BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

MIAKA 44 YA MUUNGANO…TUSHEHEREKEE! April, 26, 2008

Leo ni siku ya kusheherekea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika miaka 44 iliyopita na kutupa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania tuijuayo hivi leo. Sherehe za kitaifa za kuadhimisha kumbukumbu hiyo zinafanyikia jijini Dar-es-salaam.Watanzania tunazo kila sababu za kusheherekea. Basi na tusherekee!

Pichani anaonekana Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar kama ishara ya muungano rasmi.

Hapa wanaonekana Baba wa Taifa,Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(kushoto) akibadilishana na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume(kulia), nyaraka rasmi za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar miaka 44 iliyopita.

Picha zote kwa msaada wa Muhidini Issa Michuzi.

Advertisements
 

9 Responses to “MIAKA 44 YA MUUNGANO…TUSHEHEREKEE!”

 1. Mswahilina Says:

  Tusherehekee, Muungano umetimiza miaka 44.
  Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

  BC (au mdau yeyote) ninaomba kujua majina ya hao Watanzania wengine walioko kwenye hizi picha.

 2. Mfalme Kisisina Says:

  Angekuwepo Mzee Karume
  angeshauvunjilia kwa mbali

  *Kwanza sio halali kisheria, umeshinikizwa
  *Inaingia nusu karne, maji ya kunywa hakuna
  *Umaarufu pekee: Umalaya na madawa ya kulevya

  Na Ali Nabwa

  Salim Said Rashid ni miongoni mwa watu wachache leo wenye haki ya kudai kuwa wanaijuwa historia ya karibu ya siasa Zanzibar. Ameshiriki kwa karibu katika harakati za ukombozi za Visiwa hivi tangu akiwa mwanafunzi wa skuli ya sekondari katika miaka ya ’50. Akaendelea na mapambano akiwa anasomea masuala ya uchumi na sheria ya kimataifa katika Chuo maarufu cha London School of Economics(LSE). Akawa Katibu Mkuu wa kwanza Baraza la Mapinduzi wiki moja tu baada ya mapinduzi. Aliendelea akawa Naibu Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano; Naibu Waziri wa Fedha na Utawala wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Afrika Mashariki, Balozi Guinea na baadae Etheopia.

  Salim amekubali kutowa maoni yake kwa An nuur kuhusiana na Muungano ambao alikuwa jikoni wakati unaundwa.

  Suali: Sheikh Salim, Wewe ulikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi wakati Muungano unaanzishwa na baadae ukashika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Muungano, unaonaje, Muungano huu umekuwa na mafanikio ?

  Jawabu: Muungano mpaka leo umezongwa na migogoro tangu siku ulipoundwa. Hakuna mafanikio yoyote yale yaliyopatikana, si upande wa Tanganyika hata upande wa Zanzibar. Muungano huu bila ya shaka inaeleweka haukuundwa kutokana na hisia ya Watanganyika na Wazanzibari. Muungano umeletwa kwa shinikizo la mataifa ya kigeni.

  Swali: Unadhani Mzee Karume angekuwa hai leo angefikiria upya kuhusu Muungano ?

  Jawabu: Angelikuwa Mzee Abeid Amani Karume yuhai leo, pasingekuwa na Muungano kwani inaeleweka na watu wengi, pamoja na mimi, kwamba Mzee Karume alichukulia suala la Muungano kama la muda. Unaelewa kwamba wakati Muungano ulipoundwa hali halisi ilikuwa ya vitisho; ilikuwa kama jambo ambalo Zanzibar imelazimishwa kulikubali.

  Swali: Kwa vipi ?

  Jawabu: Kwa sababu wakati huo ilikuwa wakati wa Vita Baridi. Kulikuwa na madola ya Mashariki na madola ya Magharibi. Madola ya Mashariki yalikuwa yameyapokea na yameyakubali mapinduzi ya Zanzibar. Madola ya Magharibi yaliyakataa, yakafanya kila mbinu kuhakikisha yakwamba Zanzibar haiendelei na kusalia kuwa dola huru.

