BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“NIPO TAYARI KUIKABILI CHANGAMOTO HII”-MICHUZI September, 24, 2007

Filed under: Blogging,Blogs,Photography/Picha,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 9:27 PM

Kama utani, miaka miwili iliyopita, mpiga picha maarufu nchini Tanzania, Muhidini Issa Michuzi, alianzisha kitu ambacho tunaweza kusema kimekuwa ‘a national phenomena kama sio international phenomena”. Alichokianzisha ni blog ambayo hivi leo ndio imetimiza miaka miwili tangu kuanzishwa kwake rasmi.

 

 

 

Kwa mara ya tatu Michuzi ametupa nafasi adimu ya kufanya naye mahojiano.Wakati huu tumeongea naye kuhusiana na siku hii ya kusheherekea miaka miwili ya blog yake, kutafakari pamoja muelekeo wa blog yake katika siku za mbeleni, ushauri wake kwa vyombo vya habari kuhusiana na tekinolojia n.k. Unajua Michuzi anaogopa mambo gani maishani? Nini siri ya mafanikio yake? Kwa majibu ya maswali hayo na mengine mengi haya hapa mahojiano kamili yanayoambatana na picha kibao;

 

BC: Kwanza hongera sana kwa kutimiza miaka miwili tangu uanzishe rasmi blog yako kule Helsinki, Finland. Karibu tena ndani ya BongoCelebrity.

 

 

MM: Ahsante sana kwa heshima hii ya kutinga tena katika BongoCelebrity kwa mara ya tatu. Kwa kweli nimehemewa kwa hilo na pia kubaini kwamba kweli siku hazigandi kwani ile kufumba na kufumbua miaka miwili imekatika toka niianzishe www.issamichuzi.blogspot.com kama mchezo vile kama ulivyosema kule Helsinki Finland siku kama hii. Nakumbuka muda ulikuwa saa saba na robo wakati tumetoka kwa mapumziko ya mchana ya mkutano wa Helsinki nami nikalekea chumba cha mawasiliano ambako nilimkuta kaka Ndesanjo Macha ambaye hakufanya hiyana nilipomuomba anielekeze namna ya kuanzisha blog. Baada ya hapo, na kama wanavyosema, mengine ni historia


BC: Hivi kwa nini unasherehekea leo na sio Septemba 8 siku ambayo Ndesanjo alikualika rasmi na hivyo tunaweza kusema ulianza rasmi ku-blogu?

MM: Swali zuri sana. Ukienda kwenye link ya huo mwezi September 2005 http://issamichuzi.blogspot.com/2005_09_01_archive.html) utakuta kwamba ukurusa wa mwezi huo wa kwanza kuanza kublogu unaishia Septemba 25, 2005 siku ambayo niliweka picha ya kuku anayelea bata. Maoni mawili yaliyotumwa siku hiyo ndiyo yaliyonifanya niamue kufanya kweli na sio utani kama nilipoanza hiyo Septemba 8. Hivyo kaa ukielewa mimi nahisi kwamba kama ni mimba iliingia Septemba 8 na blogu ikazaliwa Septemba 25.

Michuzi at 10 Downing Street,makazi ya waziri mkuu wa Uingereza.

 

BC:Muasisi wa blog za Kiswahili Ndesanjo Macha alipokuwa nchini Afrika Kusini hivi karibuni katika mkutano wa Digital Citizen Indaba alikaririwa akitoa mfano wa blog yako kama mojawapo ya mafanikio makubwa ya blogs za Kiswahili. Nini siri ya mafanikio yako?

 

MM: Siri ya mafanikio ni kuweka maslahi ya wadau mbele na yangu binafsi nyuma.Huwa sina raha kuwaacha wadau wangu wanaotegemea mambo mapya ama jambo jipya kila siku watoke patupu, labda iwe nina dharura nzito ama niko eneo ambalo halina mtandao.

 

 

Michuzi akiwa na wadau wake.

BC: Ni mambo yepi matatu uliyoyategemea na pia matatu ambayo hukuyategemea kutokea ulipoanzisha blog yako miaka miwili iliyopita?

