BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

JIJI LETU October, 5, 2007

Filed under: Serikali/Uongozi,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 9:01 PM
Tags: , ,

Zamani paliitwa Mzizima. Inasemekana kilikuwa ni kijiji kidogo tu cha wavuvi. Mwaka 1862 Sultan Seyyid Magid aliyekuwa mtawala wa Zanzibar akapependa kisha akapabadilisha na kupaita Dar-es-salaam yaani “Bandari ya Salama”. Baadaye wenyewe tukapaita “Bongo”. Leo hii nchi yetu inajulikana sana kwa jina hilo ingawa sio jina rasmi.

 

 

Mara nyingi ni vigumu sana kuzungumzia watu maarufu wa Tanzania(bongo celebrities) bila kulihusisha jiji la Dar-es-salaam kwa njia moja au nyingine. Wengi wamejipatia umaarufu wao wakiwa jijini Dar. Wengine wanadiriki hata kuliita New York ya Tanzania.

 

Ndilo jiji kubwa kupita yote na pengine tajiri kupita yote pia nchini Tanzania. Ni mojawapo kati ya majiji yanayokua kwa kasi sana duniani. Mpaka mwaka 1996 ndipo yalipokuwa makao makuu rasmi ya nchi yetu kabla ya kuhamishiwa Dodoma ingawa mpaka leo safari ya kuhamia Dodoma haijakamilika!

Zitazame picha hizi na uone kama unaweza kuyatambua baadhi ya majengo au mitaa. Kama upo nje ya nchi hivi sasa unakumbuka nini kuhusu Dar-es-salaam?

Picha zote kwa ruhusa na hisani kubwa ya Brian McMorrow.

Advertisements
 

6 Responses to “JIJI LETU”

 1. TanzanianDream Says:

  Home Sweet Home,Ebana BC +whoeve kaiweka hii Picha Much Respect Wakubwa mmenifanya nizidi kuipenda bongo…Pamoja

 2. fidelis tungaraza Says:

  Jeff,

  Kuna wakati huwa najikuta mawazo yangu yanagongana na mawazo yako kiajabu sana. Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa nikitafakari juu ya jiji la Dar es Salaam. Nadhani tafakuri hii ilitokana na baadhi ya picha ninazoziona mabloguni za majengo mapya jijini Dar es Salaam. Kila nikitazama picha za majengo mapya ya Dar huwa najawa na karaha badala ya furaha.

  Miongoni mwetu tumeshuhudia mabadiliko mbali mbali tangu enzi ya Dar ya wilaya tatu; Ilala, Temeke na Kinondoni. Dar ya enzi za DMT (Mabasi ya Leyland) hadi UDA (Ya Maikarusi na Scania) mpka daladala za makombi vicoaster, vihiace, na chai maharage.

  Tunakumbuka tangu ilipokuwa Kisutu, Kisutu hususani pale palipojengwa Chuo cha Elimu kwa Njia ya Posta. Palikuwa pana kijiji ambacho kilisawiri Sophia Town, Johanesburgh. Naikumbuka Kisutu ile iliyopakana na Maktaba Kuu ya Taifa, Makaburi ya Mabohora, Maskani ya Wahindi masikini wanaoishi nyumba za mabati nyuma ya shule ya Upanga, karibu na maskani ya Mississipi. Kisutu iliyokuwa inatazamana na Barabara ya UWT. Pale palikuwa Sodoma na Gomora. Uzinzi wa aina zote ulipatikana pale. Kadhalika ulevi wa kunywa na kuvuta, na hata mabwana fanya (hitman) walikuwa wanapatikana pale. Sikumbuki ilikuwa amri ya nani, kwa sababu gani, na chini ya uongozi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar sijui alikuwa Ndugu Muhavile au Rwegasira Kisutu ikabomolewa, bomoooohhh. Wakazi wake wakatapanyika kuelekea wanakokujua wenyewe. Wakazi wa Upanga, Kisutu, na hata kariakoo, Jangwani, na Magomeni wakahema pumzi ya auheni, puuuuu…Wakamshukuru aliyebomoa Kisutu kwa kuwapunguzia adha na woga wa majambazi na wezi, wasambazaji wa bange na gongo, na maasherati, makahaba na mashoga waliokuwa wananyang’anyana nao wake na waume zao. Nadhani baadhi ya makahaba walihamia Gerezani na wengine Kinondoni kwenye yale madanguro maarufu.

  Pia palikuwa na Kariakoo. Kariakoo ya Wazaramo, Wamanyema, Wanyamwezi, Waarabu, na Wahindi. Kariakoo palipozaliwa TAA na TANU na ndiyo iliyokuwa kitovu na kitivo cha ujanja na maarifa ya kijamii ya taifa. Kariakoo ya Pombe shop siku hizi DDC Karikoo na Soko jipya. Kariakoo ya Hayati Mwamba Majuto wa Simba Sports Club, Tabu Mangara wa Dar Young Africans (Yanga), Mansur Magram wa Cosmopolitan, na Shiraz Sharif wa Pan African FC.

