BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

MAGAZETI YA UDAKU:YANAJENGA AU KUBOMOA JAMII? July, 8, 2008

Filed under: Blogging,Magazeti,Mahusiano/Jamii,Uandishi — bongocelebrity @ 9:58 PM

Mjadala kuhusu mchango wa magazeti ya “Udaku” katika kujenga au kubomoa jamii una historia ndefu sana. Ni mjadala ambao ulikuwepo,upo na utaendelea kuwepo labda mpaka hapo itakapotokea kwamba maisha na watu watapotea katika sura ya ulimwengu.

Binadamu anabakia kuwa kiumbe mdadisi anayependa kupata habari,kujua kinachoendelea na pia hata kujua alichokifanya jirani yake jana usiku kama sio alichokifanya au anachokifanya mkuu wa nchi awapo mapumzikoni.

Nchini Tanzania, baada ya mapinduzi ya habari na mawasiliano,yaani baada ya kuvuka kile kipindi ambacho kulikuwa na magazeti matatu na kituo kimoja cha redio, paliibuka magazeti ambayo baadaye tumekuja kuyaita “magazeti ya udaku”. Hapo ndipo nasi tulipoingia rasmi kwenye mjadala wa; Je magazeti haya yana mchango gani katika jamii? Yanajenga au yanabomoa?

Hivi karibuni tulipata fursa adimu ya kufanya mahojiano na Abdallah Mrisho Salawi (pichani) Meneja Mkuu wa kampuni inayoongoza kwa uchapishaji wa magazeti ya “udaku” nchini Tanzania ya Global Publishers.Pamoja na mambo kadha wa kadha kumhusu yeye binafsi, Abdallah Mrisho anajaribu kueleza kuhusu kazi zao kama wanahabari na mchango wao au ubomoaji wao wa jamii.Hiyo itatokana na unavyoona wewe hasa baada ya kusoma alichotuambia Abdallah Mrisho.Pia anatoa ushauri muhimu kwa jamii hususani vijana kuhusiana na majanga kama umasikini,ukosefu wa ajira,ukimwi nk.Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Unaweza kutuambia historia ya maisha yako kwa kifupi? Ulizaliwa wapi,ukasomea wapi nk

AM: Nilizaliwa February 24, 1968, Bukene Tabora, nikiwa mtoto wa nne, kati ya watoto 9 wa Mzee Salawi. Katika familia yetu tulizaliwa jumla ya watoto 10, tupo hai 8, wavulana 5, wasichana 3. Wawili walishatangulia mbele ya haki.(Mungu awarehemu).

Elimu yangu ya msingi niliipata Bukene Primary School, kisha Ngerengere Secondary School ambayo inamilimilikiwa na Jeshi la Wanannchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha anga, ambacho ndicho kinadili na ufundishaji wa marubani wa ndege za kivita nchini tanzania. Nilipata Stashahada yangu ya Business & Sales Letter Writing kutoka Chuo cha International Correspondence Schools cha Glasgow, UK mwaka 1993.

BC: Ilikuwa vipi na lini ulipoamua kuingia kwenye masuala ya habari?

AM: Kilichoniingiza kwenye media naweza kusema ni passion na niliingia kupitia mgongo wa picha. Nilianza kupenda kupiga picha tangu nikiwa shuleni ambako nilikuwa napiga picha wanafunzi wenzangu.Baadaye hata nilipoanza kazi niliendelea kupiga picha mitaani, kwenye harusi na function mbalimbali za kijamii.Huko ndiko nikajikuta pia napiga picha za habari ambazo ndizo zilizonikutanisha na GLOBAL PUBLISHERS LTD ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama SAFEGUARD TANZANIA LTD ikiwa ina magazeti mawili, Uwazi na Kiu na baadae Ijumaa.

Pamoja na kuwa hivi sasa ni Kiongozi wa kampuni, naendelea na upigaji picha kwani ndiyo fani yangu na nimeendelea kujifunza kila wakati na hata kusoma On Line sanaa mbalimbali za upigaji picha (Art of Photography). Chuo cha New York Institute of Photography (www.nyip.com) kimenipa maarifa mengi ya fani hii. Baadhi ya kazi zangu unaweza kuziona hapa: www.mrisho.faithweb.com. Pia nimejifunza na kusomea vitu vingi vya Information Technology (IT), Ghaphics na Printing.

