BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

DR.ASHA-ROSE MTENGETI MIGIRO. September, 29, 2007

Filed under: Bunge,Serikali/Uongozi,Siasa,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 5:43 PM

Tarehe 1 Februari mwaka 2007 ni tarehe ambayo Dr.Asha-Rose Mtengeti Migiro hawezi kuisahau kirahisi. Hii ndiyo siku alipokabidhiwa rasmi ofisi na majukumu ya unaibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa cheo ambacho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997 kilikuwa hakijawahi kushikiliwa na sio tu na mwanamke yeyote mweusi bali pia mwafrika yeyote. Kwa maana hiyo Dr.Asha-Rose Migiro ndiye mwanamke wa kwanza mweusi kushikilia wadhifa huo na pia mwafrika wa kwanza. Mwanamke mwingine ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kushikilia cheo hicho alikuwa ni mzungu raia wa Canada Louise Frechette ambaye alianza kukitumikia cheo hicho mapema mwaka 1998.

 

Dr.Migiro anayo historia nyingine ya kujivunia. Yeye ndio alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961. Aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 2006.

Hivi leo Dr.Asha Rose Migiro ambaye ni mke wa Professa Cleophas Migiro na pia mama wa watoto wawili wote wakiwa wakike, ni fahari ya Tanzania. Ndiye “balozi” wa Tanzania anayetambulika kirahisi zaidi kimataifa hivi sasa. Yeye mwenyewe, katika mahojiano mbalimbali aliyofanya na vyombo vya habari kufuatia uteuzi wake, anasema uteuzi ule ulimshangaza lakini pia aliuona uteuzi wake kama sifa kwa bara zima la Afrika. Waliowahi kufanya naye kazi wanasema hawakushangaa kusikia kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Kin Moon amemchagua Dr.Migiro kwa sababu ni mchapakazi, mnyenyekevu na msomi aliyebobea katika masuala ya sheria. Unyenyekevu, utu na uungwana ni sifa zingine ambazo zinafanya majumlisho ya siri ya mafanikio yake.

Dr.Asha-Rose Migiro na mume wake Prof.Cleophas Migiro.

Lakini Dr.Asha- Rose Migiro ametokea wapi? Historia yake inaonyesha kwamba alizaliwa Songea, Kusini mwa Tanzania mnamo tarehe 9 Julai mwaka 1956. Wazazi wake ni wenyeji wa mkoani Kilimanjaro ambako ndipo ilipo asili yake. Kikabila ni mpare.

Alianzia elimu yake ya shule ya msingi katika shule ya msingi Mnazi Mmoja iliyopo jijini Dar-es-salaam mwaka 1963 mahali ambapo aliposoma mpaka mwaka 1966 alipohamia shule ya msingi Korogwe iliyopo Korogwe,Tanga kuanzia mwaka 1967 hadi 1969 alipomalizia elimu yake ya msingi. Kuanzia mwaka 1970 hadi 1973 hapo alijiunga na shule ya sekondari ya wasichana WeruWeru iliyopo Moshi,Kilimanjaro. Kwa elimu ya high school Dr.Migiro kuanzia mwaka 1974, alisomea katika shule ya Sekondari ya Korogwe iliyopo Korogwe,Tanga ambapo alihitimu mwaka 1975.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam mwaka 1977 kuchukua shahada ya kwanza ya sheria. Alihitimu mwaka 1980. Baada ya hapo alifanya kazi ya uwakili kwa muda mfupi. Kuanzia mwaka 1982 hadi 1984 Dr.Migiro alirejea tena katika Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam kwa ajili ya shahada ya pili ya Sheria (Masters).

Dr.Asha-Rose Migiro akiwajibika Umoja wa Mataifa.

Safari ya kimasomo ya Dr.Asha-Rose Migiro haikuishia hapo kwani mwaka 1988 alijiunga na Chuo Kikuu cha Konstanz kilichoko nchini Ujerumani kwa ajili ya masomo ya kutoka chuo hicho hicho kikuu cha Dar-es-salaam mnamo mwaka 1984. Baada ya hapo alikwenda nchini Ujerumani kusomea shahada ya udaktari wa falsafa (PhD) katika masuala hayo hayo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Konstanz ambapo alihitimu masomo yake mwaka 1992.