  Palikuwa na city centre iliyosheheni ikulu, wizara na idara kuu zote za nchi. Centre ya maraha ya kumbi za sinema; Empire, Empress, Avalon, New Chox, Odeon na Cameo. Na migahawa, baa na kumbi za muziki: Emms Hotel iliyoungua/zwa moto, Cosy Cafe, Mbowe hotel, na Magot kwa Watanzania wa kawaida. Kwa Watanzania wasio wa kawaida na wageni Kilimanjaro Hotel na New African Hotel na Mawenzi Hotel na Motel Afrique na Motel Agip. Na Skyway Hotel kwa makahaba wa bei ghali kidogo ukilinganisha na wa Kisutu.

  Kigamboni kulikuwa na Wazaramo na Wasukuma wakulima na wauza maembe dodo na mazao mengine ya msimu. Palipokuwa na kitalu cha kuotesha na kuendeleza itikadi za siasa za ujamaa na kujitegemea. chini ya uongozi wa kina Ndugu Daudi Mwakawago, Pius Msekwa, John Mhavile, Bismark Mwansasu na wengineo. Vivuko vya Usiwe Kupe na Ukombozi vilikuwa bure na ukumbi wa dansi ulikuwa Flamingo Bar na CCM. Si Kigamboni ya leo. Palikuwa na Feri(Lebanoni), Utani(Kwa Marehemu Gwachemara) na bageji room palipokuwa kitivo na kitovu cha mastorowei.

  Kuna mji mkongwe wa Upanga kabla hujafika Faya ambapo ndipo ulipo mpaka na mjini na ambako ndiyo mpaka wa kujichanganya na Wahindi. Baada ya kuvuka daraja la Mowlem na Mecco unafika mji mkongwe wa Magomeni(Mapipa, Kota, Mikumi, Mwembechai na Manzese(Soweto). Halafu Ubungo, Kimara na Mbezi ya Savanah, Jambos na Safari Resort kwa Hugo Kisima palipozaliwa Masantula Ngoma ya Mpwita, Dukuduku na Ndekule. Upande wa pili Chuo Kikuu; Mlimani Park na Silent Inn na kwa Askofu Kakobe na Mwenge kwa wachonga vinyago. Na mji mpya Sinza. Kasehemu kadogo kanakogida maelfu ya lita za bia kila siku! Kenye nyumba kadhaa za “kulala wageni”.

  Na kule kwingine kulikuwepo Kurasini, Chang’ombe, Temeke, na Sabasaba. Huko ndipo palipokuwa na Uwanja wa Taifa na chimbuko la bendi maarufu za STC, Safari Trippers na Afro Sabini. Na ile guest house nzee ya wanaume(rumande!!!) Keko.

  Kulikuwa na Kigogo, Msimbazi, Ilala na Buguruni. Halafu na Yombo, Kipawa, Vingunguti, Gongolamboto na Ukonga paliposheheni zaidi Wajaluo, Wakuria na wageni wengine toka mkoa wa Mara. Huko ndipo ulipo Uwanja wa ndege, jeshi la anga, na godown wanaposwekwa watuhumiwa la Ukonga na siku hizi Segerea (Sijui kwa nini jela zinajengwa maeneo ya kule?). Na maskani ya mwanamke wa Shoka Mama Martha Wejjah aliyemtoa nishai mwenye wa Kizaramo(Huyu Mama namzimia kinoma).

  Bila kusahau Kinondoni na Mwananyamala. Kinondoni, kuna sehemu zingine sijui vipi? Kinondoni kuna Makaburi maarufu, shule ya Muslim, soko la MaTX na pale kwa yule shangazi yetu fulani mwenye danguro la muda mrefu. mitaa ya ushuani Oyster Bay na vitongoji vyake Msasani, Regent, Ada Estate, Mikocheni, Mbezi Beach na kwingineko. Wanasemaga pamefanana na ulaya!

  Tafadhali naomba unichomekee kile kibao cha Mtoto wa Mjini cha Kikumbi Mwanza Mpango Mwema, King Kiki bwana mkubwa milioni ndiyo kitatupa picha nzuri ya jiji. Namkumbuka rafiki yangu mmoja Marehemu Chilo aliwahi kuniambia “..Nimekamata Bayankata(UDA)toka central mpaka Paselepa(Mwenge).

  Mwisho napenda kuwashukuru wenyeji wa jiji hili Wazaramo kwa moyo wao mkunjufu wa kutukaribisha na kutukirimu wageni wote tulio na tusio na shukrani. Kadri siku zinavyoenda tunazidi kumsukuma nje ya jiji lake kwa hadaa ya pesa na nyumba mpya nje ya jiji la Dar es Salaam.

  Jiji letu limeingia kile Rais Nelson Mandela anachokiita “..Modern face with primitive heart..”

  Ni Miye maridhiya,

  f m Tungaraza.

