee ni mchangamfu sana

 16. van, basten Says:

  ee, bwana, sio mchezo, hsa huyu jaamaa, jinsi alivokuwa akitangaza kandanda ezi zile yeye na ahmaedi jongo, ilkuwa napenda kukaa alone niskie mpira hyuu jamaa ni mataam wa fotball, na ana maneno ya kufutia wakati akitangaza ball

 17. NDEKIA Says:

  Kwanza nashukuru sana bongo celebrity kumhoji Mtangazaji mwenzangu. Mimi ni mtangazaji wa redio moja hapa jijini. Aliyenivutia katika fani hii ni yeye mwenyewe Charles. Mimi nakumbuka kipindi alikuwa anatangaza kipindi cha habari nyepesi Radio One. Nilikuwa nachelewa darasani kwa ajili ya sauti yake kuna siku nikapewa adhabu ya kulala chini kuangalia jua kisa nimechelewa kuingia darasani,hiyo adhabu nikaiona ni ya kawaida cha kushangaza kesho pia nikachelewa darasani.Bwana Charles mimi ni mchanga sana katika fani hii nahitaji hekima na busara zako angalau nikunyemelee kidogo.

 18. Bob Sankofa Says:

  Aisee umri wa Charles kazini ni sawa na umri wangu duniani. Inatia moyo kuona mtu akifanya kazi ambayo amekuwa akiipenda siku zote kwa muda wa miaka 27 bila ya kugusa kitu kingine chochote.

  Anapozunguzmia kukoswa na risasi tunajifunza nini? Je ni watoto wangapi wamepoteza ndoto na maisha yao katika Afrika kutokana na swala zima la risasi amabzo hata hazitengenezwi Afrika? Nina hakika wameshakufa kina Charles wengi kule Liberia, Sierra Leon, sasa Sudan n.k.

  Inapendeza kuona watu kama kina Ndekia wamekuwa ni wamoja wa waathiriwa wa Charles Hilary.

  Kwa ufupi nimeipenda sana CV ya Charles.

  Once again BC, a hit on the mark.

 19. allan a mphuru Says:

  Inanikumbusha wakati ule chaaz anakuambia celestine sikinde mbunga yupo chini na refarii anapeta

 20. Editor Says:

  Baadhi ya wasomaji wetu hapo juu walipenda kujua kama Charles Hilary ni mpenzi wa Simba au Yanga? Tumemuuliza swali hali na amesema yafuatayo

  “Mimi zamani nilikuwa nikiipenda timu iliyokuwa ikiitwa ikiitwa Navy ya Zanzibar na baada ya kubadili jina nikaendelea kuipenda kwa jina la KMKM,lakini baada ya kuibuka timu ya Mlandege nikaamua kuipenda timu hiyo ingawa kwa sasa imeshuka daraja.Kwa hiyo huo ndio ulikuwa ushabiki wangu kwa soka soka ya Tanzania,sikuwahi kuzipenda Yanga au Simba”

  Natumaini mliotaka kujua kuhusu hilo mmempata.Yeye sio Simba wala Yanga!

 21. Mnette Says:

  Namoba aulizwe Charles mtangazajai bora anatakiwa awe na vigezo gani?na je,nani kwa sasa ana ubora wa juu kwa hapa nchini.

 22. Malaika Says:

  Tungepependa kujua maisha yake ya kifamilia Mzee wa Macharanga yakoje? Ameoa? ana watoto? wangapi? Kati ya watoto wake kuna yeyote anayefuata nyayo zake? Wamezaliwa wangapi kwao na asili yao ni wapi? Mahojiao yalikuwa mazuri lakini yaligusa zaidi masuala ya kazi na burudani. Ni muhumu kusikia maelezezo yake binafsi ili vijana waweze kujifunza kutoka kwake.

 23. Steve Gondwe Says:

  Nimependa sana mahojiano na mtangazaji huyu mahiri ingawa kuna vitu vidogo vidogo ambavyo vimekosekana kama vile ukubwa wa familia yake na vitu afanyavyo baada ya muda wa kazi.

