BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“UHUNI NI TABIA YA MTU”-AISHA MADINDA. October, 16, 2007

Filed under: Muziki,Sanaa/Maonyesho,Utamaduni,Wachezaji — bongocelebrity @ 10:38 AM
Tags: ,

Leo hii anaaminika kuwa mnenguaji wa kike maarufu kupita wote nchini Tanzania hususani katika muziki wa dansi. Ubunifu,uwezo wake katika kunengua na kujituma vilivyo awapo jukwaani inasemekana ndio siri ya mafanikio yake.

 

Huyu si mwingine bali ni Aisha Mohamed Mbegu maarufu kwa jina la Aisha Madinda, mnenguaji tegemeo wa bendi ya African Stars ’Twanga Pepeta’. Alijiunga na bendi hiyo mwaka 2001.Umaarufu huo ndio umemfanya Aisha Madinda awe mnenguaji au mcheza show ambaye huongelewa zaidi mitaani na pia kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania.

Hivi karibuni tulipata fursa ya kufanya naye mahojiano kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo kuhusu maisha yake binafsi,mipango yake ya baadaye nk.Pia Aisha anajibu kuhusu shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikimzunguka kama vile matumizi ya madawa ya kulevya,upigaji wa picha za uchi nk.Ukweli uko wapi katika yote haya? Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Unaweza kutuambia historia ya maisha yako kwa kifupi?

AM: Jina langu kamili ni Mwanaisha Mohamed Mbegu a.k.a Aisha Madinda. Nimezaliwa hapa hapa jijini Dar-es-salaam tarehe 5 mwezi wa 5 mwaka 1979. Nimekulia mkoani Kigoma. Nimesomea shule ya msingi pale pale Kigoma kwenye shule moja inaitwa Kiganamo.

 

BC: Ingawa ucheza show ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine, mara nyingi umekuwa ukihusishwa na uhuni au umalaya. Unadhani hii inatokana na nini na una ujumbe gani kwa watu ambao bado wana mtizamo huo?

AM: Mimi ningependa kuwaambia watu wenye mtizamo wa namna hiyo kwamba uchezaji show au sanaa yeyote sio uhuni. Uhuni ni tabia mtu na uhuni sio kwamba wachezaji show peke yao ndio wahuni kwani kuna watu ambao sio wacheza show na ni wahuni.Kwa ufupi uhuni, umalaya au wizi na tabia zingine zote mbaya kwenye jamii zinatokana tu na tabia ya mtu binafsi na sio kwa sababu zinginezo. Kwa hiyo ningependa kuwaambia wapenzi wa muziki waichukulie sanaa ya uchezaji show kama sanaa zingine zozote.

BC: Kwa mtizamo wako, umahiri wa kucheza show unatokana na mazoezi au kipaji cha kuzaliwa nacho?

AM: Nadhani kwa upande mkubwa zaidi ni kipaji. Nasema hivyo kwa sababu unaweza ukafanya sana mazoezi na usiweze kucheza. Lakini mazoezi pia yanachangia na ni muhimu.

BC: Kama zilivyo shughuli zingine za kisanii, kuna wakati utafika ambapo huna budi kustaafu na kuwapisha wengine. Nini mipango yako utakapostaafu? Je ukweli huo unakutia mashaka kwa namna yoyote ile?

AM: Mipango yangu ya baadaye hapo nitakapostaafu ni kufanya biashara zangu. Ila kutegemea na mambo yatakavyokwenda ningependelea pia kuanzisha shule ambapo nitakuwa nikiwafundisha dancers chipukizi ambao wangependa kujifunza zaidi kuhusu sanaa hii ya uchezaji show au muziki. Hii nadhani itatoa fursa nzuri kwa wengine kufuata nyayo zangu.

Kwa upande wa kipengele cha swali lako la pili; hapana hilo halinitii mashaka kwani naamini nitaamua kustaafu kwa uamuzi wangu mwenyewe na pia ni kwa sababu najua kabisa hata hivi leo kwamba uchezaji show una mwisho wake. Siwezi kucheza show mpaka nikiwa na labda miaka hamsini hivi. Kingine ni kwamba hivi sasa nimeshajipangia kwamba nikifikisha miaka 30 nitaachana na mambo ya muziki kwa mtindo ninaofanya hivi sasa. Nadhani huo utakuwa ni umri muafaka kuwapisha wengine.

 

Aisha Madinda(kushoto) akiwa na mnenguaji mwenzake Lilian Joseph Tungaraza aka Internet

BC: Ulijisikiaje baada ya zile habari za picha zako za uchi ingawa baadaye ilithibitika kwamba hazikuwa zako?

AM: Kwa kweli nilijisikia vibaya sana kwani ni kitu ambacho sikuwahi kutegemea na kwa hiyo ilikuwa ngumu hata kuamini kama mtu anaweza kufanya vitu kama vile. Nadhani mtu aliyefanya vile alikuwa na nia ya kuniharibia jina na sifa mbele ya jamii na hata kwenye familia yangu na hivyo kunimaliza kisanii. Ni kitu kilichoniuma sana na kunisikitisha sana. Sintokaa nisahau tukio lile katika maisha yangu. Hata hivyo nilifarijika kidogo watu wa baadhi ya magazeti walipompata msichana halisi aliyekuwemo katika zile picha ambapo akaelezea jinsi gani picha zile zilipatikana. Nilimsikitikia pia hata yeye kwani nasikia alikuwa ni mchumba wa mtu na kwamba anasema picha zile alizipiga akiwa tu na rafiki zake lakini kwa bahati mbaya simu iliyotumika kupiga zile picha ikapotea. Aliyeipata hiyo simu ndio akaamua kuzisambaza kwa kutumia jina langu. Sijajua kwanini.

BC: Ulijifunza nini kutokana na tukio lote lile kwa ujumla?

