BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“DINGI” NI KISA CHA KWELI-MANDOJO NA DOMOKAYA October, 1, 2007

Filed under: Bongo Flava,Muziki,Sanaa/Maonyesho,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 9:13 PM

Ukikutana nao mitaani, mara nyingi watakuwa mabegani wamebeba magitaa yao. Kwao muziki ni kila mahali. Tungo zao zinatoka sio tu kwa wanachokiona kwenye jamii bali hadithi timilifu za maisha yao wenyewe. Hivi leo huwezi kuwatenganisha. Alipo Mandojo ndipo alipo Domokaya.

 

Kama umewahi kuwaona vijana hawa wakiwa jukwaani, kusikiliza kwa hatua mpangilio wa miziki yao au kufuatilia kwa makini ujumbe uliomo kwenye nyimbo zao, basi utakubaliana nasi kwamba vijana hawa ni wanamuziki na sio tu wasanii kama ambavyo wao wenyewe wanasema. Albamu yao mpya wanaiita Nizikwe Hai, imesheheni nyimbo zinazozungumzia hali halisi ya mtanzania, kuanzia mlalahoi mpaka yule mwenye nazo.

Wiki chache zilizopita tulifanya nao mahojiano ambayo tunakuletea hivi leo. Lakini ili upate raha kamili ya mahojiano haya naomba nikupe ushauri kwanza. Kwanza itazame video ya wimbo uuitwao “Dingi” .

Kama utakumbuka siku za nyuma tuliwahi kuitaja kama mojawapo ya video zilizowahi kupendwa na wahariri wote wa hapa BongoCelebrity.Ukishautizama wimbo huu, endelea kusoma mahojiano kamili;

BC: DomoKaya na Mandojo karibuni sana ndani ya BongoCelebrity. Kwa kifupi tu, mnaweza kutueleleza historia za maisha yenu?Mlizaliwa wapi, na mmesoma wapi mpaka kufikia hapa leo.

DOMOKAYA: Aah, mimi nimezaliwa hapa hapa Dar, nimekulia na kusoma shule ya msingi inayoitwa Hananasif iliyopo Kinondoni. Kwa upande wa secondary nilisomea Arusha shule inayoitwa Amboseli mpaka 2002, nilipokuta na Dojo.

MANDOJO: Mimi nilizaliwa Mwanza ni mtoto wa nne katika familia ya watoto sita.Nimesoma shule ya msingi Manyoni mkoani Singida na baadaye nikajiunga na shule ya sekondari Sanza. Nilipomaliza hapo nikaenda high school Dodoma shule moja inaitwa Jamhuri. Baada ya hapo ndio nikahamia Arusha kwa kaka yangu na huko ndipo nilipokutana na Domokaya.

BC: Kwa hiyo mlianza lini rasmi shughuli za muziki na ilikuwaje leo mko pamoja kama kundi lenye wasanii wawili mahiri namna hii?

DOMOKAYA: Tulikutana mwaka 2002 ambao mimi nilikuwa form two. Wakati huo yeye Dojo kama alivyosema, alikuwa amekuja Arusha kumtembelea kaka yake. Tulikutana katika nyumba ambayo alikuwa anakaa rafiki yangu niliokuwa nasoma nae, yeye na Dojo walikuwa wanakaa nyumba moja. Sasa kila nilipo kuwa nikienda kumtembelea rafiki yangu, tulikuwa tunakutana na Dojo, tukafahamiana na kugundua kwamba yeye wote wawili tuna vipaji vya kuimba. Dojo alikuwa anajua sana kuimba na kupiga gitaa, na mimi nilikuwa najua sana ku rap, tukafundishana ujuzi wetu, yeye akanifundisha kupiga gitaa, na mimi nikamfundisha kurap. Mwaka 2003 ndio tukaamua kuja Dar kurekodi nyimbo yetu inayoitwa “Nikupe”. Lakini ki mziki tulianza zamani sana, wakati mimi niko Dar na Dojo yeye yuko Manyoni.

MANDOJO: Labda niongezee tu kwamba tangu shuleni nilikuwa najishughulisha sana na mambo ya muziki katika kuimba nyimbo za gospel zaidi.

BC : Nini chanzo cha majina yenu Mandojo na Domokaya? Majina yenu halisi ni yapi?

Mandojo : Jina langu halisi ni Joseph Francis Michael. Jina la Mandojo nililipata nikiwa shuleni, Wakati huo nilikuwa mtundu sana, nilikuwa navaa viatu fulani hivi vikubwa sana kama raizoni, Wanafunzi wenzangu wakawa wakiniona tu wananiita Mandojo kutokana na ukubwa wa viatu vyangu na mimi nilivyokuwa mdogo.Jina hilo likawa limestick mpaka leo.

DOMOKAYA: Mimi Jina langu halisi ni Precioust Juma. Lakini Domakaya Limetokana na washkaji, Si unajua vile maneno ya verses. Wakati unaandika nyimbo, mtu hufikirii ndio chanzo cha jina lako, wakati huo mimi mwenyewe nilikuwa najiita jina tofauti kabisa. Kwa bahati nzuri au mbaya jina la Domokaya ndio lilioshika kirahisi sana wakati tuko underground. Tulipokuja kurikodi tena, ilibidi nitumie hiilo hilo kwasababu lilikubalika zaidi.

BC : Jina lako la Usanii la Kwanza likikuwa nani?

DOMOKAYA : Nilikuwa najiita Feloo. Sasa ilibidi kuwa DomoKaya Feloo. Jina la Domo Kaya lilishika zaidi ya Feloo kwani Feloo lilikua la kizungu sana, halikushika kwa watu kama vile livyoshika DomoKaya jina la kiswahili, unaona eeeh.