 24. Editor Says:

  Bado baadhi ya wasomaji wetu wanaendelea kumimina maswali kwa Charles Hilary.Yaelekea mashabiki wa “Mzee wa Macharanga” walikuwa hawajui mengi kumhusu.Bila kusita,tumeyasaka tena majibu ya (maswali ya nyongeza) Majibu ya Charles ni kwamba;

  Ana familia, ameoa na ana watoto wawili,wote wa kile.Wa kwanza anaitwa Josephine ambaye Mungu akipenda anatarajia kufunga pingu za maisha mwezi wa Novemba mwaka huu.Mwanae wa pili anaitwa Faith, anasoma, yupo college jijini London akichukua Diploma ya masuala ya utalii.

  Kwa wazazi wake Charles wamezaliwa watatu. Kaka yake mkubwa anaishi Zanzibar, ni mwanasiasa.Baada ya kaka yake huyo ndio akafuata yeye Charles na baadaye mdogo wake ambaye kwa bahati mbaya aliiaga dunia mwaka 2001.Angelikuwa hai hivi leo angekuwa na miaka 44. Pia anasema anao wadogo zake wengine kwa upande wa baba.Hao wapo saba na kwa bahati nzuri wote ni watu wazima wanaojitegemea.

  Baada ya kazi Charles hupenda sana kuangalia taarifa za habari katika televisheni na pia hupendelea kuangalia mechi mbalimbali za mpira wa miguu hata zile za madaraja ya chini.Hii anasema humsaidia kuweka kumbukumbu iwapo baadhi ya wachezaji wa ngazi hizo za chini watafikia kiwango cha kuchezea timu kubwa hapo baadaye. Halikadhalika, hupendelea kutizama mchezo wa mieleka,ngumi na pia mchezo wa snooker katika ngazi ya kimataifa.

  Kila apatapo nafasi hupenda kukutana na ndugu,jamaa na marafiki,kupiga gumzo,kamvinyo kidogo na hivyo kubadilishana mawazo.

 25. kabambo Says:

  NIMEFURAHI SANA KUPATA HISTORIA YAKO YA MAISHA YA UTANGAZAJI HOGERA SANA
  NI MIMI DAVID NI JIRANI WAKO WA SINZA,NAISH MORI.

 26. sinza Says:

  great talent in terms of voice, and a bit of creativity.lakini tatizo la charles kama walivyokuwa watangazaji wengi wa radio tanzania, ni kwamba shule hawakuipatia kipaumbele.

  nasikitika kusema kwamba, licha ya sifa zote hizo charles ana limitations katika options as ni kazi gani apart from broadcasting in kiswahili anaweza kufanya, for instance hawezi kufunza chuo kikuu kusambaza ujuzi alionao kwa vijana wanaochipukia.

  imagine, anamfagilia maulid kitenge ambaye naye shule ni sifuri licha ya kuwa na kipaji cha hali ya juu – anyway vyuo havijafungwa they can still catch up.modern media practices lazina ku-embrace elimu na teknolijia.

 27. ANNA GABRIEL Says:

  Big up Chaaaz Hilary,
  Keep it up and and gud luck.
  Thanks.

 28. Chris Says:

  This is the tank of his field. Ila alianza kwa gundu?Na battery alinunua home wamsikie, na bado TANESCO wakakata umeme.

 29. mukrim Says:

  ya nawashukuru kwa maojiano mazuri nadhani alie sema yanakasoro akumbuie kwua akuna kitu kilichokosa hali hio lakin wka asimilia 100% wbinafsi yangu yametulia mzee wa macharanga ful mzuka .. enzi zile si mchezo ingawaje nilikwua mdogo lakin nayakumbuka madude yani kama ya nako2 nako kwa sasa au wazee wa 3-0 TMK so kifupi imekamilika yote big up.

 30. Prof Buhendwa Eluga Essy Says:

  Kazi nzuri, Chaz.
  Nakumbuka sana nilipokuwa mkimbizi Tz na hapo majuzi umenipa interview tokea BBC mimi nikiwa Uvira.
  Ahsante na hongera


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s