BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

KWA KINA NA FREDDY MACHA-PART II February, 5, 2008

Tangu tuweke hewani sehemu ya kwanza ya mahojiano yetu na Freddy Macha wiki chache zilizopita,siku imekuwa haipiti bila kupokea barua pepe,simu au ujumbe mfupi kupitia simu za viganjani nk.kutoka kwa baadhi yenu wasomaji na wachangiaji wa BC mkitaka kupata uhondo wa sehemu ya pili.Hatuwezi kuwalaumu,tunaelewa ni jinsi gani Freddy Macha,iwe ni kupitia uandishi,ushairi na pia muziki,anagusa hisia za wengi.

Kama tulivyoahidi,hii hapa sehemu ya pili ya mahojiano yetu na Freddy Macha akizungumzia zaidi kazi zake za muziki,mambo mbalimbali ya kijamii na mengineyo kedekede.Kama ilivyo katika uandishi na ushairi,kwa upande wa muziki Freddy Macha pia kajaa tele.Anayo mengi ya kusimulia na kuweka wazi kuliko unavyoweza dhania.

Unataka kujua Freddy ametokea wapi mpaka kujikita kwenye sanaa ya muziki? Je una habari kwamba huyu bwana ni mtaalamu na mcheza karate wa kutupwa? Anasemaje kuhusu muziki wa kizazi kipya?Ana ushauri gani?Nini chanzo cha Kitoto Band?Je…

Mwisho wa mahojiano haya,utaweza kusikiliza baadhi ya nyimbo za Freddy akiwa na kundi lake lijulikanalo kama Kitoto Band.Hiyo ni zawadi maalumu kutoka kwa Freddy Macha na BC kwako msomaji,mchangiaji na hususani mpenzi wa muziki.Kwa hakika,kama wengi wenu mnavyopenda kusema,haya ni “mahojiano-shule”.Fuatana nasi;

BC: Unakumbuka nini zaidi ukifikiria historia yako katika ulimwengu wa muziki?Ulipokuwa mdogo ulipenda kuwasikiliza wanamuziki gani?

FM: Watu wa kwanza kuwasikia walikuwa wazazi wangu. Baba alikuwa akipiga gitaa na Mama akiimba. Mama pia alipiga gitaa. Wakati nikiwa mdogo walirekodi albam zao Kenya kwa hiyo rekodi zao zilikuwa zikipigwa TBC (Tanganyika Broadcasting Company) ilivyoitwa Redio Tanzania enzi za ukoloni. Baba anasema angekuwa mwanamuziki mkubwa sana lakini marehemu baba yake aliyekuwa mchungaji mkali hakupenda ashikilie uzi huo. Badala yake alifanya kazi ya uganga. Kila akirudi kazini wakati akisubiri chakula kiive, nakumbuka nikimwona na magwanda yake meupe ya uganga akicharaza gitaa, akijiburudisha na kutuburudisha.

Nikiwa darasa la kwanza wazazi hawa hawa walitufundisha namna ya kucheza mitindo ya miaka ya sitini : chachacha, rumba na pachanga. Nakumbuka nyimbo hizo zilizokuwa katika santuri zilizoitwa 78 RPM zilikuwa za wanamuziki toka Kenya : Daniel Gatuga, Phil Karashani, Peter Tsostsi wa Afrika Kusini. Tulipewa zawadi tulipocheza vizuri. Baada ya muda mfupi baba na mama walianza kunipeleka kuona sinema pale Plaza na Everest mjini Moshi. Mtu aliyesisimua mwaka 1963- 64 alikuwa mwimbaji wa Kimarekani, Elvis Presley. Nilikuwa darasa la pili. Kumwona tu alivyochangamsha dimba na gitaa lake, nikaamua na mimi nataka kuwa mwanamuziki.

Kitu kingine nilichopenda ilikuwa ngoma ya Wachagga iliyoitwa “Mtingo.” Ngoma hii ya “Mtingo” ilirembwa na pembe ndefu ya ng’ombe na nilipowaona wale wazee pale Mgombani ilinisisimua sana. Miaka mingi baadaye nilitunga nyimbo nyingi kufuatilia mapigo yake.

Redioni kila aina ya muziki ulikuwa ukipigwa. Nikiwa darasa la nne mwaka 1965 nilikuwa nikipanga “Kumi Bora” ukutani. Walipigwa wanamuziki wa Bongo: Kilwa Jazz, Western Jazz (wana Saboso), Dar es Salaam Jazz ( Mundo) Wazaire (akina Franko, Johnny Bokello na Dk Nico Kassanda) Miriam Makeba wa Afrika Kusini na Beatles toka Uingereza. Wimbo uliovuma wakati huu ulikuwa wa Franko ulioitwa “Polo.” Polo likawa kuwa baadaye neno la Kiswahili lililoimanisa kuchacha, ulofa au umaskini. Wote hawa niliwahusudu. Toka nikiwa mtoto nilianza kupenda miziki niliyosikia lakini kilichosukuma ari ilikuwa wazazi. Familia ya Macha ilipenda sana muziki. Shangazi, Mama wadogo, Wajomba, Baba wadogo wote walipenda kucheza dansi na kwao kulikuwa na kila aina ya muziki. Wachagga lakini tulipenda sana muziki wa Kizungu. Kwa hiyo miaka yangu ya kwanza nilisikiliza zaidi miziki ya kutoka Ulaya na Marekani.

Nilipokuwa Mzumbe kidato cha tano, mwaka 1973, nilianza kupata mwamko wa kisiasa na kutaka kubadilisha jina langu la Kizungu. Nilipowauliza wazazi kwanini waliniita “Frederick” waliniambia ni kwa ajili ya mwanamuziki wa Kizungu, Nina na mkewe Frederick waliovuma wakati nikizaliwa. Hiyo ilinipa ishara kuwa wazazi walishataka niwe mwanamuziki.