Kabla ya kuelekea Ujerumani, kikazi tayari alikuwa ni mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa mkufunzi msaidizi mwaka kuanzia mwaka 1981 na baadaye, baada ya kurejea toka masomoni Ujerumani, kupanda katika ngazi za mhadhiri msaidizi, mhadhiri hadi mhadhiri mwandamizi, cheo alichokuwa nacho mpaka mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa. Aliingia kwenye siasa na moja kwa moja kugombea ubunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa taasisi za elimu ya juu.

Dr.Asha-Rose Migiro na Raisi Jakaya Kikwete.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi, aliteuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2005. Huyo ndio Dr.Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, umoja ulioanzishwa mnano mwaka 1945 na wenye makao yake makuu New York nchini Marekani.

Advertisements
 

20 Responses to “DR.ASHA-ROSE MTENGETI MIGIRO.”

 1. Dinah Says:

  Mpangilio wake wa mavazi ndio unanifurahisha na jinsi alivyojaaliwa umbile la kawaida ndio kabisaa. Mfano mzuri kwa wanawake wengine kiutendaji, mavazi na utunzaji wa mwili (sio kujiachia).

  Kila la kheri ktk utendaji wako wa kazi Dr Mingiro.

  Kazi nzuri BC.

 2. Lotte Says:

  Bravo! Now you are talking BC, we need to hear about successful stories like this one. I hope Dr. Migiro na wengine walioko UN watakuwa ni changamoto kubwa kutufungulia nasisi waTz njia ya kuingia Umoja wa Mataifa. Sina maana kwa kupendeleana tu bali kwa wale wanaostahili na wenye sifa zinazokubalika (academically). Uwakilishi wa Watanzania sehemu nyingi za kimataifa ni mdogo mno na hiyo inatufanya sisi kubakia nyuma siku zote, siamini kwamba hatuna watu wenye uwezo bali nadhani hatuna marefa wakutosha. Ulimwengu wa sasa bila kuwa na mpiga kipenga hatuwezi kufika. Pia ni njia mojawapo ya kutangaza Taifa letu ulimwenguni. Hongera sana mama Migiro!

 3. Mbughi,Regnald Says:

  Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kukuteua wewe kati ya maelfu Dr. Rose. ukwanza wako katika madaraka mazito kama hayo unaashiria wazi kwamba Mungu anatambua mchango wako katika umma hivi kukufanya mpendwa wake.

  Hongera sana.

 4. Ahsante sana BC.Mama huyu ndio Da Mija anawaita Wanawake wa Shoka.Nakubaliana kabisa na mchangiaji Lotte hapo juu.
  Watanzania tuna vigezo vya kutosha sana kufanya kazi UN tatizo ni moja.lack of Information ndio tatizo kubwa ambalo sasa watanzania tunaanza kulikimbia taratibu.

 5. Chriss Says:

  Mama yetu, Dr. Migiro tuko nyuma yako. Wewe ni mfano wa kuigwa.

  Dinah, mavazi hajiachii!!! ulikuwa unategemea ajiachie. Yeye ni mheshimiwa, MB, Waziri, Mhandhiri na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Sio Ray C. Nafasi yake haiwezi kumruhusu kufanya hayo unayoyafikiria. Unajua maana ya Professionalism. Watanzania elimikeni – acheni ulimbukeni tu. Yaani unataka kila mtu avae kama Mariah Carey. Watu wengine bwanaaaa!!!!!!!!!!!!