  Swali: Unakusudia kusema kwamba walimtisha Mzee Karume ?

  Jawabu: Ndio, walimtisha kuwa watatumia nguvu ya kijeshi kuivamia Zanzibar na kuiondoa Serikali. Walimtisha kuwa nchi za Magharibi zitafanya kila kitu na hazitokubali Zanzibar iselelee kuwa taifa huru la kimapinduzi kwa khofu kuwa wanaweza wakapeleka umaarufu wa mapinduzi katika kanda hii ya Afrika. Lilikuwa jambo gumu hili na utakumbuka mambo yote yalikuwa siri. Hata wahusika katika Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar hawakufahamishwa kitu gani kinatokea mpaka siku ya mwisho.

  Swali: Sasa wewe ulikuwa karibu sana na Mzee Karume na mimi najuwa alikuamini sana, alikueleza habari ya vitisho hivi ?

  Jawabu: Alinieleza na nilihisi mimi ya kwamba……Sisi tulikwenda Dar es Salaam siku 10 kabla ya muungano na tulipofika kule Karume akakutana na Nyerere. Mimi akaniambia Mwalimu niende nikanyowe (kwa vile nilikuja kuamshwa mapema sijawahi kunyowa ndevu) Kwa hiyo mimi sikuwapo katika mazungumzo yao. Hapo ndipo alipofahamishwa mipango ya dola za Magharibi kuhusu Zanzibar na kuepukana nayo alilazimika kujiunganisha na Tanganyika, lakini napenda kusisitiza kuwa kwa Mzee Karume hili lilikuwa jambo la muda, vitisho vikiondoka na akahisi Zanzibar ishajijenga vya kutosha kuhami maslahi yake muungano usingekuwepo.

  Swali: Lakini mbona baadhi ya wasomi wameandika mlikuwa na kikao cha pamoja wewe na Mzee Karume na Mwalimu Nyerere ?

  Jawabu: Mimi nilikwenda Dar es Salaam, lakini tulipofika ikaonekana Mwalimu asingependa mimi niwepo kwenye kikao kile, nikaona bora niwaachie wao wawili wazungumze. Lakini baada ya siku mbili tatu yakaletwa Unguja, Zanzibar, makaratasi yenye mapendekezo ya muungano. Tangu hapo mimi na Mzee Karume tukazungumzia makaratasi hayo na nilikuwa namfahamisha kila kitu. Lakini kitu kimoja muhimu kifahamike, huu muungano tangu kupendekezwa mpaka kusimama kwake haikuchukuwa wiki mbili. Na kabla kuitwa Mzee Karume Dar es Salaam na Nyerere, ulikuja hapa ujumbe wa Tanganyika na wa Kenya wakamletea barua Mzee Karume.

  Swali: Barua hiyo ilisema nini ?

  Jawabu: Barua hiyo ilikuwa ya kumtisha Karume kuwa hapa Umma Party ingeweza ikamuumiza, ikammaliza. Ilikusudiwa kuleta mtafaruku ambao haukuwepo ,ila ni vitisho vya dola za kigeni tu, na Zanzibar ni taifa dogo na lisingeweza kujihami na tulikuwa katika Vita Baridi, ilikuwa mazingira ya taabu sana kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na naweza kusema kuwa tulilazimishwa.

  Swali: Lakini baadhi ya wataalamu, hasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanadai huu ulikuwa muungano wa hiyari na uliridhiwa na Baraza la Mapinduzi (BLM), wewe ulikuwa Katibu Mkuu wa BLM wakati unaohusika, unasema nini kuhusu hili ?

  Jawabu: Kuwa Muungano ulikuwa wa hiyari au si wa hiyari tusizingatie maneno ya wataalamu wa Chuo Kikuu tu, bali hata vitabu vya waliohusika wakati ule, hasa wanadiplomasia wa Kimarekani. Ukisoma vitabu vyao utaona ulikuwa muungano wa hila, si wa halali. Si wa halali kwa sababu Baraza la Mapinduzi halijapata kuitwa hata katika kikao kimoja kuzungumzia Hati ya Muungano, kuithibitisha na kuipitisha kama ilivyopasa kufanywa na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.

