BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“KUJIHESHIMU NDIO SIRI”-STARA THOMAS January, 16, 2008

Filed under: Burudani,Mahusiano/Jamii,Maisha,Muziki,Utamaduni,Wanawake na Watoto — bongocelebrity @ 12:10 AM

Ukishakuwa mtu maarufu na mwenye mafanikio fulani, ni jambo jema sana kujitolea,kwa njia moja ama nyingine,kuihudumia jamii yako. Wenzetu wa magharibi hupenda kusema (kwa kutumia lugha yao) “Giving back to your community”.Stara Thomas(pichani),mwanamuziki maarufu wa miondoko ya zouk nchini Tanzania,anatambua hilo.

Stara amekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuunga mkono juhudi za kuhakikisha vifo vya watoto na kina mama wakati wa kujifungua vinapungua kwa asilimia kubwa kama sio kutokomea kabisa.Kwa kifupi Stara ni “balozi” wa uzazi salama.Anafanya hivyo kwa kutumia kipaji chake,kupitia muziki wake. Mfano mzuri ni wimbo wa “Play Your Part” wimbo ambao umekuwa ukitumiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama UNFPA.

Sauti yake ni mojawapo ya sauti ambazo zinatambulika kirahisi.Ukiusikia wimbo wake,ni rahisi kutambua kwamba huyo ni fulani. Mwaka 2003 alipata tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike nchini Tanzania. Mwaka huu wapenzi wa muziki wake watarajie albamu ya tatu kutoka kwake. Nini kinamsukuma katika kujitolea katika jamii? Nini mtazamo wake kuhusiana na muziki wa kizazi kipya?Ana ushauri gani kwa wadada wengine wanaotaka kujiingiza kwenye muziki?Je, ana mpango wa kuingia kwenye siasa? Ili kupata majibu ya maswali hayo na mengineyo,fuatana nasi katika mahojiano yetu na “mama wa zouk” nchini Tanzania

BC: Stara karibu sana ndani ya BongoCelebrity.Kwa kuanzia,unaweza kutueleza kwa kifupi tu historia ya maisha yako?Ulizaliwa wapi,ukasomea wapi na vitu kama hivyo?

ST: Mimi nimezaliwa Mwanza, ni mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto wanne,mmoja akiwa ni mvulana na waliobakia ni wasichana.Mimi ni wa tatu kuzaliwa. Shule ya msingi nimesomea kwanza Lake Primary School huko Mwanza mpaka darasa la tatu nilipohamia Dar-es-salaam na kumalizia Upanga Primary School.Sekondari nimesomea Mzizima Secondary School.Baada ya Mzizima nilichukua Diploma ya mambo ya Tourism and Airlines.Baada ya hapo nikasomea mambo ya kompyuta nk ili kujiandaa na kazi ambapo nimefanya kazi mbalimbali kama vile Public Relations, kwenye tour and airlines mbalimbali kabla sijafanya kazi ya utangazaji wa radio East Africa Radio.

BC: Nini hasa kilikuvutia mpaka ukaamua kujiingiza kwenye masuala ya muziki?Na je unaweza kukumbuka baadhi ya majina ya wanamuziki ambao pengine uliwaona kama “role models” wako kiasi kwamba wakachangia uamuzi wako wa kuingia kwenye muziki?

ST: Kwa ujumla ni mapenzi binafsi tu katika muziki ndio yaliyochangia.Yes,majina kama Lionel Richie,Whitney Houston, Mariah Carey(huyu nilikuwa naimba sana nyimbo zake wakati nikiwa shule). Pia wanamuziki kama Papa Wemba, Tabu Ley,Mbilia Bel,Tshala Mwana, Yvonne Chakachaka walikuwa wananivutia.Wengi wa wanamuziki hawa nilikuwa nazisikia nyimbo zao nyumbani kwani baba alikuwa anawapenda pia na hivyo mara nyingi yeye ndio alikuwa akileta miziki yao nyumbani.

Kwa upande wa Tanzania, kwa ujumla bendi zote za wakati huo(bahati mbaya nyingi zimeshakufa) zilikuwa zinanivutia sana…hii ni pamoja na waimbaji wake.Ingawa hivi leo sikumbuki majina halisi ya wanamuziki wengi wa enzi zile,nyimbo zao nyingi bado zikipigwa hata hivi leo nazikumbuka vizuri.

BC: Wazazi wengi nchini Tanzania wamekuwa hawapendelei kuona watoto wao wakiingia kwenye masuala ya muziki kutokana na dhana (potofu) kwamba muziki ni uhuni.Kwa upande wako wazazi wako walichukulia vipi uamuzi wako wa kuingia kwenye muziki?

ST: Kwanza kabisa ningependa kukuambia kwamba wazazi wangu,wote wawili,walikuwa ni waalimu. Kwa hiyo ilikuwa ni ngumu kwa kiasi fulani.Lakini kama unavyojua tena,ukiwa mbishi unakuwa mbishi tu.Kwa hiyo tulikwenda hivyo hivyo,mara wanakubali mara wanakataa.Kwa bahati nzuri mimi nilikuwa sifanyi muziki katika namna ambayo wao walikuwa wanaifikiria.Kwa hiyo nilikuwa natoka kisha narudi.Hata kama walikuwa wanafoka mimi mwenyewe nilikuwa najua kwamba nikitoka siendi kufanya kitu chochote kibaya. Nadhani hili ni kawaida katika mahusiano ya mtoto na mzazi.Mara nyingi mzazi anakuwa anakazania zaidi kukusomesha.

