BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“TUSIBWETEKE”-FRESH JUMBE September, 23, 2007

Filed under: Muziki,Tanzania/Zanzibar,Utamaduni — bongocelebrity @ 1:12 PM

Wengi wetu tumetokea kumjua kama Fresh Jumbe ila kwa kirefu na kikamilifu jina lake ni Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima.Kila mwaka ifikapo tarehe 19 mwezi wa kumi (Oktoba) husheherekea kumbukumbu ya kuzaliwa.Alizaliwa mwaka 1968 katika hospitali ya Ngamiani iliyopo katikati ya jiji la Tanga. Anatoka kwenye familia ya watoto nane, wanne wa kiume na wanne wa kike. Wazazi wake wote wawili wametokea wilaya ya Pangani mkoani Tanga.Mama
akitokea katika kijiji cha Bweni kinachoangalia mto Pangani na baba
kwenye tarafa ya Mkwaja kijiji cha Buyuni kitopeni kilichopo mpakani
kabisa kati ya wilaya ya Pangani na Bagamoyo.

 

Akiwa Tanga sehemu anayoiita nyumbani ni Makorora “Mti Mkavu” karibu kabisa na shule ya msingi Makorora ambayo ndipo alipoanzia elimu yake ya msingi kabla ya kuelekea Bakwata Sekondari kwa ajili ya elimu ya sekondari.

Hivi sasa Fresh ni mmojawapo wa “mabalozi” wetu nchi za nje kupitia muziki.Anafanyia shughuli zake za muziki nchini Japan.Lakini walio wengi bado wanamkumbuka Fresh akiwa na bendi maarufu nchini Tanzania kama vile Sikinde,Msondo,Bicco Stars,Safari Sound nk. Kwa hakika Fresh Jumbe ni mojawapo ya majina ambayo washika dau katika medani za muziki hawawezi kuyasahau.

Siku chache zilizopita,tulipofanya naye mahojiano Fresh Jumbe alitueleza mengi.Katika mengi hayo suala la muziki wa Tanzania, inaposimama bongo flava alilipa kipaumbele cha aina yake. Tunaweza kudiriki kusema kwamba Fresh ametoa changamoto ya aina yake kwa wanamuziki wenzake,yeye mwenyewe,mapromota wa muziki,wana habari na kwa ujumla washika dau wote wa muziki nchini Tanzania. Ni changamoto gani? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Ulipokuwa mdogo kule Tanga unakumbuka ulikuwa ukisikiliza miziki ya kina nani? Je ilikuwa ni ndoto yako tangu utotoni kuwa mwanamuziki?

FRESH: Wakati wa utoto wangu nilikuwa nikisikiliza sana miziki ya wanamuziki wote kama vile kina Moshi Wiliam, Zahir Ally, Hassan Bitchuka, Shaaban Dede, Muhidin Mwalimu “Gurumo”, Cosmass Chidumule, Beno Villa, Shem Karenga, Msafiri Haroub, Hemedi Maneti, Salehe Kakere, Juma Mrisho “Ngulimba wa ngulimba”, Juma Ubao “King Makusa”, King Kikii na Ndala Kasheba. Pia nilikuwa nikisikiliza sana mabendi yote maarufu kama vile Msondo Ngoma, Sikinde, Bima Lee, Vijana Jazz, Urafiki Jazz, Safari Sound, JKT Kimulimuli, Mwenge Jazz, Polisi Jazz, Maquis, Mzee Makassy, Simba wa nyika, Tabora Jazz na nyinginezo. Pia nilikuwa nikisikiliza sana wanamuziki wa nje kama vile kina Franco, Tabu Ley, Verkys, Kanda Bongo Man, Pepe Kalle, Nyboma, Nzaya Nzayadio, Madilu System, Pepe Ndombe, Bob Marley, Michael Jackson, Lionel Richie, James Brown, Fela Kuti, Manu Dibango, Papa Wemba na wengineo. Nilimpenda sana pia Abeti Masikini kwa uimbaji wake. Pia nilizipenda sana bendi za Orchestre Kyam, Belabela, Fukafuka n.k.

Lakini zaidi ya wote hao, niliyekuwa nikimsikiliza zaidi, kuvutiwa naye na hata kutaka niwe kama yeye alikuwa ni hayati Marijani Rajabu “JABALI LA MUZIKI” Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.

SIKIA SAUTI YA FRESH HAPA AKIWA DAR INTERNATIONAL NA JABALI LA MUZIKI KATIKA NYIMBO “BWANA MASHAKA” na “MASUDI”

 

Ndiyo, nilikuwa na ndoto ya kuwa muimbaji. Nakumbuka wakati fulani nikiwa bado katika shule ya msingi kule Tanga, niliwahi kuapa kuwa maisha yangu ya ukubwani, kama yatakuwa ni ya kimasikini au ni yakitajiri au vyovyote vile, basi yatakuwa yametokana na miziki. Niliapa kuwa uimbaji ndio utakaoongoza maisha yangu. Kwahiyo ndoto yangu hiyo nilianza kuifuatilia mapema tu nikiwa bado mdogo kabisa na matokeo yake ni kuwa, mpaka leo maisha yangu ni miziki na miziki ndiyo maisha yangu.

BC: Je jina la Fresh ni jina lako halisi au ni la kisanii tu? Kama ni la kisanii nani alikutunga jina hilo ?

FRESH: Fresh ni jina langu halisi. Jina langu kamili ni Fresh Jumbe Mkuu, au kwa urefu zaidi ni Fresh Jumbe Mkuu Waziri Kungugu Kitandamilima.

BC: Mbali na kuimba unaweza kutumia vifaa gani vingine vya muziki kama vile gitaa,ngoma nk?

FRESH: Pamoja na kuwa uimbaji ndiyo hasa shughuli yangu, pia nina uwezo wa kupiga kinanda (Keyboards), gitaa la besi na pia napiga ngoma zote tu ikiwa ni pamoja na konga na drums. Pia nina ujuzi wa kurekodi muziki na kuchanganya sounds.

BC: Ni wanamuziki gani ambao unadhani walisaidia kwenye uamuzi wako wa kujiingiza kwenye kazi ya uanamuziki?.

FRESH: Marijani Rajabu kutokana na utungaji wake, uimbaji wake na ufanyaji wake wa kazi akiwa jukwaani alinifanya nitake kuwa kama yeye. Mwingine ni kaka binamu yangu “Marika Mwakichui” ambaye alikuwa muimbaji wa bendi ya Tanga International ya Tanga. Yeye pia alikuwa muimbaji mzuri na ndiye aliyenipandisha kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza ili niimbe baada ya kugundua uwezo wangu wa kuimba nikiwa bado niko darasa la sita. Alinipa moyo sana na kuniambia kuwa mimi naweza kabisa kuimba kuliko hata baadhi ya waimbaji wakubwa wa wakati ule. Kwahiyo namshukuru sana huyu brother kwa msukumo na msaada alionipa na kunifanya nijiamini na niingie kikamili kwenye miziki mpaka kufikia nilipofikia leo hii.

BC: Mojawapo ya nyimbo zako zilizotamba sana ni ule wa Tuhifadhi Mazingira. Ilikuwaje ukautunga wimbo ule wakati ule ambapo masuala ya mazingira hayakuwa yakiongelewa sana kama ilivyo hivi sasa?.