Nilipoanza kujifunza gitaa nikiwa kidato cha pili, Ilboru, mwaka 1970, Baba alikuwa mbele kunifundisha na kunipa moyo. Mjomba wangu marehemu Harrison Mlinga alikuwa mtu wa kwanza kunipa gitaa. Baadaye nilipounda kikundi cha Sayari, Dar, mwaka 1980, Mama alikuwa akihudhuria maonyesho yetu na kutushangilia.

Kwa hiyo n’kitazama nyuma, familia ilikuwa chimbuko kuu la mapenzi yangu ya muziki…

BC: Muziki ni sehemu muhimu sana ya maisha kwa Waafrika walio wengi.Umetumika kuburudisha,kuelimisha,kuonya nk.Kwako wewe binafsi,muziki una nafasi gani?

FM: Watu weusi kwa ujumla tunasemwa kuwa tuna muziki na ridhimu katika damu. Muziki wa watu weusi ndiyo unaotawala dunia ingawa projuza maarufu wa Kimarekani, Quincy Jones (aliyekuwa akimtoa Michael Jackson enzi akiwika) kasema ingawa sisi weusi ndiyo chimbuko la muziki wa “pop” duniani wanaochuma na kutawala kiuchumi bado ni wazungu. Wasanii matajiri wakubwa wa muziki ni weupe na wao ndiyo wanaofaidi kifedha pia. Majina makubwa kama Elvis, Beatles, Rolling Stones na Madonna ni ya wazungu. Hadi leo wanamwita Elvis “mfalme wa Rock” ilhali hiyo Rock and Roll ilianzishwa na wanamuziki weusi akina Chuck Berry, Little Richard, Fats Domino na James Brown (babu wa Hip hop) miaka ya Hamsini.

Waafrika tumechangia sana katika utamaduni wa muziki hususan karne ya 20 ambapo watumwa toka barani wamekuza muziki wa pop ulioanzia na mahadhi ya Blues. Blues imechanganya ngoma na jazz kuzaa rock and roll, soul, funk na hatimaye leo, hip hop.

Kwangu, muziki ni sehemu mahsusi ya kujieleza, kuandika na kuishi. Ndiyo maana sitenganishi Fasihi , (uandishi wangu) na utunzi wa muziki. Maonyesho yangu siku zote huchanganya muziki na fasihi. Mseto huu ulianza kupea wakati nikiwa mwanakikundi wa Sayari tulichokiunda Dar es Salaam mwaka 1980 na kuendelea kufanya maonyesho hadi mwaka 1984. Sayari ndiyo iliyonitoa Bongo na ilichanganya ushairi, dansi, muziki wa mseto na maigizo mafupi ya haraka yenye ujumbe, maonyo na visa mapenzi.

Baadaye nilipokwenda Brazil kusoma na kuishi (1988 -1994) niligundua jinsi ambavyo wanamuziki kule ni wasomi. Jambo nililozoea nyumbani ni kuwa mwanamuziki ni mpiga chombo tu lakini kule nilikuta wanamuziki wengi na shahada zao wana ujumbe mkali wa kifasihi na kifani. Pia muziki si lazima uwe wa bendi ya watu wengi kama kwetu. Brazili zipo shoo chungu nzima za msanii mmoja na gitaa lake kajaza uwanja au ukumbi. Muhimu ni thamani na uzito wa ule muziki si kiasi cha wapigaji.

Kwa hiyo hadi leo msimamo wangu ni kuwa muziki ni sehemu mahsusi ya elimu, starehe na fasihi. Kazi ya muziki si tu kustarehesha bali kusaidia kugeuza jamii na kuleta maendeleo ya kifikra na kimaisha.

Kati ya wanamuziki wakubwa ninao wahusudu ni wale wenye mseto na msimamo huo: Gilberto Gil na Caetano Veloso (Brazil), Gil Scott Heron na Bob Dylan (Marekani), Fela Kuti (Naijeria), Francis Bebey (Kameroon) , Miriam Makeba (Afrika Kusini) na wanamuziki wa reggae akina Bob Marley na Steele Pulse.

BC: Kwa muda mrefu sana kumekuwepo na tatizo la muziki wa Tanzania kutouza sana kimataifa hususani ukilinganisha na wanamuziki kutoka nchi zingine.Pia tumekuwa hatujulikani sana linapokuja suala la muziki ulimwenguni.Unadhani hii inatokana na nini?Unashauri nini kifanyike?

 

FM: Tatizo hili limeniathiri mimi mwenyewe nikiwa kama mwanamuziki wa Kitanzania ninayeishi ughaibuni. Wakati nikiishi nyumbani na kipindi nikiwa na Sayari hatukuwa na studio au nyenzo za kutoa muziki. Kwa hiyo wanamuziki wengi wa Kibongo walihama au wakarekodi nchi za nje. Magwiji wakubwa Salum Abdullah (aliyefariki mwaka 1965) na Mbarakah Mwinyishehe a(aliyefariki 1978) walilazimika kwenda kurekodi Kenya. Hata mzee wangu mwenyewe niliyemsema awali alikuwa akisafiri hadi Mombasa kwa hela yake kurekodi miaka ya Hamsini.

Kutokana na tatizo hili hatukuuza muziki. Mwanamuziki wa kwanza kuuza au kutengeneza CD alikuwa Mzaire, Remmy Ongala, ambaye alihamia Bongo na ari na moyo wa Kitanzania, akaimba Kiswahili na kubeba bendera yetu. Hata muziki wake aliuta “Bongo Beat.” Mwingine alikuwa wa jadi, marehemu Hukwe Zawose, aliyepiga marimba ya Kigogo na kutupa sifa nje. Hawa leo ndio wanaojulikana kimataifa kama wanamuziki wenye Sauti au Lahaja ya Kitanzania.

Wengine wote ama tunapiga mitindo yenye mseto wa Kikongo, Reggae au hii Bongo Fleva. Matokeo hatuna staili maalum.

