BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

ANA KWA ANA NA “MWENYEKITI” MAGGID MJENGWA. August, 17, 2008

Kama wewe ni msomaji mzuri wa magazeti na majarida mbalimbali kutoka Tanzania,basi sina shaka kabisa kwamba jina Maggid Mjengwa (pichani) litakuwa sio geni kwako! Makala zake za kusisimua,kuchokoza hisia na kujenga hoja za nguvu ni miongoni mwa vivutio muhimu vya wasomaji wa magazeti ndani na nje ya Tanzania. Leo hii tunaweza kabisa kuthubutu kusema kwamba Maggid ni miongoni mwa wanahabari bora tulionao kwani hana uoga wowote pale anapokuwa anaandika au kuongelea jambo ambalo analiamini kwa dhati.

Lakini Maggid,kama ambavyo pengine unafahamu tayari, haishii magazetini tu bali pia ni blogger maarufu hivi sasa. Blog yake ya picha ambayo mwenyewe anaiita “kijiji” na hivyo wasomaji wake na watembeleaji wake “wanakijiji”, imejipatia umaarufu sana kwa kuonyesha au kwenda kule ambapo ndiko kunahesabika kuwa kwenye hali halisi ya maisha ya mtanzania. Ukiitembelea na kuisoma blog yake vizuri kwa kutizama picha lukuki zinazoipamba blog yake,utaweza kuwa jaji mzuri kama “bongo ni tambarare” au bado zile ahadi za uchaguzi uliopita ni mbwembwe za kisiasa tu.Mwenyewe anasema blog yake ni kimbilio na sauti kwa wale ambao kila mara huwa wanasahauliwa!

Maggid pia ni mjasiriamali.Yeye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ijulikanayo kama Ikolo Investment Co ambao ndio wachapishaji wa Gozi Spoti; jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani linalotoka kila Jumatano. Maggid pia ni mwanamichezo,mpenda michezo na shabiki mkubwa wa soka.

Hivi karibuni,baada ya kumsaka kwa muda mrefu kutokana na ratiba zake za kazi kumbana,tulifanikiwa kupata fursa ya kufanya naye mahojiano utakayoyasoma hivi punde.Kama ambavyo ungetegemea,Maggid anatoa “darasa” katika mahojiano haya.Mbali ya kukupa historia ya maisha yake kwa undani,Maggid anakumbusha vipengele fulani fulani vya historia ya nchi yetu ambavyo ni muhimu. Lakini kwa mapana, anaongelea kuhusu suala la uandishi na pia blog yake bila kusahau changamoto ambazo nchi yetu inakabiliwa nazo hivi leo katika nyanja mbalimbali. Fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;

BC: Maggid Mjengwa,karibu sana ndani ya BongoCelebrity

MJENGWA: Asante sana!

BC: Kwanza kabisa ningependa kupata kutoka kwako mwenyewe historia fupi ya maisha yako.Ulizaliwa wapi,lini,ukasomea wapi,unatoka kwenye familia ya watoto wangapi na mambo kama hayo.

MJENGWA: Awali ya yote, natanguliza shukran zangu za dhati kwako Jeff kwa heshima uliyonipa kwa kufanya mahojiano nami kupitia jukwaa hili la kijamii. Naitwa Maggid John Ramadhan Mjengwa. Nina bahati ya kuwa na asili zaidi ya moja. Nina asili ya pwani na bara. Nimezaliwa Kliniki ya Ocean Road, Dar Es Salaam. Mimi ni mmoja wa wale ambao huwaita wa kizazi cha Azimio la Arusha la mwaka 1967. Nimekulia Ilala, Mtaa wa Iringa nyumba namba 27. Baadae familia yangu ilihamia Kinondoni Biafra, mwaka 1977.