BC: Kabla ya hapo uliwahi kufanya kazi zingine mbali na uandishi na masuala ya habari kwa ujumla?Ilikuwa ni kazi gani?

AM: Kabla na baada ya kuingia kwenye media nikiwa kama mpiga picha na mwandishi wa habari za entertainment, nilikuwa nafanyakazi katika kampuni nyingine. Nilianza kufanyakazi na Car & General Trading yenye ofisi zake pale Azikiwe Street karibu na Posta mpya nikiwa upande wa kiwandani kule Chang’ombe Industrial Area ambako nilikuwa Salesman. Jamaa walikuwa wana dili na utengenezaji na uuzaji wa matairi ya magari.

Hapo nilifanya kazi kwa miaka kama 5, (1990-95), then nikahamia kampuni ya K. J. Motors mwaka huo wa 95 mwishoni kama sikosei, enzi hizo kampuni hii ikiwa inaongoza nchini kwa uuzaji wa magari aina ya Isuzu, Honda na pikipiki aina ya Honda Excel na 110 trail. Niliajiriwa kama Administration Officer.

BC: Ni mwandishi gani wa habari, vitabu au makala nchini Tanzania anayekuvutia zaidi? Kwanini?

AM: Naweza kuonekana namfagilia bosi wangu, lakini nasema ukweli tu kwamba mwandishi wa vitabu anayenivutia ni Shigongo. Sababu kubwa ni jinsi ambavyo anaweza kuandika kila siku hadithi na zikapendwa na wasomaji wake. Hebu fikiria, Global ina jumla ya magazeti sita ambayo yanatoka kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi na kila gazeti lina hadithi ya ukurasa mmoja.

Katika hadithi hizo, kila moja inajitegemea isipokuwa magazeti mawili ambayo hadhiti zake zinaendelea kutoka toleo moja hadi jingine. Lakini kikubwa zaidi ni jinsi anavyoweza kuandika mwendelezo wa hadhithi zake ambao unawavutia sana wasomaji wake.Huwa najiuliza points anapata wapi nashindwa kupata jibu. Naona ana kipaji cha kipekee ambacho si watu wote waweza kuwanacho. Amekuwa akiandika hadithi hizo karibu miaka kumi sasa na hajawahi kurudia stori.

Wengine wanafikia hatua ya kudai kuwa anatafsiri kutoka novel za kiingereza. Hana sababu ya kufanya hivyo.Shigongo ana kipaji cha kipekee cha kuandika hadithi, nafikiri comments za wasomaji wake wa kwenye mtandao zinajieleza, wanaguswa sana na hadithi zake! Mwenyewe hutuambia kuwa kuandika hadithi haoni kama ni kazi ngumu bali ni kama burudani, anapoandika huwa ana enjoy sana!

Kwa upande wa waandishi wa habari, naweza kusema navutiwa sana na Absolom Kibanda, mwandishi na mhariri mkuu wa gazeti la Tanzania Daima. Nampenda jamaa kwa sababu ana aina fulani ya uandishi wa habari ambao unatakiwa nchini, ujasiri usiokuwa na woga. Scoop ya kifo cha Balali nafikiri ni ushahidi tosha wa ujasiri wake!

Abdallah Mrisho(kushoto) akiwa na Marehemu James Dandu(katikati) na Erick Shigongo(kulia).Hii ilikuwa mwaka 2001.

BC: Ni jambo gani unalipenda zaidi kuhusu maisha yako kama kiongozi wa kampuni ya media na mwandishi wa makala? Lipi usilolipenda?

AM: Napenda ninapoona kampuni yangu inafanya jambo ambalo linainufaisha jamii na kubadilisha maisha ya mtu. Pia napenda pale ninapoandika makala zangu (You are what you eat) ambazo wasomaji zinawasaidia kuokoa maisha yao kwa kwa njia moja ama nyingine na kufikia hatu ya kunipigia simu na kuthamini kile nilichokiandika. Hali kadhalika kwa upande wa habari za entertainment, napenda kuandika kuhusu habari nikiwa wa kwanza kuiandika na kuihabarisha jamii.

Nikiwa kiongozi wa kampuni ya habari, sipendi kuona mtu yoyote anaonewa. Pale ninapoletewa malalamiko na msomaji akilalamika kuonewa kwa kuandikwa vitu ambavyo hakuvifanya huwa nakosa amani ndani ya nafsi yangu.Siku zote tunajaribu kusimamia uwazi na ukweli, sipendi kumuonea mtu kwa kitu cha uongo.