 3. Mavuto Says:

  Watu wengi wanayachukulia majengo ya kihistoria kama utajiri mkubwa wa enzi. Ni ushahidi wa kihistoria na mitindo ya maisha waliopata kuishi waliotutangulia mbele za haki. Hiyo yote ni ili tupate kujua wapi tulikotokea na wapi tunaenda.Asiye na historia mtumwa!.

  Wengine wanahisi kwamba, majengo hayo yaliyopata kuwa ya kisasa wakati fulani, ni utajiri wa kihistoria wa aina ya watu waliopata kuishi mahali hapo. Pia vielelezo vya utamaduni vya hao walioyajenga na kwamba wanastahili heshima na hata kupongezwa. Na sio kulaaniwa kwa kuyabomoa na kuyaita uchafu, kwa kauli za hadaa ithibati “Nyundozzz”.

  Kwa maoni yoyote yale, inaonekana waziwazi kwamba katika historia nzima jamii nyingi zilifikia hatua ya maendeleo ambayo ilitokana na ubunifu wa majumba, ambayo wenzetu wanayatunza kwanini sisi tumekuwa mafundi wa kubomoa, ilhali kujenga kunatushinda?.

  Naam! haiba na historia ya Mzizima au Azania inazidi kudidimia. Ukiangalia kwa makini hazina ya jiji la Mzizima au Dar kama linavyojulikana na wengi, inazidi kupotea. Agharabu, hakuna jitihada za maana zinazoonekana kuokoa kile kidogo tulichobaki nacho tunachoweza kujivunia kama historia ya wapi tulipotoka ili wanetu wajue wapi tunapokwenda.

  Dar ni mji mkuu (kama utapenda kuuita hivyo)wa pekee katika miji ya Afrika mashariki na kati,ambao una hazina ya majengo kuanzia enzi ya Mwarabu, Mjerumani na Mwingireza.

  Wenzetu Kenya, Uganda, Congo, Kigali na hata Burundi hawana bahati hii ambayo sisi tunayo. Sio rahisi kukuta kwenye nchi hizo majengo yaliyobeba historia nzito ya Taifa kama ilivyo Dar kwa majengo ya Ikulu, Makao Makuu ya Magereza, Hospitali ya Ocean Road, Chuo cha Utalii,Mahakama ya kuu na ya rufaa, Ofisi za Ardhi na Ramani, jengo la forodha, Posta ya Zamani na hata jengo marehemu la Saramander ambalo kilichotokea kitabakia kuwa aibu ya kitaifa kwa miaka dahari ijayo.

  Ni fedheha na utani wa ajabu kwa jiji lililo na historia hiyo, ‘Nyundozzz’ kuwa msamiati wa kuvutia. Ni aibu ya ajabu kwa jiji lililo na siha njema kihistoria, kuonekana halina umuhimu wowote hasa kwa wapenda fedha wenyewe wanawaita ‘wawekezaji wazalendo’.

  Hii ni kuendelea kuvunja hazina zetu ni kuendelea kuchefua nyoyo za Watanzania na kuzidisha simanzi za wengi kwani majengo ya BOT (Minara ya aibu), Mafuta House na mengineyo, chanzo cha pesa zake za ujenzi sio tu zinaondoa picha mbaya ya majengo hayo bali inazidisha uchungu wa wananchi kwa kuwa majengo hayo ni kielelezo cha ufisadi usiomithirika. Inasikitisha kuona ufisadi huo ukibatizwa jina na kuitwa kielelezo cha maendeleo!. Ni nani asiyejua mapesa ya wezi wa mali za umma ndio yanatumika kujengea majengo hayo, ama kwa kuhalalisha wizi au kusafishia pesa haramu?.

  Mavuto

 4. Samahani, natoka nje ya somo!

  Njoo tumalizie kujadili kipengele, ili tuende kwenye hatua nyingine ya kuboresha wanajumuiya wa jumuiya ya Watanzania wanao tembelea au wanao blogi.

  Tembelea hapa : http://blogutanzania.blogspot.com/
  ilia tumalize kujazia dondoo ili tu anze na kipengele kingine.
  Idumu JUMUWATA!

 5. gabriel Says:

  kwa kweli mti mkubwa umeeleza ktk retrospect nzuri sana ya ki-documentary ,tena ni perspective ya kijana wa mjini wa miaka ile .
  ee bwana hiyo retrospect yako yaani iko very visual!
  nimeipenda sana
  mimi najifunza sinema hapa canada
  nataraji siku moja kufanya documentary feature film ya dsm .nitakutafuta nitapata contact zako kwa tunga
  kila la kehri
  Loh sitasahau -paselepa-mwenge

 6. chuma Says:

  Mimi hata jiji hili likikua kama newyork, haitanipa utamu wowote ule.
  It is an artificial expression of the real life of a tanzanian, nenda kilometa ishirini utaona watu ambao hawajui watakula nini jioni.
  Maisha ya miji yanatakiwa yaende sambamba na yale ya shambani, isiwe kama hapa nigeria,ukivuka lagos kilometer 20 utaona watu wasiovaa viatu. ni nini hiyo?


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s