Lakini wenzetu wa Kenya (ambao hawajatuzidi kimuziki) wana moja. Wanachotuweza ni kuimba Kiswahili na pia kushirikiana. Mmoja akianza mtindo, wenzake nao wanauipiga mtindo ule ule. Wazaire hivyo hivyo. Mmoja akianza “Ndombolo,” wengine wote wanaingia wanapiga hiyo hiyo “Ndombolo.” Wanaijeria hivyo hivyo. Mmoja akipiga “Afro-beat” (Fela) wenzake wanapiga hiyo hiyo “Afro Beat.” Wasenegal hivyo hivyo : mmoja akipiga “Mbalax” wengine wote wanaingia katika “Mbalax.” Matokeo taifa linakuwa na Sauti na Lahaja moja ya muziki. Karibu miaka arobaini na kitu sasa kila mwanamuziki wetu anataka kuwa na staili yake. Mwingine Saboso, mwingine Mundo, mwingine Afrosa, mwingine Sikinde; wanaofuatana ni Wanataarabu tu.

Leo vijana wa Bongo Fleva ( muziki wa Kizazi Kipya) wana sauti na mapigo ya aina moja. Haya ni mabadiliko mazuri sana. Pili, nyumbani leo kuna studio ambapo miaka ishirini iliyopita wakati nikiishi Bongo hatukuwa nazo.

Ila, tatizo lililopo, ni hili. Wengi hawajifunzi muziki. Wanachofanya ni kurapu au kuandika maneno yaliyo katika ushairi. Hiyo ni safi sana, lakini, haitoshi. Muziki unataka kujifunza ala fulani. Kujifunza ala ya muziki kuna maana kusomea kuandika, kwa kukuuza fani ya uandishi, kusomea kuimba kwa kujifunza mantiki ya mapafu, pumzi na koo; pia, kupiga vyombo sawasawa. Watunzi, nchi zilizoendelea mathalani husoma vitabu vya fasihi; je kwetu wanamuziki na watunzi wangapi wanaoona haja ya kusoma mashairi na riwaya? Na je, utaendelezaje lugha yako kama husomi riwaya mashairi (fasihi)?

Nilipokuwa nikiishi Brazil, niligundua kila mwanamuziki anakwenda kusomea nadharia ya muziki. Hakuna eti ile kusema mtu una “kipaji cha kuzaliwa.” Haitoshi tu kuwa na “kipaji cha kuzaliwa” maana muziki ni sayansi. Pale ambapo tutaanza kupata wanamuziki wanaojibidisha kufanya hiyo kazi ya uanamuziki basi tutaanza na sisi kujulikana shauri tunaanza kuwa na sauti moja.

 

Freddy akipiga ngoma ya Kibrazili iitwayo Pandeiro, karibuni. Ngoma hii ni muhimu katika mchezo/ mapigano yaitwayo Kapoeira ambayo alijifunza kwa undani akiishi Brazili mwaka 1988-1994. (Picha na Sia V. Macha).

BC: Hivi sasa nchini Tanzania kuna huu muziki unaoitwa muziki wa kizazi kipya.Pamoja na mafanikio ambayo aina hii ya muziki imepata,kumekuwa makundi mbalimbali ambayo yanaupinga yakisema hauna uasili,ni wa kihuni nk.Nini maoni yako katika hili?Na unadhani kuna nchi duniani yenye muziki wake wa asili kabisa bila kuchukua vionjo kutoka hapa na pale? Unautofautishaje muziki huu wa kizazi kipya na ule wa zamani?

FM: Kila nchi duniani imeparamia muziki wa “Hip Hop” ulioanzia Marekani. Marekani imekuwa chimbuko la miziki ya pop kutokana na sababu nilizosema awali za kuwa watu weusi waliohamia kule wameuendeleza kihistoria ( mseto wa Blues na ngoma). Halafu, Marekani kama nchi tawala tajiri duniani inahodhi na kutawala utamaduni wa dunia. Kila kitu kinachotoka Marekani kinapewa hadhi na kusukumiwa nchi changa (watu maskini) kwa maguvu kupitia vyombo vya habari, sinema za Hollywood na hata mitutu ya bunduki (vita vya Iraki ingawa vya kikatili vinaelezwa ni vya kuleta amani na kuondoa ugaidi). Kwa hiyo vijana duniani wanakua wakihusudu mtawala huyu anayetumia lugha inayovutia macho lakini kiundani haina upendo wala jamala.

Muziki huu umekuuzwa pia na biashara ya kuuza sura na wajihi fulani wa watu weusi Marekani ambao hawana furaha wala raha na maisha yao. Upinzani wa maisha ya kuteswa na kunyanyaswa umekuuza tabia ya kuvaa na kusema na kurapu kinamna fulani ambapo kwa jadi na mtindo wa maisha yetu havifanani.

Vijana duniani wanapenda kuiga mtindo huu shauri kila jamii duniani inayo matatizo dhidi ya utawala, wazee na jamii. Baadhi ya tabia kama kujipenda, kujiamini au kupinga udhalimu si mbaya hata kidogo. Ila kuna mambo ambayo hayajafafanuliwa sawasawa. Mfano mkubwa ni ile tabia ya kuvalia suruali makalioni ambapo hatuelezwi ukweli kuwa ni mtindo ulioanzia kwa wasenge weusi wa Kimarekani miaka ya 1930. Vijana wengi wanadhani ni “ubabe” ulioanzia kwa wafungwa, jela. Hawaelezwi kuwa tabia ya ufirauni ilianzishwa na wasenge weusi wa Kimarekani waliokuwa wakijificha vichochoroni miaka hiyo themanini iliyopita, enzi ufirauni ukikatazwa kisheria. Wasenge walijionyesha kwa kuvalia suruali matakoni kujitambulisha kwa firauni wenzao. Hoja hii imeelezwa vizuri pia na msenge mshoni mmoja aliyeandika katika gazeti (la watu weusi) la “Voice” miaka michache iliyopita hapa Uingereza. Usenge hii leo umekubalika Uzunguni na kupitishwa na sheria za kiserikali kuwa tabia inayokubalika. Kwetu si mila wala desturi. Kidini pia zinapingwa na viongozi wanaosema ni dhambi. Uingereza mathalani imepitishwa sheria ya kifungo cha miaka saba kwa mtu atakayetumia dini kupinga ufirauni.