BC: Hivi sasa wewe ni meneja katika kampuni ambayo karibuni magazeti yote yanaandika habari ambazo zinazoitwa za “udaku”. Kwa maoni yako nini mchango wa magazeti ya “udaku” katika kuijenga au kuibomoa jamii?

AM: Mchango wa magazeti haya, ambayo sasa ‘yanaitwa magazeti pendwa’ kwa jamii ni mkubwa sana katika kuijenga zaidi kuliko kuibomoa. Japokuwa jamii hukasirika pale inapokosolewa kwa kwenda kinyume na maadili yetu na hiyo ni kawaida kwa binadamu yoyote, kwani siku zote ukweli huuma.

Lakini kupitia magazeti haya watu wameweza kupata haki zao walizokuwa wamedhulumiwa. Kupitia magazeti haya watu wamepona magonjwa ambayo yangeweza kuondoa uhai wao.Kupitia magazeti haya watoto wa masikini wengi wamesoma na wengine wanaendelea kusoma kwa kulipiwa ada na kampuni.Kupitia magazeti haya watu wengi wamepewa misaada ambayo imeweza kubadili maisha yao, achilia mbali familia za wafanyakazi na wauzaji wa magazeti haya walioko nchi nzima wanavyoweza kumudu maisha yao ya kila siku kwa kutegemea uuzaji wa magazeti hayo.

BC: Kama sikosei, changamoto moja kubwa ambayo lazima mnakabiliana nayo kila mara(kama sio kila siku) ni lawama mbalimbali kwamba magazeti ya udaku yanapotosha jamii hususani vijana na watoto na kwa maana hiyo kuchangia katika kuporomoka kwa maadili katika jamii. Je unakubaliana na lawama hizi? Kama hukubaliani unadhani lawama kama hizi zinatokana na nini?

AM: Hatukubaliani na lawama hizo.Kama nilivyojibu hapo juu, jamii wakati mwingine hukasirika pale inapokosolewa hata kwa jambo ambalo kweli imelifanya. Magazeti yetu siyo ya kulaumiwa, wanaopaswa kulaumiwa katika kupotosha vijana na watoto ni hao wanaofanya mambo yanayokwenda kinyume na jamii hadharani, kosa letu lisiwe kukemea kwa kuandika ukweli na kila mtu akajua.

Siku zote tunapoandika habari ya kashfa au ya ngono iliyofanywa na mwanajamii, hususan wale ambao wanaaminika kuwa ‘kioo cha jamii’, lengo letu huwa ni kukemea tabia hiyo ili isiendelee na kuonekana kama kitu cha kawaida kwa vijana na watoto.

Na hili limesaidia sana kubadili tabia za watu wengi, hasa hao ‘kioo cha jamii’ ambao zamani walikuwa wanaweza kufanya ufuska wa aina yoyote hadharani bila woga. Kadri siku zinavyokwenda ni wachache sana wanaodiriki kufanya ufuska hadharani kwani wengi wao wanaogopa kuumbuka.

Abdallah Mrisho(wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya wasanii maarufu wa Tanzania.Hiyo ilikuwa ni mwaka 2003 wakati wa uzinduzi wa filamu ya GirlFriend jijini Dar-es-salaam.

BC: Wapenzi wa magazeti ya udaku wanasema wamechoka kila mara kusoma habari za kutishatisha tu kama vile mauaji,vita,njaa,ukimwi na mambo kama hayo.Wanaosema hivyo wanadai kwamba kuchoshwa huko ndiko maana magazeti ya udaku ni muhimu ili kubalance jamii.Unakubaliana na hoja hii? Kivipi?

AM: Unajua, hulka ya binadamu ni mabadiliko. Jambo lolote ukilifanya kwa muda mrefu litakuchosha.Hata kama ukiwa unapenda sana kula ‘chips kuku’, ukipata fursa ya kula chakula hicho kila siku bila kupumzika, kitakukinahi. Hivyo hivyo hata kwenye tasnia ya habari.Kama sisi tungeingia kwa staili ya uandishi ule ule ambao umekuwepo tangu mwaka 50, leo hii tusingefika hapa tulipo.Watu wanataka kusoma mambo yanayowahusu moja kwa moja, mambo yanayoathiri maisha yao ya kila siku.

Habari tunazoziandika zinatoka katika jamii ya mtanzania wa kawaida, ambao ndiyo wako wengi nchini. Jamii hii tunaiheshimu sana na siku zote tumekuwa mstari wa mbele kupigania haki zao pale wanapodhulumiwa.