Isitoshe,kipindi kile muziki ulikuwa haulipi ukilinganisha na ilivyo hivi leo.Maisha ya wanamuziki wengi wa wakati ule yalikuwa yanakatisha tama.Kwa hiyo wazazi walikuwa wakiona mtoto wao naye anataka kujiingiza kwenye muziki,lazima iwe ngumu.Lakini baadaye walipoona tofauti na pia nikawa nimeshakua,walikuwa hawana jinsi bali kukubali.Kwa hiyo mwanzoni ilikuwa ngumu.

BC: Wengi leo hii tunakufahamu kama “Mama wa Zouk” kwani miziki yako ipo zaidi katika staili hiyo ya muziki.Kwanini uliamua kupiga zaidi muziki wa aina hiyo na sio aina zingine kama chacha,rhumba nk?

ST: Unajua kusema ukweli siku za nyuma nilikuwa nikiimba pia aina zingine zote za muziki ikiwemo hiyo uliyoitaja. Nyingi wakati huo zilikuwa ni kukopi kutoka kwa wanamuziki wengine. Sasa wakati naingia rasmi kwenye muziki wa kitanzania(pindi ilipoonekana wazi kwamba muziki wa kitanzania/Kiswahili) sasa unakubalika zaidi na unalipa) nilikuwa nishakuwa mama.Kwa hiyo kabla sijaingia nikajiangalia mimi mwenyewe,umbo langu nk.

Hapo nikagundua kwamba miziki hii ya kibongo flava,sio yangu tena.Kwa hiyo nilikaa nikasema nataka nipige aina ya miziki ambayo hata nikisimama mbele za watu,wataukubali kutokana na mimi mwenyewe nilivyo na pia maudhui ya ule muziki ambayo yananiwezesha hata mimi nikisimama kwenye steji nicheze.

Hii ni tofauti na miziki kama bongo flava ambayo ukifika pale stejini inabidi urushe miguu,mikono n.k kitu ambacho kinakuwa tofauti ukizingatia muonekano wangu na mambo mengine.Kwa hiyo hizo ndizo sababu zilizonisukuma mimi kuamua kufanya muziki wa zouk kwani nilitambua kwamba nitakuwa comfortable zaidi na muziki huu.

 

Stara Thomas akiwa jukwaani.

BC: Stara,kitu kingine ambacho kinakutambulisha wewe zaidi ni sauti yako.Mara nyingi mtu anayefuatilia muziki wa Tanzania akisikia tu sauti yako anatambua kwamba huyo ni Stara Thomas.Nini siri ya sauti yako na unafanya nini ili kuhakikisha inabakia namna hiyo?

ST: Mimi nafikiri siri anayo Mungu mwenyewe.Nasema hivyo kwa sababu mimi mpaka naanza kuimba sikuwa najua kitu chochote kuhusiana na sauti.Nilikuwa naona ni sauti ya kawaida tu.Kwa hiyo nadhani ni Mungu tu ndio amenibariki na hiki kipaji na hivyo sauti pia amenipa yeye.

Lakini pia aina ya nyimbo ambazo nilikuwa napenda kuziimba tangu utotoni zilichangia.Labda nikuambie kwamba kwa sababu nilishajiona nina sauti nzito kidogo nilipenda sana kuimba nyimbo (au vipande vya nyimbo) kwa mfano, za T-Boz yule wa kundi la TLC la Marekani kama unalikumbuka.Nilikuwa nafanya mazoezi mengi sana ya kuimba kama yeye.Kwa hiyo yule naye amechangia sana katika kuimarisha uimbaji wangu.Lakini kwa ujumla,siri ya sauti yangu anaifahamu Mungu kama nilivyosema hapo mwanzo.

Mtizame Stara katika wimbo Nipo kwa Ajili Yako kwa kubonyeza hapa.

BC: Katika kuangalia baadhi ya video za miziki yako,ni wazi kabisa kwamba unajitahidi na unathamini sana suala la kudumisha mila na utamaduni wa mwanamke wa kitanzania kuanzia kwenye mavazi,muonekano nk. Unafikiri kuna umuhimu gani wa kuendelea kuzitukuza mila na tamaduni zetu hata linapokuja suala la muziki?

ST: Mimi nadhani umuhimu upo,tena sana tu.Kwa mfano kama mimi,naweza kutengeneza video nikiwa nimevaa mavazi kama suti nk.Lakini,kwa mtizamo wangu,sidhani kama nitakuwa na utofauti wowote.Kwanza ukiangalia,mimi ni mswahili/mwafrika. Kwa hiyo ninapokuwa navaa nguo za kiafrika na halafu zinanipendeza,nadhani hilo ni jambo zuri zaidi.