AM: Cha msingi nilichojifunza ni kuwa makini zaidi na watu walionizunguka. Pia kuepuka na mambo yanayohusisha vitu kama kamera hivi kwa sababu huwezi jua zinaweza kumfikia nani. Nasema hivyo kwa sababu nina uhakika kama yule mtu aliweza kufanya vile,siwezi jua hivi sasa anajaribu kuniharibia jina langu kwa namna gani.

BC: Siku hizi wewe sio tu mcheza show bali pia mwimbaji katika muziki ujulikanao zaidi kama muziki wa kizazi kipya. Nini kilikuvutia kuingia kwenye uimbaji pia? Mpaka sasa mambo yanakwendanje kwenye uimbaji?

AM: Kwanza ni mapenzi yangu katika uimbaji. Napenda sana kuimba. Pili ni kwamba nikiwa na vitu viwili, yaani uimbaji na uchezaji, nitakapostaafu kucheza kwa mfano ninaweza nikaendelea na muziki kwa upande wa uimbaji. Yote inatokana na ukweli kwamba muziki uko kwenye damu na muziki ndio umenipa jina na maendeleo yoyote niliyonayo mpaka sasa hivi.

Mpaka sasa mambo sio mabaya ingawa bado nasaka mdhamini ili niweze kumalizia kutengeneza albamu yangu ambayo ndio itakuwa ya kwanza. Kama nitapata mdhamini natarajia kuitoa mapema iwezekanavyo.Vinginevyo nitaendelea kuitengeneza taratibu taratibu tu kama nifanyavyo hivi sasa.

 

BC: Kama mcheza show na kwa namna unavyocheza ni wazi kwamba mara nyingi huwa wanatokea wanaume mbalimbali ambao wanajaribu kukushawishi au kukutaka kimapenzi. Huwa unakabiliana vipi nao?

AM: Ni kweli unavyosema. Kwanza kabisa ni kwa kujiepusha nao kwa sababu kwanza mimi nina mtu wangu tayari. Pili mimi ninapokuwa stejini ninakuwa nipo kazini. Nikitoka pale ninarudi zangu nyumbani kupumzika. Kingine ni kwamba mimi sina makundi makundi zaidi ya kundi langu mimi na wanamuziki wenzangu. Nikitoka kazini ni nyumbani. Kwa hiyo naepukana nao vizuri tu bila matatizo.

BC: Unadhani nini faida na hasara ya kuwa mtu maarufu?

AM: Kwa upande wa faida ni kwamba vipo vitu vingi sana ambavyo hivi leo nimeweza kuvipata kutokana na umaarufu kupitia kazi yangu ya muziki. Namshukuru mungu kwa hilo. Hasara ni kama unaposingiziwa mambo ambayo sio ya kweli kabisa kama hilo la picha za uchi. Ni mambo kama hayo.

BC: Aisha naomba sasa tuweke mambo fulani sawa hapa. Kumekuwepo na habari kwamba wewe ni mtumiaji mzuri wa madawa ya kulevya. Je habari hizo ni za kweli? Je labda ulishawahi kutumia madawa ya kulevya siku za nyuma?

AM: Hapana kabisa. Kwa kweli habari hizi mimi pia nazisikia na zinanisikitisha na kunishangaza sana. Nadhani habari kama hizi ndio hasara ninazozizungumzia za kuwa mtu maarufu. Mimi binafsi madawa ya kulevya siyajui hata yanafananaje. Sijawahi hata siku moja kutumia madawa ya kulevya na wala sina mpango huo.

BC: Katika shows zote ambazo umeshawahi kufanya mpaka hivi sasa, ndani na nje ya nchi, ipi ambayo unaikumbuka zaidi?

AM: Kwa ujumla show zetu zote ni nzuri. Kila mara watu wanakuwa wengi na tunapokelewa vizuri na mashabiki wetu. Pamoja na hayo show ya uzinduzi wa albamu ya “Mtu Pesa” naikumbuka zaidi na pia show tuliyowahi kufanya jijini Amsterdam nchini Uholanzi nadhani zilitia fora.

 

BC: Unalo lolote ambalo ungependa kuwaeleza wapenzi wa uchezaji show wako na pia muziki wako?

AM: Ningependa tu kuwaambia wacheza show wenzangu wakaze buti na wasijibweteke.Wafanye sana mazoezi na wafanye kazi zao kwa ustadi kama nifanyavyo mimi. Pia wakiwa kazini wasionyeshe kuchoka bali waonyeshe ujuzi wao kwa bidii zao zote. Bidii zangu mimi ndio zimenifikisha hapa nilipo.

BC: Swali la mwisho. Je umeolewa au una watoto?

AM: Bado sijaolewa ila nina mchumba. Nina watoto wawili,mmoja anaitwa Side na mwingine Naomi.

BC: Asante sana Aisha kwa muda wako. Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.

AM: Asanteni nyie pia kwa kutambua mchango wangu katika sanaa ya uchezaji show.

Advertisements
 

32 Responses to ““UHUNI NI TABIA YA MTU”-AISHA MADINDA.”

 1. mesa Says:

  honera sana mahojianao mazuri ila hao watoto ni wa fikiri madinda au mwingine?

 2. mesa Says:

  Dinah uwapi umelala nasubiri point zako mama kazi njema na BIG UP

 3. Dinah Says:

  Mesa nilikwenda Doha kula Eid 🙂

  Aisha wewe bonge la mnenguaji keep it tight mamaa, (wewe mmanyema nini? hehehe mana’ke wale dungu zangu matata sana kwa viuno) nimefurahishwa na ujibuji wa Msanii huyu,inaonyesha katulia kumkichwa.

  Kweli uhuni ni “choice” ya mtu ambayo huizoea nakuwa tabia, uhuni sio unenguaji(kazi), mavazi au muonekano n.k so anybody can do it 4 a reason (uchumi, upweke, ujinga au kutafuta attention).