BC: Kumekuwepo pia na shutuma mbalimbali kwamba waandishi wa magazeti ya udaku mara nyingi hawazingatii misingi na miiko ya uandishi wa habari.Unasemaje kuhusu shutuma kama hizo?

AM: Waandishi wetu ni kama waandishi wengine popote duniani.Suala la kuzingatia misingi na miiko au maadili ya uandishi wa habari ni la kwanza na ni la lazima. Mwandishi anayekiuka miiko yake kwa makusudi huyo hana nafasi kwetu.Uongozi umekuwa mkali sana katika hilo na wafanyakazi wengi wameshawahi kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu,ikiwemo kufukuzwa kazi, pale wanapokiuka maadili ya kazi zao kwa uzembe. Hivyo ieleweke kwamba maadili yanazingatiwa, na wakati mwingine kuliko hata hayo yanayoonekana ‘serious’…

BC: Ni hatua gani mnazochukua mnaposhuhudia ukiukwaji wa maadili ya na sheria za nchi? Mfano mzuri ni mwaka jana mojawapo ya magazeti yako yalipoandika habari ya njemba mmoja kufumaniwa akiwa na mwanafunzi mdogo huko katika viwanja vya nane nane mkoani Morogoro. Huwa mnawaarifu polisi au mnatoa ushirikiano gani kwa wanausalama katika mambo kama hayo?

AM: Polisi siku zote wamekuwa marafiki zetu katika kupambana na uhalifu na maovu. Tumeshafanya operation nyingi kwa kushirikiana na jeshi la polisi nchini na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wanaokiuka maadili ya kijamii na wale wanaofanya ufisadi wa aina mbalimbali.

Siku zote jamii imetufanya kuwa kimbilio lake pale inapokuwa inahitaji msaada wa haki.Matatizo mengine tunayoletewa kabla ya kuchukua hatua ya kuandika, hulishirikisha jeshi la polisi na kufanikiwa kuwanasa wahalifu ‘red handed’ na kesi zao kufikishwa mahakamani.

Katika siku za hivi karibuni, jamaa mmoja alitaka kumtapeli mfanyabiashara mmoja mamilioni ya shilingi kwa kutumia jina la IGP Said Mwema.Baada ya kupata taarifa hizo, waandishi wetu, wakishirikiana na askari wa TAKUKURU, waliandaa mtego na jamaa alikamatwa red handed akipokea minoti na kupigwa picha, kesi yake iko mahakamani na ushahidi unaomkabli ni mzito! Mifano iko mingi, nafikiri mingine umeisoma katika magazeti yetu.

Abdallah Mrisho(kushoto) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Ulinzi,Dr.Emmanuel Nchimbi.

BC: Sina uhakika kama kampeni hii bado ipo lakini mwaka jana, kupitia kampuni yenu ya Global Publishers mliamua kutoa shilingi moja kwa kila gazeti linalonunuliwa kwenda katika mamlaka ya elimu Tanzania ili kuchangia watoto wasiojiweza na mayatima. Nini kiliwasukuma mfanye hivyo?

AM: Kama nilivyokwisha sema hapo awali, jamii imetufanya sisi kama ndiyo kimbilio lake pale inapokuwa na shida. Kwa kuwa watoto wengi wa watanzania wa kawaida wanasoma katika shule za serikali, shule ambazo zinakabiliwa na matatizo mengi ya madawati, vitabu, n.k, tuliona nasi tutoe mchango wetu kwa serikali kupitia mamlaka ya elimu Tanzania (TEA) katika kuboresha sekta hiyo, ili mwisho wa siku watoto wa masikini wasome katika mazingira mazuri.

Ahadi yetu bado inaendelea na mpaka sasa tumeshatoa karibu milioni 3 na Julai mwaka huu tunatarajia kukabidhi michango iliyosalia… na hizi ni pesa ya wasomaji wetu, kila anayenunua gazeti letu ajue ana shilingi yake inasaidia elimu mtoto wa mwenzie.

BC: Kwa maoni yako nini kifanyike ili kupunguza kasi ya kuongezeka kwa watoto wa mitaani na yatima wanaotokana na majanga ya kibinadamu kama ukimwi?