 6. Mr Tom Says:

  Kwa kweli watanzania tuna kila sababu ya kujivunia mama huyu ambaye kwa hakika ameiletea sifa njema nchi yetu na bara la Afrika kwa ujumla.Ni mama mtulivu sana,mwenye hekima nyingi na mwenye uwezo mkubwa na upeo mpana wa kuchanganua mambo.Nakumbuka Katibu Mkuu wa UN Mh.Ban Ki-moon alipomteua aliorodhesha majukumu atakayompatia huku akielekeza kukasimu madaraka makubwa kwake.Mimi kama mtu niliyebahatika kuwa naye karibu alipokuwa huko nyumbani Tanzania,sikuwa na shaka yoyote kwamba ataweza kuimudu nafasi yenyewe pamoja na majukumu atakayopewa na bosi wake.Ni hii ni kwa sababu ya utendaji wake makini sana niliofahamu tangu akiwa waziri katika serikali ya mzee Mkapa na baadaye katika serikali ya Mh.JK.Na nashiwishika kuamini kwamba mama huyu sitakuja kushangaa kuona watanzania wakimpa dhamana ya kuongoza taifa letu kama yeye mwenyewe atapenda kufanya hivyo wakati wa kufanya hivyo ukiwadia.Maana naamini kwa wakati huo atakuwa amejizolea uzoefu mkubwa sana katika nyanja za kimataifa na kujulikana kila pande ya dunia.Uzoefu huo na kujulikana huko itakuwa ni mtaji tosha kwake katika kukuza uchumi wa nchi na maisha ya watanzania kwa ujumla.Tuzidi kumuombea mama huyu maana kwa hakika ni hazina kubwa kwa taifa letu na hata kwa Afrika nzima.Mungu mbariki Dkt Asha Rose Mtengeti Migiro,Mungu ibariki Tanzania.

 7. Dinah Says:

  Chriss nasikitika kusema kuwa hukunielewa nilikuwa na maana gani. Niliposema kujiachia nilikuwana maana kunenepena ovyo na kutojipenda ktk uvaaji kama viongozi wengine ktk Serikali ya Bongo na Afrika kwa ujumla.

  Mavazi yake ukimuona tu unajua huyu mtu means business, hata kama akivaaga vitenge still huwa natoka vizuri kwa vile anajijali na kujipenda japokuwa anamajukumu mengi kimataifa.

  Nilisha sema mazuri mengi kuhusiana na upeo, uwezo wake kikazi na bidii mara baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa kwanza mwanamke wa mambo ya nje na Ushirikiano wa kimataifa na ndio maana nikazungumzia muonekano wake.

  Jifunze kuelewa sio kukurupuka tu kwa vile unachukia mavazi ya vijana au wasanii.

  Chukulia kawaida.

 8. mohamed Says:

  mama migiro keep it up,BC vitu hivi ndivyo tunavyo vitaka – FAHARI YETU WATANZANIA
  Muddy

 9. Chriss Says:

  Dinah,

  Sikukurupuka kabisa lakini nilisoma “between the lines of your words”.
  Anyway tusigombane. Turudi kwa mama yetu Migiro ambaye kwa kweli ametuweka sehemu nzuri sana kwenye global business/politics. Samahani kwa maneno yangu na naomba usisikitike sana. Nakupenda!

  TUENDELEE

 10. Mr Tom Says:

  Kwa kweli nimefurahishwa sana na namna ambavyo hawa ndugu (Chriss na Dinah) walivyolimaliza suala la mkanganyiko ambao ulitaka kujitokeza kufuatia kutokuelewana katika maoni yao.Kwa kweli hata mimi bwana Chris alinipa taabu kidogo namna alivyojibu hoja ya huyu ndugu Dinah.Maana hata mimi nilivyomuelewa Dinah ni kwamba alilenga zaidi kuonyesha mvuto anaokuwa nao mama yetu katika suti za kufa mtu anazotoka nazo pale UN.Na hilo halina ubishi kwani hata mimi ninapowasiliana naye kwa simu siachi kumpa credit kwa namna anavyopendeza na mavazi yake ya hali ya juu,Na hili ni jambo la kawaida hata hapa Marekani mtu ukitoka vizuri hawaachi kukusifia.Anyway, sina nia ya kuendeleza mjadala huu ukizingatia bwana Chriss amejibu hoja kiungwana na kwa ustaarabu wa hali ya juu.Hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa kwa watu wenye busara na hekima kuomba radhi pindi inapotokea kuna mkaraganyiko katika maoni na zaidi sana ukuzingatia kuwa hoja yenyewe ilikuwa ni kumpongeza mama yetu Migiro,hivyo isingekuwa busara hoja hii njema ikazua marumbano ambayo hayakustahili.Once again,Chriss umeonyesha ukomavu wa kupigiwa mfano katika kuchangia hoja.Keep it up!