 

MM: Duh! Hili ni bonge la swali. Haya, nitajaribu. Matatu makubwa ambayo nilitegemea ni (1) Kubobea katika fani ya mawasiliano ya kisasa na kujulikana dunia nzima (2) Kupata shida katika kuchuja pumba na mchele kwenye maoni (Ndesanjo alinikanya mapema kwamba endapo naamua kuruhusu anonymous na wakati huo huo kuchuja, nijiandae kwa kazi nzito; na kweli. Huwa kuna wakati nakuta maoni yanayohitaji kusomwa na kuchujwa zaidi ya 600, hasa hasa kama nitazembea kupitia blog mara tatu kwa siku), na (3) Kuona kwamba wadau wengi wana hamu ya kujua mengi, kucheka na kutaniana na kutambua watu ama sehemu mbali mbali duniani.

Matatu ambayo sikuategemea ni (1) Blog yangu kuwa maarufu na kujulikana na karibu kila mtanzania aliye nje ya nchi na pia hata watu wasio watanzania bali wazungumzaji wa Kiswahili. Siku hizi napata barua pepe toka vyuo vikuu mbalimbali duniani kuniuliza hili na lile na kuna mialiko kama mitatu hivi ya kwenda kutoa somo juu ya kuwa bloga wa Kiswahili (2) Kupata wadhamini (3) Kufanya watu wengine wahamasike na kujikuta wana hamu ya kuwa na blogs zao. Nami huwa napenda sana kusaidia watu kama hawa kwani peke yangu ama wachache tulio na blogu, hasa za picha, si wengi wa kutosheleza mahitaji kwani mambo ni mengi na Tanzania ni kubwa sana.

Michuzi na Hasheem Thabeet walipokutana huko Boston,Marekani mwaka jana.

 

BC: Kadiri siku zinavyozidi kwenda ni wazi kwamba watanzania wengi wanazidi kukutegemea wewe kupitia blog yako katika kuwaletea ” breaking news”,picha na matukio zaidi. Unajiandaa vipi kuendelea kukabiliana na changamoto hiyo?

 

MM: Nakabiliana na changamoto hii kwa kuendeleza libeneke bila kuchoka na wakati huo huo kuangalia uwezekano wa kuhamasisha Watanzania kuikumbatia teknolojia hii ya habari kwa hali na mali kwani ndio muelekeo wenyewe wa huko tunakokwenda. Nashukuru na kufurahi kukuta hata mwajiri wangu Daily News ameweza kuitambua kiu hiyo na kunihamisha toka kitengo cha picha na kunikabidhi kitengo cha mawasiliano ya mtandao huku akinipa changamoto ya kukiunda upya kitengo hicho ili nacho kiende na wakati. Hivyo kwa sasa mimi sio tena Photo Editor bali ni Online Editor wa magazeti ya serikali ya Daily News, Habari leo, Sunday News, na hivi sasa niko mbioni kuiunda upya tovuti ya vyombo hivyo ili iwe nzuri na yenye wageni wengi kama blogu yangu.Ni changamoto nzito hasa ukizingatia wengi wetu bado hatujastuka kwamba habari kwa mtandao inakaribia kuwa sawa kama si kuipiku ya magazeti kwa usomaji na hata kibiashara. Hivyo kuna wakati wengine hudhani nimenoa stepu kwa kwenda kwenye kitengo ambacho sio cha fani yangu, yaani picha. Nami nakaa kimya na kuwangojea siku watakapoona nina maana gani ya kukumbatia teknolojia hii ya habari. Ni kama enzi zile nakumbuka nilikuwa masomoni Ujerumani mwaka 1992 ambapo CD ndo zilikuwa zinaingia na waundaji wa kaseti walipiga vita sana nyenzo hiyo mpya. Sasa utaona kanda za kaseti si mali kitu tena na CD imeshika hatamu. Hiyo pia inakwenda sambamba na vita iliyoko sasa kati ya picha za filamu na digital, hapo hakuna ubishi kwamba digital atakuwa mfalme. Hivyo nikirudi kwenye kukujibu swali lako ni kwamba mimi tayari nimejiandaa kupambana na changamoto hiyo kwa kuendeleza blogu na pia tovuti.