Hata majina yetu nayo tulipokuja kuyaita Man Dojo na Domo Kaya wakati wa kurekodi, watu wengi walituashauri tusiyabadilishe, yaani tusitumie hata jina la Crew tena. Wakati huo sisi tulikuwa na Crew yetu tunaiita ‘Wandava Crew’ . Tukakubaliana na washauri wetu ili angalau tutumie hayo majina ya kinyumbani zaidi. Hivyo tukaepuka majina ambayo yana sound kizungu zungu jambo ambalo lingeweza kusababisha isibambe sana.

BC: Sasa huku tukiwa tushatambua kwamba mlikutana mjini A-Town wote mkiwa vijana tayari. Mnaweza kutuambia, mmoja wenu, maisha yako ya utotoni yalikuwaje? Unakumbuka mambo gani unapofikiria maisha yako ya utotoni?

DOMOKAYA : Daah. Wakati ule kaka yangu David Robert alikuwa anafanya mziki, walikuwa na crew yao moja nzito wanajiita ‘Black Gangstars’ walikuwa wana rap. TID alikuwa ni mmoja wa kundi hilo, wakati huo alikuwa hajaanza kuimba bado. Alikuwa na yeye ana rap tu. Wakati huo nilikuwa bado mdogo sana napendelea kukimbizana na football tu, unaona eeh, nilipokuwa narudi nyumbani nakuta David na mashairi yake kwenye room, tulikuwa tunakaa room moja double decker, nilikuwa napitiapitia mashairi yake yalipokuwa yanazagaa zagaa, najaribu kujifunza ku ya rap kidogokidogo. Wote mimi na yeye tulikuwa hatujui kama siku moja nami nitakuwa mmoja wa wanamuziki.Nilikuwa nafanya mchezo mchezo tu, mpaka tulipohamia Arusha ndio nikaanza kufanya serious kidogo, kwasababu nilikuwa peke yangu, na nilikuwa sina marafiki wengi na niko kwenye mji mgeni ndio nikaanza kuandika mashairi mwenyewe. Nikawa na mimi nime advance. Kwahiyo matokeo yake ndio niko hapa, lakini hata siku moja sikutegemea kuwa mimi nitakuwa artist mkubwa wala nini.

BC : Kila kukicha vipaji vipya vinaibuka katika fani ya muziki wa kizazi kipya. Mfumuko huu wa artists unawaumiza kichwa hata kidogo? Mnafanya nini cha ziada ili kubakia kwenye game?

DOMOKAYA : Eeh, kama unavyojua kuwa sisi wenyewe tuko kitofauti, yaani hata watokeee wasanii ishirini kila siku bado tunaamini tutaendelea kwenda sambasamba nao. Hii ni kwa sababu sisi mbali na kuimba tunatumia vyombo kama gitaa na instruments zingine zingine ambazo tunapiga sisi wenyewe. Halafu pia ukizingatia sio wasanii wote wa kitanzania wanapiga vyombo. Isitoshe sisi tunatumia muda mwingi kufanya kazi yetu, tunajifunza na kui develop kazi yetu zaidi kila siku hasa katika kutumia vyombo vya muziki.

Tukiangalia katika soko la kibongo hivi sasa na nafasi tuliyo nayo, zaidi ni utofauti wetu na wanamuziki wengine wa hapa Bongo ndio unaotufanya tuwike. Sasa hata wakitokea wasanii wengi labda waje kwa staili yetu ndio tunaweza tukashtuka, lakini sio mtu anakuja na hizi staili staili zao za kawaida, hatutashtuka sana. Na kuongezea tunafanya kitu kinachotoka moyoni ( natural feeling ) jambo ambalo linafanya hata kuwa ngumu kwa producer kukubadilisha au kukudanganya.

MANDOJO : Kuongezea kama unavyojua kila mtu ana kipaji chake kwenye usanii na pia kila mtu anakuja na utundu wake katika fani. Lakini muhimu ni kusema ukweli. Sisi bado hatujastuka na mtu yeyote, kwa sababu bado hatujaona mtu ambaye anaweza kutumia instruments kama tunavyofanya sisi. Sisi tunaweza tukawa « live « sana kuliko wasanii wengi.

 

BC : Style ya muziki wenu ndio iliwafanya mkatoka na kukubalika kirahisi katika fani. Kwanini mliamua kuchagua style hiyo mliyonayo ambayo ina utofauti fulani na style tulizozioea?

MANDOJO: Unajua kama ulivyosema hapo juu, kwenye muziki wa kibongo, kila siku wanaibuka wasanii chungu mbovu.Kwa hiyo usipokuwa tofauti, ni wazi kabisa kwamba mambo yatakuwa magumu sana. Kwa kuzingatia hilo sisi tulikaa sana kabla ya kufikiria kurekodi tukipractise kwa takribani miaka miwili tukiandaa nyimbo na kujifunza jinsi ya kutumia vifaa.

Nia ilikuwa ni kujaribu kutoka na vitu tofauti kidogo na pia kujitahidi kuwa wanamuziki zaidi ya wasanii.Si unanielewa? Tulizingatia zaidi jinsi ambavyo wanamuziki wa zamani walikuwa wanatumia vifaa halisia vya kimuziki tofauti na sasa ambapo muziki karibuni wote unaweza kutengenezewa katika chumba cha studio tu bila kutumia vifaa vingi sana. Kwa hiyo nadhani utumiaji wa vifaa kama magitaa ndio uliofanya tukakubalika kirahisi mbele ya mashabiki wa muziki.

BC : Mnaiitaje style yenu?

MANDOJO: Sisi tunaiita Hip hop Banjo yaani maana hiphop na gitaa.