Hiyo moja. Kuna tabia za kuwaimba wanawake na kutukana ovyo. Haya ndiyo mambo ambayo hip hop imewafanya wengi Tanzania (na pia nchi nyingine) kutopenda utamaduni huu wa dharau na usenge. Kuhusu kuiga. Kila msanii anaiga mahali. Lakini kuiga kunataka pia ugunduzi. Nikirudi tena Brazili. Utagundua kuwa wao wanapoiga wanaweka utamaduni wao, wanapachika muziki wao wa Samba na hisia zao. Matokeo Brazili kila siku inagundua mitindo mipya ya muziki. Sisi tunapashwa kujua moja. Kila mtu duniani anaiga. Ila tunapoiga iwe hivi. Asilimia 20 uigaji na iliyobakia asilia yetu. Wenzetu wa Afrika Magharibi wametupita kwa kuwa wanathamini sana utamaduni, mila na desturi zao. Matokeo sasa hivi kuna wanamuziki wengi wa Afrika Magharibi ndiyo wanaobeba bendera ya muziki wa Kiafrika duniani: Salif Keita, Baaba Mal, Angelika Kidjo, Youssou Nd’our. Na hawakuanza leo. Miaka ya Sabini bendi maarufu ya Osibisa ilitingisha ulimwengu nzima. Ilichanganya ngoma asilia za Kighana, muziki wa Soul na kuunda kitu kipya kilichoitwa “Afro-Rock.” Waliheshimiwa.

Kuhusu muziki wa sasa na wa zamani siku zote kutakuwa na zogo kuwa wa zamani ni bora kuliko wa sasa. Lakini si kweli. Muziki wa zamani ulikuwa na mambo mazuri na mabaya jinsi ambavyo ulivyo wa sasa. Tofauti kubwa hata hivyo ni ile niliyosema kuwa wanamuziki wengi wa kileo hawasomei, hawajifunzi kupiga muziki sawasawa. Wanamuziki wa zamani walikaa siku nzima wakitia tizi, matokeo melodi zao zilikuwa za kuvutia, ilhali leo mashine zinatumika kutoa ridhimu za kupendeza. Muziki mzuri( popote pale duniani) ni ule unao-oanisha melodi murua isiyosahaulika, ridhimu na ujumbe uliopangwa (“arrangement”) vikapangika. Wimbo ambao kila mtu yeyote (bila kuchagua kabila, umri au jinsia) akisikia anataka kusikiliza tena na tena; hausahau. Muziki mzuri kama ndege anayeimwimbia Mungu.

 

Freddy Macha akitumbuiza mashairi kwa muziki wa Berimbau, shule ya Sekondari, Malory, mjini London, mwaka 2002. Kwetu Bongo, Berimbau inaitwa “Mandondo” na hupigwa haswa na Wagogo. Ala hii ya Kiafrika ina zaidi ya miaka 5,000 na hutumiwa katika muziki wa mapigano yaitwayo Capoeira,mchezo uliokuuzwa na watumwa wa Kiafrika, Brazili.

BC: Kwa upande wa muziki huu wa kizazi kipya,Bongo Flava,kuna wanamuziki wowote ambao unawafuatilia na kuzipenda kazi zao?Ni kina nani hao?

FM: Mimi ni mpenzi wa wanamuziki wanaotunga na kujibidisha kupiga chombo fulani. Mwaka 2006 nilimwandika magazetini (katika safu zangu za Mwananchi na Guardian) mtunzi na mwimbaji kijana, Vitali Maembe. Ninachompendea Vitali ni hili. Kachukua muda kutafiti mapigo (au ridhimu) mbalimbali ya Kibongo na kuchanganya na utunzi wake wa kisasa. Haigi tu mapigo ya “hip hop” ya nje na kuishia hapo hapo. Halafu maudhui ya nyimbo zake yana ujumbe wa maana na ushairi umepangika. Vile vile kapanua hadi kutunga nyimbo zenye lafudhi za Kiswahili fasaha kama ule anaoshangilia Asalaam Aleikum ya Waislamu, visiwani. Utaona pia ma-DJ wetu walivyo na kasumba. Maembe alipoanza shughuli zake vyombo vya habari havikumjali wala redio hazikuupiga muziki wake shauri haimbi matusi wala upuuzi wa kibangi bangi.

Mara moja moja hupenda nyimbo fulani kwa kuwa imefanyiwa kazi ikaiva. Nilipenda sana Lady JD alipourekodi wimbo wa zamani wa marehemu Shabani Marijani, “Si Wema”, katika mtindo wake mwenyewe. Mtindo wa kuimba nyimbo zilizotungwa na wasanii wa jamii moja, kuimbiana na kujengana umeenea nchi nyingi duniani. Sisi Bongo hatufanyi hilo. Kila mmoja na lwake. Mfano wa Lady JD unastahili kuendelezwa na sisi wanamuziki wote.

Au ule wimbo unaoitwa “Kikombe” uliotoka mwaka 2006. Nikuchekeshe? Nilikutana na mtunzi wa “Kikombe” katika basi mwaka jana wala sikujua ni yeye. Baadaye nilipoambiwa ni yeye nilijilaumu kwanini sikumpongeza, ingawa nilimsalimia… “Kikombe” umefinyangwa ukafinyangika; sauti nzuri maneno ya kupendeza yenye maana nyingi kufuatana na mtazamo au akili ya msikilizaji. Huo ndiyo utunzi bora. Unakumbusha nyimbo maarufu za marehemu Patrick Balisidja; au nyimbo za zamani za mapenzi za Wanataarabu; mathalani “Kapu” (Shakila) na “Sabalkheri” (Asmahani). Fasihi ya Kiswahili ikidundana kimapenzi na muziki.

BC: Ungependa kuwapata ushauri gani vijana,hususani wanamuziki wa bongo flava?Nini wanatakiwa kufanya ili kuhakikisha kwamba muziki wao unadumu vizazi mpaka vizazi tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo miziki mingi ya bongo flava inaingia katika historia ya kupoteza ladha na msisimko kwa kasi kuliko aina zote za miziki zilizowahi kutokea nchini Tanzania?