Michuzi akiwa na Mzee wa Macharanga, Charles Hilary na afisa wa BAKITA

 

BC: Unadhani blogs zinatoa changamoto ya aina gani na kiasi gani kwa vyombo vya habari vya kawaida kama vile magazeti,televisheni na redio?

 

MM: Nadhani jibu lililopita limejibu sehemu ya swali hili. Cha kongezea ni kwamba tutake tusitake magazeti, TV na redio vijiandae mapema kwani hivi sasa teknolojia inakua kwa kasi sana na atayezubaa ataachwa nyuma. Mfano mdogo wa changamoto hii ni namna ambavyo utamaduni wa watu kujisomea unavyomomonyoka kwa kasi kutokana na kuwepo kwa TV na redio hadi kwenye mitandao. Kichekesho ni kwamba waandishi na wachapaji hawafanyi utafiti wa kina kujua kiini ni nini na wafanyeje. Kwa upande wa usomaji vitabu iko haja ya kuanza sasa kutafuta njia mbadala ya kuhamasisha watu wasome vitabu kupitia teknolojia inayoshika hatamu badala ya kutegemea usomaji wa nakala ngumu (hard copy) pekee. Na huu usomaji sio wa vitabu tu, bali hata magazeti kwani ughaibuni na baadhi ya nchi za Afrika takwimu zinaonyesha usomaji wa magazeti unashuka na vitu kama kompyuta, simu za mkononi na hata saa ambazo zinabebeka na kuwezesha mtu kusoma habari kwa urahisi ndivyo vitu vinavyopendelewa zaidi kila siku. Wengine wameanza kusema kwamba magazeti ni mzigo unaorundikana nyumbani bila sababu, hivyo haina haja ya kuyabeba. Hii nazungumzia Tanzania ya miaka 10 ama 20 ijayo ambapo tunatakiwa tujiandae leo…

 

 

 

Issa Michuzi na waandishi wa habari na wapiga picha wenzake wakiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania siku ya kuapishwa kwake ikulu jijini Dar-es-salaam.

 

BC: Kumekuwepo na baadhi ya wasomaji wa blog yako ambao wamekuwa na hisia kwamba unakipendelea chama tawala CCM katika kuwaletea habari na picha za matukio yake ukilinganisha na yale ya vyama vya upinzani. Je kuna ukweli wowote katika hilo?Kama hakuna unadhani malalamiko hayo yanatokana na nini?

 

MM: Hahahaaaaa!!! Acha nicheke kidogo. Najua unategemea jibu la ‘mkono mtupu haulambwi’. Hapana. Kwanza naomba niweke wazi kwamba itikadi za kisiasa na kidini najaribu kuwa mwangalifu sana kwani faida na hasara zake nazijua. Kama ulivyosema ‘ni baadhi ya wasomaji wa blog’ wenye hisia hizo. Hivyo sio wote. Ndio kusema tuhuma hizo hazina msingi hasa ukizingatia kwamba huwa nafanya kila juhudi kuweka uwiano sawa katika hilo kwa kadiri ya uwezo wangu, nikitambua fika kwamba upinzani si uadui bali ni kutofautiana kiitikadi na kimawazo.

 

Issa Michuzi akiongoza mtumbwi kutembelea maeneo ya Chalinze. Mmojawapo kati ya abiria ni Raisi Jakaya Kikwete.Wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na mbunge wa jimbo hilo la Chalinze.

BC : Hivi karibuni umeanzisha tovuti mpya ya www.tztimes.com ambayo tayari imeanza kujipatia umaarufu. Je, kimsingi kuna tofauti gani kati ya habari za kwenye blog yako na zile za kwenye tovuti ya tztimes? Unaweza kutudokeza kidogo mipango ya mbeleni ya tztimes.com?