 11. Ally Says:

  Hahaha anajua kuchangia hoja kila mtu anakuwa na mawazo yake na kila mawazo ya mtu yanatakiwa kuheshimiwa kutokana hivyo ndivyo anavyoona yy sio!tunampongeza mama yetu kwa hatua aliyofikia kuwa mwanamke wa kwanza africa kushika wadhifa huo safi sana japo mi siono kama ni mkomavu sana ktk siasa coz hajakaa kiivyo kwenye hiyo game!mama anapendeza sana akiwa ktk mpangilio wake anaouweka japo cki moja moja abadilishe ile style yake ya nywele ishakua ya mda mrefu sana hahahaa

 12. jennifer mhando Says:

  haya ndiyo tunayoyataka, hongera mama Migiro pia BC, tupeni hizi habari maana mawasiliano ndiyo silaha na hasa yakiwa na ukweli.

 13. Chriss Says:

  Ahsante Mr. Tom.

  Unajua sisi ni watanzania. Mila yetu amani na upendo. Wajibu wetu kuleta suluhu penye utengano. Ni vema tukijisahau wenyewe tuwe wepesi wa kuliona. Ahsante sana kwa maneno yako ya hekima pia.

  TUENDELEE

 14. Tanzania tunajidai kwa kweli, walitufanyia roho mbaya kwa Salim Ahmed Salim kaibu miongo mitatu iliyopita alipokaribia lakini sasa hakuna ubishi. Nchi yetu imejaliwa watu wenye heshima, hadhi na vipaji; tatizo ni kwamba hatujagundua ujanja wa kufuta umaskini wetu!

 15. John Kipandwa Says:

  Kwanza nampongeza dokta kwa kazi aliyopata. tatizo kubwa tulilonalo watanzania ni wivu. hivi sasa nafasi zipo nyingi sana UN. lakini nyingi ni ni za mikataba mifupi. na serikali yetu inakuwa ngumu kuwapata watu likizo bila malipo ili watafute ujuzi zaidi na pesa kwa maendeleo ya nchi.Mimi nimebatika kupata kazi katika UN. lakini viongozi wangu hawakuniruhusu mpaka nikaacha kazi. Nchi kama Ghana , kama unaenda kufanya kazi UN unaruhusiwa kirahisi unafanya halafu unarudi kuitumikia nchi. Kazi kama polisi na jeshi ni hot cake huko kwani askari wengi wanapelekwa misheni kwa kipindi kifupi na wengi wana maisha mazuri. Ningependeza serikali yetu iangalie upya suala la kuwaruhusu watu kufanya kazi na UN. Pia wajitahidi kuwapeleka askari wetu kwa zamu katika majeshi ya DPKO.