  Kazi njema binti Madinda…..fanya yote ila kumbuka Kujipenda, jali, tunza na thamini utu wako.

  BC kazi nzuri!

 4. TanzanianDream Says:

  “Uhuni ni tabia mtu na uhuni sio kwamba wachezaji show peke yao ndio wahuni kwani kuna watu ambao sio wacheza show na ni wahuni.”

  Mwenye akili yeyote anaelewa hayo maneno maana yake i wish lisingekuwa jibu la swali husika ila ndo jibu lenyewe……

 5. maya65 Says:

  neno “uhuni” lina maana gani kwa kiswahili?
  je mwajua asili lilikotokea?
  malaya ni muhuni,mvuta bangi ni muhuni,basha ni muhuni,ukitukana hovyo ni muhuni,ukivaa mavazi yasiyo na heshima ni muhuni,ukisema uongo ni muhuni, tapeli ni muhuni….sasa uhuni unaoongelewa hapa ni uhuni gani?
  kwa lugha ya kichina “hun” ina maanisha mtu asiyekuwa na kazi maalum ya kufanya au mzurulaji….sasa kiswahili je? ni maana ipi ya “muhuni” inayozungumzwa na Aisha Madinda?
  haya mwageni sera zenu!!!!!

 6. Manda Says:

  Mdau Kichina? Mandarin au kichina kipi unaongelea mdau maana sie tuko china na hilo hatulijui.
  Haya

 7. maya65 Says:

  manda…pole kama hujui neno “HUN” hii ni mandarin…
  mimi nilisoma beijing mwaka 1990 hadi 1995 na nikaishi huko miaka 8 baadaye!!!! nilikuwa peking language and culture university…..any way kama hulijui hili neno si kosa lako maana lugha huisomi darasani peke yake, inabidi ujichanganye na wenyeji!!!
  any way tuwasiliane mimi bado niko huku huku Asia nicheck kupitia : present40stone@esnips.com

 8. nusrat Says:

  kazi ni kazi dada, bora mkono uende kinywani, unenguaji ni fani kama zilivyo fani nyingine, aisha keep it up!! bora kunengua kuliko kuwa changu, cha msingi akili kichwani mwako tu maana ukweli ni kwamba wanenguaji wanapata tabu sana kutoka kwa mijitu yenye tamaa, lakini dada utachotakiwa kufanya ni kuwa na msimamo wako katika maisha maisha. KEEP IT UP DADA!!!!!!

 9. scholastica Says:

  kazi ni kazi tu bora maisha dada aisha usihofu piga kago mtu wangu majungu ni kitu cha kawaida kwa walimwengu mi mwenyewe ile picha ilinishtua sana

 10. Dinah Says:

  Uhuni maana yake ni kama ulivyosema maya Ila ktk jamii watu hutumia neno hilo kama ustaharabu lakini wanamaanisha “malaya”.

  Kwa case ya Aisha wakisema muhuni wanamaanisha Malaya.

 11. Kenny Says:

  Asante Dinah nilitaka kumjibu maya65, naona umjibu barabara. ongeda bidd binti wa watu,kazi unayoifanya ni kazi ya kawaida tuu, piga buti, mambo yako yatakuwa mema muda si mrefu.

 12. Dinah Says:

  TanzanianDream(nimecheka); unajua uwezo wa kujieleza ni kipaji sio kila mtu anajua kujieleza ili aeleweke na pia kiswahili ni kigumu japo ni Lugha ambayo tunaizungumza kila leo.

  Nafikiri Binti Madinda alimaanisha kwanini wacheza show peke yao wadhaniwe kuwa malaya(wahuni) wakati kuna watu kibao sio wacheza show na ni Malaya wa kutupwa.

  Mtu yeyote mwenye upeo na mstaarabu atakuwa kaelewa nini huyu binti amemaanisha.

  Chukulia kawaida 🙂

 13. Mr Tom Says:

  Kwanza niwapongeze wote waliochambua kwa ufasaha maana ya jumla ya neno mhuni.Kwa mtizamo wangu mdau wa uchina Maya ulichanganua vizuri sana maana ya neno mhuni,japo sasa sikuelewa kwa nini tena umehitaji msaada wa tafsiri ya neno mhuni.Maelezo yako yanajitosheleza kabisa kuelezea maana ya hilo neno uhuni.Kimsingi nakubaliana nawe kwamba neno hili linabeba maeneo mengi sana kama ulivyofafanua.Sina haja ya kurudia.Ila kwa maana ya mada iliyopo kuhusiana na majibu mazuri sana ya bibie Aisha kuhusiana na suala la wanenguaji kuhusishwa na uhuni,kimsingi nakubaliana kabisa na wadau wengine ambao wamefafanua kwamba alichokuwa akimaanisha bibie Aisha ni uhuni uliopo katika eneo la umalaya.Sasa,mimi naweza kuwa na maoni tofauti kidogo.Kwanza siamini kabisa kwamba unenguaji kama fani yenyewe ilivyo ni uhuni(umalaya).Hilo sio kweli,ni fani kama zilivyo fani zingine.Hatahivyo,pia siwezi kukataa kwamba wapo wenenguaji ambao kwa namna moja ama nyingine hutumia fursa hiyo ya fani ya unenguaji kutimiza haja zao.Hilo liko wazi.Sina tatizo na Aisha,ninamfahamu kwa tabia akiwa tangu binti mdogo.Ni mwanafunzi wangu katika hiyo shule ya msingi aliyosoma.Wakati huo nilikuwa nikichukua mafunzo ya ualimu kwa vitendo(BTP) nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa 2 Kasulu Teachers College.Wakati huo alikuwa STD VI-V11(1990-1992).Alikuwa binti mtulivu mwenye kujiheshimu.Anyway,najua binadamu anaweza badili wakati wowote.Sasa hilo halinihusu maadamu sijamshudia akifanya vitendo vya kuonyesha kubadilika,achilia mbali uzushi wa jumla jumla usiokuwa na uthibitisho na pengine wenye lengo la kupakana matope.Hilo ni jambo la kawaida katika maisha ya binadamu kwani hat viongozi wakubwa na watu wenye heshima zao huzushiwa mambo.Sasa ninachotaka kusema hapa ni kwamba inawezakana kabisa pia kwamba wapo wasanii(wanenguaji) wanaoshiriki vitendo vya kihuni(umalaya) kwa lengo la kukidhi haza zao na hivyo kuipaka matope fani ya unenguaji.Lakini pia la muhimu zaidi ni kujiuliza kwanini wanafanya hivyo? Kama unenguaji ni kazi kama kazi zingine kwa nini basi baadhi yao wasiridhike na hiyo kazi? Hapa kuna majibu mengi.Wengi wamezungumzia tabia,hata bibie Aisha nadhani amesema hivyo,sina tatizo na jibu hilo.Maana kama wadau wengine walivyochangia,ni kweli hata wafanyakazi wa fani zingine wanaweza kuwa wahuni(malaya).Lakini katika kufanya utafiti wowote ule kimsingi unaangalia ni kundi lipi linaandamwa na tuhuma husika.Sasa ni kwa nini tuhuma za uhuni(umalaya) zinaelekezwa kwa wanenguaj( wanawake maana kuna wanenguaji wanaume pia)? Kimsingi hii ni mada ndefu.Lakini kifupi mimi kwa mtizamo wangu napenda pia nielekeze lawama kwa wamiliki wa bendi na vikundi vingine vyenye fani hiyo.Kwa nini? tuonane kesho,nakimbilia darasani….
  Mr Tom,Bowling Green State University,Ohio-USA(mwasata@bgsu.edu)