 

MM: www.tztimes.com ina tofauti kubwa na www.issamichuzi.blogspot.com kama yalivyo majina yake. Utofauti wake ni kwamba habari za kwenye blogu aghalabu ni nyepesi nyepesi, picha kibao na maneno kidooogo. Tovuti ni habari ngumu zaidi na baadhi ya picha husika. Pia tofauti na blogu, tovuti hii siko peke yangu katika kutafuta na kubandika vitu, wakati blogu siruhusu mtu kuigusa na hata vitu vyake ni vya mtazamo wa binafsi na sio vinginevyo.

BC: Wapo baadhi ya watu duniani wenye imani kwamba kama binadamu,tukifa huwa tunapata tena nafasi ya kurejea duniani kama viumbe au vitu vingine. Je kama imani hiyo ni ya kweli, ungependa kurudi kama nani au nini?

 

MM : Ningependa kurudi kama Robinson Crusoe, yule stelingi wa kitabu cha zamani cha mtunzi Daniel Defoe ambaye alipoharibikiwa na merikebu yake na kubaki kwenye kisiwa kisicho na mtu, aliweza kubangaiza na kupambana na shida zote kwa miaka 40. Kisa hicho ndicho mhimili wa maisha yangu ambapo naamini kujikwaa si kuanguka. Na kuanguka sio kushindwa bali ni changamoto ya kujiinua na kuanza moja. Kwa maana nyingine mtu hutakiwi kukata tamaa mradi Mungu amekujalia uhai. Ukianguka, amka anza moja na endeleza libeneke kama Robinson Crusoe. Nakumbuka sinema yake ya ‘Man Friday’ ambayo nakumbuka alikuwemo Peter O’Toole kama Crusoe na Richard Roundtree ama Shaft kama Friday. Vile vile niliangalia kwa msisimko ‘Robinson Crusoe’ iliyochezwa na Pierce Brosnan (James Bond 007 aliyepita) ambapo William Takaga alicheza kama Friday. Nazitafuta sana filamu hizi na mwenye kuzipata naomba anitumie. Hasa nyie wa BC kwani maudhui yake ingawa ni ya kimagharibi lakini yaweza kumpata (na humpata) mtu yeyote.

Michuzi akiwa na wadau katika sehemu za maakuli.

 

BC : Tangu kuzaliwa mpaka hivi leo, ni ushauri gani binafsi ambao ulishawahi kupewa na mtu yeyote ambao hujawahi kuusahau na umekuwa ukiuzingatia siku zote za maisha yako? Nani alikupa ushauri huo?

 

MM : Ushauri alionipa marehemu Mama yangu wa kwamba usivimbe kichwa kwa fanaka yoyote utakayopata. Sintousahau na hadi leo nauzingatia. Na sidhani kama nitakuja uacha hata kama nitakuja kufanikiwa kweli kimaisha – Inshaaaaallah!

 

Michuzi akiwa na Flora Nducha wa idhaa ya kiswahili BBC walipokuwa Dar kusherehekea miaka 50 ya idhaa hiyo ya kiswahili mwaka huu.

BC : Hapa kwetu BongoCelebrity, tuna baadhi ya wasomaji wetu ambao huwa kuna nyakati wanatusahihisha, kutukumbusha na hata kutukosoa katika mambo mbalimbali tunayoyaandika,mahojiano tunayofanya nk.Tunawashukuru watu hao kwa sababu tunaamini tunakua kutokana na michango,ushauri na mawazo yao. Je kwa upande wako, katika miaka miwili iliyopita ni ushauri gani ambao ulipewa na « mdau au wadau » wako ambao uliufuata na kuutilia maanani achilia mbali kujifunza?

 

MM : Ushauri wa aina nyingi umekuwa ukija kwangu, mkubwa ni kufanya jitihada ya kujaribu kusahihisha makosa aidha ya kiuandishi ama kimaandiko kila yatokeapo. Ushauri mwingine ni kuruhusu michango ya picha na habari za watu wengine, jambo ambalo matunda yake yanaonekana na nayafurahia sana kwani hivi sasa kila mtu anajihisi ni mdau na kwamba hii blogu si ya Michuzi tena bali ya kila mmoja wao. Mwingine ni kupiga chini matusi ya aina yoyote na kashfa nzito dhidi ya wanaotundikwa bloguni. Nimejifunza kwamba Watanzania ni watu wanaopenda utani, wenye kutoa yaliyo moyoni bila kuficha (ingawa wengine wanapitilizaga), na ni wavumilivu.