AM: Wanaume wasizae nje ya ndoa na ambao hawajaoa, wazae pale wanapokuwa tayari kufanya hivyo. Pia watu wazae idadi ya watoto wanaoweza kuwalea, si kila mtoto na riziki yake..hiyo haipo siku hizi!

BC: Nini tathmini yako kuhusu uongozi wa raisi wetu mheshimiwa Jakaya Kikwete. Je anaelekea kuishinda vita ya rushwa,umasikini,njaa na maradhi?

AM: Bado ana kazi ngumu. Dhamira yake ni nzuri, kweli anataka kumkomboa mlala hoi, lakini hana timu kamili yenye dhamira kama yake na hapo ndipo penye ugumu.Askari hata awe hodari vipi, lakini hawezi kupigana vita akiwa peke yake!

Abdallah Mrisho(kushoto) akiwa na Rais Mstaafu,Ali Hassan Mwinyi mwaka 1998.

BC: Una ushauri gani kwa vijana wa kitanzania kuhusiana na masuala kama ajira,ukimwi na maisha kwa ujumla?

AM: Tufanye kazi kwa bidii pale tunapozipata. Kila mtu mwenye nia ya kufanya kazi hakosi kazi, kwani kazi ni kazi mradi huvunji sheria na unapata mlo wako wa kila siku. Kikubwa ni kujitambua unatoka wapi, unaenda wapi na nini unatakiwa kufanya kufika huko uendako.

Ukimwi unabaki kuwa maneno hadi pale mtu anapoukwaa.Hivyo vijana wenzangu kama hawawezi kuchukua tahadhari yoyote sasa kwa kudhani wako salama, wajielewe wanatakiwa waishi vipi pale wanakapokuwa taabani kiafya, hilo ndiyo kubwa la kujiandaa nalo!

BC: Kuna lolote ambalo ungependa kuongezea ambalo hatujakuuliza?(Hapa unaweza kuweka suala zima la ninyi kuamua kuingia mtandaoni ili kuwafikia watu wengi zaidi nk)

AM: Hadhiti za Eric Shigongo zina wasomaji wengi sana nchini na hadithi zake ni ndefu sana kiasi kwamba unaweza kuwa nchini hadi unaondoka kwenda ughaibuni, hadithi inaendelea na ukiwa huko unatamani sana kujua mwisho wa hadithi fulani.

Tulipata maombi mengi na kilio hicho kutoka kwa wosomaji wa hadithi, njia pekee na ya kisasa kuwafikia wasomaji wetu popote walipo duniani, tukaona ni kuwa na mtandao(www.globalpublishertz.com) wenye kila kitu msomaji anachopenda kukisoma na kujua kuhusu Bongo.

Hivyo kuanzia July mwaka jana, tukaingia kwenye mtandao ambao umepokelewa vizuri na wasomaji wetu, ndani ya kipindi hicho kifupi kuna wageni waliotembelea hadi sasa karibu milioni 2 na idadi inaongezeka kila siku. Hivyo wanaopenda kuzisoma hadithi za Shigongo watembelee tovuti yetu ambapo pia watapata “udaku” na mambo mengine chungu mbovu.

BC: Asante sana Mrisho.Tunakutakia kila la kheri katika kazi zako/zenu.

NB: Abdallah Mrisho pia ni mwanablogu na blogu yake inapatikana kwa kutumia anuani hii; http://www.abdallahmrisho.blogspot.com

Advertisements
 

26 Responses to “MAGAZETI YA UDAKU:YANAJENGA AU KUBOMOA JAMII?”

 1. Ed Says:

  Nadhani haya magazeti hayajapa law suit ya kisawa sawa. Yanafanya cut and paste mara kwa mara ili kushinda kibishiara. Watanzania wengi hasa icon figures hawajui sheria ndio maana haya magazeti yanawachukua picha na kuzifanyia editing.

  Kwa upande mwingine yanasaidia kuwaweka sawa hao so called celebrities.

 2. Frateline Says:

  Hi guys, kutoka Helsinkii-Finland.