FRESH: Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1988 nikiwa katika bendi ya Safari Sound “Ndekule”, taasisi ya kuhifadhi mazingira ya Tanzania kupitia chama cha muziki wa dansi Tanzania “CHAMUDATA” iliteua baadhi ya watungaji iliyoamini kuwa ni watungaji wazuri, ili watunge nyimbo mbili za uhifadhi wa mazingira ili zikawakilishe nchi yetu kwenye Tamasha la kuhifadhi mazingira la Afrika katika siku ya mazingira duniani, ambapo wakati ule kwa upande wa Afrika, lilifanyika Nairobi Kenya. Mimi nilikuwa mmoja kati ya walioteliwa kutunga nyimbo hizo. Nakumbuka tuliitwa mimi, Cosmass Chidumule, Marehemu Hemedi Maneti, Jah Kimbute, Marehemu Eddy Sheggy, Marehemu Jerry Nashon “Dudumizi” na wengine kadhaa ambao kwa sasa siwakumbuki. Tulipewa maelekezo ya kila mtu kutunga nyimbo moja ya mazingira. Pia tulielezwa ni masuala gani muhimu yanayotakiwa kuzungumzwa kwenye hizo nyimbo. Tukapewa wiki mbili za kutunga nyimbo. Pia tuliambiwa kuwa, haya ni mashindano na washindi wawili watakaopatikana, yaani watakaotunga nyimbo mbili za kwanza zitakazokubalika zaidi na taasisi ya mazingira ya Tanzania, watapata zawadi ya pesa na pia wao ndio watakuwa wawakilishi wa nchi yetu kwenye hilo tamasha la mazingira huko Nairobi. Kwa bahati nzuri, nyimbo yangu ikawa namba moja na ya Cosmass Chidumule ikawa ya pili.

Kweli tukapewa kazawadi kidogo ka pesa na pia tukapelekwa Nairobi kuiwakilisha nchi kwenye tamasha hilo. Hilo ndilo lilikuwa chimbuko la wimbo wa “Tuhifadhi mazingira”

SIKILIZA TUHIFADHI MAZINGIRA HAPA

BC: Wanamuziki mbalimbali maarufu wa Tanzania wamewahi kutumia vipaji na umaarufu wao kuongelea mambo mbalimbali ya kisiasa. Wewe hujasikika sana ukifanya hivyo.Unadhani kwanini? Je siasa za nchi ni jambo unalolifuatilia kwa karibu?

FRESH: Mimi ni mfuatiliaji mkubwa wa mambo ya siasa. Si za nchi yetu tu, bali hata siasa za dunia. Naamini kuwa usipofuatilia siasa hasa za nchi yako, unakuwa kama mbwa uliyefungwa kamba ya shingo na “master” wake na kuburuzwa akielekezwa asikokujuwa. Kawaida yangu mimi sipendi kuropokaropoka bila mpangilio kuwaunga mkono au kuwakashifu wanasiasa au hata mtu yoyote yule bila ya kuwa na hoja ya msingi na ya uhakika. Binafsi nadhani nina nafasi nzuri sana ya kuweza kuzungumzia lolote nitakalo ikiwa ni pamoja na siasa kupitia muziki. Kwahiyo mimi niliamuwa kuwa, kuongea kwangu kuhusu jambo lolote ikiwa ni pamoja na mambo ya siasa, itakuwa ni kupitia kazi yangu ya muziki na mfano mzuri ni huu wimbo wangu mpya nilioupa majina mawili, unaweza kuuita “We can do it” au “Tusibweteke” ambao umesababisha watanzania wengi wanaonifuatilia kunitumia ujumbe kupitia website yangu wakinipongeza kwa niliyoyasema kwenye huu wimbo na wengine wakisema kuwa wimbo huu unaonesha kama nawatupia madongo wanasiasa wetu. Kwahiyo mimi nazungumza kwa njia hiyo.

Unaweza kuusikia wimbo huo hapa chini

BC: Ni onyesho gani lako kimuziki ambalo unalikumbuka sana? Lilifanyikia wapi na ilikuwaje?

FRESH: Pamoja na kuwa maonesho yangu karibu yote ninayoyafanya hapa Japan na Asia ni mazuri na yanayojaa watu kutokana na waandalizi wa huku wanavyofanya mambo yao kiuhakika, lakini maonesho yangu sita siwezi kuyasahau maishani mwangu, matatu yakiwa ni ya Dar es salaam, mawili hapa Japan na moja lilikuwa ni Kualalumpur Malaysia. Kwa Dar onyesho la kwanza liilikuwa ni lile lililofanyika pale DDC Magomeni Kondoa siku mimi nilipojiunga na Sikinde nikitoea Msondo. Mashabiki wa Sikinde waliokuwa wamejaa kupita kiasi, walinibeba juu kwa juu mpaka ikafikia wakati nikashindwa kuimba kutokana na msongamano wa mashabiki walionizunguka kwenye jukwaa huku wakinitunza pesa.

Onyesho la pili ni pale tulipohama wanamuziki saba kwa mpigo, mimi, Max Bushoke, Cosmass Chidumule, Chipembele Saidi, Hamisi Juma, Huruka Uvuruge, na Ali Jamwaka kutoka Sikinde kwenda Ndekule. Siku ya onyesho letu la kwanza pale Safari Resort Kimara palikuwa hapatoshi na show tuliyoifanya ilikuwa ni ya kihistoria. Show nyingine ya Dar ambayo ndiyo iliyofunga kazi kwa upande wangu nikiwa bado niko Tanzania, ni siku ya krismasi ya mwaka 1989 pale DDC kariakoo. Sikinde waliniita nirudi kwenye bendi nikitokea bendi ya Bicco Stars. Sikinde walitangaza vizuri na kuwaambia mashabiki kuwa krismasi hii Fresh Jumbe atakuwa amerudi na wimbo wake mpya “Kinyozi hajinyoi”. Siku hiyo ilipofika hakuna aliyeamini, hata mimi mwenyewe nilishangaa. Watu waliofika siku hiyo, ilikuwa ni rekodi kwa bendi ya Sikinde tokea ilipoanziswa. Kwa mujibu wa meneja wa bendi aliyekuwepo wakati ule “Hezron Mwampulo” pamoja na mhasibu wa bendi, mapato ya siku ile yalivunja rekodi tokea bendi ilipoanzishwa. Kwa jambo kama hilo kutokea kwenye bendi kama ile kwa sababu yangu, ni jambo nisiloweza kulisahau maishani mwangu. Pesa niliyotunzwa na mashabiki wakati nikiimba nyimbo zangu kama vile “Conjesta”, “Ndoa ya Lazima” na hiyo mpya niliyoingia nayo siku hiyo “Kinyozi Hajinyoi”, ilikuwa ni malaki kadhaa ambapo pia ilikuwa ni rekodi kwangu. Wanamuziki wenzangu nao pia walifaidika sana kwa kuokota pesa nyingi zilizoanguka kwenye stage wakati nikitunzwa.