Isitoshe, kwa kufanya hivyo ninakuwa wala sina haja ya kuhangaika kujiremba sana kwa sababu nakuwa tayari kwenye culture yetu sisi waafrika kwani waafrika ni wazuri.Kwa hiyo ukivaa tena kiafrika ndio inanoga zaidi.Ni vizuri pia kudumisha mila na desturi zetu kwani kwa ujumla ni nzuri.Ukivaa nguo ya kiafrika haikuachi uchi.Pia mavazi ya kiafrika yana rangi nzuri,ni mavazi ya heshima. Hiyo inakusaidia mtu kuheshimika ndani ya jamii jambo ambalo linasaidia maisha yako kuwa mema.Halafu unakuwa huondoki kwenye msingi wa Mungu kwani mavazi ya kiafrika,kama nilivyosema hapo juu,yanasitiri mwili.

 

Stara Thomas akiwa katika tabasamu.(Picha na Ahmad Michuzi)

BC: Kuna suala la wasanii kujitolea muda na wakati mwingine hata pesa zao katika kusaidia jamii.Wewe umekuwa ukijitolea kupitia kampeni ya Umoja wa Mataifa ya White Ribbon Alliance. Nini kinakusukuma katika kujitolea na unadhani kuna umuhimu gani kwa celebrities kujitolea zaidi kwa jamii zao?

ST: Unajua unapokuwa artist/celebrity,watu wengi sana wanakuwa wanakufikiria tofauti tofauti,moja.Pili unakuwa na nafasi ya pekee kuwafikia wanajamii wengine ambao sio wasanii. Mimi kama msanii,toka zamani nilishajiwekea malengo kwamba ikifikia mahali nikaona kwamba katika hili naweza kusaidia basi ni lazima nisaidie.Hii ni kwa sababu mimi ni muimbaji na pili ninaamini kwamba ninaheshimika kutokana na jinsi ninavyoona nikikutana na watu wazima,watoto wadogo nk na jinsi wanavyozungumza na mimi.

Kwa hiyo naamini kabisa kwamba sauti yangu mimi,kwa mfano,kwenye suala zima la uzazi salama itaweza kusaidia kwa sababu kwanza kabisa mimi ni mama. Ninachokizungumza kinakuwa ni kitu ambacho ninakifahamu.Kwa maana hiyo hata mtu akiniamsha usiku wa manane akanipa microphone na kuniambia nizungumzie suala la uzazi salama mbele ya watu wa idadi yoyote,nitafanya hivyo bila kutetereka hata kidogo.Hii inatokana na ukweli kwamba kwanza nafahamu vizuri kabisa kuhusu labor pain kwani mimi mwenyewe nimeshazaa(nina watoto wawili), nimeshakutana na watu wengi tu ambao wamenieleza matatizo yao mengi ya uzazi. Kwa hiyo ninafahamu,nafikiri nafahamu.Kwa hiyo,mimi kama msanii ambaye ninaamini nina nafasi katika jamii naona nina wajibu muhimu wa kuwaelimisha wanajamii wenzangu.

BC: Muziki wa kizazi kipya umekuwa ukitupiwa lawama kwamba unachuja haraka sana.Maneno kama Big G nk yamekuwa yakitumika kuelezea hali hiyo.Kwa maoni yako unadhani nini kesho ya muziki wa kizazi kipya?Unadhani unaweza kupotea kabisa kama ambavyo aina zingine zimepotea au kupoteza umaarufu?

ST: Unajua muziki wa kizazi kipya ni muziki mzuri tu. Tatizo ni kwamba wengi wanaouimba hawana knowledge ya muziki. Kwa hiyo unakuta vitu vingi wanavyoviimba ni vitu ambavyo vimekwisha tengenezwa,vimeshaimbwa nk.Ndio maana hata mtu ukiusikia baada ya muda unakuta ile hamu imeshaisha kwa sababu unakuwa umeshawahi kuusikia tena na tena sehemu fulani. Lakini kama watabadilika katika hilo na kukaa chini na kujiuliza ni jinsi gani tufanye muziki wetu nao udumu kwa muda mrefu,nadhani inawezekana mabadiliko yakatokea. Muziki wenyewe kama muziki hautopotea kabisa.Watakaopotea ni wasanii, wengi watalost na hivyo kupotea kabisa kwenye fani.

Mimi nafikiri kinachotakiwa kufanyika hapa kwa sababu naona muda umeshapita sana (wasanii wengi wameshalost) ni kuangalia upya jinsi gani wanaweza kutoa japo single(sio lazima albamu) ambayo watakuwa wameikalia kwa muda mrefu zaidi katika kuitengeneza.Kisha hela wanazopata wazitumie katika kujiendeleza vilivyo katika masuala mazima ya muziki kama vile elimu ya muziki yenyewe,muziki kama biashara,utawala(management) ya biashara ya muziki na burudani nk.

Kama wataona muziki haulekei kuzuri basi mapema kabisa waangalie ni wapi waegemee ili maisha yao yawe mazuri zaidi.Hapa nina maana mtu using’ang’anie fani.

BC: Kama nimekuelewa vizuri unamaanisha wasanii wasikurupuke katika kutoa nyimbo kila kukicha sio?

ST: Ndio,nasema hivyo kwa sababu naturally kabisa kama wewe ni mtunzi mzuri na unaelewa kabisa hali ilivyo,huwezi kuwa unatoka nyimbo kila siku kwa sababu kwanza kutunga wimbo mmoja tu ni kazi ngumu sana. Ni muhimu kutengeneza nyimbo au wimbo kiutulivu ili ukitoka unatoka na kitu kizuri zaidi.