FM: Kijumla katika miaka 15 iliyopita muziki dunia nzima umechuja na kuwa hafifu sana ukilinganisha na utunzi kabambe wa miaka ya Sabini. Hata huku nchi zilizoendelea redio na runinga hazipigi muziki uliokomaa. Bendi zinazowika hasa za Kizungu zimetengenezwa tu (“manufactured music”) ili kuuza huu uchafu. Kwetu Afrika hatutakiwi tuwe vile maana sisi ndiyo chimbuko la muziki duniani. Hivi tunavyoongea kila mtu anaangaza macho Marekani ya Kusini na kutamkiwa na miziki ya Kilatino hususa “Samba” ya Brazil na “Salsa” ya Kyuba. Uhaba huu unaridhisha kuwa Walatino ndiyo wanaotimiza kanuni za utunzi na ugunduzi wa muziki bora.

Je, Tanzania tufanye nini? Ushauri nimeshausema hapo juu kwa kutoa mfano mdogo wa kile Vitali Maembe na Lady JD walichojaribu kukifanya. Kwanza muziki si maneno tu au kupiga kelele na kuiga marapa wa Kimarekani. Hata baadhi ya hawa marapa wa Kimarekani wameanza kugundua kuwa muziki wao umesinyaa. Puff Diddy kaanza kuangalia melodi na kutunga nyimbo zisizo na matusi au dharau. Rapu inasemekana ina makelele shauri wale wanaoitunga wana hasira, wanatukana wanawake na kuzungumzia kupigana na mauaji. Muziki si kelele bali sanaa ya kutuliza moyo, kuleta amani na mapenzi duniani. Wanamuziki wetu wanatakiwa wafanya utafiti zaidi.

Pale ambapo vijana wetu watakaporudi katika asilia yao (kama walivyo Afrika Magharibi) na kuanza kutafiti utajiri wa muziki wetu na kuanza kujifunza nini muziki ndipo tutakapoona mabadiliko.

Mwaka 1980-84 nilipokuwa na Sayari tulikaa siku nzima tukifanya mazoezi ya mwili na vyombo. Tulisikiliza ngoma, nyimbo na kutia tizi. Kama ukikosea unasahihishwa. Bendi kubwa za zamani hii leo nyumbani kama “Tanzanites” na “Wana njenje” bado zinashika uzi huu. Muziki ni kazi.

 

Freddy akipiga kinanda cha umeme (keyboards) na bendi ya Os Galas, mjini Rio Je Janeiro, Brazil, mwaka 1988. Alikuwa na bendi hii kwa miaka mitatu na kuboresha sana ujuzi wake wa kuimba na usanifu wa vyombo (Picha na Clori Ferreira).

BC: Sasa hebu tuambie kidogo kuhusu bendi yako ya Kitoto Band?Kwanini uliamua kuiita Kitoto?Ina wanamuziki wangapi? Maonyesho yenu huwa mnafanyia wapi zaidi?

FM: Nilikuwa Brazil mwaka 1988 nikapata barua toka kwa mtunzi maarufu wa zamani Bongo ( ingawa hajulikani siku hizi kwa wengi) James Mpungo ambaye zamani aliongoza bendi ya Sunburst iliyowika sana Dar es Salaam mwaka 1970-75. Bendi ya Sunburst ilitumbuiza pia sherehe za uhuru wa Msumbiji mwaka 1975. James na mwenzake marehemu Kassim Magati (mpiga piano) walikuwa wakichukua ngoma za jadi za Kitanzania na kuzipiga katika mapigo ya kisasa. Walikuwa wakijaribu kufanya jambo ambalo bendi maarufu ya Osibisa ilikuwa ikilifanya. Mpungo na Magati walikuwa wanamuziki wazuri sana (nimesahau majina ya wenzao wawili lakini nao walikuwa wakali sana). Mpungo ni mtunzi na mwimbaji mzuri na kwao ni kusini kabila Mngoni. Marehemu Magati alikuwa Mzaramo na alichukua ngoma za pwani, kama Ukuti, ndiyo maana Sunburst ilinisisimua sana kama mwanamuziki. Sasa niko Brazil mwaka 1988 nasomea muziki. Ikaja barua toka kwa Mpungo. Nilipopokea ile barua kwa kuwa nilikuwa ugenini, nikasisimkwa na kuandika wimbo wa Kitoto kama heshima yao kaka zangu hawa wa Sunburst. Baadaye wimbo huu wa Kitoto ukawa jina la bendi yangu.

“Kitoto Band” ilizaliwa nikiwa bado mjini Rio de Janeiro, mwaka 1991. Madhumuni yake ilikuwa kukusanya wapigaji waliopenda kupiga mitindo mbalimbali ya muziki. Hadi leo imekuwa hivyo. Mimi mwenyewe napenda kusikiliza na kupiga miziki ya mitindo mbalimbali kuanzia ngoma za kiasili hadi jazz.

Kitoto basi ni bendi ya mseto wa miziki ya Kibongo, ndombolo, soukous, rapu, reggae, jazz, samba na inao wapigaji saba na wachezaji steji shoo wawili, wakataji viuno na ngoma. Kitoto Band imeitwa shule ya muziki kwa kuwa wengi waliopitia kupiga nasi wamejifunza sana. Wamekuja kupiga na bendi kubwa. Yuko mmoja leo anapiga na Ricky Martin, mwanamuziki mashuhuri wa Kimarekani mwenye asili ya Ki-puerto Rico. Kitoto pia hubadilika kufuatana na mahitaji ya wateja. Mara nyingine tunaweza kuwa wawili, tukipiga ngoma tupu, watatu tukipiga jazz wanne au shoo kubwa kabisa.