Michuzi akiwa na Lady Jaydee,msanii wa muziki wa kizazi kipya siku ya kusheherekea miaka 50 ya BBC idhaa ya kiswahili ambapo Lady Jaydee alitumbuiza.

BC : Ni mambo gani matatu unayoyahofia zaidi katika maisha?

 

MM : Duh! Haya… (1) kutotimiza ndoto zangu za kuja kuwa kama yahoo ama google wa Afrika (2) Kunyimwa ama kunyang’anywa haki yangu ya msingi ya kupashana habari kwa uhuru (3) Kukata tamaa kwa lolote litalonifika.

 

BC : Wewe ni mpenzi sana wa klabu ya Liverpool ya nchini Uingereza ambayo unapenda kutafsiri jina lake kwa Kiswahili na kuiita ‘Bwawa la Maini’, je hapo nyumbani wewe ni mpenzi wa klabu ipi na kwa nini?

 

MM : Pan African Football Club kwa kuwa ni klabu pekee ya Bon hia hia…

 

BC : Tunakutakia kila la kheri Michuzi.

 

MM : Mimi pia naitakia kila la heri Bongo Celebrity katika kazi hii ya kukusanya watajika na kuwaweka kwenye kumbukumbu kwa njia ya mtandao. Ni ubunifu unaostahili pongezi kwani ni wachache waliowaza hili, achilia mbali kuwa na muda na uwezo wa kutekeleza. Ushauri wangu ni kwamba msiishie tu kwa watajika wa fani tajika tu, tunao maselebriti wasioimbwa katika kila nyanja ikiwa ni pamoja na siasa, utamaduni na sanaa, urubani wa meli na ndege n.k. Hata hivyo msikate tamaa. Roma haikujemgwa siku moja na safari ya maili 1000 inaanza na hatua moja. Alamsiki na asante kwa kunipa nafasi hii ya kusherehekea miaka miwili ya kuzaliwa kwa issamichuzi.blogspot.com na nitakuwa mtovu wa fadhila nisipowashukuru wadau wote ambao wamekuwa pamoja nami katika shida na raha hadi kufikia hapa. Sina cha kuwalipa ila ahadi ya kuendeleza libeneke na AHSANTENI SANA

 

BC : Shukrani Michuzi kwa ushauri na support.Tutaufanyia kazi barabara.

Advertisements
 

28 Responses to ““NIPO TAYARI KUIKABILI CHANGAMOTO HII”-MICHUZI”

 1. Mahojiano yamesimama mahali pake.Hongera sana muhidin miaka mi2 si mchezo! na BC.

  …..kujikwaa si kuanguka.Na kuanguka sio kushindwa bali ni changamoto ya kujiinua na kuanza moja.Kwa maana nyingine mtu hutakiwi kukata tamaa mradi Mungu amekujalia uhai. Ukianguka, amka anza moja…

  maneno ya bwana Michuzi yanatoa nguvu sana haya.Dunia hii kupigwa mtama ni jambo la kawaida sana,tupigwe mitama na tuamke.

 2. Happy Says:

  Well and good Michuzi!mahojiano yako yana ‘challenge’ kubwa mno!Ninachoweza kusema,kila la heri.

 3. Farida Says:

  Hongera Bwana Michuzi,wewe ni mfano wa kuigwa na vijana wenye malengo maishani: Its my birthday today I am so happy we celebrity together.

 4. Bob Sankofa Says:

  Hongera Issa Michuzi, baba wa blogu za fotografia Tanzania. Mungu akuzidishie umri mrefu pamoja blogu yako/yetu.