BC : Anga za muziki wa kizazi kipya au Bongo Flava mara nyingi umekuwa ikitawaliwa na ukosefu wa maelewano au BEEF kama inavyojulikana zaidi. Nini chanzo cha beef miongoni mwa wasanii na mnadhani nini kifanyike ili kuepuka rabsha kama hizo ambazo hazijengi bali kubomoa?

DOMOKAYA: Mimi binafsi, siwezi kuwa ndani ya beef. Ila watu wegine wanaweza kukuletea beef ndani ya mistari bila hata wewe mwenyewe kujua. Mimi naamini kitu kimoja, mtu usiyeshindana naye hawezi kukushinda’, hata kama atashindana na wewe vipi. Wewe unakuwa unafanya kazi tu. Sasa kuepukana na beef inabidi usisisikilize ya mtu.

Kitu ambacho unaweza kuzingatia ni ushauri wa wale watu wa karibu. Kwahiyo hata mtu akiongea vibaya kuhusu wewe kama kukutukana ama vinginevyo inakuwa haisadii kwa sababu wewe unaendelea kufanya kazi inayokubalika. At the end of the day ni washabiki tu wenyewe ndio watakaokubali matokeo. Kwa kweli beef hazijengi bali zinabomoa tu. Sana sana unapoteza muda tu na beef, kupambana kama mipasho.

BC : Wasanii wengi tuliofanya nao mahojiano wanasema wanaandika wao wenyewe mashairi au lyrics zao. Je nanyi pia ni hivyo hivyo? Kama ndio mnadhani nini umuhimu wa msanii kuandika mashairi yake mwenyewe badala ya kuandikiwa na song writers kama ambavyo wasanii wengi wa kimataifa wanafanya?

DOMOKAYA: Pia sisi tunaandika na kutunga wenyewe. Tunapenda kufanya hivyo kwani tunaamini kuwa kwenye kuimba ni wewe unayewakilisha feeling zako. Sasa kama unaandikiwa na mtu mwingine maanake ni feeling za yule mtu mwingine na sio wewe mwenyewe. Unakuwa kama vile una act zile feeling za mtu mwingine. Kwa hiyo kama utakuwa unawakilisha nyimbo ya mtu mwingine haitakuwa natural kama invyokuwa ukiwa unawakilisha wimbo wako wewe mwenyewe.

MANDOJO: Sisi pia tunatumia magitaa na tunaamini hakuna mtu anaweza kutuandikia vizuri kama tutakavyoandika wenyewe. Kwahiyo kuandika mwenyewe ni kitu kikubwa na muhimu zaidi.

BC: Maeneo mawili makuu ya muziki ni kuelimisha na kuburudisha. Tukiongelea upande wa kuelimisha, mnadhani elimu ipi inakubalika na kueleweka kirahisi zaidi miongoni mwa vijana, kati ya elimu wanayoipata shuleni na wanayoipata mtaani ikiwemo kupitia muziki?

DOMOKAYA: Vyote vinakubalika kwa kweli.Lakini mimi nadhani elimu ya mtaani inakubalika zaidi wasababu elimu ya mitaani ni vitu tunavyokutana navyo daily na sio vitu vya kuambiwa. Kwa mfano tunakutana na vitu vingi saana mitaani, vibaya na vizuri. Wakati unaandika vitu vinavyokuja kwenye feeling na zaidi kuvikumbuka wakati ninaandika ni vile ambavyo nakutana navyo na kuviona mara kwa mara jambo ambalo sio sawa na darasani kwani mara nyingi darasani tuna hadithiwa tu na walimu na hivyo ni rahisi kuvisahau.

Kwa hiyo, nionavyo mimi vitu vinavyokubalika zaidi naona ni elimu ya mtaaani zaidi ya elimu ya shuleni.

Lakini elimu ya shule nayo ni muhimu kwasababu inabidi kujua mambo mengi tuu kutokana na hali halisi yenyewe, ma techonolojia na utandawazi ni muhimu sana katika dunia tunayoishi sasa hivi.

MANDOJO: Kuongezea tu mambo mengi sana watu wanajifunza mitaani. Shuleni mtu unaenda unasoma, unajifunza halafu unarudi mtaaani. Kitu cha mtaani kinamuelimisha mtu moja kwa moja kwasababu atakuwa anaki face kile kitu kila siku anapokuwa anarudi mtaani. Kwasababu shule utasoma utamaliza na inabidi urudi mtaani. Kwahiyo elimu ya mtaani inamgusa mtu moja kwa moja kwa kweli.

BC: Wasanii wengi wa muziki nchini Tanzania wanasemwa walipoanza shughuli za muziki wazazi na ndugu zao hawakufurahia sana uamuzi wao. Kwenu ninyi ilikuwaje?

MANDOJO : Kwa upande wangu naweza kusema nilipata bahati kidogo kwa sababu mama yangu alikuwa anapenda kuimba na mpaka sasa hivi bado anaimba kwenye kwaya. Kwa hiyo tangu nipo mdogo nilikuwa beneti na mama katika mambo ya kuimba kanisani nk.Kwa hiyo wazo la kwamba siku moja naweza kuwa mwimbaji au mwanamuziki halikuwa mbali sana. Baba kidogo alikuwa mkali kwa sababu ya kudhani kwamba nikijikita zaidi kwenye uimbaji nitakuwa sihudhurii masomo fresh nk. Lakini kadiri siku zilivyozidi kwenda wote wakakubaliana na uamuzi wangu wa kujishughulisha na muziki.

DOMOKAYA :Kwa kweli hiyo ni hali halisi kwa wanamuziki wengi wakitanzania tofauti na kama wenzetu huko nje ya nchi ambapo wanapata support tangu mwanzoni kirahisi. Mimi mwenyewe nilipoanza nilipata ku face mambo magumu sana. Mama yangu mwenyewe alikuwa hataki kabisa mimi nije huku Dar alikuwa anataka nibaki Arusha niendelee na masomo. Ikabidi nimwambie mama ngoja kidogo nikajaribu inaweza kuwa ndio mwanzo wa my career, kwani mimi siogopi kujaribu lazima nijaribu kuchukua hii risk.