 

Stara Thomas(kushoto) akiwa na Ray C,msanii mwingine wa kizazi kipya.(Picha na Ahmad Michuzi)

BC: Lipo suala ambalo limekuwa likilalamikiwa kwamba linachangia sana kurudisha nyuma maendeleo ya wasanii.Nazungumzia masuala ya haki miliki na pia kudhulumiwa na “wadosi”.Kwa mtazamo wako,nani hasa anastahili kulaumiwa?Ni serikali,wasanii wenyewe,Djs au?

ST: Mimi nafikiri sote tunaweza kulaumiwa kwa njia moja au nyingine ikiwemo serikali,vyombo husika nk. Lakini lawama nyingi hivi sasa zinaweza pia kumwendea msanii mwenyewe hususani hivi sasa ambapo sheria zipo na vyombo kama COSOTA vipo tayari kushirikiana na wasanii katika kulinda kazi zao. Hili linaipunguzia serikali lawama.

Kwanini nasema msanii naye anastahili lawama?Sikiliza,mambo ya COSOTA yanakuja baada ya msanii kuwa ameshamaliza kutunga,kurekodi na kila kitu. Kwa maana hiyo process yote ya kuanza kuibiwa kazi za msanii inaanzia mikononi mwake yeye,labda na producer wake.Kwa hiyo nadhani msanii anatakiwa apate elimu ya ujasiriamali. Lazima kwa mfano msanii ajue jinsi yak u-negotiate na wauzaji,wasambazaji nk. Msanii asipoweza ku-negotiate hapa mwanzo ni wazi kwamba huko mbele ataendelea kuibiwa tu.Ndio maana nikasema hapo juu kwamba elimu kwa wasanii juu ya masuala mazima ya utawala wa biashara ya muziki,usambazaji wa kazi zetu nk ni muhimu sana.

BC: Tanzania mpaka hivi leo hatujaweza kuwa na muziki ambao tunaweza kusema huu ni muziki wa kitanzania.Unafikiri hii inatokana na nini? Nini kifanyike ili tuweze kupata identity yetu kwenye anga za muziki?

ST: Mimi kwa mtazamo wangu naweza nikasema,unajua sisi Tanzania ni kweli kwamba wazee wetu wamepiga muziki na ulikuwa unaonekana kabisa kwamba muziki huu unatoka Tanzania. Sasa kwa sababu kulikuwa hakuna video na kwamba walikuwa hawajawahi kuurekodi hivyo na pia kwa sababu Tanzania tuna makabila kibao imekuwa ngumu sana kuhakikisha kwamba muziki wa aina fulani ni kutoka Tanzania. Kuchelewa kwetu kimaendeleo kumechangia sana wakati mwingine hata kuporwa kilicho chetu kisanii.Wenzetu wanaweza kuwa walikuja na kuona tunafanya kitu fulani kisha wakakichukua na kuitangazia dunia kwamba ni chao.Baadaye sisi tukikifanya tena tunaonekana kama tunaiga tu.

Cha msingi ninachotaka kusema ni kwamba sisi Tanzania,sisi wa kizazi kipya kwa mfano,tunaweza kubadilisha hali hiyo. Ingawa,kama nilivyosema hapo juu,maendeleo yetu yamechelewa kuja.hivi sasa tunaweza kubadilisha focus yetu iwe ya kuanzia ndani na sio nje kama ambavyo imekuwa kwa muda mrefu.

Cha msingi ni kila msanii ajiheshimu na kujitahidi kuwa mbunifu zaidi,afahamu nini anafanya.Si unaona mimi kwa mfano napiga zouk.Lakini nakuhakikishia nikisimama America watu watajua nimetokea Tanzania.Why? Kwa sababu muziki ni ule ule.Cha msingi ni wewe mwenyewe uko vipi katika sanaa yako unayoifanya.Unajiwakilisha vipi? Je wewe mwenyewe unajiona mzungu,mwafrika au? Kwa hiyo kutambulisha muziki wetu inatokana na package nzima.Na isitoshe kwa sababu sisi kimaendeleo tumechelewa kidogo ukilinganisha na baadhi ya nchi zingine za Afrika kinachotakiwa hivi sasa ni sisi kujitambulisha kama sisi ili nasi tuchanue.Mbali na kuimba tu.

BC: Nchi zetu bado zimetawaliwa na mifumo inayoitwa “mifumo-dume”. Sasa wewe ukiwa kama mwanamke kwenye kazi ya muziki, imeshawahi kutoka ukakumbana na matatizo fulani fulani ya kiutendaji kwa sababu tu wewe ni mwanamke? Ni matatizo gani?

ST: Mimi kwa kweli naweza kumshukuru Mungu kwamba alinipa moyo fulani wa ajabu sana. Yaani kitu chochote kwangu mimi huwa sio tatizo.Mara nyingi huwa najiandaa vilivyo kutegemeana na kazi inayonikabili mbele yangu. Zaidi ya hapo matatizo huwa ni ya kawaida bila kuzingatia jinsia.Isitoshe,najiheshimu sana jambo ambalo linafanya iwe ngumu kwa watu kuniingilia kwa mfano katika kunitongoza nk.Unajua kujiheshimu inasaidia sana.Usipojiheshimu hata ukikutana na mbwa anaweza kukufanyia chochote anachotaka.