  Swali: Wewe ulikuwa Katibu Mkuu wa Baraza, si ilibidi ushiriki vikao vyote ?

  Jawabu: Ilibidi ndio, na mimi ndiye niliyekuwa naviitisha.

  Swali: Sasa ilikuwaje katika kikao hiki muhimu ambacho kilithibitisha muungano wewe hukuwapo ?

  Jawabu: Mimi nastaajabu, na si dhani kama kulikuwepo kikao kama hicho. Pengine suala hili lilipata kuzungumzwa na Mzee Karume kwa baadhi ya wajumbe wa Baraza lakini si katika kikao. Kulikuwa na mtindo wa Wajumbe wa Baraza kuitwa mbali mbali State House (Ikulu) kuelezwa baadhi ya mambo, lakini hakukuwa na kikao rasmi kuhusu suala hili, Baraza likapitisha sheria inayohusu muungano, ikatiwa saini Amri ya Rais (Presidential Decree) na Rais na mimi kama Katibu wa Baraza.

  Swali: Inasemekana kulikuwa na kikao cha pamoja cha BLM na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Kikao hicho kilizungumzia nini ?

  Jawabu: Hakukuwa na kikao kama hicho. Kilichotokea ni kwamba Mwalimu alikuwa anahutubia Bunge na wajumbe wa BLM wakaalikwa kusikiliza; hakukuwa na mjadala.

  Swali: Inasemekana Mwanasheria Mkuu wa wakati ule, Wolfang Dourado hakushirikishwa katika hatua za kuelekea kwenye Muungano, bali alishiriki wakili kutoka Uganda, Dan Nabudere.

  Jawabu: Sio Mwanasheria Mkuu tu ambaye hakushirikishwa, bali hata wizara, pamoja na wizara muhimu ya Mambo ya Nje ya Zanzibar, haikushirikishwa. Hii ilikuwa sera binafsi ya Rais wa Awamu ya Kwanza wa Zanzibar na Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanganyika. Kuhusu upande wa pili wa suali lako kuhusiana na Dan Nabudere, huyu nilimleta mimi hapa baada kuona umuhimu wa Serikali kupata ushauri wa kisheria. Lakini bahati mbaya alipofika hapa ilikuwa mkataba ushatiwa saini na akaondoka bila kufanya chochote.

  Swali: Inasemekana kulikuwa na Wizara za Muungano hapa Zanzibar, ilikuaje zikaondoshwa ?

  Jawabu: Baada Muungano walikuja mawaziri kufunguwa ofisi za Muungano hapa, lakini Serikali ya Mpinduzi ikakataa. Na napenda kukufahamisha kwamba, namna muungano ulivyoendeshwa katika awamu mbali mbali za Zanzibar inahitilafiana. Awamu ya Kwanza Zanzibar ilikuwa inaendeshwa kama taifa huru.

  Swali: Kwa vipi ?

  Jawabu: Kwa kuwa ilikuwa na jeshi lake, ilikuwa na idara zake, hakukuwa hapa na wafanya kazi wa Muungano, ilikuwa na chama chake, ilikuwa na kila kitu chake, na mamlaka yake ya kimataifa. Mambo yaliyokuwa yanafanya kazi yalikuwa mambo ya Muungano tu. Hata hayo ilikuwa matatizo. Kwa mfano, sarafu ya fedha za kigeni ya Zanzibar, ambayo ilikuwa nyingi, haikuchanganyishwa na ile ya Tanganyika na ilikuwa chini ya mamlaka ya Zanzibar, haikuwa chini ya mamlaka ya Muungano.