 14. maya65 Says:

  kwa mantiki hii ina maana kuwa “uhuni” ni umalaya…poa nimewaelewa
  master key kwa kiswahili huitwa ufunguo “malaya” ina maana ni “ufunguo wa kihuni”!!!!!
  haahaahaaaaa…..mambo hayo!!!!

 15. lee Says:

  Kazi ni kazi da Aisha ili mradi mkono uende kinywani. Kuna ubaya gani mtu kutumia raslimali yake kwa njia sahihi ili kujipatia rizki? Mbona hao wanaokaa na kutembea uchi kwenye majukwaa kwa kisingizio cha u-miss nanihii sijui hawasemwi? Malaya ni mtu (mwanamke au mwanaume) ambaye kwa ufupi anagawa uroda kwa watu chungu tele,iwe bure au kwa kujipatia kipato. Sasa mtu kunengua jukwaani, kamgawia nani? Uhuni! Nani kasema kunengua uhuni! Sasa tusemeje kuhusu hawa wanaume wazima wanaotumia sehemu kubwa ya siku mbele ya vioo wakijipodoa na kujiremba ili mradi wapendeze kuliko hata dada zao!! Hao wanaume wenye vipini vya pua na hereni nzito masikioni!! Da Aisha…kama JB Mpiana…’pesa mokongo tanda biloko ,toleka…pesa bango lopeleeee..’ lete raha..

 16. gabriel Says:

  hivi jamani hakuna wachezaji au waneneguaji wa muziki wa dansi kama mnavyowaita wa KITANZANIa?
  mimi binafsi inanishangaz sana blog kama hii inapooona ni fahari kupromoti wanamuziki au muziki au bendi za KIKONGO KAMA VILE TWANGA PEPETA.WANMUZIKI WAKE WANATIA KINYAA ,ASK ME WHY? KWA SABABAU WAMEDHIHIRISHA KWETU SOTE KWAMBA WAO HAWANA VIPAJI VYA KUDANCE AU KUFANYA MZIKI WA KITANZANIA .MBAYA ZAIDI WATU WENYE UFAHAMU KAMA HAWA WENYE HII BLOG NAO WANSHABIKIA HILO NA KUWAPA PUBLICITY NA MISIFA MIINGI ! LOH! INASIKITISHA SANA !

  ASIHA MADINDA ,LET ME GET TO THE BOTTOM OF THE ISSUE ,MY SISTER IF I HAVE TO CALL YOU, UNAFANYA KAZI KWELI KWELI TENA YA NGUVU SANA NA KUTOKA JASHO SAANA MWENYEWE UKIFIKIRI KWAMBA ARTISTICALLY YOU’RE ON TOP OF THE BUZZ.
  LAKINI UKWELI MIMI BINAFSI NAKAUONA HUNA VISION HUNA FOCUS NA HUNA UBUNIFU KISANII(WEWE UKIWA KAMA MTANZANIA MZALENDO)
  UNACHOJARIBU KUFANYA NI KUANGALIA TAPES ZA MUZIKI WA CONGO NA KUIGA TENA KWAW NGUVU ZOOTE ILI UCHEZE KAMA WACHEZAJI AU WANENGUAJI WA KOFI OLOMIDE,NA WENGINE WENGI TUU WANENGUAJI WA BENDI ZA KIKONGO.
  AISHA UNAJITAHIDI SANA KUNENGUA KAMA MKONGO VILE
  HAKAIKA HUU NI UPUMBAVU NA NI USHENZI HUNA LOLOTE HIYO MIGONGO YENU MNAYOJIFANYA KUJISIFIA NAYO NI STAILI YA KIKONGO ! UNABISHA?
  UNAJISIFIA KWA USANII UPI DADA? WA KIKONGO?
  NGOJA NKUELEZEE DADA YANGU ,KITU KIMOJA KTK HISTORIA YA SANAA YOYOTE ILE HAIJAWAI KUTOKEA MSANII YEYOTE YULE AKAPATA MAFANIKIO NA KUKUMBUKWA NA HISTORIA YA SANAA KWA SABABU YA KUIGA SANAA ZA WENGINE ,KAMA YUPO BASI WADAU MNIAMBIA ,KWA KUIGA UTAVUMA LEO KESHO HAUPO NA HISTORIA INAKUSAHAU COMPLETELY.
  AISHA MADINDA NA WENZEKO WA TWNAGA HAMANA NYIMBO NINYI SASA MIMI KAMA MTANZANIA NITAJIVUNIA NINI KUTOKA KWENU LABDA UNIAMABIA .NITAONA TOFAUTI GANAIA KATI YA UNENEGUAJAIA WAKO NA ULE WA ACUDO.FM ACADEMIA AU HATA ULE UNENGUAJI WA KOFI OLOMIDE.
  HIVI LEO HII IKITOKEA MMEALIKWA KUPERFORM HUKO PARIS (NFANO)PALE ZENETH,NA KOFI NAYE AKAALIKWA KUPERFORM NA BENDI YAKAO WAKASEMA BENDI KUTOKA TANZANIA NA BENDI KUTOKA CONGO,MBELE YA HALAIKI YA WATU MAKUMI YA MAELFU HIVI MTASUBUTU KUNEGUA AU HATA KUPIGA HIZO SBENE FEKI MBELE YA WENYEWE .ORIGINALS .SITOSHANGAA KAMA MKIZOMEWA NA KURUSHIWA MAWE!
  AISHA WACHA UJINGA NI WAKATI MZURI SASA UJIULIZE:

  HIVI NI NINI SABABAU YA KUNENGUA KIKONGO?

  MPAKA LINI NITAENDELE KUNENGUA MAMABO YA MOPAO?

  NINI TOFAUTI YANGU NA WANENGUAJI WA KOFI AU HATA FM ACADEMIA?
  JE MANUFAA GANI NITAPATA KWA KUJITAHIDI KUWAFIKIA WACONGO KIUNENGUAJI?

  JE NI MUHIMU KWELI KUTAFAKARI HILI SUALA LA STAILI ZA UNENGUAJI?

  KWA NINI SIWEZI KUBUNI UNENGUAJI AMBAO PURELY UNATOKANA NA STAILI ZA KITANZANIA?

  NI NINI FUTURE YANGU KATAIKA ZAMA HII YA CHOREOGRAPHY?

  MBONA SOUTH AFRIKA WANA DANCE KI-KWAITO,KIZULU NA MBANG’ANG’A NA HAWAIGI WACONGO NA WANAUZA BIG TIME?

  HIVI MIMI AISHA NI KWELI NINAIGA WACONGO KIUNENGUAJI AU NINANEMGUA KITANZANIA NA NINI FAIDA NA HASARA ZA KUENDELE KUNENGUA KIKONGO KWA MAISHA YANGU KITAALUMA NA YA WANMUZIKI WENZANGU?

  PIA MWISHO KWA KUONGEZEA NIMEONA SHOO ZENU NYINGI TUU KWAW KWELI NASIKITIKA KUSEMA CHOREOGRAPHY YENU HAINA U-PROFESSIOMALISM YAANI SHOO ZENU ZINA ONEKANA SO AMATEURISH KUANZIA COSTUME , HATUA MPAKA EMPATHY AU EMOTIONS KAMA UKIPENDA MANNEGUA TUU KUJITAHIDI KUWA WAFIKIA WENYEWE WACONGO LAKINI KUNA UPUNGUFU MKUBWA SAANA WA PROFESSIONAL APPEAL KWA UJUMLA
  AISHA HEBU JIULIZE HIVI NI KWA NINI UTAKUTA MWANAMUZIKI ANAIMBA TUU BILA VYOMBO WALa kucheza lakini umati huko wako hoi hysterical na wengine wanalia machozi ya furaha kwa sababau ya shoo ya mtu mmoja tuu bila kucheza au sebene .hapa ninamaana kwamaba kucheza shoo ni zaidi ya unenguajai kwa nguvu inahusisha pia ni jinsi gani unvyoingia hatau baada ya hatua bila kuonyesha wasiwasi wa kukosea au kaungalia jirani yako anenda hatua gani .yaanai ile confidence.pia uso wako.uso wa wanenguaji wengi hapa nyumbani hauonyeshi halai kupenda mnachofanaya,hakauna uhusiano kati ya hatua na uso yaani emotions na tena mkimulikwa taa ya video ndio bwana wee hapo anakufa mtu…
  kuna mengi tuu mnayopaswa kurekebisha nendeni pale bagamoyo mkajifunze ile nidhamau ya uchezji shoo.mtanufaika sana!
  TWANGA PEPETA AU EXTRA MUSICA WA TANZANIA SUCKS!
  AISHA MADINDA SUCKS BIG TIME!
  HEKO KWA SAIDA KAROLI,MSONDO,CHE MUNDUGWAO, MLIMANINA WENGINE WOOTE WANAOFANAYA JUHUDI KUPROMOTI UTANZNAIA NA UBUNIFU KTK MUZIKI WA TANZANIA
  THE SAME GOEES TO THE BLOGGERS NAWAPA HONGERA WOOTE MNAOTUMIA NAFASI YENU KUPROMOTI MUZIKI WA KWELI WA TANZANIA
  JAMANI NI MUHIMU NASI TUKAWA NA PRIDE NA VITU VYA NYUMBANI KWETU TANZANIA KUIGA ATHARI ZAKE NI NYINGI WACHA TUU UKOSEFU WA COMMERCIAL SUCCESS LAKINI PIA UZALENDO, UTAIFA WETU ,KITAMBULISHO CHETU NA UBUNIFU WEETU VYOOTE HIVI VITAATHIRIKA
  HIVI SISI NI TAIFA GANI TUNAOONA FAHARI KU -EMBRACE MUZIKI WA MATAIFA MENGINE (KONGO)
  MBONA WAKONGO WENYEWE HAWATAKI KUSIKIA MUZIKI WOWOTE ULE BALI NI WAO TUU TENA WANUPENDA NA WANJIVUNIA WEWE NENEDA KONGO CHUKUA DIAMAA ZAO LAKINI MUZIKI WAACHIE WENYEWE
  SOUTH AFRIKA WAKO SO PROUD NA WANEMBARACE SAANA TUU KWAITO NA AINA ZAO NYINGI TUU ZA MIZIKI NA HAWANA MPANGO NA MUZIKI WATANZANIA AU HATA WAKONGO

 17. Mwali Says:

  Gabriel southa afrika nao wameingiliwa na kidudu mtu cha Congo siku hizi wacha kabisa kuwa tetea!!!!