BC: Kwa upande wa Tanzania ya hivi leo,ni wanamuziki gani ambao kazi zao zinakuvutia na ambao hujawahi kufanya nao kazi ilhali ungependa kufanya hivyo katika siku za mbeleni?

ST: Wapo wasanii kadha wa kadha ambao wanachipukia hivi sasa na ambao ningependa kufanya nao kazi. Lakini kusema ukweli, hivi sasa focus yangu ipo zaidi katika kufanya muziki wa kimataifa zaidi. Isitoshe muziki hapa nchini Tanzania hivi sasa umedorora kidogo. Mastaa wa zamani hivi sasa wameanza kuachana na muziki na wanajijenga katika mambo yao mengine.Wengine wamelost.

BC: Kwa upande wa kimataifa kama unavyosema ungependa kufanya kazi na kina nani?

ST: Kwa upande wa nje ningependa kufanya kazi na wasanii kama Mary J,Blidge, Akon nk.Kwa upande wa barani Afrika ningependa kufanya kazi na wasanii kama Papa Wemba (hata kama sio kurekodi naye nyimbo mpya basi kurudia japo baadhi ya nyimbo zake). Halafu ningependa sana kukutana na mtu kama Quincy Jones na Lionel Richie.Hawa ningependa japo kupata fursa ya kukutana nao na kuongea nao ili kupata ushauri mbalimbali wa masuala ya kimuziki.Kufanya nao kazi ingekuwa big bonus.

BC: Mpaka hivi sasa umeshatoa albamu mbili.Ya kwanza uliita Nyuma Sitorudi na ya pili Hadithi. Hivi sasa unajiandaa kuibua albamu yako ya tatu.Je umeshaipa jina? Na je wapenzi wa muziki wako wategemee mabadiliko yoyote?

ST: Mabadiliko lazima yawepo.Kama umesikia single ya Wasiwasi wa Mapenzi utakuwa umepata vionjo ni kwa jinsi gani wapenzi wa muziki wangu wategemee vitu vikali zaidi,vionjo murua zaidi nk. Sijaipa jina bado.

BC: Katika albamu zote mbili ambazo umeshazitoa,ni albamu gani unadhani ilikuwa ngumu zaidi kutengeneza?Kwanini?

ST: Ninachoweza kusema ni kwamba unapotengeneza albamu ni wazi kwamba albamu zote lazima zikupe tabu. Nasema hivyo kwa sababu unakuwa so sensitive kuhakikisha kwamba unatoa kitu ambacho kitawavutia wapenzi wako.Kwa hiyo kwa ujumla albamu zote huwa ngumu.

Hata hivyo,albamu hii ya tatu ninayotarajia kuitoa naiona kama iko more reasonable kwa sababu sina pressure kama nilizokuwa nazo wakati wa kutoa albamu mbili za mwanzo. Hii ya tatu naifanya mwenyewe.Zile zingine nilikuwa nazifanya kwa mikataba na “wadosi” jambo ambalo linafanya kila kitu ufanye under pressure kwani jamaa wanataka siku fulani wimbo utoke,siku fulani video itoke nk.Pia competition wakati ule ilikuwa kubwa kuliko hivi sasa kwani kimsingi muziki hivi sasa unashuka kidogo ukilinganisha na miaka michache hapo nyuma.

BC: Nini mipango yako katika miaka mitatu/mitano ijayo?

ST: Kwanza ni kutoa albamu yangu ya tatu.Pili ni kujaribu kuuza muziki wangu kimataifa zaidi hususani barani Ulaya. Tatu ni kuzidi kutengeneza miziki yenye kiwango cha kimataifa.

BC: Umekuwa ukijihusisha na masuala ya kijamii sana.Labda una mpango wowote wa kuingia kwenye siasa katika miaka ya baadaye?

ST: Hapana.Mimi sidhani kama naweza kufanya siasa moja kwa moja. Ninachoweza kufanya ni kuhamasisha tu labda kupitia muziki wangu. Lakini hapo zamani niliwahi kufikiria kuwa mbunge.Hivi sasa wazo hilo sina tena.

BC: Una ujumbe gani kwa vijana hususani kina-dada wanaotaka kuingia kwenye muziki hivi leo?

ST: Kwanza kabisa ambaye anaona yeye sio artist wala asijiingize kwenye muziki.Aendelee tu na shule na mambo mengine. Nasema hivi kwa sababu ukweli ni kwamba muziki si lelemama.Unataka moyo na kipaji.

Pili wasiingie kwa kuiga,waingie baada ya kujifanyia tathmini haswa na kuona wanaweza.Wajifunze kwanza,wasome muziki.Mbali na hapo kitakachotokea ni kwamba watatengeneza albamu moja na kisha kupotea kabisa.

BC: Ahsante sana Stara kwa muda wako,tunakutakia kila la kheri katika kazi zako.

ST: Asanteni na nyie.Kazi njema.

Kama asante yako ya kusoma mpaka hapa, pata burudani na kibao maarufu cha Stara Thomas kinachoenda kwa jina Mimi na Wewe.