Hapa Asia onyesho moja lilikuwa ni miaka miwili iliyopita kwenye hall moja kubwa iitwayo Astro iliyopo hapa katikati ya jiji la Tokyo.Lilikuwa ni onyesho la charity kusaidia waliokumbwa na tsunami kule Indonesia. Watu walifurika kupita kiasi. Wengi wao hawakuwa wakijuwa sana miziki yetu ya kiafrika. Walikuja kuona onyesho langu kwa mara ya kwanza na pia kutoa misaada kwa waathirika wa tsunami. Matokeo yake kwa namna moja au nyingine, walichanganyikiwa kwa miziki yetu. Ingawa wajapani na wazungu (ambao ndio asilimia kubwa ya watu wanaokuja kwenye show zangu) ni watu wenye nidhamu ya hali ya juu, lakini siku hiyo nilishangaa kuona watu wamebadilika. Waliwazidi nguvu walinzi wa stage, wakavamia stage na kuanza kucheza nami bila kujali. Show ilibidi isimame kwa muda wa dakika 15 na watu wakaombwa wateremke kutoka kwenye stage, vinginevyo show itakuwa imekwisha. Wakateremka na show ikaendelea huku watu wakishangilia kwa nguvu isiyo ya kawaida. Show hiyo ilinisaidia kupata wapenzi wapya wa muziki wangu na ndipo hivi karibuni nikafanya show nyingine hapa hapa Tokyo sehemu inayoitwa Ayase, ambapo watu wengi walijitokeaza (wengi wao wakiwa ni wale waliokuja kwenye ile show iliyopita). Jambo kubwa kwenye show hii ni pale kwa mara ya kwanza nilipoona watu kadhaa wakitoa machozi mbele yangu huku wakiniangalia nikiimba na kucheza. Nilishangaa na sikujuwa kilichokuwa kikiwaliza maana nilikuwa na uhakika kuwa hawakuwa wakielewa ninachoimba maana nilikuwa naimba kwa kiswahili. Na jingine ndiyo hilo la Malaysia miezi mitatu iliyopita ambapo liliandaliwa vilivyo na nikaona umati wa watu ambao kusemakweli sikuutegemea, hasa kwenye nchi ambayo sikuwa nikijulikana. Show ilifana sana hasa kwasababu mimi mwenyewe pia siku hiyo nilikuwa kwenye perfect condition kimwili na kiakili. Nikajijengea jina kubwa na nimeitwa tena mwaka ujao. Hayo yote ni maonesho yangu ya kihistoria ambayo sitayasahau kwenye maisha yangu ya kimuziki mpaka hivi sasa.

MSIKILIZE FRESH HAPA KATIKA “NDOA YA LAZIMA” ALIPOKUWA NA SIKINDE NGOMA YA UKAE.

BC: Wananchi wa Japan huwa wanaupokea vipi muziki wako uwapo jukwaani? Huwa unaimba kwa kutumia lugha ya kijapan pia?

FRESH: Muziki ni “Universal language”. Kama unapiga muziki mzuri, ambao unaonekana ni original yako/yenu na ukiwa na mvuto wa kuwavutia watu unapokuwa jukwaani, mtu hata kama asipoelewa lugha, ataupokea muziki wako vilivyo. Lakini ni lazima ufanye kazi nzuri uwapo jukwaani, vinginevyo utaangukia pua. Hasa ukizingatia kwamba watu hao unaowaimbia watakuwa hawaelewi uimbacho, kama melody pia ni mbaya, midundo isiyoeleweka na huonekani kuwa ni professional jukwaani, utakwama. Wajapani wote pamoja na watu wengine wanaohudhuria show zangu, nafurahi kusema kuwa wananipokea mimi mwenyewe pamoja na muziki wangu vizuri na kwa heshima ya hali ya juu. Hiyo imesababisha mimi na bendi yangu pamoja na balozi wetu wa hapa Japani tualikwe na kutembelea sehemu nyingi sana za hapa Japan huku tukiitangaza nchi yetu na miziki yetu vizuri sana.

Mimi naimba kwa kiswahili kwa asilimia 99. Sitaki kuimba kwa kijapani kwasababu nataka watu waendelee kuelewa kuwa mimi ni mtanzania, napiga miziki ya kitanzania na naimba kwa kiswahili kwasababu ndiyo lugha yetu ya Tanzania. Ni nyimbo chache sana ninazoimba kwa kijapani na kiingereza. Kwenye show moja hazizidi nyimbo mbili.

 

BC: Hivi sasa nchini Tanzania muziki unaoitwa wa kizazi kipya au bongo flava ndio unatamba sana. Nini mtizamo wako kuhusiana na muziki huu? Ungeambiwa uchague wanamuziki watatu wa muziki wa kizazi kipya ili ufanye nao collaboration ya wimbo au nyimbo ungewachagua kina nani?

FRESH: Kwanza kabisa napenda sana hili jina “BONGO FLAVA” na nampongeza aliyelibuni. Lina uzalendo ndani yake na linaleta maana na changamoto. Kwa mtazamo wangu jina hili lilitakiwa lichukuliwe serious na lifanyiwe kazi na wanamuziki wote, wadau wote wa muziki, vyombo vya habari na hata serikali na wananchi kwa ujumla. Kwa ninavyochukulia mimi, neno “BONGO” linawakilasha Tanzania au hata kama tukisema Dar, yote ni sawa tu, na neno “FLAVA” nadhani linasimama kama Flavour ambapo maana yake ni “LADHA”.

Kama hivyo ndivyo, nadhani ilitakiwa wanamuziki wa Tanzania kwa pamoja, wakubwa kwa wadogo kwa nguvu moja, tutengeneze miziki yenye ladha ya kibongo ambayo itakuwa inafanana na hilo jina “BONGO FLAVA”. Vyombo vya habari navyo vifanye kazi kubwa ya kuutangaza “ule ambao kweli ni wa bongo flava” kwa wananchi wa Tanzania wenyewe na pia nchi za jirani na za ng’ambo. Na wananchi kwa ujumla wao wauunge mkono muziki wao hasa ule uliopigwa vizuri. Sasa matatizo ninayoyaona hapa ni kwamba, kwanza nyingi ya hizo nyimbo zinazoitwa za bongo flava, ukiondoa lugha ya kiswahili wanayoitumia kuimba na kurap, hazina ladha yoyote ya bongo. Hata wanamuziki wenyewe, wengi wao utawasikia wanasema kuwa wao wanapiga hiphop. R&B, Zouk, Kwaito n.k. Okay, si mbaya kupiga muziki wa aina yoyote ile ilimradi una watu uliowalenga kusikiliza muziki wako. Lakini kwanini tusiumize vichwa na kuchukuwa hiyo hiphop au R&B au aina yoyote ya muziki, tukaitia ladha halisi ya “BONGO?”. Hatuwezi kufanikiwa kimataifa kwa kupiga tu simple hiphop. Ukitaka hiphop yako imshitue mtu hata huyo mwenyewe mwenye hiyo hiphop (MMAREKANI), umiza kichwa ndani ya hiyo hiphop, ifanye isikike kama vile si hiphop kwa kuiongeza rangi yako mwenyewe ambayo itaifanya isikike na flava ya bongo. Pengine hata huna haja ya kuiita hiphop, unaweza kuiita tu bongo flava na ikakubalika. Utafiti nilioufanya binafsi kuhusu mafanikio ya kimataifa kwa wanamuziki kutoka bara letu la Afrika nimegunduwa kuwa, wengi wa wanamuziki kutoka barani Afrika ambao wamefanikiwa kwa kiasi cha kuridhisha ulimwenguni, wametumia njia ya kuchanganya miziki ya kimagharibi na miziki yao asilia. Sikiliza miziki ya Angelique Kidjou, ni mchanganyiko wa Funk, Blues, R&B na miziki yake ya asili ya kwao Benin. Yussou Ndour, Morry Kante, Baaba maal, Salif Keita na hata mkongwe Manu Dibango, wanachanganya miziki ya kimagharibi na miziki ya asili ya nchi zao. Wote hawa wako internationally recognized ingawa wazungu ni watu ambao hawakubali kukuweka juu yao kabisa, lakini hawa wamefanya vizuri. Sikiliza Reggae ya Lucky Dube wa Afrika ya kusini. Ni reggae yenye ladha ya Afrika ya kusini na inatambulika kuwa ni reggae ya Lucky Dube. Hata yule mwanamuziki wa kimarekani “Poul Simon” alifanya vizuri sana na ile album yake “Graceland” aliyorekodi na wanamuziki wa Afrika ya Kusini ambapo alichanganya midundo ya kimarekani na kiafrika ya kusini “Kwaito” akatoka na kitu fulani cha aina yake.