Hata tulipofika Dar tulipitia matatizo mengi sana kabla hatujapata mafanikio ya kurekodi mpaka karibu kutukatisha tamaaa lakini hatukata tamaa, tukakomaa nayo, tukawa tunajipa tuu moyo kusema siku moja hata mama na wengine wataelewa tuu tukiwa tayari tumefanikiwa kidogo. Na ndicho kilichotokea. waliokuwa hawakutubali baadae walikuja wakaelewa unaona eeh. Tena sasa hivi support kubwa tunaipata kwao hao hao wazazi, hasa mama yangu Kimawazo nk. Nikiwa upset kwa mfano yeye ndio anakuja kunishauri nifanye nini na mambo kama hayo. Unajua tena kina mama, mama yeyote hakubali mtoto aanze kupigana na maisha, mtoto kwa mama hakui, bado wanaona kama vile bado umtoto mdogo, lakini wewe mwenyewe kichwani, inabidi upige akili ku mkichwa si unajua. Unapata matatizo, unafight lakini njia utakapoiona taa inawaka.

BC: Mashairi au lyrics zenu zimejaa visa vya maisha ambavyo watu wengi wanaguswa navyo kwa kuhisi pengine mnawazungumzia wao na mambo kama hayo. Nini kinawaongoza katika kutunga lyrics kama hizo. Huwa inawachukua muda kiasi gani kukamilisha lyrics za wimbo mmoja?

DOMOKAYA: Ah! Yaani huwezi kuamini, kuna wakati mwingine inabidi tu utunge mashairi pale pale studio, lakini mara nying sisi tunapenda kuandaa nyimbo kutoka nyumbani ndio maana nakwambia feeling unayo anza nayo ile natural feeling kutoka nayo nyumbani na kwenda nayo studio kwa producer, inakuwa ngumu sana kuibadilisha. Ni maisha yale tunayokutana nayo kila siku, hata kama saa nyingine tunaimba mapenzi, lakini ni yale yale maisha tunayokutana nayo naamini kama mimi naweza kukutana na haya lazima kuna mwingine amekutana nayo tayari, hata kama sio hapa, inaweza kuwa nchi nyingine yatakuwa yamemkuta. Inawezekana asielewe lugha tunayoitumia (Kiswahili) lakini tunayoyazungumzia yakawa yameshamkuta. Tunachofanya ni kuwa tunaandika yale maisha ya kila siku yanayotokea ili usiwe muongo. Ndio maana tunajifunza sana kupiga vyombo. Unajua kuna usanii na uanamuziki. Usanii kwa tafsiri ya kawaida kwa sisi vijana ni ujanja ujanja tuu. Sisi hatuwezi kujihesabu kama wasanii, sisi tunajihesabu kama vile wana muziki, kwasababu tuna practice na watu wale wenye bendi zao, wanatufuata hata majumbani na ku practise nao kwasababu wanatukubali. Utakapotukuta kokote, maanake tuko tayari tuko full hatuhitaji producer, tukiwa na gitaa zetu mziki umekamilika, tunaweza tuka perfom ukatuelewa. Na ndio maana tunaandika vitu tunavyokutana navyo kila siku, hatuandiki vitu kijuu juu tu.

 

BC: Wapenzi wengi wa muziki, tukiwemo sisi hapa BongoCelebrity, tungependa sana kujua, je wimbo wenu ujulikanao kama Dingi ni kisa cha kweli au utunzi tu? Nani alitunga wimbo huu?

DOMOKAYA : Nyimbo hiyo ya “Dingi” nimeitunga mimi mwenyewe hapa. Mimi kama Domo,lakini pia wakati natunga, nilikuwepo na mwenzangu ManDojo. Ila kisa chenyewe kinanihusu mimi zaidi. Maisha yangu pamoja na nilivyoishi na baba yangu. Lakini kuna vitu venginie kidogo tumetunga kama vionjo vile ili verse itoshe na ili uweze kusikiliza. Lakini part kubwa ya lyrics ni true story. Yaani hata mama na kina mamdogo huko wanapousikia huu mwimbo wanaona kabisa ‘huyu kamwimba baba yake huyu’ kama nilivyokwambia sisi tukitunga nyimbo tunajaribu kutunga kitu kile kile ambacho kinatokea katika maisha ya kila mtu, kama mimi yamenikuta yale yalionikuta mimi na baba yangu, kuna watu wengine yamewakuta mabaya zaidi na baba zao kuliko yalionikuta mimi ,unaona? Kwahiyo kila unapoandika na unapowakilisha wengi sana yanawagusa pia.

MANDOJO : Kwa upande wangu kuna wimbo wa “wanok nok …wanafiki nafiki watu” ile ni historia ya kweli kidogo. Kipindi tunakaa Arusha watu wengi walikuwa wanatuona kama wahuni fulani tu, walikuwa wakituona na magitaa tukitembea temeyabeba wakawa wanaongea vibaya kuhusu sisi kama watoto wa kihuni. Na mbaya zaidi tulikuwa tunakaa kwa brother sehemu ya line police, kwa hiyo watu wakawa wanatuona watoto wa line police wahuni wale halafu ukizingatia tulikuwa tunaenda kufanya mazoezi kwenye mito pamejifichaficha wakawa wanasema maneno kibao, tunavuta bangi kule mitoni, yaani maneno yakawa mengi. Kwa hiyo tukaona bora tuwaimbe tu kwani ujumbe utawafikia hata juu kwa juu kuliko kuwaface direct. Kwa hiyo suala la “wanok nok” lina ukweli wake kidogo ingawa kuna usanii pia unaingia ndani ndio kama hivyo anavyosema Domo, “Dingi”ni kisa cha kweli cha mzazi wake Domo na nyimbo zingine nyingi hata kama hazijatutokea sisi lakini ndio haya haya mambo yanayotokea kwenye jamii.