Advertisements
 

46 Responses to ““KUJIHESHIMU NDIO SIRI”-STARA THOMAS”

 1. Papin Says:

  Huyu mama nampa kubwa ametulia sana tofauti na wasanii wengine. Wasanii wengine waige mfano wake. Amependeza kishenzi kama mke swafi wa mtu, Ingawa sina uhakika kama ameolewa!!!!!!!!!

 2. shally Says:

  kwa kweli dada anajiheshimu kwa tanzania superstar akijiheshimu anaonekana mshamba kumbe ndio anakuwa hachokwi na watu for example stara, mr.paul hivi jamani dully ukisikia tu jina si unasikia kichefuchefu kwa tabia zake?

 3. Matty Says:

  Mungu akubariki kwa unayoyafanya hasa masuala ya kina mama, pia unasauti nzuri na unavaa kiheshima kulingana na umbile lako.

 4. Ally Says:

  Huyu anavaa kulingana na umbile lake sio kiheshima naomba muelewe hilo.

 5. KionaMbali Says:

  Tehe! teh! tee!
  We Matty we, huo sasa uchokozi huo!
  Mi simo! Shauri lako!

 6. Mwanamama makini na muziki makini.

  Kudos Stara.

 7. Kimori Says:

  Unfortunately, we have remained without some of the dtails, despite of the long interview!

 8. Mkabahati Says:

  Napenda sana nyimbo za Stara, she’s so down to earth nyimbo zake naweza ku-relate nazo.I must say, i am impressed with her work na uzazi wa mpango maanake we need that for real; educate wazazi wannabees coz siku hizi sio kwenda ovyo ovyo tu, life is expensive and women need to look out for their health as well as that of their unborn children..

 9. Upendo Furaha Says:

  Ukweli huyu mama (dada Stara Thomas) amependeza sana. Na hata ukiangalia mikanda yake ya video huwa anajiheshimu sana.
  Kisaikolojia anajiheshimu maana ameolewa na pia inaonekana anamheshimu hata mumewe. Maana hata wengine wameolewa lakini vaa yao utafikiri ndio wanakwenda kwenye madanguro.
  Ninamuombea Mungu huyu mama (Stara Thomas) pamoja na familia yake awabariki ili kipaji chake kikue na aweze kupata kipato cha kumtosha.

 10. Dinah Says:

  Mzuri, kabarikiwa sauti njema, Hana skendo, anajua kujieleza, hachanganyi maisha yake binafsi na kazi au umaarufu na ni mfano mzuri kwa wanawake wengine nyota wa Kibongo.

  Kila la kheri ktk shughuli zako.

 11. Msukuma wa shy Says:

  Hongera Mama!!
  Ila mbona hujaelezea kinga ubaga kuhusu huo uzazi wa mpango?
  Nitafurahi ukitupa elimu hiyo.

 12. any Says:

  Amependeza mama wa watu. Na anavaa kiheshima, maana sio wote wanaovaa kulingana na maumbile yake.~
  Ata Fidelisi Iranga anavaa kulingana na umbile lake, heeeeeeeeeeeeeee! nimecheka hadi basi~

 13. Edwin Ndaki Says:

  Inapendeza sana kuona wasanii ambao ni mfano mzuri kwenye jamii kama wewe.

  Kila la kheri endeleza kipaji chako.

  Watanzania tusaidie kuinua sanaa ya tanzania kwa kununua kazi halali.

  wasalaaam

 14. Matilda Says:

  Yap safi sana dada,Unasura bomba sana kupita maelezo mwanawane,tabia nzuri ya kuvutia sana,unamaendeleo mama unajua nn unachokifanya,unanivutia,Keep it up.

 15. Mama wa Kichagga Says:

  Stara,

  Hongera sana kwa kuwawakilisha vema wanawake. Nyimbo zako zitadumu milele kwani ni tungo endelevu na ni mambo yanayoikabili kila jamii.

  Nina kanda zako nyingi sana ila ningefurahi iwapo ningepata nafasi ya kuhudhuria onyesho lako lolote. Kazi zako ni nzuri endelea dada, napenda mavazi yako na zaidi huwa NAKUONEA WIVU SANA KIFUA CHAKO YAANI SIO SIRI! UMEJALIWA! HALAFU UNAJIAMINI NA KAZI ZAKO NA MAISHA YAKO! HONGERA SANA NA UBARIKIWE DADA.

  VIBAO VYAKO NI MOTO HASA HIVI VIWILI:

  http://www.eastafricantube.com/media/142/K._Basil_feat_Bizzman_&_Stara_-_Riziki/

  http://www.eastafricantube.com/media/2287/nipo_kwa_ajili_yako–stara_thomas/

 16. Matty Says:

  Sasa kiona mbali mimi nimekosea nini na Any je alivyosema umesikia???

 17. Kekue Says:

  Nampenda sn anaimba vizuri, sauti yake ni nzuri mno alafu anapendezaga sana na nguo zake anazovaaga, Matty pamoja na kuwa anavaa kulingana na umbo lake huyu dada (mama) anajiheshimu sana kwa sababu kuna wengine wana maumbo mh yani Mungu nae jamani!!!!!!! akiamua kukuviringa anakuviringa haswa sasa waangalie wanavyovaa du!!! kwi kwii kwiii uuuwii mbavu zangu jamani!!! nakupa big up sn Stara na kila la kheri katika shughuli zako zote mamaaaa!!!!!!!!