Naomba nisieleweke vibaya hapa maana kuna watu wengine wanakuwa wagumu kuelewa. Sisemi kuwa hiphop ni mbaya au tusipige hiphop, la. Ninachosema ni kuwa tusibweteke, kama umependa rhythm ya hiphop chukuwa, lakini ifanyie kazi, umiza kichwa na uifanye itoke kivingine, rangi ya hiphop iwemo ili kujaribu kuwakamata wamagharibi ambao inawawia vigumu kuielewa rhythm yetu ya kiafrika pamoja na wengine wenye ugonjwa wa rhythm hiyo, na rangi ya “ubongo” wako iwemo ili kuonyesha uwezo na uhalisi wako. Hapo utaheshimiwa na waungwana wanaojuwa mambo ingawa mambumbumbu wengine hawatakuelewa. Hapa mtu anaweza kuuliza mbona wewe mwenyewe Fresh hufanyi hivyo?, Ntamjibu kuwa, sikiliza nyimbo zangu mpya kama vile WEMA, CHUKI, TUSIBWETEKE, GIMI LAV, AMINA na SUGAR MUMMY. Ataelewa ninachosema, na huo ni mwanzo tu.

Hilo ni jambo la kwanza. Jambo la pili ni vyombo vya habari, vinawafanya vijana waamini kuwa miziki na mambo ya kimarekani ndiyo bomba, inasikitisha. Unajuwa vijana huwa ni watu wa kufuata mkumbo. Sasa vyombo vyetu vya habari badala ya kuwa-encourage vijana ili wapige miziki yenye asili yetu, wao wanaweka mbele umagharibi na umarekani. Matokeo yake vijana wanakuwa na ndoto ya kuwa kama Jz, PD, 50cents, Beyonce n.k badala ya kutaka kutoka kiasili yao wenyewe.

Wale wanaopiga muziki mzuri wenye hadhi ya kuitwa bongo flava kwa maana ya kuwa na ladha halisi ya kibongo na pia quality (I mean performance quality and not recording quality) hawapewi nafasi kabisa kwenye vyombo vyetu vya habari. Vikundi kama vile IN AFRICA BAND ambao muziki wao unaweza kabisa kututoa kimasomaso popote pale duniani, almost hawasikiki kwenye vyombo vyetu vya habari. Wale jamaa wa TATUNANE (wamesambaratika sasa hivi), walikuwa na muziki hasa ambao ndio ungestahili kuitwa bongo flava. Kutokana na kazi yao nzuri walishaanza kujipatia umaarufu mkubwa duniani na kutuwakilisha vizuri sana (hata hapa Japan wanawajua na kuwaheshimu). Kwa masikitiko makubwa vyombo vyetu vya habari na hao wanaojiita mapromota hawakuwajali hata chembe. Kuna kikundi kimoja nilikiona wakati fulani nilipotembelea Bongo miaka michache iliyopita. Walikuwa wakifanya mazoezi pale kwenye nyumba ya sanaa wanaojiita “SISI TAMBARA” ni vijana wenye sense hasa ya kuchanganya miziki na ikaeleweka. Sijui ni kwanini hao mapromota wa nyumbani pamoja na watu wa habari hawawaoni vijana kama hawa na kuwapa nafasi sawa kama wanayowapa hao wa “hiphop” wanaorap kwa maneno ya kusema “KAMA BANGI NAVUTA, POMBE NAKUNYWA, NAPITIA WASHKAJI TUNACHUKUWA MADEMU N.K..) wimbo ambao nilikuwa nilikuwa nauona kwenye baadhi ya TV za bongo mara nyingi kwa siku nilipotembelea huko. Sijui ni kwa faida ya nani.

Halafu kwa mtazamo wangu vijana wetu kama wataishia kuwa watungaji wa mistari “mashairi” tu na kutegemea watengenezewe miziki na ma-producer, basi baada ya miaka kama 15 au 20 hivi, nchi yetu itapungukiwa kwa kiasi kikubwa na wanamuziki wenye ujuzi wa miziki. Yaani hatutakuwa na wajuzi wa mambo ya muziki wanaojuwa Keys ni nini, Cords ni nini, Rhythm hasa ni nini, Harmony ni nini au beats ni nini. Nasema hivi kwasababu mambo haya yote nimeshaanza kuyaona kwenye nyimbo nyingi tu za baadhi ya waimbaji na marapa wetu wa kisasa ambao tayari ni maarufu sana. Binafsi nasikia aibu sana nikiwa niko na watu wanaojuwa miziki, halafu tuwe tunasikiliza muziki fulani wa staa wetu wa Tanzania ambae amepromotiwa kwa nguvu zote na vyombo vya habari na kufikia umaarufu wa hali ya juu, anapoimba na kufanya makosa ya kiufundi kwenye uimbaji wake. Ni kitu kinachonitia aibu na kunisikitisha sana kama mwanamuziki wa Tanzania. Kwa wenzetu utakuta baadhi ya waandishi wa habari za muziki, nao pia muziki wanaujua kwa kiasi fulani, hivyo wanaposikiliza muziki wanajua uzuri na makosa yake, wakati mwingine anampiga maswali ya kiufundi mwanamuziki yahusuyo muziki na mwanamuziki anatakiwa ayajibu kwa ufundi wa hali ya juu.Vinginevyo unakuta mwanamuziki unaaibika vibaya. Sidhani kama tuna wanahabari wa aina hiyo huko kwetu, kitu ambacho kwa kiasi kikubwa pia kinapotosha muziki huo. Kwasababu wengi wa wanahabari wetu, kitu wanachofanya ni kusifia tu muziki au mwanamuziki wamtakae hata kama anafanya utumbo na kuleta aibu.

Sisi wengine ingawa hatukupitia kwenye shule za kusomea muziki, lakini kilichotusaidia ni kupiga kwenye mabendi pamoja na watu wenye ujuzi mkubwa wa muziki. Kwenye mazoezi unaimba nje ya key unaambiwa “E BWANAE UKO NJE, RUDI KWENYE KEY”. Unaimba ovyo unaambiwa “HIYO MELODI YAKO ANGALIA VIZURI, KUNA NOTE NYINGINE UNAZOPITA HAZIMO KWENYE KEY”. Au unaambiwa tu “USIENDE KWENYE NOTE HIYO, IKO NJE”. AU unaambiwa “IMBA KWENYE TIME” au “INGIA KWENYE RHYTHM, MBONA UNAYUMBA?” na mambo kama hayo. Sasa mambo kama hayo kwa miaka miwili mitatu hivi, unakuwa umeshajifunza na kujuwa nini ni nini kwenye utungaji na uimbaji. Ndiyo maana vijana kama kina Banana na Kalala Junior wanawafunga magoli sana wenzao kwasababu kwanza wanajifunza toka kwa baba zao ambao ni wanamuziki wajuzi, na pili ni kwasababu wamepiga kwenye mabendi yenye wanamuziki wajuzi.

Kwahiyo kwa ufupi mtazamo wangu kwenye muziki huu wa bongo flava ni kwamba, ni chimbuko zuri ambalo limeweza kuchipua vijana wengi wenye vipaji pamoja na kuwapatia vijana wengi ajira. Hata hivyo bado tuna safari ndefu sana ya kuwafanya vijana waelewe kabisa muziki ni nini, siyo tu kutunga mashairi, kuonekana kwenye TV na kusikika redioni tu basi, hapana. Tuwafanye waelewe kabisa kuelekezana na ma-producers wao wakati wa kutengeneza nyimbo zao ili waweze kufanya muziki wa bongo flava ya kweli na si kopi ya miziki ya kimagharibi mojakwa moja.