Natoka katika familia ya watoto tisa. Wawili hawako tena duniani, mmojawapo ni kaka yangu, Grey John Ramadhan Mjengwa. Alifariki katika ajali ya basi mkoani Tanga zaidi ya miaka kumi iliyopita. Grey ndiye aliyenitangulia kwa kuzaliwa. Na mimi nilikuwa wa pili kuzaliwa. Elimu ya msingi na Sekondari nimesomea Dar. Nilimaliza Tambaza Sekondari mwaka 1987, baadae nilisoma Kidato cha Tano na Sita mkoani Mbeya pale Sangu Sekondari. Baada ya Sangu nilijiunga na JKT kwa mwaka mmoja ( Operesheni Kambarage 1990-91). Kisha nikaamua kwenda kuishi na kufanya kazi za kujitolea wilayani Njombe, Iringa. Niliishi kijiji cha Igagala. Huko nilifundisha kwa kujitolea kwenye Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi, Ulembwe. Kilomita 15 kutoka Njombe mjini. Nilipewa pia eka moja ya kulima. Nililima mahindi, viazi na maharage. Vile vile nilipiga picha na kuandika habari za huko na kutuma kwenye magazeti, mojawapo ni Daily News. Baada ya mwaka mmoja na nusu kijijiji hapo nilikwenda nchini Sweden. Huko nilikaa kwa miaka 12. Nimesoma kozi kadhaa kwenye vyuo vya Sweden na hatimaye kuhitimu shahada ya ualimu kwenye Chuo Kikuu cha Linköping. Nimefanya kazi pia ya kufundisha kwenye baadhi ya vyuo vya maendeleo vya Maendeleo ya wananchi vya nchini Sweden.

Naam. Nimesema nina asili mbili; pwani na bara. Nitafafanua. Baba yangu alizaliwa kijiji cha Nyeregete, kwenye bonde la Usangu, Mbeya. Babu yangu, Chifu Mtenji Ramadhan Mjengwa alikuwa kiongozi wa kijadi mongoni mwa watu wa kabila la Wasangu. Babu yangu mzaa mama, Fundi Pazi alitokea kwenye kabila la Wahehe wa Iringa. Yeye alifanya kazi ya ujenzi wa barabara. Katika kazi yake akaja kukutana na bibi yangu mzaa mama, Amina Binti Muhando Mwaruka. Hivyo basi, babu mzaa mama akalowea pwani na hususan Uzaramoni. Bibi yangu, Amina binti Muhando Mwaruka ( alifariki mwaka jana akiwa na umri wa miaka zaidi ya 87) anatoka kwenye ukoo maarufu wa Mwaruka. Ni ukoo huu anaotoka mwanamuziki mahiri, Marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka. Mbaraka alimwita bibi yangu shangazi. Nyumba ya marehemu bibi yangu kijijini Mzenga inapakana na nyumba ya Marehemu Mwinshehe Mwaruka, baba mzazi wa marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka.

Labda mpaka kufikia hapo kuna watakaoanza kunielewa kwanini napenda sana maeneo ya pwani kama vile Bagamoyo. Hakika, ni kutokana na asili yangu hiyo ya pwani kwa upande wa mama yangu. Kutoka Bagamoyo mpaka kijijini kwa mama yangu, Mzenga, Kisarawe ni mwendo wa dakika 45 kwa gari ndogo kwa kupitia njia ya mkato ya Bagamoyo-Miembe saba hadi Mlandizi.

BC: Unakumbuka wakati ukiwa mdogo au ukiwa shule ya msingi ulitaka kuwa nani pindi ukimaliza shule? Na labda kuongezea tu,ni waandishi gani wa habari uliokuwa ukipenda zaidi kuwasoma enzi hizo?Kwanini?