  Swali: Kwa maelezo yako, na unavyoonekana kwa jumla mwenendo wa muungano huu, ni wazi kwamba suala hili liliharakishwa. Kwanza kwa nini ikawa hivyo ? Pili, hakuna uwezekano kwamba kutokana na msukumo huu Karume mwenyewe hakuelewa kinachoendelea hasa ?

  Jawabu: Sijuwi alikuwa anaelewa au haelewi, lakini kasi hii ilikuwa kwa sababu nchi za Magharibi zilikuwa zinataka kuleta majeshi hapa. Wasingekubali iwepo SMZ na ikawa hawana muda, walitaka hili jambo lifanyike haraka sana. Lakini makosa yaliyotokea ni kwa upande wa Tanganyika na upande wa Zanzibarar kutoshirikiana na dola nyengine za Afrika na zilizoendelea ulimwenguni kuelezea suala hili kimataifa, kwenda Umoja wa Mataifa kuonesha ile pressure ambayo ipo hapo wanayofanyiwa mataifa mawili huru ambayo kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wanayo haki ya kuamua wanavyotaka kuhusu mustakbali wao.

  Swali: Kuna uwezekano kutokana na vitisho vilivyokuwepo Mzee Karume alijuwa hila za Mwalimu Nyerere lakini yeye mwenyewe alikuwa na maslahi yake ya muda ?

  Jawabu: Hapa kuna maslahi ya namna mbili. Kuna maslahi ya Tanganyika na maslahi ya Zanzibar. Na kuna maslahi ya wale viongozi wa wakati ule. Bila ya shaka Karume alitishwa na aliogopa na akaihofia Zanzibar na ndio maana akakubali haraka haraka mipango ya muungano. Lakini Tanganyika haikutishwa na haikuwa na khofu. Ilikuwa hakuna sababu kwa Tanganyika kuliharakisha suala hili.

  Swali: Kwa hivyo unadhani ungefika wakati, hasa kwa mambo yalivyojitokeza baadae, Mzee Karume angevunja Muungano ?

  Jawabu: Hata hii leo ikiwepo kura ya maoni Zanzibar asilimia 90 nadhani watasema wanataka mpango mwengine, hawataki mpango wa hivi sasa. Hili suala la muungano kwa sababu umma haukushirikishwa 1964, ulifanywa siri, ilikuwa siri ya watu wachache na tangu hapo hadi leo kuna malalamiko. Na Mzee Karume akisema, “Muungano ni kama reli, mnyonyoro unaounganisha behewa na behewa shoka la kuukata liko Zanzibar”, na mimi aliwahi kuniambia mara kadhaa shoka karibu atalinyanyuwa ili mnyonyoro ukatike, behewa la Tanganyika liende upande wake na behewa la Zanzibar liende upande wake. Nataka kusisitiza kwamba, hii miaka 42 hawezi mtu kusimama akasema kuwa Watanganyika na Wazanzibari wamepata manufaa kutokana na Muungano. Hakuna.

  Swali: Kwa upande wa uchumi wako wanaodai kuwa Muungano umeudumaza uchumi wa Zanzibar. Wewe kama mtaalamu wa masuala ya uchumi unasemaje ?

  Jawabu: Ingekuwa Tanganyika na Zanzibar ni kama Kenya na Uganda na Tanganyika, dola zinazolingana kwa ukubwa ingelikuwa suala jengine. Lakini Zanzibar ina watu milioni moja tu, hakuna soko hapa. Pili hakuna miradi ya pamoja ya Muungano, labda jengo la Benki ya Tanzania.

  Swali: Kuna miradi ya TASAF ?

  Jawabu: Ukizungumzia uchumi unazungumzia sarafu, benki kuu, viwanda, mafuta, mali asili, miundo mbinu ya uchumi, n.k. Uchumi wa Zanzibar na Tanganyika ni tafauti. Hata sera tafauti. Hapa hakukuwa na vijiji vya ujamaa, ambavyo ndivyo vilivyokuwa mhimili wa sera ya Mwalimu ya Ujamaa na Kujitegemea. Aliikataa Karume.