Hii inaweza tu kufanikiwa iwapo vyombo vya habari vitaacha ubaguzi walionao sasa hivi na kwamba vyombo vya habari viwaunganishe wanamuziki wa rika zote ili waweze kushirikiana kwa pamoja. Wakubwa waweze kutoa mchango wao kwenye muziki ambao ni wa watanzania wote na wadogo waweze kujifunza na kupata ujuzi kutoka kwa wakubwa wenye kujua kila kitu kuhusu miziki. Kinachoonekana hapa ni kama vile wanahabari wanajitahidi kwa njia zao zote kuwatenganisha wanamuziki na kulazimisha ikubalike kuwa wanamuziki chipukizi ndiyo bora zaidi kuliko wanamuziki wa aina nyingine za muziki wa nyumbani.

Pia ushauri wangu kwa vijana ni kuwa, waanze kujiamini na kufanya live performances zao wakiwa na bendi kamili ili waonyeshe na kuwahakikishia watu umahiri wao wa kuimba jukwaani, na si kuchezeshachezesha midomo jukwaani huku CD ikifanya kazi yote. Tukifanikiwa kwenye mambo yote hayo, basi tutakuwa tumefanikiwa kupata bongo flava ya kweli na ya kuweza kujivunia.Tuking’ang’ania ma-hiphop ya kimarekani tutakuwa tumepotea step.

Angalia wenzetu walio wajanja, hata wale walio jirani kabisa na Marekani yenyewe, hawababaiki sana na hiphop. Nchi kama Cuba, huwaambii kitu na salsa yao, Brasil na samba yao, Jamaica na reggae yao na Argentina na Mambo yao. Ni nchi ambazo ziko pua na mdomo na Marekani, lakini wananchi wake wanapenda sana miziki yao na moja ya sababu zinazowafanya wapende miziki yao ni kwa miziki yao hiyo kupewa nafasi ya kutosha kwenye vyombo vyao vya habari. Marekani yenyewe, kila aina ya muziki ina nafasi yake kwenye vyombo vya habari na ndiyo maana aina zote za miziki yao ziko juu na zinapendwa na watu tofauti tofauti. Vyombo vyetu vya habari vibadilike kwenye habari za miziki. Vitoe nafasi kwenye aina zote za miziki ikiwa ni pamoja na ngoma zetu za asili, taarab, rumba na nyinginezo. Siyo kufanya upendeleo ambao wenyewe wanaona kama ndiyo wanajenga kumbe wanabomoa utamaduni wetu.

Kuhusu kama ningeambiwa nichague wanamuziki watatu wa muziki wa “kizazi kipya” ili nifanye nao collaboration ya wimbo au nyimbo, nadhani ningesema naomba nipewe nafasi sita, yaani watatu wanaume na watatu wanawake. Kwa upande wa wanaume ningewachaguwa Bizman na Bob Rudala wote wa kundi la InAfrica Band (Sasa sijui kama hawa mnawaweka kwenye hilo kundi la kizazi kipya au la). Na mwingine ni huyu kijana anayeitwa Q Chief (kama sijakosea jina lake). Huyu kijana anaimba vizuri sana. Kwa upande wa wanawake, ningewachaguwa Stara Thomas, halafu kuna mtoto mmoja anaitwa Keisha na Ray C.

 

Fresh Jumbe jukwaani na bendi yake ya The Tanzanites Band.

BC: Je unafanya kitu gani kuweza kusaidia wanamuziki chipukizi wa Tanzania?

FRESH: Uongo mbaya, mpaka sasahivi sijafanya lolote kubwa zaidi ya ushauri kwa baadhi ya wanamuziki chipukizi wa nyumbani. Lakini muda si mrefu nitatoa mchango wangu mkubwa kwa wanamuziki chipukizi na wakongwe pia, pale ndoto na mipango yangu niliyoipanga tokea miaka kama minne hivi iliyopita itakapokamilika kwenye miaka kama miwili/mitatu hivi ijayo. Mambo mazuri na makubwa hayataki haraka. Nina mpango wa kufungua shule ya kufundisha mambo ya muziki huko nyumbani, kufungua studio ya kurekodi na pia kufungua studio za kufanyia mazoezi ya muziki.


Mungu akijaalia ndoto yangu ikitimia, basi naamini nitakuwa nimewasaidia wanamuziki wenzangu, si kwa chipukizi tu ambao watajifunza muziki, bali pia kwa wale wenye ujuzi wa mambo ya muziki, kwani watapata kazi ya kufundisha vijana. Pia kama nitafanikiwa nina mawazo ya kuanzisha lebo yangu chini ya jina la “FRESH PRODUCTION” ili niweze kuwasaidia chipukizi wenye vipaji kuweza kutoa nyimbo zao. Uzoefu ninao tayari nilioupata kwa kuuza miziki yangu mwenyewe. Inshaalla Mwenyezi Mungu atajaalia na ndoto itatimia.

BC: Kwa maoni yako unadhani ni kitu gani kifanyike ili muziki wa Tanzania uwe maarufu zaidi kwenye nchi za kigeni tofauti na ilivyo hivi sasa?

FRESH: Kama nilivyosema hapo mwanzo, kwanza tuwe wabunifu, tuumize vichwa kwa ku-create vitu ambavyo ni vya kimataifa. Hii ina maana kwamba tuchanganye vitu fulani vya kimataifa ambavyo vitakuwa rahisi kueleweka na hizo nchi za kigeni ambazo ndizo zina wanunuzi wengi wa muziki, tuchanganye na utamaduni wetu kwa ufundi wa hali ya juu na tujaribu kurekodi kwa quality ya hali ya juu kadri tutakavyoweza. Baada ya hapo tujitahidi kujipenyeza kwenye masoko yao ambayo kwasasa si ngumu sana vile kuyaingia kutokana na connections zilizopo kwenye teknolojia hii ya internet. Si rahisi sana vile, lakini ni lazima tujitahidi kujaribu tena na tena na mwisho wake tutaeleweka tu na kukubalika hata kwa kiasi kidogo, maana wazungu nao pia wanakuwaga na ubaguzi kwenye mambo haya, lakini tusikate tamaa. Kwa kufanya hivyo naamini tutafika tu bado hatujachelewa.

 

Fresh na Tanzanite Band katika Tokyo-African Fiesta mwaka huu.

BC: Katika baadhi ya maonyesho yako mmojawapo kati ya wacheza show wako alikuwa ni marehemu Shenaz aliyetutoka hivi karibuni kutokana na ajali ya basi la SABCO. Unamuongeleaje marehemu Shenaz na unaweza kukumbuka mlikutana wapi kwa mara ya kwanza?

FRESH: Kwanza nimeshituka na kusikitika sana kwa kupata habari hii toka kwako. Nilikuwa busy kwenye tour ya kusini mwa Japan na sikupata nafasi ya kusoma magazeti ya nyumbani kwa karibu mwezi mzima sasa. Tafadhali niambie kama kuna habari ya kifo chake kwenye gazeti lolote au taasisi yoyote ya habari ili niisome na nielewe vizuri. Shenazi ni mfanyakazi mahiri mwenye uwezo na mvuto wa kipekee jukwaani. Ana nidhamu ya hali ya juu awapo kazini. Tofauti na wenzie, sikuwahi kumuona akiwa amelewa au anakunywa pombe tukiwa kazini, in fact hata sidhani kama alikuwa anakunywa pombe, sidhani. Nilikuwa najivunia sana Shenazi na nilikuwa na matumaini makubwa kwa siku za baadae kwenye show zangu.