 18. Kiki Says:

  Duu Gabrieli, unaonekana ni mtu mwenye usongo saaana. Tunajua kwamba nia na madhumuni yako ni kutengeneza sanaa ya nyumbani, Kwa kweli ukiangalia ni kweli hizi bendi zinaimba kwa stely ya ki congo, lakini ukiangalia pia kuna vionjo vya kitanzania, kama kukata kiuno sio style ya kikongo peke yake, ni uafrica, hakuna sanaa isiokuwa imeigwa ila unatakiwa kuifanya iwe personal, na mimi nahisi bendi zetu zinajitahidi kuzipersonalise, hata hivyo usiwalaumu sana hawa wachezaji, hawa wanawapa funs vitu wanavyovitaka, ukizungmzia utamaduni woote, inabidi sana uangalie kwenye kila sanaa ya Tanzania. Media doesn’t embrace our own culture, tanzanians don’t embrace it either, sasa kumlaumu dada hapo juu na bendi nzima ni kujaza tu magunia maji, kwani chanzo kipo na hicho chanzo ndicho kianze kubadilika. Hebu gabrieli tuambia culture ya Kitanzania ni ip?????

 19. Dinah Says:

  Gabi usemayo ni kweli kabisa,
  Kuna mawili aidha kulala njaa au ku-promote utamaduni wako. Watu wanafuata kule kwenye soko (mtindo gani unapendwa) ili wapate kupitisha siku,kusomesha watoto wao, kupata mahali pa kujisetiri n.k.

  Tuangalie pande sote sio kukandamiza upande mmoja kwa vile tu hufurahishwi.