BC: Baada ya kupata lyrics, mnachagua vipi beats zitakazoendana na lyrics? Kazi ya kuchagua beats inafanywa na ninyi au prodyuza zaidi?

DOMOKAYA : Sisi tukitunga nyimbo tunaanza kwanza na gitaa, tunajaribu kutunga mzunguruko wa codes inafuata melody, ukishapata melody inakuwa rahisi kwasababu melody inapokuwa inaenda tuu tayari maneno yanajiunga humo humo. Tunafanya kama mzaha lakini pale melody inapojiunga na nyimbo nayo inakuwa easy kueleweka. By the time ukimaliza sio mtu mzima, mtoto mdogo na watu wote wanaielewa kirahisi zaidi. Na kwasababu feeling inakuwa umeanza nayo mbali tangu kwenye codes hata ukiienda kwa producer huwezi kumuachia akakupa beat yeyote aitakayo. Tunakuwa tayari tuna na codes na nyimbo imetungwa kutokana na hizo codes. Kama nimetunga juu ya A minus au B minus nyimbo lazima ifuatane na codes hizo. Tukizungumzia codes mfano wa hiyo nyimbo ya “dingi” ipo kwenye codes za gitaa. Bila keyboard bila beats za producer au chochote sisi wenyewe tunaweza kuiimba vile vile unavyoisikia kwenye redio.

MANDOJO: Kwa hiyo tunapoenda kwa producer tunakuwa tayari in control, tunamuonyesha producer codes zetu na tunaomba producer atafute beats kutokana na melody yetu. Kwa mfano ile Dingi ukiisikiliza unaisikia gita, na tumerikodi na kuingiza ile gitaa, ni mimi nilieingiza ile gitaa kahiyo kama producer anataka kingiza kee board mix, inawezekana lakini gitaa lipo palepale. Kwahiyo ile feeling uliootoka nayo nyumbani na gitaa inakuwa rahisi zaidi kwetu kupata tunachokitaka kwa producer kuliko mtu mwingine.

Kwahiyo kazi yetu hatumuachiagi producer afanye mwenyewe, beat zetu na producer ni benet kabisa, yaani bene bene tunashirikana sana na tunahakikisha instruments zetu zinafanyiwa kazi.

BC : Mojawapo ya changamoto ngumu katika maisha ni maelewano katika kazi. Je huwa inatokea mkakosa kuelewana katika kazi yenu kama wasanii wa kundi moja? Huwa mnarekebisha vipi hali kama hiyo?

DOMOKAYA : Aah. Unajua nini, kukosona kupo.Lakini uzuri ni kwamba tunaangalia kule tulipotoka. Mara nyingi watu mkikumbuka mlikotoka especially kama mlikaa pamoja mambo mengi zaidi mnakuwa mmepitia mpaka hapo mlipofika. Kwahiyo hamuwezi kuruhusu vitu vidogodogo tu viwaharibie kama vile ulevi na vitu vingine vya kijinga kuharibu uhusiano wenu. Kwahiyo sisi tunajitahidi sana, hata kama tuligombana jana tunanajaribu kusameheana na kusahau na ukituona utashangaa, tuko vile vile kama kawaida, tuko huru na hata hatukumbushani mambo ya jana. Tunajitahidi sana kuishi kwa amani namna hiyo. Tunafanya hivi kwa sababu tunaamini amani ni kitu kikubwa sana na hiyo inafaya watu mpeane support kubwa kuliko mkiwekeana chuki.Mkiwekeana chuki hakuna mafanikio. Pia kila mtu anakosea na kama mnaweza kuweka moyoni hamuwezi mkawini, lazima kuangalia kuwa hivi ni vitu vya kupita tuu, visije vikaja kuharibu mafanikio au malengo yetu.

Hizo ni challenges ambazo kama binadamu wengine wowote tunazi face, ukishazielewa na ukishajua kuishi na mtu ni vigumu sana kutengana. Yeye Dojo ameshazoea kuishi na mimi ndio maana hatuwezi kuachana, na mimi nimeshamuelewa, na najua kuishi nae ndio maana hatuwezi kugombana. Na ikija kazi tunajua hii ni kazi na tunapiga kazi hata kama hatujawahi kukorofishana hata siku moja.

MANDOJO : Kweli kama alivyosema mwenzangu hapo juu unajua binadamu wote ki ukweli ni kwamba hatuko sawa,hatuko kamili, na kweli kama mnakaa pamoja mara nyingi lazima mtakosana hata kama ikiwa ni mzazi wako,mdogo wako. Sana sana huwa ni hasira tu za haraka haraka. Kwa hiyo kama nimeona mimi labda nimekosea au Domo kakosea au inaweza ikatokea mabishano na nini tunachofanya ni kwamba at the end of the day mnakaa na kusameheana. Sisi ni wanaume halafu tumetoka mbali kwahiyo mmoja wetu akikosea anakubali makosa kisha yanaisha.

Na kukosana kwenyewe sio lazima mtupiane ngumi bali mnaweza tu kuwa mnatupiana hata maneno na nini.Lakini baadaye mmoja anajishusha,kikubwa ndio hicho.Ukiona mwenzio kakasirika sana wewe unaaamua kujishusha unakuwa mdogo ..yeye mwenyewe anaweza akakaa akafirikiria akaona dah hapa nimekosea. Nadhani hiyo ndio njia nzuri sana ya kusolve matatizo madogo madogo na hapo ndio mnaweza mkaishi.