Alikuwa ni nyota na nimekuwa nikisumbuliwa sana kwa maswali kutoka kwa watu mbalimbali kote duniani wakitaka kununua video ambayo yeye yumo na ikiwezekana niwe naye hapa Japan na sehemu nyingine za dunia kwenye show zangu. Mfano nina mpango wa kuzuru London na nchi mbili tatu za ulaya kwa maonesho kadhaa mwaka ujao, na moja ya mazungumzo tuliyozungumza na huyo promota wa huko ni kwamba, mimi nitakwenda huko na bendi yangu tukitoea hapa Tokyo, halafu Shenazi nae na kundi lake watakuja huko wakitokea Dar na tukutane huko. Sasa hilo ni pigo kubwa sana kwangu na kwa wapenzi wa muziki.

Mara ya kwanza nilikutana na Shenaz Dar es salaam mwaka 2003 nilipokwenda kufanya tour yangu ya kuzunguka Tanzania. Nilifanya tour hiyo na bendi ya InAfrika Band ambapo wao ndio walionikutanisha naye, kunitambulisha na kuniambia kuwa, kwa nyimbo zangu zile za mduara au chakacha, Shenazi na timu yake wangekuwa perfect kwenye uchezaji. Kwahiyo nikawa na timu mbili za wachezaji, Shenazi na timu yake kwenye mduara, na wale wengine kwenye rumba. Hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana na Shenazi na nilifanya nae show pale Diamond Jubilee kwa mara ya kwanza, halafu Zanzibar, Morogoro, Dodoma na tukaenda wote mpaka Mwanza. Nilikutana nae tena mwaka 2005 nilipokwenda bongo na nikamtembelea nyumbani kwao alipokuwa anaishi pale magomeni. Masikini kumbe hiyo ndiyo ilikuwa ndiyo mara nyangu ya mwisho kumuona. Mungu amlaze mahali pema peponi.

KATIKA VIDEO HII HAPA CHINI MAREHEMU SHENAZ NI ALIYEVAA GAUNI LA LIGHT BLUE. R.I.P SHENAZ

BC: Baada ya kuishi na kufanya shughuli za muziki nje ya Tanzania kwa muda wote huu, umejifunza mambo yapi kuhusiana na maisha na pia muziki?

FRESH: Nimejifunza mengi sana. Kwa upande wa maisha nimejifunza kuwa hakuna kisichowezekana hapa duniani, cha muhimu ni kuwa na nia, kujiwekea malengo na kuyafuatilia kwa bidii zako zote. Nimejifunza kuwa wenzetu ni wachapakazi kwa bidii kuliko sisi. Nimejifunza kuwa wenzetu hata wakipata mafanikio makubwa kiasi gani, huwa hawajifaragui, kujiona au kujisifia, wanabakia tu simple mbele ya jamii. I wish na sisi sote tungekuwa hivi. Nimejifunza kuwa wenzetu neno “kutoa msaada” ni la kujivunia na neno “kuomba msaada” ni neno la aibu. Tofauti kabisa na sisi ambapo wengi wetu (nadhani hata serikali zetu) tunaamini kuwa hatuwezi kujifanyia chochote wenyewe bila kuomba misaada na kusaidiwa.

Nimejifunza pia kuwa, wenzetu wa huku mtu hata akiwa nacho hajioneshi, lakini sisi mtu hata kama hana atapenda aonekane kuwa anacho. Nimejifunza pia kuwa, sisi waafrika kwa ujumla wetu ikiwa ni pamoja na viongozi wetu, hatuheshimiwi sana duniani. Hii imetokana na kuwa, ingawa inajulikana wazi kuwa bara letu lina utajiri mkubwa wa maliasili na ardhi yenye rutuba, lakini sisi wenyewe zaidi ya kujisifia tu utajiri huo kwa maneno matupu, hakuna lolote la maana tunalofanya kuifanya dunia iweze kutuheshimu. Tunachukuliwa kama ni ombaomba tu. Tunachukuliwa kuwa kama ndio watu wa mwisho kabisa duniani. Hata viongozi wetu hawaheshimiwi sana vile. Nimejifunza pia kuwa kwenye nchi za wenzetu, wananchi na vyombo vya habari, wana uwezo zaidi wa kuweza kuzishinikiza serikali zao kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi, tofauti na kwetu unaona wazi kuwa wanasiasa wanaishi maisha ya kimilionea na asilimia kubwa ya wananchi wa kawaida wanaishi katika hali ya umasikini wa kutupwa na kutia huruma sana. Pamoja na hayo yote, pia nimejifunza kuwa sisi waafrika tuna utu na ubinaadamu zaidi kuliko nchi nyingi zilizoendelea. Watu wa huku kila mtu anajali mambo yake, hakuna cha jirani wala nini, hakuna cha mjomba, shangazi wala binamu huku, kila mtu ni yeye na familia yake tu ambayo ni mke, watoto na pengine na mbwa au Paka.

Sasa sisi tunaoishi huku tusipojiangalia na kuiiga tabia hii, tunaporudi kwetu tunaonekana strange.

Kuhusu miziki, pia nimejifunza mengi. Nimejifunza kuwa miziki yetu haijulikani sana kwa sababu haitangazwi sana, lakini kila tunapofanya show zetu, watu huifurahia sana miziki yetu. Ni miziki mizuri lakini wazungu ambao ndio wenye power ya kuinyanyua au kuiangusha, hawataki kabisa ikubalike hivyo, kwahiyo wanaiminya ki aina. Wanataka lazima tufuate njia yao. Nimejifunza pia kuwa wamarekani kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kututeka na kutufanya watumwa wao kiakili. Wanamuziki na wadau wengi wa muziki wa nchi nyingi duniani ikiwemo hii ninayoishi Japan pamoja na nchi yetu Tanzania, tumeoshwa ubongo na tumekuwa tunaamini kuwa muziki wa kimarekani na umarekani kwa ujumla ndiyo mambo yote. Utaona watu wanafurahia sana wanaposikia kuwa MTV imeingia sehemu fulani kama Japan, Korea au hata MTV Africa. Lakini wasichokiona ambacho kinafanyika ni kwamba, wamarekani wanatumia MTV hizo kupromoti wanamuziki wao wa kimarekani zaidi kuliko hao wa hizo nchi zao husika. Wanamuziki wa Marekani wanaonyeshwa sana kwenye MTV za nchi nyingine lakini wanamuziki wa hizo nchi nyingine hawaonyeshwi kwenye MTV ya Marekani, hii ni unfair. Inatakiwa nasi tujiendeshe kivyetu, vinginevyo tutaendelea kuwa watumwa kimawazo miaka nenda rudi. Pia nimejifunza kuwa it’s ok kama utapata mkataba na kampuni kubwa ya kuuza kazi zako, lakini si lazima sana vile, unaweza kufanikiwa kwenye biashara ya muziki wako hasa kwenye uuzaji wa CDs na Videos zako bila ya kuwa na mkataba na kampuni kubwa. Ukijiamini ukajioganaizi vizuri na kupanga mipango yako vizuri, unaweza kuuza kazi zako vizuri duniani kote, tena kwa faida nzuri tu, siku hizi kila kitu kinawezekana.

BC: Mpaka hivi sasa umeshatoa albamu ngapi? Ipi ni ya hivi karibuni? Inapatikana wapi kwa wapenzi ambao wangependa kuinunua ?