 20. Mr Tom Says:

  Mimi nadhani bwana Gabriel ametoka nje ya mada.Sina tatizo na mawazo yake.Lakini nadhani amekurupuka kwa sababu zake binafsi kuanza kumshambulia huyu bibie na fani ya muziki wa dansi wa baadhi ya bendi za Tanzania kwa ujumla kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe.Na mbaya zaidi ni kutumia lugha na maneno makali.Sijafurahishwa na hilo.Mtu unaweza kufikisha ujumbe uliokusudia bila ya hata kutumia maneno yenye kuonyesha kebehi na kashfa.Sasa nikirudi kwenye mada tuliyonayo hapa, hatujadili mtindo gani unastahili kuwa ndio alama ya sanaa ya unenguaji wa Tanzania.Na nimefuatilia sana mahojiano hayo.Sijaona mahali limezungumziwa suala la kama mitindo ya unenguaji wa baadhi ya bendi za Tanzania ni sahihi ama sio sahihi.Hoja iliyopo hapa ni je unenguaji ni uhuni(umalaya)au ni kazi kama kazi zingine? Hilo ndilo swali hapa bwana Gabi,sio suala la mitindo ya unenguaje.Na kama mimi ningekuwa mwalimu wako katika swali hili ningekupa ‘F’ kabisa.Maana umeenda nje kabisa ya swali husika.Mawazo yako ni mazuri kama hoja ingehusu mitindo ya unenguaji inayostahili kwa wasanii wa Tanzania.Hatahivyo kuna maswali mengi ingebidi yajibiwe kutokana na maoni yako kabla ya kufikia maafikiano.Lakini katika hali ya kushangaza, hujagusia hata kidogo juu ya hoja iliyopo kama fani ya unenguaji ni umalaya ama la.Hili ni tatizo.Na madhara yake ni kwamba umetuchanganya wadau makini kama sisi,kututoa nje ya kile tulichokuwa tunakijadili.Wakati mwingine jaribu kuwa makini na kuona kile unachochangia ndicho kilichopo katika meza ya majadiliano.Sikatai,unaweza na uko huru kutoa hisia na dukuduku lako kwa namna upendavyo.Lakini la kuzingatia ni kuangalia wakati na mahali muafaka wa kufanya hivyo.Vinginevyo,kwa wadau makini tutakutafsiri kwamba unaongozwa na hisia,jazba na hoja za nguvu katika kutoa michango yake,na walio sio umakini, ustaarabu na nguvu za hoja.Sasa nikiachana na mdau Gabi,napenda nianzie pale nilipoishia jana katika mjadala wetu wa kuona kama unenguaji ni uhuni ama ni kazi kama kazi zingine.Kabla sijaendelea na pale nilipoishia jana,mdau wa uchina(Maya) amekuja na swali lingine.Mara hii anataka kujua sasa kama umalaya ni uhuni,je vipi kuhusu funguo zinazoweza kufungua makufuri ama vitasa tofauti tofauti ziitwe malaya? je hizo Ufunguo/funguo hizo ni za kihuni? Mimi nadhani sasa unataka kujua maana ya neno malaya.Sasa kwa kukusaidia ni kwamba,malaya(prostitute) kwa tafsiri ya jumla ni mtu (hasa mwanamke) anaposhiriki tendo la ngono kwa minajiri ya kujipatia kipato.Hiyo ndio tafsiri nyepesi.Katika kazi hii/biashara hii ambayo kimsingi ni haramu katika sehemu nyingi duniani,mhusika anakuwa na wateja wengi.Yaani anashiriki ngono na wanaume mbalimbali.Sasa nikija kwenye swali lako la msingi,kwamba mbona sasa funguo ziitwe malaya?Kwa tafsiri hii je funguo hushiriki tendo hilo la ngono? bila shaka Maya hili ndio swali ambalo lingefuatia.Sasa kama nilivyosema kwenye jibu la msingi mwanamke anayesheriki katika biashara hiyo haramu ya kuuza mwili wake anafanya hivyo kwa wanaume wengi.Sasa kitendo cha funguo kuitwa malaya ni kwa sababu funguo hiyo huweza kufungua makufuri/vitasa tofauti tofauti na hivyo kuweza kufananishwa na kitendo cha yule mwanamke malaya anavyoweza kushiriki ngono na wanaume wengi.Bila shaka tumeelewana.Kama bado,karibu tena.Sasa jana nilimalizia kwa kuelekeza lawama kwa wamiliki wa bendi na vikundi mbalimbali vyenye fani ya unenguaji.Kumekuwapo na malalamiko kutoka wa wasanii wanenguaji na wengine juu maslahi duni wanayopata kutoka kwa waajiri wao.Wamiliki wamekuwa wakijari sana maslahi yao binafsi na kuwasahau wasanii wao ambao kimsingi ndio wanachangia kwa asilimia kubwa mapato ya bendi/vikundi.Sasa kwa binadamu yeyote yule anahitaji kujitosheleza kwa mahitaji yake ya kila siku.Inapotokea mapungufu ndipo mwanadamu huyo analazimika kujitafutia njia mbadala za kujiongezea kipato.Sasa njia mbadala hizo zaweza kuwa halali ama sio halali.Sitangia sana kujadili kipi ni halali na kipi sio halali maana ni somo tofauti.Ninachotaka kusema ni kwamba katika hali ya kutafuta njia mbadala za kujiongezea kipato,inategemea mazingira ya kazi ya mhusika.Mfano,mwalimu ataanzisha masomo ya ziada,daktari anafungua duka la dawa,nk.Sasa kwa bahati mbaya sana, hawa dada zetu walioko kwenye kazi hii ya unenguaji,mazingira yao ni magumu sana.Muda mwingi wanautumia kwenye mazoezi na kwenye maonesho hivyo kukosa muda wa kuweza kubuni shughuli zingine za kujiingizia kipato.Muda mchache wanaopata ni kwa ajili ya kupumzika.Na lazima tukumbuke hii kazi ni kazi ngumu sana kwa kuwa inahusisha nguvu za mwili na akili.Na ndio maana kwa mataifa yaliyoendelea kama hapa USA,wanaofanya kazi za unenguaji wana kipato kikubwa mno kushinda hata maprofesa wetu.Si watu ambao unaweza hata kuwasogelea.Wanaendesha magari ya kifahari na kuishi kwenye majumba ya kifahari.Hali ni tofauti kabisa na dada zetu wa huko nyumbani ambao hali zao ni duni sana ingawa ratiba na shuruba za mazoezi kwa mnenguaji wa Twanga Pepeta na yule wa Beyonce,Nelly,Jay Z,Usher(kwa kutaja wachache) hazina tofauti kimsingi.Sasa hapo ndipo linapokuja tatizo kwamba kwa mazingira ya mnenguaji wa Tanzania yuko kwenye mazingira yanayomshawishi akijitumbukize kwenye vitendo vya umalaya na hivyo kuonekana kwamba fani ya unenguaji ni uhuni.Kazi ya sanaa ili ikamilike inategemea hadhira(audience)au wateja kwa lugha nyepesi.Sasa kwa utafiti uliopo ni kwamba wateja wengi wanaposhiriki maonesho ya unenguaji,asilimia kubwa wanaume ndio huguswa zaidi na umahili wa akina dada wanenguaji na sio wanawake.Na kwanini wanaume zaidi?sababu ni kwamba kuguswa huko kunaambatana zaidi na tamaa ya mwili katika kushiriki ngono.Tukumbuke kitalaamu mwanaume ndio huvutiwa zaidi na kile akionacho kwa macho.Sasa na kwakuwa nguo zinazotumika katika kazi ya unenguaji zinaruhusu maumbile ya mwanadada kuonekana vizuri,hapo ndipo tamaa za mwanaume(mkware) zinapokolea.Mwisho wa siku mwanaume huyo atahitaji kulala na mnenguaji aliyevutiwa naye.Sasa kutokana na hali halisi ya wanenguaji wa Tanzania(pengine na nchi zingine masikini,naamini hivyo) kama nilivyoilezea hapo juu,wanashawishika kirahisi kujikuta wametumbukia kwenye vitendo vya umalaya pengine bila hata ya ridhaa yao ili mradi kukidhi haja zao.Kwa hiyo haitoshi kuhitimisha kwa kusema umalaya ni tabia ya mtu,,hapana.Ni sawa,inaweza kuwa ni tabia ya mtu.Lakini mazingira ya kazi husika na kipato cha mtu husika,huchangia kwa kiasi kikubwa kuibadili tabia ya mtu husika.Kama nilivyotafsiri awali kwamba umalaya ni biashara ya kuuza mwili.Sasa siamini kama kuna mwanamke ambaye ana kipato kizuri akajiingiza katika biashara ya kuuza mwili,hata kidogo.Sasa nimalizie kwa kutoa ombi kwa wamiliki wa bendi/vikudi husika,kuwaona wanenguaji kama sehemu muhimu ya vitega uchumi vyao,hivyo wajitahidi kuwapa maslahi yatakayowawezesha kuishi kwa kuitegemea kazi yao na hivyo kutojiingiza katika vitendo vya umalaya na hivyo kuondoa dhana ya kuuhusishha unenguaji na umalaya.