  Mimi naona hii TASAF ni kama vugu vugu la ushirika la wakati wa ukoloni. Zile zilikuwa jitihada za nyongeza tu, lakini kulikuwa na mipango madhubuti ya uchumi hapa kabla ya Mapinduzi. Zanzibar ilikuwa ya pili kwa maendeleo ya uchumi na elimu katika Afrika chini ya Sahara. Ilizidiwa na Ghana tu, ukiacha Afrika Kusini. Leo iko wapi ?

  Swali: Kulikuwa na mambo mangapi ya Muungano ?

  Jawabu: Yalikuwa 11

  Swali: Sasa yamefikia 23, na wengine wanasema ukiyachambuwa kwa undani ni zaidi. Unadhani hatua hii ni halali na njia zilizotumika ni halali ?

  Jawabu: Si kuwa ni halali au haramu, lakini muungano ulikuwa baina ya marais wawili, kwa hiyo utaratibu halali ni baina ya Serikali ya Muungano, ambayo inachukuliwa kama Serikali ya Tanganyika, kukaa na Serikali ya Zanzibar kuyazungumzia mabadiliko yanayotaka kufanyika, sio Bunge.

  Swali: Lakini Spika mstaafu wa Bunge la Muungano, alidai kuwa Wazanzibari walishiriki katika maamuzi yote.

  Jawabu: Yeye akisema haya anachukulia wabunge, Hawa watu hawawakilishi Wazanzibari. Katika suala hili Zanzibar ingewakilishwa na Rais na Serikali yake. Halafu, hawa watu wanaoshiriki katika vikao mbali mbali vya Muungano hawafikirii maslahi ya Zanzibar.

  Swali: Sasa inaonesha pande zote mbili za Muungano haziridhiki na mambo yalivyo, sasa wewe ukiwa na uzoefu wa suala hili la Muungano tangu mwanzoni kwake unauonaje mustakbali wa Muungano na nini kinahitajika kufanywa ?

  Jawabu: Mustakbal Muungano hauna, kwa sababu watu hapa Zanzibar hawautaki ijapokuwa wanakhofu kusema, hii ndio hali halisi. Leo ikifanywa kura ya maoni ni wazi kabisa kwamba Wazanzibari zaidi ya asilimia 90 watakataa Muungano na watadai uhuru wao. Sasa tuzungumzie kipindi cha mpito. Muhimu suala hili lichukuliwe kidugu na kirafiki kati ya Bara na Visiwani. Mimi nahisi Tanganyika na Zanzibar ni mataifa pacha ambayo maslahi yao lazima yawe mamoja, lakini mataifa huru, kila mmoja anajiamulia vile anavyotaka kwa upande wake mpaka litapokuja Shirikisho la Afrika Mashariki au Umoja wa Bara la Afrika. Hivi sasa hakuna jambo hilo, kuna mataifa huru tu, lakini muungano ni baina ya Tanganyika na Zanzibar peke yao, na ndio hivyo muungano wenyewe haujakaa sawa. Umefika wakati viongozi wakae watathmini mambo haya na kutoa mwanya wa kufunguliwa ukurasa mpya.

  Swali: Lakini Muungano ndio upo, tukitaka tusitake, sasa ni hatua gani unadhani zingefaa kuchukuliwa hapa tulipofika ?

  Jawabu: Kuna haja ya mjadala wa kitaifa, hasa hapa Zanzibar. Hili suala lijadiliwe na watu wote. Serikali ianzishe mjadala huo utaoshirikisha umma, upatikane msimamo wa Kizanzibar, kwa sababu wakati kuna msimamo wa Kitanganyika, hakuna msimamo wa Kizanzibar. Hii ndio muhimu sana. Nikisema msimamo wa Zanzibar nakusudia msimamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, sio Wazanzibari, kuhusu suala zima hili la Muungano na kusimamia maslahi ya nchi ya Wazanzibari. Huo ni ufumbuzi wa ndani. Lakini hili ni suala la kimataifa pia, kwa hiyo ufumbuzi wake hauna budi kushirikisha jumuiya ya kimataifa. Hizi ni dola mbili zilizoungana, kwa hiyo moja kwa moja ni suala linalohusu Umoja wa Mataifa, ambao lazima ushirikishwe.