 16. Musa Awadhi Says:

  Sijui kama Mama Migiro anasoma hii website. Nashauri bwana Michuzi umshari kuwa kuna page ya wabongo wanaongelea juu ya wewe kuchaguliwa kuwa M/Katibu Mkuu. Kwanza nakupongeza kwa kuchaguliwa ,nikiamini mahela utakayo yapata utakuja kujenga Tanzania na kuleta maendeleo Tanzania. Pili ,pamoja na kuamini falsafa ya binadamu wote ni sawa lakini damu ni nzito kuliko maji.Hebu tujiulize ukiona watoto wawili wako katikati ya reli na treni inakuja.Hao watoto wa wawili mmoja ni mtoto wako na mwingine humjui. Mtu yoyote mwenye akili timamu atamuokoa mtoto wake kwanza. Ninamaanisha Mama Migiro kuwa huu ni wakati wa watanzania kujaa katika UN na kuleta mapesa Tanzania kwa faida ya Tanzania. Angalia mwenzako alivyofanya, Kofi Annani aliweka watu wa West africa katika nafasi za kuajiri ndio maana wako wengi kwenye UN. NAWE TUNAKUOMBA uwaweke wabongo katika hizo post za ajira. Pia jitahidi kuwa wanajeshi na polisi wetu waende kwa wingi katika misheni. Kwa faida ya watu wasiojua mahela ya UN. mwanajeshi au polisi akienda kwenye misheni pamoja na mishahara kila siku analipwa pesa isiopungua dila 100,japo inaweza kubadilika kidogo kulingana na AINA YA NCHI. Na kwa mwaka mmoja anaweza kuserve pesa zisizozidi dola 24000 ambazo zinatosha kujenga nyumba.Usiogope saidia nchi, huu ni wakati wetu sasa. Nakuhakikishia ukifanya hivyo utasaidia uchumi wa taifa letu kwa kiasi kikubwa. Naomba watanzania wenzangu ambao mpo karibu na huyu mama mumufikishie ujumbe wangu kwake. Asante na mungu ambariki.

 17. david benjamin Says:

  I was very much impressed by Dinnah’s and Chriss’s argumentations.u guys know what ur doing.Unajua arguments kama hizi ni nzuri pale zinapotumika in a more intellectual manner.

  Neither dinnah nor chriss was wrong as regards to Dr.Migiro’s personality.

  On the other hand,mr Tom had also played a vital role in trying to clear up some of the misunderstandings that were likely to get fuelled if no immediate measures were to be taken.

  Big up 2 all of u and more importantly to Dr Migiro.

 18. Mama wa Kichagga Says:

  Dr. Migiro hongera sana. Umetukomboa wanawake wengi sana hata kwa mawazo tuu kwa kitendo cha kuteuliwa kwako kama mama. Kwa wanawake wote hasa wa Kitanzania NIDHAMU KAZINI NA NYUMBANI NI MUHIMU SANA KATIKA KULETA MAENDELEO YAKO, YA FAMILIA NA TAIFA KWA UJUMLA. Hongera za pekee zimwendee mwalimu wetu mpendwa MRS MARY KAMM aliyekuwa Mkuu wa Shule ya wasichana Weruweru kwa niaba ya walimu wote nchini kwa malezi na makuzi yao mema ya kiroho na kimwili. Mama Kamm alikuwa anasemaga: MWANAMKE SHULE! MWANAMKE SHULE! MWANAMKE JITUME! MPENDE MUMEO! FANYAKAZI KWA BIDII! Matunda ndo hayo dada Migiro. BIG UP!

 19. Mushi Says:

  This is amazing achievement for the former minister ,This is an inspiring story to Tanzanian women and men too .Hongera mama

 20. Evelyne Says:

  Big up mama kila siku kumbuka kumuomba Mungu akupe Hekima na Maarifa ya kuweza kuongoza vyema gurudumu la maendeleo na kuzidi kulitangaza vema jina TANZANIA huko kwenye umoja wa mataifa.

  Nimekuasa uombe Hekima na Maarifa ili uweze kutofautiana na viongozi wetu wa hapa Bongo ambao wao kila kukicha wanaomba Mungu azidi kuwalimbikizia mali[fedha, magari ya kifahari, majumba ya kifahari na n.k] na mpaka kufikia kupewa majina ya “MAFISADI”.

  Nakuombea sana kwa Mungu aendelee kukupa “Hekima na Maarifa” kama alivyoweza kumpa mfalme Suleimani na kuweza kuliongoza vyema taifa la Israel, iwe na kwako pia ukauongoze
  vyema umoja wa mataifa na Mungu akawape akili ya kusikia na kuelewa wale wote unaowaongoza.

  Hongera sana Mama wewe mbele nasi tu nyuma yako tuzidi kuombeana. NAKUPENDA SANA.

  Evelyne


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s