Kwa hapa Uingereza shoo zetu nyingi ni zile za pati za faragha: arusi, sherehe za kuzaliwa na pati za vijana katika vyuo mbalimbali, kwa jumla. Wateja wanatupenda shauri sisi hupiga mitindo ya mseto na kazi kubwa ni kuwafanya wateja wacheze na kufurahi. Hizi shoo za namna hii zina malipo mazuri maana mabaa na vilabu hayana maslahi,hutegemea tiketi za mlangoni. Kwa namna maisha yalivyo aghali Ulaya huwezi mtu kulipia bili na chakula kwa shoo za mabaa na kusubiri wateja wa mlangoni.

 

Kitoto Band, bendi yake Freddy(pichani mwenye suruali ya njano) aliyoanzisha mwaka 1991. Bendi hii inao mseto wa kimataifa na kimuziki na hutumbuiza shughuli za karamu za binafsi na arusi. (picha na Barry)

BC: Ni onyesho gani ukiwa na Kitoto Band ambalo hutolisahau kamwe?Ilikuwa wapi na kwanini hutolisahau?

FM: Lazima nisisitize kuwa si shoo zangu zote ninazofanya na bendi ya Kitoto tu. Mara nyingine hupiga peke yangu kutumbuiza watoto mashuleni, wafungwa katika jela wagonjwa mahospitalini, makanisani, hata barabarani na vichochoroni. Huo ndiyo uzuri wa kazi ya muziki huku Ulaya, kinyume na nyumbani ambapo muziki ni wa mabendi, mabaa au maholi tu.

Pia mimi hufanya kazi kama mwanamuziki anayeimbia au kupiga ngoma na nyombo vingine kwa bendi kadhaa za watu wengine. Hii ni kazi ya malipo inayoitwa pia “session work.”

Ila kujibu swali lako, kumekuwa shoo ambazo nimezifanya zikafana sana. Mojawapo ilikuwa kando ya mto Thames hapa London, nje, ambapo pati ilikuwa vijana wa Kizungu waliokuwa wakipinga uchafu wa mazingira, mwaka 2003. Kila mtu alikuwa akipiga kelele na wapigaji tukafurahi sana.

BC: Wakati tukisaka habari zako mtandaoni tuligundua kwamba umeshafanya maonyesho na wanamuziki kadha wa kadha ulimwenguni na wenye majina makubwa kama kule Brazili na hata Uingereza unapoishi hivi sasa. Ni wanamuziki gani barani Afrika wanaokuvutia zaidi? Kwanini?

FM: Nafikiri nimeshawataja juu ila nitafafanua kidogo zaidi. Nyumbani waimbaji wa Taarabu, Asmahani na Shakila, kisha wapiga ngoma wote wa jadi na asili. Marehemu Hukwe Zawose ni mmoja wanamuziki ninaowahusudu hasa kwa utunzi, sauti na nguvu zake. Yeye ni kipimo kama mtu unataka kujua nini asili ya muziki wa Kitanzania. Marehemu Patrick Balisidja pia nilimuusudu sana hasa kwa melodi zake za Kigogo na ki Afro kisasa. Halafu kuna hawa Wazaire waliohamia Tanzania, King Kiki kwa melodi na sauti yake (hana bahati Kiki lakini ni mwanamuziki mzuri sana); Remmy Ongala (ambaye niliwahi kumwandikia kitabu mwaka 1985) namuhusudu kwa utunzi wa maneno, ucheshi na kuihakiki jamii. Ukiingia barani: Miriam Makeba, mpiga gitaa wa Kikongo, marehemu Dk Niko Kassanda, bendi ya Osibisa yenye asili ya Ghana (hadi leo wanawika hawa wazee), Fela Kuti kwa msimamo wake wa Kiafrika, Salif Kaita kwa sauti yake asilia, Pierre Akendengue wa Gabon, mwanamuziki kipofu ambaye wengi hawamjui lakini amekuwepo miaka mingi sana. Pia nawapenda waimbaji wa Kiarabu toka Misri, Algeria na Moroko na Mmisri maarufu, marehemu, Oum Kulthum. Waarabu wanajua sana kughani sauti na huimba kwa hisia kali sana: wanaume kwa wanawake. Hapa London mara nyingi hupiga na M-Algeria Farid Adjazairi ambaye ni mzawa wa Algeria anayetwanga Oud na muziki unaoitwa Berberai wa kuchungia kondoo na mbuzi kwao.

 

Gwang (toka Grenada), Freddy na ngoma ya Kibrazili ya Pandeiro na Tina Binder mwimbaji wa Kitoto toka Japan. Baada ya gigi la chakula cha mchana, Jumapili, hoteli ya Great Eastern, Liverpool street, Londonm Mei, 2007. Maonyesho mengi ya Kitoto huwa katika mahoteli, pati au sherehe za binafsi. (Picha na Tom Brasil)

BC: Mbali na uandishi na uanamuziki, wewe pia ni mtaalamu wa mchezo wa karate,(na jamii zake) na pia mpenzi mkubwa wa mazoezi. Nini kilikuvutia kuingia katika michezo hii? Una ujumbe gani kwa wasomaji wa mahojiano haya kuhusu mazoezi,afya nk?

FM: Hili ni swali zuri na muhimu sana. Afya ya mwili kwangu ni kitu cha kwanza kabisa. Kuna usemi ulioenea Magharibi unaoitwa “Wewe ni kile unachokula.” Kama unakula sana matope utakuwa matope. Ila kula peke yake hakutoshi, ni kama kuwa na nyumba ikaharibika bila kuikarabati. Ukichunguza maisha ya watu wengi walioendelea maishani watakwambia huwa na mchezo fulani unaowapa nidhamu. Alipokuwa jela Nelson Mandela alifanya Yoga na ngumi. Mwanamuziki maarufu Bob Marley alicheza mpira. Mwanamuziki mpiga tarumbeta wa jazz, hayati Miles Davis alikuwa akichora na kucheza ngumi. Ngumi ndiyo iliyomfanya Miles akaacha kunusa unga na madawa mengine ya kulevya. Hakuna kitu muhimu kwa mtunzi na msanii kama michezo. Michezo huurutubisha mwili na kujenga hisia na akili. Wasomaji na watu unaowasterehesha msanii ni watu wanaojifunza kutoka kwako, huwezi tu kutegemea akili ya Mwenyezi Mungu; lazima ujipende. Ndiyo maana makala zangu nyingi nyumbani na hata ughaibuni husisitiza juu ya afya ya mwili na kujipenda zaidi.