 5. […] amefanya pia mahojiano ya maadhimisho haya kule kwenye blogu ninayoiheshimu mno ya Bongo Celerity, bofya hapa ucheki ameosha vipi kinywa. Msemo wa “waosha vinywa” ni msemo uliorutubishwa kwa […]

 6. Hongera Michuzi kwa kazi nzuri. Wewe ni mfano wa kuigwa. Picha zako zinasaidia kuondoa upweke kwa sisi waBongo tuliyo mbali na nchi yetu. Asante.

 7. Maricha Says:

  Hongera Michuzi kwa kutimiza miaka hio sio mchezo mie nilifungua bulogu yangu baada ya wiki nikaishiwa cha kusema nikanyamaa kimya hadi leo lakini siku is neva misi pale kwako, naon akila nnachotaka nakipata pale. Nikibangai kwa akina Mjengwa na metty na apa BC aaaaah nafurai na roo yangu

  Michuzi kuwa kama guugo na yahuuu toa huduma bureeee kule tztimes wao ni wa bureeee hao kisha wanapata feza kiaina kutoka sehemu zingine.

 8. Dinah Says:

  Nitakuja kusoma baadae, lakini kwa vile ni Michuzi najua mahojiano yalikuwa mema tu. Ningependa kuonana kitaaluma na Michuzi ili na mimi nimhoji(nimbane) nione ujanja wake.

  Kila la kheri ktk usherekeaji wa miaka 2 ya Michizi Blog. Kazi nziri BC!

 9. Lotte Says:

  Congratulations Michuzi! Kamani mtoto basi huu ndiyo wakati wa kukaza miguu sawasawa, kazi kubwa iko mbele yako hasa kwavile tayari wengi wetu tunatarajia kusoma na kusikia habari za nyumbani kutoka kwako kuliko hata vyombo vingine vya habari. All the best kaka! Hongereni sana BC, you’re the best!

 10. muddy Says:

  Kaka Michu Pan ya marehemu mzee Mangara mimi na wewe damudamu lakini kwa bwawa la maini aaa mimi ni bunduki

  Michu hongera sana ndugu yangu kaza buti kwani kazi ndio hiyoooo imeanza na kama ni mtoto hata kindagateni hajaanza CHEMKA MZEE UFIKE MBALI!!

 11. Huyu ndiye aliyenipa mimi hamasa na changamoto kubwa ya upigaji picha za habari,amenipa mawazo na ushauri wa mambo mengi mbalimbali ikiwemo sanaa hii ya upigaji picha.! nakumbuka siku moja tumekaa tu sebureni tunapiga stori,aliniambia kuwa “usipokata tamaa, ukawa mwepesi wa kujituma na mbunifu basi utafika mbali na utanizidi mimi” maneno hayo yalinipa faraja sana kiukweli.Na kweli mawazo yake yameanza kunipa mwanga mkubwa sana.Namshukuru sana sana na mungu azidi kumpa afya njema kila siku ili aweze kuwa changamoto kwa kila mtu na popote pale.Leo hii na mimi namiliki blog yangu ya picha.MUNGU AMUONGOZE SANA KWA KILA JAMBO !

 12. Mwalyoyo Says:

  Hongera sana Bw Michuzi kwa kutimiza miaka miwili. Hakika tunaikubali kazi yako na tunaona manufaa yake kwa ujumla. Nakutakia kila la heri katika kuendeleza libeneke.

 13. stambuli Says:

  Nampongeza Michu kwa kazi nzuri,hata mimi huwa siku haipiti bila kupitia blog yake.Namshauri asichuje maoni kama mtu anatoa Lugha siyo nzuri wee mlete tutamrekebisha usifiche maradhi,au mengine yakugusa ndio maana unachuja,kuchuja maoni ni tabia ya Ki-C.C.M na Serikali yake kila kitu wao Ni Siri.

  By Stambuli

 14. Jamila Hamisa Says:

  Michuzi sio mtu wa kuamini, ni kigeugeu vile vile ni mpenda makuu kwa vile marafiki zake wakubwa ni wakina Jackie Pemba.