BC : Moja la kitu tunachowapenda ni umoja wenu, ma group mengi yamesambaratika, nini hasa mlichojifunza kwa wale waliosambaratika na wale walioshikilia umoja. Kama ninyi hivyo. Na mnawashauri nini vijana wanaoanzisha group yao?

DOMOKAYA : Mimi nawashauri umoja ndio nguvu na utengano ni udhaifu. Wakubwa walishasema hivyo kwasababu watu walishaona kwamba watu wakitengana kunakuwa na udhaifu na watu wanapokuwa pamoja panakuwa na nguvu. Hii misemo lazima itiliwe maanani kwasababu yalishatokea na wakaona matokeo yake. Aidha mmoja ashuke chini sana na mwingine awe juu sana au wote mtaanguka.

Kwahiyo wadogo zetu na wakubwa zetu wanaoanzisha group zao sasa hivi inabidi wazingatie tu upendo. Waelewe tu kuwa haya ni maisha na wakumbuke lengo lao ambalo ndio siri hasa ya mafanikio. Lazima waweke dhamira na mazoezi. Wasitilie maanani ma ugomvi kwani kugombana kupo tu. Zaidi watilie maanani lengo lao. Hivyo ndivyo watu wanavyofanikiwa. Vinginevyo hamna kitu utaishia kama upepo. Na haya yanatokea sana kwa wadogo zetu wanaoanza muziki, lazima mjifunze kukaa na watu zaidi na kujifunza.

BC : Hivi karibuni mnatarajia kufyatua albamu yenu mpya itakayokwenda kwa jina la Nizikwe Hai.Itakuwa na nyimbo ngapi na kwanini mmeamua kuiita Nizikwe Hai?

DOMOKAYA : Hii albamu tumeiita Nizikwe Hai kwasababu ya matatizo yaliyowahi kututokea au yanayotutokea na pia yanayowatokea watu wengine.Na nyimbo zenyewe zilizo humu ndani ni kama vile Elimu ya juu, Next Door( hii inahusu tatizo pale mtu anapofumaniana na girlfriend wake chumba hiki na hiki. Girlfriend wake yuko chumba hiki na mwanaume mwingine na boyfriend yupo chumba kile na mwanamke mwengine halafu wanafumaniana. Elimu ya juu, tunazungumzia matatizo mtu amesoma mpaka form six lakini kingereza bado hajui. Na nyinginezo nyingi. Kwahiyo hii album inahusu matatizo ambayo tunakutana nayo kila siku na ya kawaida sana. Yaani mtu anakuwa ana matatizo mpaka anaona bora azikwe hai au la mungu amtoe uhai. Mambo kama hayo.

MANDOJO : Album yetu itakuwa na nyimbo kama 11 ambazo tayari zote tushazifanya, kuna nyimbo nyingine kwa mfano inaitwa ‘Mbuga ya Mademu’. Kwa ujumla itakuwa ni albamu ambayo imesheheni nyimbo kali tupu.

BC : Mmewashirikisha wasanii gani katika albamu hii? Imetengezwa katika studio gani na prodyuza gani?

DOMOKAYA : Album hii tumefanya na producer Alan mapigo, nyimbo kama mbili, moja inaitwa hiyo Next Door nyingine inaitwa Bosi. Nyimbo nyingine tumefanya na Double B wa FM Studio alipokuwa anafanya Mika Mwamba ambako ndio tulifanya albamu yetu ya mwanzo iliyoitwa Taswira. Zilizobakia zote tumefanya na Mika Mwamba.

BC : Mmemtaja Mika Mwamba na nikakumbuka kwamba kwa muda mrefu sasa mmekuwa mkifanya kazi zenu na prodyuza Mika Mwamba. Kwanini mmependelea zaidi kufanya kazi na Mwamba?

MANDOJO : Unajua tunapenda kufanya kazi na Mika Mwamba kwa sababu yeye ni zaidi hata ya producer. Tunaweza kusema yule jamaa anatuwezea sana kwa sababu anapenda sana magitaa, ni mwanamuziki kabla ya uproducer. Na sisi tunapenda kufanya naye kazi kwa sababu kwanza tunaelewana naye sana, halafu ni mtu wetu wa karibu sana. Na kama ulivyosema tumeshafanya naye kazi nyingi kwa hiyo tunamkubali. Na ndio kama hivyo kazi nyingi ambazo tumeshafanya naye tunazikubali sana haswa kwa upande wetu sisi ambao tunapenda kutumia instruments zetu. Tofauti na maproducer wengine ambao hawajui hata kutumia instruments nyingine. Ukiangalia hata albamu yetu hii inayokuja ambayo bado haijatoka karibia nyimbo nyimbo zote kafanya huyo huyo Mika Mwamba.

DOMOKAYA: Mika mwamba anajua kupiga gitaa,anajua key board, sio producer wa uongo uongo hata ukimpelekea nyimbo yako ya gitaa, na unamuonyesha zile codes yeye mwnyewe atachukua gitaa na atajaribu kuzipiga kwanza ili aifeel kwanza ile nyimbo. Mika Mwamba sio sawa na maproducer wengi ambao hawajui kupiga hata kifaa kimoja halisi cha muziki. Ukiwafuata maproducer wa namna hii wanataka kwanza uwapigie gitaa halafu wao wakufuate tu kwa kuongeza base line. Hiyo inakuwa kazi ngumu sana.