Moja ya kazi zangu kubwa hapa Uingereza ni kufundisha na kabla sijaanza warsha fulani iwe ngoma au kuandika hupenda kuwachangamsha vijana kwa mazoezi ya mwili. Kwetu nyumbani wengi bado tunadhani mafanikio maishani maana yake ni tumbo kubwa (kitambi) na kulewa pombe. Ukweli tungekuwa tunafanya mazoezi tungeishi maisha marefu zaidi ; lakini ukiangalia wastani wa urefu wa maisha yetu ni miaka 44-46; ilhali wenzetu nchi zilizoendelea wanazidi kusonga mbele washafikia miaka 75-80.

Nikiwa mtoto nilicheza mpira, baadaye sekondari nikawa mkimbiaji wa mbio ndefu. Nilianza kucheza ngumi nikiwa jeshini na mwaka 1973-74 tulianzisha mchezo wa Karate (Goju Ryu ya Okinawa Japani) pale nyumbani chini ya mwalimu Bomani toka Marekani, shule ya Zanaki. Mchezo huu ulitufundisha kuwa na nidhamu na kupambana na maisha. Baadaye nilipokwenda Brazili nilijifunza Kapoeira ambayo ni mseto wa mapigano, sarakasi mieleka na hutumia pia muziki wa kijadi unaoitwa Berimbau. Nchini Brazili, Kapoeira inachukua nafasi ya pili baada ya mpira kama sehemu ya utamaduni.

Karibuni mimi na wenzangu London tutafungua shule ya watoto na wazazi wao kufundisha kujikinga kusaidia mauaji yanayowapata vijana hasa kwa visu, mjini hapaa. Baadaye ndoto yangu kuu ni kufungua shule kadhaa za aina hii nyumbani, Bongo.

Ninaamini kila Mtanzania na Mtu Mweusi duniani lazima ajitayarishe kujihami kwa kujifunza Masho Ati. Dunia bado imejaa ubaguzi. Leo Ulaya Mashariki kuna vikundi mbalimbali vya wazungu vinafanya mazoezi kuwapiga watu wasio weupe. Makundi haya ya mkono wa kuume (manazi) hufanya mazoezi makali (tena vizuri sana) na mara nyingi Waafrika wamepigwa (wengine kuuawa) nchi hizi. Miaka ya karibuni Watanzania wamepigwa wengine kuuawa ugenini.

Mwanzoni mwa mwezi Januari, waandishi wa habari wawili wa Mwana-Halisi walipigwa na majambazi waliolipwa na vigogo, mjini Dar. Sisiti kusema kuwa wangejua kujihami wangenusurika angalau kiduchu. Msomaji ukitaka kujua zaidi mambo haya pitia blogu langu la kitoto.wordpress.com.

 

Freddy akifanya mazoezi ya Kichina kwa ajili ya pumzi, mapafu, uwiano na afya yaitwayo Tai Chi Chuan mwituni, Uingereza. (Picha na Amita T. Macha).

BC: Wewe ni mwandishi na pia mwanamuziki. Unadhani kuna uhusiano gani kati ya fani hizi mbili? Usingekuwa mwandishi au mwanamuziki ungependa kuwa nani?

FM: Nisingekuwa msanii ningependa sana kuwa askari. Naipenda ile nidhamu yao makachero na walinzi wa jamii. Napenda sana kazi ya polisi na kutunza amani katika jamii.

Sioni ukinzano, utofauti wala sipendi kutofautisha fani ya fasihi na muziki, shauri toka utotoni nimekuwa nazifanya zote pamoja. Hata wasanii ninaowapenda sana katika fani hizi mbili ni wale wanaozioanisha kama Gil Scott Heron (Mmarekani mweusi anayesifiwa kama mwanarapu wa kwanza) yeye hupiga piano na keshaandika riwaya na kuchapa vitabu vya mashairi. Mwingine ni Mzungu Tom Waitts ambaye pia ni mpiga piano na mwigizaji sinema. Halafu wanamuziki wa Brazil yaani Gilberto Gil na Caetano Veloso. Hawa wawili nawahusudu kwa kuwa ule muziki wanaopiga ni mzuri na pia ujumbe wa maneno yao vile vile wa maana. Hakuna kilichozidi chenzake. Miye siku zote hujaribu kufikia lengo hilo katika fasihi na muziki wangu: kuoanisha fani, umbuji na maudhui.

BC: Wewe ni mtu ambaye umezunguka katika nchi nyingi duniani zikiwemo za Ulaya,Marekani ya Kaskazini na Kusini. Kwa maana hiyo umepata bahati ya kukutana na kuona mila na tamaduni mbalimbali.Umejifunza nini hasa katika kukabiliana na mila na tamaduni hizo tofauti?

FM: Jambo la kwanza nililojifunza liko katika mwongozo na katiba ya CCM unaosema binadamu wote ni sawa. Ukweli popote utakapokwenda utawakuta wanadamu wanahofia na kufikiria jambo moja. Kila mtu anataka kuwa na furaha na amani na familia yake na maisha yake. Kila mtu anataka kupenda au kupendwa na kila mtu anatafuta furaha kwa njia mbalimbali.

Kinachotatanisha ukisafiri kwanza kabisa ni namna ambavyo sisi Waafrika tunavyodharauliwa. Tunadharauliwa kutokana na propaganda zinazoonyeshwa na vyombo vya habari. Mathalani nilipokuwa Paraguay (Marekani ya Kusini) mwaka 1994 nilishangaa kuulizwa kama sisi tuna mbalamwezi au bado tunakula wadudu.

Nisingekuwa msanii kuna sehemu au miji fulani ambayo wala nisingekanyaga, ila muziki, michezo na sanaa huwafanya wanadamu wakutane na kupatana. Kwa hiyo nimeweza kuibeba bendera yetu na kukubalika ugenini kupitia ala hizo.