FRESH: Nimeshatoa albamu 4 na ya tano nategemea kuitoa mwishoni mwa mwaka huu. “Kinyozi hajinyoi” na “Baba sukari” nilizitoa wakati nikiwa naishi Nairobi Kenya mwanzoni mwa miaka ya tisini. Albamu hizi mbili pamoja na nyingine ya tatu “Fresh Out of Africa” ambayo niliitoa mara tu baada ya kuhamia hapa Japan, nimesimamisha kuziuza kimataifa (kule nyumbani bado kaseti zinauzwa kama kawaida kwa MAMU na pia kwa KIBONGE). Nimesimamisha kuziuza kimataifa kwasababu nataka kuzirekodi na kuzitoa upya katika arrangement nyingine na quality ya hali ya juu zaidi. Hii ni moja ya mambo niliyojifunza. Ili kuweza kutambulika, kuheshimika na kukubalika kimataifa, ni bora uchelewe kutoa nyimbo au albamu, lakini ukitoa uhakikishe kuwa iko kamili kwenye kila kitu, kuanzia kwenye creativity, originality, lyrics, melody, composition, arrangement na pia recording quality. Kwahiyo najichulia kama naanza upya, hizi nitazirekodi tena na kuhakikisha mambo yote hayo nimeyakamilisha vilivyo ili niweze kuu-face ulimwengu kikamilifu.

Albamu ya 4 ndiyo hii ya “Penzi ni kikohozi” ambayo haina tatizo na kwa bahati nzuri nimeshauza kopi nyingi tu na naendelea kuziuza kwa wingi kote duniani.

Albam mpya na ya tano ambayo nategemea kuitoa mwishoni mwa mwaka huu inaitwa “WEMA” ambayo midundo yake itakuwa si ile ya kawaida kama watu waliyonizoea kunisikia nikiipiga. Ndiyo kama vile nilivyokuambia hapo mwanzo, najaribu kufuata njia za kina Angelique Kidjou sasa lakini kivyangu, nataka niu-challenge ulimwengu na si Japan na Asia peke yake. Nataka pia niji-challenge na mimi mwenyewe pia nione ntakapofikia.

Kwa hapa Tokyo, kazi zangu ziko kwenye maduka ya muziki ya HMV la Shibuya na WAVE la Ikebukuro. Lakini huwa nauza zaidi kila ninapopiga kwenye show zangu na mashabiki wangu wengi wameshazowea hivyo.

Kama uko Japan (mbali na Tokyo), Asia au Marekani na Canada, unaweza kununuwa kazi zangu kwa kubofya kwenye link hii

http://www.freshjumbe.com/cddvdshop.htm Utalazimika kutumia credit card, kama huna hutaweza kununuwa. Kwa wale wa Uingereza na ulaya kwa ujumla, mnaweza pia kutumia link hiyohiyo hapo juu na ukatumiwa CD toka huku Japan au, bofya kwenye hii link hapa chini ambayo ni ya maajenti wangu wa uingereza.

http://www.supertoniccds.com/pages/products.asp?CatID=21

Baadhi ya miziki mipya ya Fresh kuonyesha anakoelekea kimuziki ni hii hapa.Wa kwanza ni WEMA na wa pili ni CHUKI.Zisikilize hapa

 

 

BC: Usingekuwa mwanamuziki unadhani ungekuwa nani?

FRESH: Ningekuwa bingwa wa ngumi za kulipwa za uzito wa juu duniani, au pengine by now ningekuwa naitwa “bingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa za uzito wa juu duniani”. Napenda sana mchezo wa ngumi kuliko mchezo mwingine wowote ule. Hata hivi sasa huwa nafanya mazoezi ya ngumi kwenye gym hapa karibu na nyumbani kwangu.

Au kama kwa sababu moja ama nyingine nisingeweza kufikia hapo kwenye ngumi, basi ningekuwa baharia. Kwasababu vijana wenzangu karibu wote niliokuwa nao, pamoja na mimi mwenyewe tulikuwa kwenye line hiyo.

BC: Shukrani Fresh kwa mahojiano haya.Kila la kheri.

Unaweza kusikiliza zaidi nyimbo mpya za Fresh kwa kubonyeza hapa.

Website rasmi ya Fresh Jumbe ni www.freshjumbe.com

 

27 Responses to ““TUSIBWETEKE”-FRESH JUMBE”

 1. joan Says:

  huyo sio fresh,jina lake halisi ni fereshi,hivi kwanini watanzania hatutaki uhalisia?

 2. neema Says:

  Aiseee. Hii interview bab kubwa. Fresh umenifundisha mambo ya muhimu sana. Mimi ni msanii wa hapa Bongo, siku zote najiuliza jinsi ya kuuza international, asante sana kwa mawazo yako. Inabidi tujitahidi sana sisi wana bongoflava tudumishe mila na desturi, na inabidi tupiganie sana media icheze nyimbo za tamaduni. Big up BC kazi nzuri.

 3. Ed (USA) Says:

  My my my! Jamani sipendi kujipendekeza kutoa sifa, lakini kwa faida ya wabongo wapenda maendeleo kupitia sanaa, nampongeza Fresh kwenye hii interview na BC.

  Fresh umeonyesha kukomaa, kujali na uzalendo kwa kuelimisha wengi kwa kipaji ulichojaliwa katika sanaa ya muziki.

  Aliyoeleza Fresh yanahitaji kupewa umuhimu na vyombo vya habari katika kuwaelimisha wasanii wa Tanzania.

 4. Max Says:

  Sijawahi kusoma mahojiano matamu na ya uhakika kwe BC kama haya ya Fresh . Ebwana Fresh, wewe kweli mwanaume wa shoka na msema kweli. Tena unaonekana huna roho mbaya kabisa kwa namna unavyowasomea jamaa na kuwapa ushauri. Na nyinyi BC nawapongeza, haya ndiyo mahojiano tunayoyataka kuyaona ya watu makini kama hawa. Hongera Fresh, honereni BC.

 5. Dinah Says:

  Mh! Mahojiano haya yanakufanya mtu urudie kusoma tena na tena, Fereshi Jumbe hakika ni mfano mzuri kwa wasanii wa Bongo walioko Bongo na wale walioko nje.

  Unaongea mambo ya msingi, huonyeshi kunata wala kujidai, unaonekana ni mwema na si mchoyo wa maendeleo bilakusahau ukuaji wa kiakili yaani unabusara.

  Nimependa hiyo Pic ya mwanzo, umetoka vema sana na unavutia. Kila la kheri ktk shughuli zako.

 6. Dinah Says:

  BC mahojiano bab-kubwa! Keep it up.

 7. muddy Says:

  Jumbe mkuu inatia moyo kaza buti!

 8. Big Willy Says:

  Mahojiano safi sana Big up BC crew keep it up Fresh Jumbe

 9. Big Willy Says:

  Keep it Up Fresh Jumbe and kazi nzuri Bc endeleeni kutuletea vitu adimu kama hivi!

 10. Ally Oda Says:

  safi sana Fresh Jumbe endelea na moto huo huo pia Big kwa wadau wa BC kazeni buti

 11. muddy Says:

  nasikia una watoto tena mmoja anaitwa salama, jumbe na mwingine marehemu, ni kweli

 12. muddy Says:

  isitoshe kuna mwanamke uliyezaa nae mtoto uliwahu kumtungia mwimbo wa pamela na mtoto mwimbo wa slima bc tunataka kujua kama ni kweli au la kazi yake ni nzuri sana

 13. Ibrah Says:

  Duh! jamaa anaongea kama profesa. Watu kama hawa wanatakiwa warudi bongo wapewe nafasi wawaongoze wenzao maana anaonekana anajuwa mambo na ana nia ya kubadilisha mambo. Nina hamu ya kumuona usokwauso ili nimlinganishe na haya maongezi yake. Anaonekana hana ushamba huyu, ni balozi wetu kweli. Fresh kaza buti. BC asanteni sana kwa kututafutia mtu kama huyu. Na wewe sijui ndiyo Muddy wewe acha ushamba, maswali gani ya kijinga hayo unayoulizauliza, ooh sijui watoto sijui mwanamke alizaa nae wewe inakuhusu nini? wacha udaku. Kama huna lakusema bora ukalale kuliko kuuliza maswali mbuzi hayoo. Wabongo wengine bwana! ovyo sana. Mtabaki hivyohivyo na udaku tu bila maendeleo yoyote.