Tunajaribu sana kufanya kazi na mtu ambae anaweza kufanya kitu ambacho hata wewe mwenyewe utafurahi na uta feel kama ulivyokuwa una u feel mwimbo ulipotoka nao nyumbani. Tunapenda kufanya kazi na producer wale ambao wanauwezo kama anapiga key bord basi awe anapiga key board fluently na kama anapiga gita basi awe anajua kweli. Hilo ndilo tunalojaribu kufanya siku zote kwa hiyo hatumfuati producer kwa kukurupuka kwa sababu ya jina lake tu au nini. Tunamfuata producer ambaye tunaamini anaweza kufanya kazi kama tunavyotaka.

BC : Wanamuziki wengi wanasema muziki wa bongo flavour sasa hivi una pesa kidogo na unawafanya wanamuziki kuwa better kifedha. Mnaweza kutuambia kitu gani hasa mlinunua kwa matokeo ya kazi yenu. Na nini uchotakuwa unakitaka sana kabla ambacho sasa hivi umeshakipata.

MANDOJO: Yeah yeah ndio ni kweli kabisa namshukuru mungu kwamba hii kazi yetu ya muziki imenisaidia sana nimepata vitu vingi. Nilikuwa sina hata dream ya kuwa na nyumba yangu mwenyewe ambayo yaani muziki huu huu ndio umenisababishia nimejenga nyumba yangu hata wazazi wangu sasa hivi wanashukuru kwa sababu wanaishi kwenye nyumba ambayo nimejenga mwenyewe. Ninapokaa najitegemea mwenyewe mpaka sasa hivi sina kazi nyingine zaidi ya huu muziki. Kwa hiyo kikweli mpaka sasa hivi nasurvive na niko mbali na wazazisiwategemei wazazi tena. Kwa kweli umenisaidia kwa mambo mengi, mengi sana ambayo hata siwezi kuyataja yote.

DOMOKAYA : Kazi ya muziki inatusaidia sana. Hatua kwa hatua maisha yanakwenda. Tunaweza kujikimu na maisha sisi wenyewe.Tunaweza kusaidia ndugu na jamaa na marafiki na mambo kama hayo. Hivi sasa yote hayo yanawezekana kwa sababu ya muziki. Pia nikiangalia maisha yangu huko nilikotoka na mpaka hapa nilipo hivi sasa, kwa kweli nashukuru mungu.

BC : Moja la maswali mengi ya wapenzi wenu mmmoja anauliza je ninyi mnajiona kama role models, kama ndio, ni kitu gani hasa ambacho mna sacrifice kwasababu mnaogopa kinaweza ku wainfluence watu wanao wazimia?

MANDOJO: Unajua kama unavyosema sisi kama wasanii wadogo zetu wengi hata kaka zetu pia wanatuangalia tunafanya nini kwa sababu tunauwezo na tunaelimisha jamii. Kwa hiyo kuna mambo mengi sana ambayo nayaogopa mfano kuna vitu vidogo vidogo vingi ambavyo kiukweli tukivifanya kila mtu anashangaa na kusema hata wewe unafanya hivi? Kwa hiyo kuna vitu vingi sana najaribu kutovifanya. Kwa mfano kufanya fujo sehemu au kulewa mpaka kumtukana mtu, kuiba, kwa hiyo hivyo ni vitu ninavyoviogopa sana. Vitu vibaya vipo vingi sana na hata siwezi kuviorodhesha vyote Lakini cha muhimu tu napenda hata kuwa karibu sana na vijana, na kuwaeleze kuwa mimi ni binadamu na wakati mwingine naweza nikakosea. Napenda kuwa nao karibu wanafanya vizuri katika maisha yao na ndio maana hata ukiangalia sisi kwenye kundi la vijana tuna tabia tofauti tofauti lakini tunachofanya ni kuwaweka sawa tunahakikisha tunachokifanya kiko right ili wasije wakatujudge kwamba mbona wanaimba mambo mazuri lakini mbona maisha yao hayako hivyo…kwa hiyo vitu vingi tunaogopa kuvifanya mbele ya vijana na mbele ya jamii pia.

DOMOKAYA : Kwa upande wangu hata club kwenda siku hizi ni mara chache sana. Badala yake nazingatia kazi zaidi. Badala ya kwenda club na kujionyeshaonyesha kwa watu siku hizi naona ni bora nikae nyumbani nipractise mambo yangu nk. Hiyo ni sacrifice mojawapo kwa kijana kama mimi.

BC : Je ndoto yenu ni nini baada ya miaka kumi ijayo?

DOMOKAYA : Kikubwa tunachokifikiria sisi ni kuwa siku moja tuwe na bendi yetu yenyewe kama walivyokuwa The Wailers, watu wanaimba wenyewe sio hivi unavyoana wasanii wengi wanaanzisha mabendi, unasikia tuu fulani ana bendi yake lakini ukija kuangalia watu wanaopiga instruments ni watu wa kukodi tu.Mtu anakodisha watu wanaojua instruments wale wanaopiga miziki za kukopi halafu anaanzisha bendi yake.

Sisi tunataka kufanya kama vile The Wailers ambayo ni bendi ya kudumu.Wote mnakuwa wanamuziki kikweli kweli. Na hivi kwa sababu wenyewe tunajua tayari kupiga instruments mbalimbali na pia tunajua kutunga nyimbo nk tunaamini ndoto yetu itatimia siku moja.

BC : Asanteni Mandojo na Domokaya kwa muda wenu.Tunawatakia kila la kheri.

MANDOJO NA DOMOKAYA : Asanteni pia.

Advertisements
 

17 Responses to ““DINGI” NI KISA CHA KWELI-MANDOJO NA DOMOKAYA”

 1. Chief Says:

  Hao jamaa na wakubali kabisa hicho kifaa kinaitwa DINGi sio mchezo napenda jinsi wanavyopangilia sauti zao, wanatisha kwa kweli.