  Swali: Sasa kwa kumalizia, ulisema Zanzibar kabla ya Muungano ilikuwa nchi iliyopiga hatuwa za maendeleo, lakini kuna hoja kwamba bila Muungano Zanzibar itakufa kwa sababu ni ndogo na haina rasilimali na vianzio imara vya uchumi. Una maoni gani juu ya madai haya?

  Jawabu: Ni kweli Zanzibar ilikuwa maarufu ulimwenguni kiuchumi, kibiashara, kielimu (ya dini na dunia), kidiplomasia na hata kimichezo. Nchi kubwa zote ulimwenguni zilikuwa na balozi zao hapa nusu ya mwanzo ya karne ya 19 na michezo yote ikichezwa hapa, ikiwa ni pamoja na cricket, hockey, polo, n.k. lakini leo inanuka umaskini na ufukara na umaarufu pekee iliyonao ni kama kituo cha umalaya na madawa ya kulevya. Zanzibar ilikuwa na mazingira bora zaidi ya kiuchumi kuliko Mauritius, lakini wametutupa nyuma kwa mbali, na hawajaungana na nchi yoyote. Singapore ni ndogo kulioko Zanzibar, nayo ndo kabisa haikuwa na chochote cha kuwasukuma kimaendeleo, lakini walijitoa katika muungano na Malay na leo wanahesabika katika ulimwengu wa kwanza. Rasilimali yao pekee ni uongozi mzuri. Zanzibar ina uwezo mkubwa wa kimaendeleo iwapo ipo dira sahihi. Moja katika vianzio vikubwa vya mapato Mauritius ni huduma. Hapa Zanzibar zamani meli zikipanga foleni kuchukuwa maji, lakini leo sisi wenyewe ya kunywa hatuna.

  Topic

 3. Gervas Says:

  Hawa Wazanzibari wanabaguana wao kwa wao kwanza. Hata muungano ukifa bado vurugu itakuwepo maana wapemba hawataki kutawaliwa na waunguja weusi, maana historia inawatambua wao eti ni watummwa. Nahisi ili Zanzibar itulie, wapemba wajitenge na wajitawale na kisiwa chao kama nchi afu waunguja nao wawe kivyao (weusi) kama nchi unguja. Kwa maana hiyo basi wapemba woote bara na unguja wahame na maduka yao warudi kwao pemba na watengeneze serikali yao. Si ndio uhuru wanaoutaka? Speech ya Nyerere…wao wabara, sisi wazanzibari,…..wao wazanzibara sisi wazanzibari halisi. Asanteni.

 4. mazagazaga Says:

  Kinachofanya wazanzibari washikwe na ubaridi kuhusu mustakabali wa muungano ni jinsi Bara walivyoshindwa kuiendesha nchi kiuchumi na kuvifanya visiwa vya Zanzibar vitumbukie katika umaskini uliokithiri.Laiti Bara wangefanikiwa kuja na sera za kiuchumi ambazo zingeinua kwa kiasi kikubwa hali ya maisha ya watu wake, sera ambazo zingejidhihirisha katika kushamiri kwa sekta ya viwanda na upatikanaji wa ajira, sera ambazo zingechochea ujasiriamali na uwekezaji tokana na mapato makubwa ya watanzania wenyewe, wakazi wa visiwani zanzibar wangevutiwa na maendeleo hayo na pasingekuwepo na sababu ya kutilia mashaka kuhusu mustakabali wa maendeleo na ustawi wao katika siku zijazo. Lakini miaka imepita Bara imekuwa ikijikanyaga zaidi yenyewe kutokana na kukosekana kwa mwelekeo thabiti wa kujikwamua kutoka katika dhahama hiyo. Hata pale ambapo pengine kwa kuiruhusu Zanzibar iwe na sera zilizo huru kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Bandari zake na Pwani yake hata kiasi cha kuweza kuinufaisha Bara yenyewe, Bara imekuwa ikishikwa na kigugumizi katika kutoa maamuzi na hivyo kuifanya Zanzibar iendelee kusota ndani zaidi katika umaskini.wa kujitakia. Lazima tukubali kwamba wakazi wa zanzibar wamewazidi wenzao wa Bara katika utundu na maarifa ya biashara za kimataifa. Kwa kuwalazimisha wazanzibari wapige KWATA kwasababu ya ujinga na kutokujua kwa baadhi ya wahafidhina walioko katika safu za uongozi katika serikali na chama kwa upande wa Bara ndiko kunako zua yote hayo ya kutoaminiana katika kuliongoza hili jahazi amabalo sote ni abiria wake Bara na Visiwani kuelekea huko katika USTAWI. Na mpaka hapo hili litakapo eleweka wazanzibari watakuwa na kila sababu ya kupiga kelele kwamba KIATU KINAWABANA NA SICHO SAIZI YAO!tatizo ni bara akili mgando, na wala siyo visiwani wanao ona mbali!. Mimi ni mkazi wa Bara, tena Bara hasa.

 5. Amina Says:

  Gervas usinichekeshe…na kweli wabaguzi sana hawa watu wenyewe hawapendani,mi nishaishi kule ni hatari basi ukitoka bara ukipita njiani wanakutambua utasikia mmbongo huyo..matata sana hawa watu

 6. Gervas Says:

  Amina…Hivi wewe ndo Amina ninayekujua? au ulivotaja zanzibar umenifanya nistuke.

 7. Amina Says:

  mhhh Gervas umeanza mambo yako

 8. J Bigy Says:

  Wazanzibari wana ‘amani’ kwa sababu wako katika muungano.Nje ya muungano watamalizana. Pia sioni maliasili, tekinolojia, nguvukazi ama chochote wanachowezasema wabara wanawategemea na watakikosa nje ya muungano.
  Hata hivyo tushakuwa wamoja.Kuna wapemba wengi sana kariakoo, msasani nyuma ya US embassy na kwingineko.Wamestawi sana lakini kwa sababu wabara hatuna kadhambi ka ubaguzi na udini tuko kimya tu.

 9. mazagazaga Says:

  Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, katika miaka yote hiyo ya 44 ya Muungano, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imenufaika nini kiuchumi kwa kuitumia Zanzibar kiuchumi katika nyanja mbalimbali ili kuinua hali ya maisha ya watu wake? Au sera zilizopo zimezidi kuididimiza zaidi Zanzibar ishindwe kuzitumia bandari zake kikalifu zaidi kwa manufaa ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, Zanzibar kushindwa kuendeleza zao lake maarufu la Karafuu na Mazao ya Viungo(Spices) kwa ajili ya soko la kimataifa, ishindwe kuendeleza sekta yake ya Uvuvi kwa ajili ya sosko la Kimataifa, ishindwe kuendeleza vituo vya Tafiti Mbalimbali, ishindwe kuendeleza sekta yake ya Viwanda na mengineyo mengi. Wingu la ‘Muungano’ likiwa limetanda kila pahali watu waliopaswa kuleta mabadiliko hayo kwa manufaa ya Tanzania nzima wakiwa wamegubikwa na mawazo finyu. Muungano badala ya kutoa fursa zaidi za maendeleo kwa Zanzibar sasa umegeuka kuwa KISIKI CHA MAENDELEO YA VISIWA VYA ZANZIBAR. Ni mafanikio gani ya kiuchumi viongozi wanayo yazungumzia yamepatikana katika miaka hiyo 44 ya Muungano kwa upande wa Zanzibar? Au ni hilo suala tu la kutovunjika kwa Muungano wenyewe? Kutovunjika ndiyo Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii? La Haula!


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s