  Kwa kweli nakubali magazeti ya Udaku yanamchango mzuri tu katika jamii, Lakini kuna kasoro kubwa ya magazeti haya, kwa mfano mimi yananikela sana kumuandama mtu mpaka anakosa pumzi, kwa maoni yangu haya magazeti hayakumtendea haki marehemu Amina (public image ya huyu dada kwa kiasi fulani iliharibika kutoka na haya magazeti) hata hivyo kwa kuwa alikuwa ni mjanja, akaanza kuijenga upya-kupitia ubunge, lakini hata hapo magazeti hayakumpa usingizi, kila mtanzania alikuwa anajua Amina kalala vipi na kaamuka vipi, hii ni kero na nikinyume ya haki za binadamu, the ”right to privacy”. Kila mtu anatakiwa faragha hakuna malaika dunia zote ni wadhambi hata biblia inasema hivyo, hivyo sio sahihi kuwasakama baadhi ya watu katika jamii hata kwa mambo ambayo hayaisaidii jamii bali ni kitendo cha kutaka kupata ridhiki kwa kumdhalilisha mwenzako, Pia kero yangu ya pili ni jinsi magazeti haya ambavyo ni rahisi kutumiwa na maadui, katika jamii kila mtu ana adui, kwa mfano mara nyingi wanaumme wamewadhalilisha wasichana wao kwa kuonyesha picha za uchi kwa makusudi tu, eti kisa alienda naye kunywa pombe, pia kuna vumanizi za kupanga ili kumukomoa mtu, haya mambo lazima mchunguze, je ni mtego wa adui, sio magazeti yanatumiwa pia nyie global publishers bila kujua. Lakini nawapongeza badili hizo karo, na endelea na kazi, mimi ninaamini, There is no private life, private life is public life because no one lives in a vacuum, we all live in a society. Hivyo naomba taaluma ya uandishi wa habari ifuatwe, kama ambayo kwenye magazeti yasio ya udaku yanavyo fanya, sio kila mtu ni mwandishi ni lazima uwe na taaluma, kuweza kujua source, kubalance story yako, na pia kulinda heshima ya msingi ya binadamu mwenzako panapo bidi. Hivyo waandishi wa habari hizi nategemea ni watu wenye taaluma, maana kuna tabia ktk jamii kila mtu kujifanya ni mwandishi hasa hasa, wale kanja nja, hawana Elimu , ila wanatafuta story kwa kulazimisha ili waweze kuuza, mkono uende kinywani. acha tabia hiyo. Thanks.

 3. Gervas Says:

  Udaku ndo wenyewe kwa kurekebisha tabia za wakwale. wenye tabia za kufanya vitendo vinavyobomoa maadili ya kitanzania hawayapendi magazeti ya udaku. Kila nchi ina maadili yake, hivo basi lazima katika jamii yoyote wanajamii wenyewe wawe mstari wa mbele kunyoshea kidole jambo ambalo linakinzana na maadili yetu, magazeti ya udaku ndo mojawapo. Nakama wale wanaodhani kuwa yanafanya hivo ili kuuza magazeti basi washitaki maana sheria ipo inawalinda (…Newspapers Act, 1975) mimi nasema big up Udaku newspapers.

 4. Gervas Says:

  sorry ni … Newspapers Act, 1976

 5. Pearl Says:

  mi nina swali kwa huyo mrisho lakini kabla ya swali naomba kumnukuu kama ifuatavyo:
  “Nikiwa kiongozi wa kampuni ya habari, sipendi kuona mtu yoyote anaonewa. Pale ninapoletewa malalamiko na msomaji akilalamika kuonewa kwa kuandikwa vitu ambavyo hakuvifanya huwa nakosa amani ndani ya nafsi yangu.Siku zote tunajaribu kusimamia uwazi na ukweli, sipendi kumuonea mtu kwa kitu cha uongo”. Mwisho wa kunukuu.

  Ndugu Mrisho hapa tunaongelea juu ya swala la reputation ya mtu mbaye tayari mnakua mmeshaiharibu.Mtu kama huyo mnamlipa fidia gani kwasababu sio utuambie unaishia kukosa amani ndani ya nafsi wakati jamii inamuangalia huyo mtu kwa jicho lingine la tofauti na nyie ndo mnakua mmesababisha hayo yote!!!!!