 2. gabriel Says:

  mziki (audio) ni mzuri lakini video ni takataka
  resolutions ni za chini mno,color correction kutoka scene na scene ni poor sana,haina utaalam woote wa angles mabalimbali yaani ipo dull kupita kiasi
  tena sijui hata kama wanamuziki wamefanyiwa make up!
  na costume hata kama ni gheto fabulous au hip hop kwa kweli ktk video hii ni takataka tuu!
  it’s too videoish! poor ,poor, quality! shida yetu hapa nyumbani tangu kuigia mapinduzi ya digital basi kila mwenue kikamera na computer basi anakuwa producer wa video na majina makubwa tuu kama ……productions,film works! nk jamani tukubali kwanza halafu tuache uswahili tukajifunze kwa wenzetu (watanzania)wanaofahamu mambo hayo vema ili tufanye video zenye ubora uliosimama
  waosha vinywa haya ni maoni yangu nionavyo mimi ,nayaheshimu pia maoni yenu ,sote tunaona kitu kimoja lakini ktk mitazamo tofauti
  akhsante

 3. Ally Says:

  hey baab kubwa domo na dojo mdogo mdogo cku 1 ndoto zenu zitatimia mtakuja kuwa kam mnavyotaka na kama anavyosema jamaa jaribuni kufanya na watu wanajua kufanya video sio mi nawakubali watu wangu sana dingi imekaa vizuri.

 4. Ally Says:

  halaf haya masaa mnayoandika comment imeingia ni ya wapi?

 5. TanzanianDream Says:

  Duuh ebana watz tunapenda mno kujisifia mradi tuonekane sisi ndio bora na tofauti…Embu Ona hii wamekutana 2002 wamerekodi 2003 n’ yet wamejiandaa kwa miaka takribani 2,mind u wamerekodi hiyo nikupe katikati ya mwaka 2003 sasa which is which?au SIJAELEWA?

 6. lili Says:

  kwa kweli hawa vijana wanajitahidi, Gabrieli una point hapo, lakini lazima ukumbuke dingi ni nyimbo ya zamani kidogo, kwahiyo kidogo kidogo watanzania wanajaribu kutengeneza video nzuri, wenzetu wameanza zamani sana, nenda kaangalie video za zamani za wenzentu za miaka 30s ndio ulinganishe. alafu Tanzani dream, wanachaojaribu kusema ni kuwa siku hizi vijana wana record nyimbo in a week. kwahiyo wao kuchukua mwaka mzima ku practice ni dili. kazi nzuri sana watoto, endeleeni na harakati.

 7. Dinah Says:

  Mimi binafsi napenda sauti zao kwenye nyimbo zao, kazi nzuri jitahidini mtafika mnakotarajia kufika na sisi tutajitahidi kupenda nakununua kazi zenu.

  BC Mika Mwamba, huyu jamaa anamchango mkubwa sana ktk muziki wa Bongo iwe wa kiruga (saida Kaloli), kwaya au bongo flava huyu bwana anastahili pongezi even Tuzo.

  Nakumbuka alipoanza kazi zake pale Gate way(makutano ya uhuru na mnazi mmoja)Ghorofa ya 3.Mnaweza kumpata ili tumsikie anasema nini kuhusu kazi zake na maendeleo ya muziki bongo kwa ujumla?

  Vinginevyo Kazi njema BC.

 8. mesa Says:

  i love u home boys

 9. muddy Says:

  Ally umesema kweli hata mimi masaa haya ya BC huwa yananichanganya sana!!

 10. Mpanduji Says:

  Mambo ya mashahiri hayo, ukisikiliza kwa makini, hawa vijana wanaelimu angalau ya form four kwani mashahiri yao si ya kuropoka tu; yana mpanglio wa vituo n.k.

 11. mankya nkya Says:

  big up my brothers they sing very very very very very very well hasa lile song la dingi duuh!!!!!!!!!!!!!!!! linatisha

 12. tumaach Says:

  big up dojo , kaya kazeni buti mazee

 13. mimmy Says:

  mimi kwa kweli nawakubali saaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaana mandojo na Domo yani, karibu kila nyimbo walioyotoa ni kali.

  cha kushangaza sijui kwanini hawavumi kama wajingawajinga wengine tuuu wanaobabaisha mziki.

  mi nafiriki imefika sasa, vyombo vya habari viache kuua vipaji kama hivi.

  TATIZO NI PROMO TU KWA MACHALII HAWA.

  mimi nawazimika sana.

 14. mimmy Says:

  Mimi kwa kweli nawakubali saaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaana mandojo na Domo yani, karibu kila nyimbo walioyotoa ni kali.

  cha kushangaza sijui kwanini hawavumi kama inavyostahili. utaona wajingawajinga wengine tuuu wanaobabaisha mziki ndo wanavuma.

  mi nafiriki imefika sasa, vyombo vya habari viache kuua vipaji kama hivi. viwape muda mwingi hewani. Lady J.dee kawa msanii mkubwa kwa nyimbo za kipumbavupumbavu tuu, hata Mr. nice pia. kwa nini isiwe wasanii hawa??????????????

  TATIZO NI PROMO TU KWA MACHALII HAWA.

  mimi nawazimika sana.

 15. polisi Says:

  big up bros.I like your unique stlye in music.u the best.
  Pamoja nanyi kama pua na mdomo.kama domo na dojo.
  yiiiiiiiiiiiiiiiiah.

 16. maasai boy Says:

  Nyiee! ! nyiee 1!ndo wachiziiiiiiiiiiiii weetu!

 17. neli wa ilala Says:

  ujue kitu kimoja,uwongo ni mbaya siku zote.nachojaribu kusema ni kwamba hao majamaa ni wakali sanasana.Mandojo na Domokaya keep givin us the hitssss men.ni mzuka.NJI WAKALI KUSHINDA HATA TINDIKALI.


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s