 18. amina Says:

  Ally nakuunga mkono..mnataka kuniambia angekua na umbo dogodogo siangevaa uchi nayeye kama hao mashosti wanaojiuza kupitia mziki?mnacheza na wabongo nini

 19. twin Says:

  Kekue nawe umekosa cha kusema. Eti MUNGU AKIAMUA KUKUVIRINGAhivi wewe unaweza kuumba japo unywele? Acheni kumkufuru Mungu tafadhali, Mungu amemuumba kila mtu kwa mfano wake hakuna aliyeviringwa wala nini.

 20. Matty Says:

  Kekuu yaani nilivyosoma hapo ulivyoandika nikatokwa na machozi ya furaha maana sijacheka sikunyingi kwi kwi kwi kwi kwi!!!!!!!!!

 21. KionaMbali Says:

  Sawa Matty.
  Hujakosea. Nimekubali. Anavaa kulingana na Umbile lake

 22. Kalili Says:

  Kimori ulitaka maswali gani yaulizwe sidhani kama BC watakuwa na matatizo ukiwa na maswali muhimu unataka mtu aulizwe. Tukirudia hapa, Stara Big up my dear. you are the one huge role model to all especially tanzanian artists. Keep your head up. Peace.

 23. Kiatu Says:

  Kekue Muombe radhi Mungu wewe!

 24. Upendo Furaha Says:

  Jamani, ninaona mnamshambulia sana Kekue, lakini mkumbuke kuwa “Kila Mtu ana Mungu Wake”.
  Nawasilisha.

 25. Mama wa Kichagga Says:

  Eti “MUNGU KAVIRINGA WATU”, najitolea kumuomba Mungu msamaha kwa ukosoaji wa namna hii!

  Jamani busara na ufahamu ni kitu muhimu sana katika maisha!

  Tusiwahukumu wenzetu kwa maumbile hata siku moja maana hiyo ni kazi ya Mungu na isitushe “UZURI WA MTU SIO UKUBWA WA MWILI WAKE, WAWEZA KUWA SAUTI, KIUNGO KIMOJAWAPO KATIKA MWILI WAKE (KAMA KIFUA), MGUU, MACHO, AKILI YA KUCHAMBUA MAMBO, KIPAJI, HURUMA, UWAJIBIKAJI KATIKA JAMII/MCHANGO WA MAISHA YA JAMII, LUGHA, KICHEKO NK.

  KYEKUE, watu wote wameumbwa na MUNGU kuelezea mfano na sura yake hatupaswi kumkosoa Mungu wetu – Rekebisha mtizamo na fikra zako katika jambo hili. Jua kama wewe hupendi wanene wenzio wanawazimia dada! Kila mtu anayo ladha yake binafsi na ndio maana kila mtu yupo mahala alipopangiwa. Ukibaki kukosoa kosoa kazi za Mungu utaondoka hapa duniani bila kutimiza malengo uliyowekewa na Muumba hivyo usipoteze muda fanya mambo yanayokuhusu.

  “TUSOME VITABU MBALI MBALI ILI KUONGEZEA UFAHAMU WA KUISHI NA KUWAKUBALI WENZETU”

  Kila umbo la binadamu linafaa kwa shughuli yoyote ya kijamii au ya kimaendeleo ili mradi unafahamu namna ya kulitumia (kama vilivyo vyombo vya usafiri – mabasi, saloon, landrover, Rav 4, Suzuki, Benzi, Lorry, Caterpilar, Tren, Range Rover nk mtu anajipimia kulingana na ladha na uwezo wake). Wacha kuzarau kazi za Mungu na chaguzi za watu binafsi! Angalia mambo yako binafsi na acha kuhojihoji wenzio – INACHEFUA AU VIPI? ACHA HIZO NDUGU YAKU KUWA NA SOMA MAANDIKO VYEMA.

 26. Kekue Says:

  Mimi sijamkosoa Mungu ila ninamsifu kwa kuviringa watu wa aina mbali mbali!! Au siyo Mungu anayeviringa watu jamani He!!!!!!! mbona kinawauma sana??? au mmeviringwa? Tehe tehe

 27. msema kweli Says:

  Kekue tehe tehe na wewe una mambo!!!!!!!!! afadhali hii bc iwepo tuwe tunacheka manake maisha yako wapi???? achana na wanaochonga hapo juu!!!! Kitu kidogo tu wanakifungulia mada hao ndo wale ukiwauliza 1+1 wanakuambia 11.

 28. twin Says:

  Asante mama wa kichagga kwa maoni yako mazuri dhdi ya Kekue. Mimi binafsi sikufurahishwa pia na maneno yake. Kama yeye anaona hakuviringwaviriingwa ni heri kwake, lakini sisi sote tumeumbwa kwa mfano wa Mwenyezi Mungu.Kekue aelewe kuwa kabla hajafa hajaumbika. Amuombe Mungu radhi kwa kauli zake hizo.

 29. Mama wa Kichagga Says:

  Twin,

  Amen unaufahamu ndugu yangu na unasoma maandiko hukurupuki.