 14. muddy Says:

  BC muddy huyo #9 #10 hana comments zozote ni ushamba tu unamsumbua.
  Muddy #7

 15. Max Says:

  BC wapuuzi kama hawa Muddy #9 na #10 haya maoni yao yakijinga wakati mwingine mnayatia kapuni tu hayana maana yoyote. Tunataka mawazo ya kimaendeo siyo huu ushamba na unafiki. Jamaa Fresh kazungumza mambo muhimu sasa sisi badala ya kuangalia yatawasaidia vipi vijana wa bongo flava huyu mpuuzi analeta maswali yakijinga, mfungieni huyo pumbavu!. Kama anataka kujuwa mambo si awasiliane nae mwenyewe Fresh mojakwamoja amuulize hayo maswali kuliko kuyauliza hapa ukumbini?.

 16. emanuel Says:

  ebwana wewe ni mwanamziki wa kwanza ambaye anaonyesha ukakamavu wa kimuziki na kitaifa. kwaupi mimi ni kijana ninaye ishi marekani lakini napenda sana miziki ya bongo. nakushukuru kwa maelezo yako yote uliyo yatowa sio tu yanafumbuwa macho kwa wanamziki wa bongo bali pia ni changa moto kwa watanzania wote walio nje na ndani kuweka utaifa wao mbele na kuogeza bidii na marifa maana ulimwengu huu wa sasa sio wa relemama.

 17. mole Says:

  Kaka fresh hapa umenena kweli tupu, sisi wapenzi wa muziki tukisikiliza hii miziki yetu ya bongo flava tunachokipata ni umarekani fulani tu ambao hauna maana yeyote ktk jamii, muziki wala maisha. Sasa haya mambo ya kusikiliza vitu kama mikasi, mademu ,mashoka, nk. hizi ndio staili za kina 50 cents, p Diddy, Ja, Jz na wengineo.
  ASANTE kaka Fr kwa kuvishtua vyombo vyetu vya habari. natumaini pia wanamuziki wetu wataanza kuyafanyia kazi mawazo yako.

 18. Dafity Says:

  Nami napenda kujua kama wazazi wake kweli walimuita FRESH na sio FERESH. Naamini wazazi walikuwa na maana nzuri kwa jina walilomuita, lakini ni Fresh au Feresh?
  Mahojiano ni mazuri na Nimefundishika mambo mengi, inapendeza sana.

 19. Mgumu Says:

  Safi sana Fresh hayo ndio maendeleo yanayotakiwa,
  wewe nimekukubali na MUNGU HAZIDI KUKUZIDISHIA
  Kuanzia nyimbo paka mashairi yamekwenda shule na kupa Degree na asilimia miamoja.MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU MMBALIKI FRESHJUMBE.

 20. Isaac Says:

  Hongera sana Fresh Jumbe, muziki kweli uko ndani ya damu yako, lakini kikubwa ambacho ninakusifia umepata bahati ya kutambua kuwa kujituma ndiyo siri ya mafanikio katika kazi zako na pia umeonyesha umekuwa mwepesi wa kujifunza mambo mbalimbali kati anga ya kimataifa.
  Nadhani unaikumbuka hii ‘…nidhamu ya kazi ndiyo msingi wa mafanikio mema kazini…’
  Kila la heri nadhani wengi tutachota hekima na busara zako.

 21. Ed (USA) Says:

  Nimerudi tena baada ya kusahau kuwapongeza BC. Kama mnapitia maoni haya naomba mpokee shukurani zangu. Mnachokifanya ni chema kinachojiuza. Mnafanikiwa kutuweka pamoja watanzania ulimwenguni kote hasa mnapofanya mahojiano ya maana kama haya na mr.Fresh

  Aliyoeleza Fresh BC, hayahitaji kuishia hapa. Naamini kuna watanzania wengi hasa huko nyumbani hawana access ya uhakika na BC. Fanyeni mnavyoweza kupenyeza haya mawazo kwingineko kwa faida ya wengi. Aliyoeleza huyu jamaa ni darasa zito kwa walio makini kujifunza.

 22. Emmanuel-London Says:

  Kweli usiwatupie Nguruwe Dhahabu wataishia kuikanyagakanyaga tu…Hazina ya maongezi ya Fresh Na Bc imesitirika kwenye uvungu wa vichwa vingi vyenye akili timamu.Jambo la maana ni kuitoa uvunguni na kuifanyia kazi.Wanamuziki chipukizi basi chipueni kwa kufuata maadili na changamoto iliyotolewa kwenu.Na wanamuziki wakongwe jikosoeni na kujiimarisha.Maana wote tunakubali muziki ndio sanaa pekee itakayo wakilisha watu wa fani zote toka pande zote duniani..

 23. migue Says:

  Fresh umetembea na umeona kuwa muziki wowote haukosi ladha kamili ya kitamaduni. Nawewe umethibitisha hivyo kwa kupiga mduara katika kazi zako.Hata hivyo ninafikiri hujaichambua vizuri art ya Mwambao wa Tanga ambayo imejaa vionjo vingi adimu. Ukiwa Japan kwenye teknolojia iliyokuwa naomba ufanyie kazi mfumo wa muziki ambao wewe mwenyewe umeshiriki ukiwa na Dar International Orchestra, OSS, Mlimani Park Orchestra na Juwata(Msondo).Nikiwa mtafiti nimegundua kuna mengi uliyoyakuta na kuyafanya ukiwa katika bendi hizo lakini leo hayapo kwani wengi ulioshiriki nao hawapo tena, kama mwalimu King Enock(DDC), Marijani Rajab, Ally Rajab,Rashid Mtani,Mohamed Tungwa William Maselenge, Evaristo Mivuba(Dar Int). Pia angalia tena chords alizotembea Kassim Mponda akikuback katika Pamela. Naamini ukirudi nyuma na kuuchambua mziki wako ukiwa Bongo na kuufanyia kazi tena, Jumbe utakuwa si mwanamuziki tu bali mwanasayansi mtafiti mwenye jukumu la kuhifadhi vile vyote vilivoifanya Tanzania kuwa mfano bora wa muziki wa kiswahili. Kila la heri na mungu atakuzidishia.

 24. AGATA Says:

  UNA EMBA VEZURE SANA!!!KEEP UP THE GOOD WORK,BECAUSE GOD HAS BLESSED YOU WITH SUCH A BEAUTIFULL VOICE.

 25. chau Says:

  he mi nilijua kandabongoman

 26. Mimi Says:

  Fresh, kwa kazi nzuri unayoifanya, kipaji ulichonacho, tungo zako za maana, sauti uliyonayo, umakini kiakili na bidii yako, mimi nakushauri urudi bongo, utaula maana hakuna ataekufikia kabisa. Hakuna cha wa bongo pleva wala nini. Utakamua bongo na utakuwa juu zaidi, pia utaweza kusaidia vijana wa bongo na nchi yako kwa ujumla. Nenda ukatoe mchango wako kwa nchi yako badala ya kuishia huko Japan, mpaka lini sasa?.

 27. Bely Kasambula Says:

  Mfano wa kuigwa kwa wanamziki wa kitanzania wote wanaokua!


Leave a Reply to muddy Cancel reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s