 6. masumbuka Says:

  Udaku uliokwenda shule unauza lakini huu utumbo ambao umo katika magazeti yenu unatia kinyaa hata kulishika gazeti lenyewe! Mimi binafsi napenda sana kusoma vichekesho, uzushi uliolenga katika kutoa burudani na siyo kutukana watu au kuwadhalilisha watu utu wao.Napenda hadithi fupi fupi za kufikirika (fiction short stories/thrillers), cartoons, lakini Uandishi wenu haujatulia hata kidogo! Matumizi ya Front Page – Ukurasa wa Mbele bado hamjui thamani yake, utakuta vichwa vya habari vya kijinga kabisa viko ukurasa wa mbele au picha za matukio ya kikatili yasiyo faa kuonyeshwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 14 ziko mbele, eti ili kuuza sana gazeti! Hakuna ustaarabu kabisa katika kuchagua maneno au namna ya kuufikisha ujumbe kwa walengwa. Kwa wenzetu kwa mfano magazeti yenye udaku mwingi sana wa ngono na uzinzi huuzwa katika sehemu maalum tu kama vile supermarkets na stores au pubs ambako watoto wadogo si ruksa kwenda.Lakini kwetu hapa utakuta gazeti lenye habari chafu kabisa linauzwa na kijana mdogo kabisa nje tu ya Kanisa au Msikiti! Lazima wasambazaji wa magazeti yenu wawe makini sana kuhusu hilo. Mimi naamini kwamba magazeti ya Udaku yakitumika vyema yana mchango mkubwa sana katika kuiweka sawa na kuiburudisha jamii. Kinachotakiwa hapa ni kwa wenye magazeti kuwa serious na biashara inayo wapatia riziki ili msij e ‘Mkanyea Kambi’. Nidhamu, Ustaarabu, Ubunifu, na Kutunza heshima yenu na ya jamii ni baadhi ya mambo muhimu sana ambayo mtapaswa kuyazingatia nyakati zote.Magazeti ya Udaku yasiwe kwa ajili ya watu ambao hawakwenda shule tu au wenye vipato vya chini.Boresheni kazi zenu ili yawe kwa ajili watu wa rika zote na madaraja yote ya vipato!

 7. Matty Says:

  Udaku juuuuuuuuuu ulitupa picha ya mrembo Nora kajiachia ile mbaya kwa raha zake…endeleeni kukamua!!!!!!!!!!!!!!

 8. DUNDA GALDEN Says:

  Udaku au umbea kama tafsiri ya mitaani una sura mbili kuna kuandikwa kwa mema au mabaya uliyofanya au unayotaka kuyafanya poin yangu inagusa mf.mabaya
  Kwa aliendikwa akiwa na ndugu au jamaa wanachukizwa sana
  Lakin kwa wengine upata uelewa nini kilitokea kwa muhusika
  Inakuwa fundisho kwa wengine kwani jamii haikupendezewa

  Lakini ukiandikwa kwa wema ugeuka na kumfagilia aliendikwa kwa tafsiri ya mitaani uwa jambo zuri sana
  Kwangu endelezeni libeneke mwageni habari kila kona na wengi wajifunze
  chafosa

 9. binti-mzuri Says:

  ah!udakuu oyeeeeeee … kwanza bei rahisi kuliko nipashe

 10. Mswahilina Says:

  Gervas, ni WAKWALE au WAKWARE?

 11. Pius Says:

  Hoja yangu ya msingi ni kuhusu wale wanaofumaniwa na kisha kuwaweka utupu kwenye magazeti tena front page. Hili nalipinga, ni kweli haipendezi mtu kutembea na mke/mme wa mtu lakini kwangu mimi kile kitendo cha kuweka uso wake kwenye gazeti chatosha kumfunza huyu mtu lakini si kumuweka wazi na “jando” lake hilo ndio tatizo kwangu. Naona kama ule ni udhalilishaji wa kijinsia na kibaiolojia kwani unakuta huyu mtu pamoja na uzinzi wake ambao kwangu ni maisha binafsi unakuta pia anafamilia na ana watoto ambao wanamuita Baba/Mama kwa ujumla pale unanyanyasa kisaikolojia familia nzima na wale wotw waliokaribu na Mfumaniwa yule, Mi nafikiri kuweka picha tuu yatosha. Nasema hivi kwa vile nimeona kilichotokea kwa jamaa yangu ambaye alikunywa sumu mara 2 kwa kutaka kujiua tangu alipotolewa kwenye gazeti mwaka jana na tangu hapo ana Msongo wa Mawazo (Depression).