  Wote hapo wanalipiza visasi vya kijinga! Mmoja ni rafiki yangu wa mwaka jana alikuwaga anatoa hoja za upupu nikaona niende nae sambamba sasa karejea kwa mtindo wa kukandia. Jina lake la ubatizo ni ……..gwani hahahaaaaaaaaa. Hawa ni size yangu nitakula nao sahani moja hadi waelimike na wawe vioo vya jamii badala ya kupotosha jamii! Halafu sasa wananiuzi kweli maana hawasomi hoja kwa makini halafu hawana sera zaidi ya kukandia.

  Kwa ajili ya hoja zao za kutaka kuipotosha jamii, kukwaza wenzao wasitegemee kunikwanza na wategemee magazeti hapa kila siku maana uvivu wa kusoma sikujaliwa mie!

  Kekue, Trii, Msemaukweli kaeni mkao wa kupambana kwa hoja hadi kieleweke! 3:1

  KARIBUNI

 30. msema kweli Says:

  Lakini kekue wewe km ni mchaga nina wasiwasi na wewe manake wachaga bwana…….. wana shepu…….. tehe tehe!!! sitaki kuthema manake mama wa kichaga atanigeukia mimi hachelewi huyu mama!!

 31. Mama wa Kichagga Says:

  Msema kweli,

  We sema tuu usiwe na nizamu ya woga ili tukupongeze kama unatoa kitu kizuri cha kutuendeleza ama nikupake upupu kama unaleta jinga jinga.

  Shepu zetu tunazipenda sana na TUNAMSHUKURU MUNGU KWA KUTUPATIA HIZO SHAPE MAANA HAZIJAWAHI KUTUKWAZA POPOTE (TUNAHITAJIKA HATA NA THITHITHIIIII HUWA WANATUZIMIA KWA VICHEKO, UKARIMU, KUCHACHARIKA NA UP-STAIRS WAMO PIA)

  Hivyo wee sema tuu ili uweze kuelimika ndugu yangu (Dont shy away as you will be left behind)

 32. twin Says:

  Mungu amsamehe Kekue kwa maana hajui asemalo.

 33. mtz kinoma Says:

  She looks so beautifull,I respect her as a woman and actually ilove her toomuch D, U have a husband,please?
  If
  udnt pls lt me know .spcl regards. mtz

 34. Nerra Says:

  Yaani huyu amina! mmh kila mahali lazima aponde duu inaelekea yuko perfect sanaa, vijana kaza buti achana na hao wanaowachemsha bila kufikiri. Stara wewe uko juu hata ungekua ni mwembamba bado ungejiheshimu maana ndiyo tabia yako wangapi wanene na wanachemsha kimavazi na tunawaona mitaani?

 35. max Says:

  Big up girl. God bless you.

 36. Saidi Situ Says:

  Nimesoma nae mzizima huyu dada. Ingawa alikuwa amenizidi madarasa 4. Mimi naingia form 1 yeye ndiyo anaingia form 4. Namjua kwa vile alikuwa bingwa wa netboli kwenye house yetu ya rufiji enzi hizo.

 37. zaina seif Says:

  big up girl

 38. zawadi Says:

  Sio siri satara yuko juu ile mbaya ana sauti yenye mvuto anajiheshimu ni mzuri mavazi yake yanarizisha inapaswa akina dada wanaochipukia kwenye mziki wafwate nyayo zake kwa kuvaa mavazi ya heshima ili wakamishe uzuri wao kwani uzuri wa mwanamke ni pamoja na kujiheshimu sio kujiachia achia wazi kila mtu aone maumbile yako mwanamke kujihifadhi.

 39. binti-mzuri Says:

  ivi jamani,kufaa nguo ndefu ndio kujiheshimu??maana kuna wanaovaa mabaibui ila ukiwakuta kwenye nyedo zao,BALAA!

  dada stara nakuzimikia,big up

 40. zawadi Says:

  This is not problem binti-mzuri ishu ni kujistiri hata ukimkuta kwenye nyendo zake,elewa kwamba atakuwa na tofauti kubwa sana na wewe uliyevaa nusu uchi na pia si baibui tu ndo vazi la heshima hata vazi la kawaida linaweza kuwa la heshima kama dada etu Stara anavyovaa.

 41. anapendeza sana anavaa kulingana na mwiliwake na nguo zake ni za heshima big up stara

 42. mlekwa Says:

  ai laik this women bikoz she knows hau to help athaz and shi doing very good job to protekt all women in awar cantry this atatiyut wich mek mi raiting this coment if awar kantry hev this taip of pipoli will bi best kantry araund the world jast imejen hau wi kan devlop awar kantry if ol of as togethar

 43. Kitomari Says:

  Nimzuri kapendeza, anasifa zote nzuri, ila kaniudhi kuto taja mwaka wake wa kuzaliwa sijui anamaana gani.

 44. Marx Schmidt Says:

  Girl, you look good.
  Gime ya number or email plz

 45. Mary Mkwaya Malamo Says:

  unanifurahisha sana mama.

 46. watubwana Says:

  hahahahahahaha…….watu bwana,,,,,hahahahahaha,,,,,,,jamani kuna watu wanachekesha sana,,,,thanx kwa kuandaa hii blog.thanx wachangiaji wote.big up wote.stara mama keep it up my dear.


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s