 15. EMMANUEL Says:

  pongezi sana kwa miaka 2 ya hii blog,siku zote natamani sana kukutana na wewe kaka michuzi kwani nina mambo mengi muhimu ya kukaa na wewe,sasa sijui tanisaidiaje?

 16. Adeline Says:

  Imekaa vema kabisa. Hongera, Swali langu kwako Bw. Isaa Michuzi, je unajisikia sikia kugombea angalau nafasi ya upresident itakapotokea chance?

 17. hongera sana kaka Michuzi kwa mutimiza miaka miwili ya SAUTI YA WATU(BLOG YAKO)

  Majadiiano ya sasa ni changamoto ya kwa waida kwa mtu yeyote anayechomoza miongoni mwa watu!

  Mgunga

 18. Subi Says:

  Kaka Michu, hongera kwa ‘globu’ kutimiza miaka miwili na wewe kuendeleza miaka miwili ya kuihudumia. ‘Globu’ imesheheni picha na matukio utadhani ipo mashindanoni na ‘SHIHATA’… ”
  Globu ya jamii” na iendelee kudumu!

 19. amani mohad Says:

  Nimeona Bw.Misupu akisafiri na Bw.J.M Kikwete(vasco da gama) kwenye ngalawa/boti,hongera kwa nafasi hiyo.

  Sasa,nini maono/maoni ya Michuzi kuhusu kama Bw. J.M Kikwete ni fisadi na au mshirika/mshiriki wa ufisadi wa moja kwa moja kwa kujua au kutokujua?
  Je,kifedha,Bw.Kikwete aliwezaje kuifikia kila kata wakati akiusaka uraisi kuliko hata mtu kama Bw.Sumaye ambae kwa wakati ule alikuwa ndie PM mwenye uwezo wa kiutendaji wa kufika alikofika Bw.Kikwete kijiografia?

 20. Mrisho Mpoto Says:

  Mwana anapo zaliwa nini maana yake,
  kuwa tumezoea maisha ya upweke,
  au tuketi nae umojani tujengeke,
  Hongra sana kaka.

 21. Muhumba Says:

  ama kweli ubongo ni ubongo kwa sababu kuna kichwa, la sivyo ni mnofu tu. Think criticaly to serve the cosmos! ama!

 22. Muhumba Says:

  ama kweli ubongo ni ubongo kwa sababu kuna fuvu la kichwa, la sivyo ni mnofu tu. Think criticaly to serve the cosmos! ama! Nyie mwenzenu amewaambia ana kazi kubwa za kusoma, kuchekecha na kupambana na changamoto za meseji nyingi we unampa tu mahongera mahongera kila mtu hongera, pongezi… mnataka abakie kuzisoma hizo asifanye mengine! Waswahili bwana kwa kujiloweka hewani…..

 23. Angeline Says:

  Hongera sana kaka Misupu, huku niliko huwa napata habari fasta kuliko walioko Bongo, nikiwapigia simu kuwauliza wanashangaa.
  Kuingia kwenye hii Blog ni kama Bismillah.
  UDUMU

 24. blog yako bomba sana kaka michuzi keep it up, lete udaku hasa napendaga mambo ya wknd inavyokuaga, unavyotuletea habari za wadau wa a.taun

 25. Gasper Lweja Says:

  Uncle upo juu,ni mbunifu,mi na watanzania wengi tunaikubali kazi yako,kwa sababu kazi yako inaitaji muda mwingi na akili ni lazima pamoja na kuongeza vionjo changamoto kubwa iwe ni kuboresha maslai zaidi(direct or indirect).Kila la heri.

 26. Uncle Michuzi upo juu sana, kazi yako ni nzuri sana nina dadaangu yupo China anapenda sana kufungua Blog yako endelea hivyox2. Hongera sana Uncle Mungu yupo nawe

 27. Uncle Michuzi upo juu sana, kazi yako ni nzuri sana nina dadaangu yupo China anapenda sana kufungua Blog yako endelea hivyox2. Hongera sana Uncle Mungu yupo nawe keep it up

 28. Ngwesa Says:

  Keep on movin’ bro’ uko juu sana


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s