Utamaduni, lugha na desturi ndiyo tatizo kubwa la kusafiri na kuishi ughaibuni. Kwa mfano mgogoro mkubwa huwa ulaji. Kupata chakula ulichozoea na kama hakipatikani kujaribu kula kile kinachokaribia na cha nyumbani. Waafrika lakini tunatia fora kwa kujifunza lugha mpya, na kama sikosei tunaongoza dunia nzima kwa wepesi wa kujifunza au kujua lugha nyingi.

BC: Ingawa unaishi mbali na Tanzania,kutokana na kazi zako za uandishi ni dhahiri kwamba unafuatilia kwa karibu siasa za Tanzania. Je unauongeleaje uongozi wa Raisi Jakaya Kikwete?Unadhani anaelekea kupambana na maadui maradhi,ujinga na umasikini ipasavyo?

FM: Pamoja na kwamba wananchi nyumbani hawaridhiki na uongozi wa sasa (au uliopita na ule mwingine toka enzi za Nyerere) Tanzania bado ni nchi inayoongoza kwa amani na unyeyekevu Afrika nzima. Ni jambo la kuchekesha lakini utagundua wanaume wengi toka nchi za Afrika Magharibi wanataka kuoa wake zetu shauri ya tabia zao. Sisi ni bado wastaarabu ukilinganisha na wenzetu.

Mtanzania, kijumla, bado ni mshamba kimawazo. Mtanzania anachokosa ni maendeleo ya kidunia, kutokana hasa na kutokusoma si tu magazeti bali kadhia mbalimbali, hususan vitabu na fasihi. Uongozi wa sasa unajitahidi. Hatuna mauaji na ukatili ambao wenzetu wanafanyiwa. Kwa mfano chukua jeshi ovu la Joseph Kony kaskazini ya Uganda. Jeshi hili hutumia watoto kwa kuwatesa na kuwafundisha kuua. Hatuna mambo aina hii.

Kuhusu Jakaya Kikwete. Kwanza anayo “personality” nzuri sana na anarihidhisha jinsi ambavyo Bongo tuna bahati ya kuwa na viongozi wapenda watu hata kama ni kwa mdomo tu; hatuna Marais wakatili, baradhuli kama wenzetu. Kile kitendo cha kutoa namba ya simu kwa mtu yeyote anayetaka kuongea naye kumpigia yeye au Ikulu ni kitendo cha maana sana. JK kashika madaraka mwaka mmoja ni vigumu kumhakiki vizuri. Itakuwa vyema kuangalia uongozi wake akishamaliza, kwani historia huwa haina msamaha.

 

Freddy Macha (kulia) akiwa na Rais wa kwanza, Mwalimu Nyerere, alipoitembelea Brazil mwezi Juni 1991. Picha na Vantoen Perreira.

BC: Lipo swali ambalo vijana wengi wangependa sana kukusikia ukilijibu.Kwa vipaji vyote ulivyonavyo,ni kwanini hurudi nyumbani(Tanzania) ili usaidie kukuza vipaji kama vyako miongoni mwa vijana kule?

FM: Nimeondoka Bongo kimwili lakini kiroho bado niko nyumbani.

BC: Unalo lolote ambalo ungependa kuongezea kabla hatujamaliza mahojiano haya?

FM: Ningependa kuwasisitiza vijana na Wabongo wenzangu kuwa na tabia ya kusoma na kujipenda zaidi kifikra, kimazoezi na kiafya. Bongo Celebrity ni njia moja nzuri ya kuonyesha Watanzania wanaojitahidi kupambana na maisha. Hivyo basi ningependa kutoa ahsante kwa kuongea kwani si mara nyingi mimi huhojiwa nyumbani. Huwa mimi ndiye mhoji. Nashukuru sana kwa nafasi hii…

Kumalizia niwaeleze wasomaji wasiojua muziki wangu kuwa tuko mbioni , inshallah, kutayarisha video ya moja ya nyimbo zangu zinazopendwa na wateja. Matumaini ni video hii kuchezwa Afrika Mashariki na kuwapa wananchi hisia ya muziki wa Kitoto Band.

BC: Freddy Macha,ahsante sana kwa muda wako.Tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako.

FM: Ahsanteni pia,kazi njema.

Sasa ni wakati wa burudani…Kibao cha kwanza kinaitwa

KILIMANJARO

Cha pili kinaitwa

KITOTO

Kibao cha tatu kinaitwa AFRICAN SEAMAN (kisa cha kweli hiki)

Ukitaka kusoma mashairi(lyrics) na habari zaidi kuhusu nyimbo hizi bonyeza hapa.

Advertisements
 

7 Responses to “KWA KINA NA FREDDY MACHA-PART II”

 1. Tabu na Malaika Says:

  Freddy,we salute you
  Nimekubali,wewe ni hazina.Kama mtu anataka kufanikiwa katika muziki,hana budi kusoma mahojiano haya kwanza kabla hajaingia kunako studio.Stay blessed

 2. Ndio Zetu Says:

  Duh,kweli haya mahojiano ni shule.Heko kwako Freddy Macha.Muziki wako pia ni mtamu.Keep it up mazee,endelea kutuwakilisha huko kwa malikia.

 3. msemakweli Says:

  Great amateur effort! Don’t quit your day job!

 4. Mdau-UK Says:

  Freddy,
  Kazi nzuri kaka.Nimependa sana ushauri wako kuhusu jinsi gani Tanzania tunaweza nasi kutengeneza muziki wa kimataifa.Kama hawa vijana wa bongo fleva wanasoma hapa,ushauri huo ni wa kuzingatiwa sana.La sivyo,tutatwanga maji tu mpaka pakuche.

 5. C mchezo kaka Freddy umetulia kwa kila kitu.Unastahili kuwa fundisho na mwongozo kwa jamii.Ni kioo!Big up.

 6. amina Says:

  kwani huyu nani?aaahhh

 7. Salam Maalam
  salam Freddy.Good job.
  All the Best
  Salam
  Farid


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s