 21. miss bee Says:

  Naomba kuuliza mtoa mada # 13 mr.Tom wewe ni mwenyeji wa kasulu au ulipita kusoma tu? mimi ni wa huko naishi wash.D.C,if so naomba e_mail yako tafadhali.Asante sana.

 22. Kimanumanu Says:

  OOh Hopeless Gabriel hukuwa na la kusema?Sometimes uhuru wa kusema hauna maana kuwa lazima useme bali hata kuwa kimya ni njia mojawapo ya kukidhi uhuru wako.Iko wapi mipaka ya utamaduni?Hakuna watanzania wanaoongea kilingala?Hakuna wakongo wanaoongea lugha za makabila ya Kitanzania achilia mbali Kiswahili?You are not focused at all na hujui unaloongea na kubaki ukiropoka tu.U better keep quiet ili watu wasijue una takataka gani kichwani.

 23. lee Says:

  HII MPYA TENA TOKA KWA BW.GABRIEL!! LABDA NIANZE KWA KUKUAMBIA TU KUWA HUNA LOLOTE UNALOLIJUA KUHUSU MUZIKI. WEWE KAA TULIA SIKILIZA TAZAMA BASI!! UNASEMA TWANGA PPT WANAIGA WAKONGO… MARA AISHA ANAIGA WAKONGO…SWALI: WAKONGO NI WATU GANI NA HAO WATANZANIA NI WAPI? KONGO (ZAIRE),TANZANIA(TANGANYIKA NA ZANZIBAR)NI MAENEO TU JUU YA USO WA DUNIA. WATU WAISHIO HUMO 98%NI WABANTU. HAWA WANA LUGHA, MILA NA DESTURI ZINAZOFANANA TOKA KABILA HADI KABILA. HIYO MIZIKI YA MSONDO,MLIMANI NK HAINA TOFAUTI NA MIZIKI YA VEVE, TP OK JAZZ, AFRISA INT. NK! LAKINI KWA VILE BW. GAB NI KIHIYO WA MUZIKI, UNAKOROMA TU! KAMA ALIVYOSEMA ALI CHOKI: HIZO NI CHUKI BINAFSI! WAPE SIFA ZAO WANA TWANGA PPT NA AISHA KWA KUZUNGUSHA HICHO KIUNO UTADHANI LOPELE(MKIA WA SAMAKI). AKINENGUA MIMACHO INAKUTOKA NA MATE KUKUDONDOKA… SI USEME TUU! HAYA KAMA KWELI WEWE UNAFIKIRIA KI-TANZANIA, HAO JAMAA WANAOBWEKA BWEKA NA KUJIFANYA AKINA KANYE-MAGHARIBI WANAFANYA VITU VYA KITANZANIA? JE WANAUME WANAOSUKA NYWELE(MARIDADI KULIKO DADA ZAO), MIHERENI NA VIPURI VYA PUA(WANAUME KAMA MABINTI) UNAWAONAJE? JE HUO NI UTAMADUNI WA MTANZANIA? KAMA NI MFUATILIAJI MZURI WA MUZIKI, HEMEDI MANETI ALIIMBA NINI(NA LINI) KATIKA WIMBO ‘NGOMA’? UNAWAPALILIA WA SA…HIYO KWAITO NI JINA AU AU MTINDO WENYE ASILI YA SA? TOFAUTI YAKE NA BONGOFLAVA NINI LUGHA AU MAPIGO? BW.GAB USITUPOTEZEE WAKATI WACHA TUJIRUSHE NA TWANGA PPT NA NIKIKUONA DA AISHA…UNANIDAI KWA KAZI YAKO MWANANA YA KULICHANGANYA JUKWAA!!ALI CHOKI LETE SAUTI, SHAKASHIA VUTA NYUZI, MCD TWANGA VIGOMA HIVO, NA AISHA MWAGA MAUNO MWANAKWETU,FAHARI YA MACHO…

 24. lee Says:

  BW.KIMANUMANU WASILIANA NAMI. SAFI SAANA!

 25. Mr Tom Says:

  miss Lee mie mimi sio mwenyeji wa Kasulu.Mimi ni mwenyeji wa Tukuyu,Mbeya kwa asili.Lakini kwa Tanzania mpaka naondoka kuja huku Marekani nilikuwa nikiishi na kufanya kazi Dodoma.Kasulu nilipita tu kimasomo, then nikawa pale Burumbora JKT kwa miezi 6.Kwa hiyo Kigoma nimekaa miaka takribani 3 .email yangu ni (mwasata@bgsu.edu)

 26. lee Says:

  Mr Tom
  Kuna tofauti kati ya Lee na Miss Bee. Soma kwa uangalifu!!

 27. Mr Tom Says:

  Oops!!! Niwie radhi Lee.Kwa kweli nilighafilika katika hilo wala sikukukusudia wewe mpendwa.Samahani kwa usumbufu uliojitokeza!!

 28. Kimori Says:

  Gabriel,

  Are you trying to talk about culture in this 21st centery or I am missing the point? Culture has got no boundaries with globalization!

  Guiters, flutes, piano, violins, trumpets, psaltery, harp, just to mention a few musical insturments…are they all authentically Tanzanian or African?

  Think again before you become so critical on someone’s means of income!

 29. robert Says:

  Aisha nakupenda jiunge na mimi tuwe marafiki

 30. Simon Siwango Says:

  Kakaa sexy sana

 31. shiku Says:

  gabi wee wacha wivu, fuata masharti kisha utoe jibu. heko kwa mwalimu tom kwa kumueleza ukweli gabi. maoni yangu kwa ‘toto shoo’ Aisha, kazi nzuri endelea, kwani wanaochafua juhudi zako hawakulishi wala kukuunywesha. nyumba hawakulipii. ni nani kasema kazi si kazi, hapo kidogo amepotoka, kazi bora iwe halali, ni kazi

 32. binti-mzuri Says:

  gabby huo wivu tu mtu wangu!


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s