 12. naj Says:

  mi napenda saaanaa magazeti hayo yawepo maaanaa kuna watu tabia zimezidi ningependa saana magazeti haya yamulike hasa masuperstaar wakibongo ila yawe yana lenga mambo ya ukweli sio mtu kakutwa tuh hajamfanya mnamnakili hata akiulizwa mambo yanakuwa tofauti inapendeza ukweli kwani maanaa halisi ya udaku au umbea wahusika wanawahi kufikisha ujumbe tuh kwa hadhira..na si kamaa jambo halipo.
  ila sio utumike unafiki maaanaa hio tena maanaa nyingine

 13. binafsi sipendi magazeti ya udaku. Lakini ni hii ni biashara. And for as long as kuna watu wanaendelea kuyanunua, these guys will keep being in business. Ingekuwa kila mtu anafikiria along the same logical lines like the ones who have posted these comments here, then magazeti ya udaki yatafilisika. Sadly most people wanna know every tad bit of detail in celebrities’ lives. Hii sio kwa nyumbani tu, hata nje.

 14. MDAU Says:

  magazeti ya udaku bomba sana.

 15. MDAU Says:

  nina maana kuwa yanafundisha kazi kwako wewe msomaji ujue mbivu na mbichi kwani kila linaloelezwa kwenye udaku kuna mengine mazuri yakufuata na mengine si mazuri. big upana.big up

 16. DUNDA GALDEN Says:

  SAMHANI WADAU NJE YA JANGWA
  MZEE WAUDAKU MIMI NATAKA VITABU AU HADITH ZA SHIGONGO NITAZIPATAJE?NIMEJARIBU KUANDIKA KWENYE MAIL ZENU SIPATI JIBU. SIKO NYUMBANI TZA KUH GHALAMA NITAZIGHALAMIA PINDI NITAKAPO PATA MAWASIANO YA UWAKIKA NA WAHUSIKA
  KWENU BC MNAWEZA KUUPEPELUSHA UJUMBE WANGU KWA MHUSIKA
  AHSANTENI SANA NA SAAHANI KWA USUMBUFU

 17. Mrisho Says:

  DUNDA: tafadhali wasiliana nami kupitia email zifuatazo ili utufahamishe unahitaji vitapi vipi na uko nchi gani. Vitabu vilivyopo hadi sasa ni Rais Anampenda Mke Wangu na Machozi na Damu:
  globalpublishers@bol.co.tz, info@globalpublisherstz.com au amsalawi@yahoo.com

 18. Gervas Says:

  Pius !! mbona mshikaji unatetea saana wazinzi??
  Mswahilina ….ni wakware na sio wakwale tunakipenda kiswahili. Hebu fikirieni nyie mnaopinga Magazeti ya udaku endapo hapatakuwa na chombo cha jamii cha kuwanyoshea vidole hawa wachafuzi wa maadili itakuwaje?

 19. Mimi nafikiri ni muhimu sana kuwepo kwa magazeti ya udaku.Cos………!!!!!

 20. DUNDA GALDEN Says:

  17 Mrisho
  Shukrani kwa kupata mawasiliano yenu nimekuandikia leo
  Shukrani kubwa sana kwenu BC kwa blog yenu ya kuutunganisha na nyumbani
  samahani wadau hii nje ya jangwa
  chafosa chai goda

 21. Matty Says:

  Jamani hicho kitabu cha Rais anampenda mke wangu ni kitabu kizuri sana daaa nilisoma mfululizo wake gazetini kipindi fulani nawapa hongera kwa kweli mtunzi anakichwa kilichotulia sana!

 22. Pius Says:

  Gervas kimsingi sio natetea wazinzi najaribu kuongelea utu wa mtu, ni vyema piucha yake iwekwe lakini sio uchi waweke sura yake tu au pichja ya uchi na sura kuzibwa.
  Anyway narudia tena sio kama natetea ila najaribu kuiangalia familia zaidi ya huyu Mkware aliyefumaniwa hehehe, Nasema hivyo kwa kuwa kama nilivyosema yule jamaa alitaka kujiua kwa aibu aliyopata.
  Anyway ni mtazamo tuu.
  By the way Kilala Heri GPL, kuendelea kuwepo kwa miaka 10 inaonyesha kuwa mnakubalika na jamii. Kaka Mrisho nakumbuka tangu enzi zile tunakutana Pre Press kwa Nyabasy/Khamis/Maluba etc na page zako hehehe umetoka mbali kaka mpaka kulifikisha hilo gazeti lilipo.

 23. hombiz Says:

  ufukunyuku ukizidi soooooo!

 24. magazeti ya udaku yanafaida kubwa sana big up wanao yaponda ni wivu wao

 25. chinga Says:

  we acha watu wajivinjali ila isiwe balaa kwa kusambaza ngoma

 26. eric Says:

  sio udaku mbona yanasema kweli tupu dont say udaku say really news.


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s