MJENGWA: Nilipenda masuala ya siasa, picha na michezo tangu utotoni. Mazingira nayo yanachangia kumfanya mtu awe kama alivyo. Pale Ilala tulikaa karibu kabisa na uwanja wa Karume. Nakumbuka niliingia uwanjani Karume kwa mara ya kwanza nikiwa na miaka sita nikiongozana na kaka yangu Grey. Ilikuwa ni mechi kati ya Simba na Cosmo Politans. Tuliingia uwanjani kwa kuruka ukuta kwenye moja ya kona za uwanja huo. Grey alinipandisha na kunishusha uwanjani. Nilishangaa mgambo hawakunifuata bali waliwafuata wengine. Leo naelewa kuwa mgambo wale walikuwa ni watu wema sana. Wangefanya nini na mtoto wa miaka sita anayetamani kuona pambano la soka? Baadae ilikuwa rahisi zaidi kuingia uwanjani Karume na hata National Stadium. Ilikuwa ni kwenda getini, unamtafuta mtu mzima mmoja, unamuamkia kisha unamwomba akushike mkono muingie wote uwanjani kama mtoto wake. Mkishavuka geti hakuoni tena, wakati mwingine, kwa shauku ya mpira tulisahau hata kusema ‘asante’ kwa waungwana wale waliotusaidia kuingia bure uwanjani.

Mapenzi yangu kwa klabu ya Simba yalianzia katika mechi ile ya kwanza niliyoiona maishani mwangu kati ya Simba na Cosmo. Simba walivaa jezi nyekundu na nyeupe. Cosmo walivaa bluu. Basi, cha kwanza kwangu ilikuwa kuchagua rangi. Nilichagua nyekundu na nyeupe. Lakini si rangi tu, Simba siku ile walicheza vizuri na kushinda pambano hivyo basi kutonifanya nibadili uamuzi wangu.

Hakika, tangu utotoni nilikuwa na mwelekeo wa kupenda masuala ya kisiasa na kijamii. Kupenda michezo na picha. Kwa namna moja au nyingine, wazazi wangu walinisaidia sana kukuza vipaji vyangu. Nilianza kusikiliza redio nikiwa na miaka minne au mitano hivi, wazazi waliniruhusu kuchezea redio. Mwanzoni nilidhani kuna watu wanaongea na kuimba ndani ya redio! ( Nadhani baadhi yenu mlifikiri kama mimi). Mapema sana nilianza kusikiliza vipindi vyenye kuelimisha. Miaka hiyo kabla hata sijatimiza miaka saba nakumbuka kuanza kusikiliza vipindi kama; mbiu ya mikoa, ujumbe wa leo na mazungumzo baada ya habari. Hicho cha mwisho ndicho ambacho Mzee Paul Sozigwa alikuwa akikiandaa. Nakumbuka pia kila Jumapili Mkurugenzi wa RTD, Mzee David Wakati alikuwa na kipindi chake chenye kujadili masuala mbali mbali. Halafu nakumbuka kufuatilia kipindi cha ‘ Umoja wa Mataifa Wiki Hii’ ambapp ‘Born Again Pagan’ maarufu kama BAP na Abdalah Mbamba walikuwa wakikiendesha kwa nyakati tofauti.

Nilikuwa na kiu kubwa ya kusoma maandishi na kuangalia picha kwenye vitabu, majarida na magazeti. Nilifungua karibu kila kurasa ya kitabu kilichokuwa nyumbani. ( Hatukuwa na vitabu vingi sana). Nakumbuka kitabu cha Patrick Lumumba wa Kongo, sikuweza kusoma ( kiliandikwa kwa Kiingereza) lakini nilifuatilia picha za kitabuni na kumwuliza baba yangu. Nikafahamu kilihusu nini. Nakumbuka pia kitabu cha John Okello( Zanzibar Revolution) Hiki nacho kilikuwa ni kwa Kiingereza, niliangalia picha na kumdadisi baba yangu, alinieleza kilihusu nini. Nilipofika Sekondari niliweza kuvisoma vitabu vyote hivyo. Hicho cha mwisho kilinifanya nifatute kila namna ili nifike Zanzibar kuona kwa macho yangu mazingira ya kisiwa yalikofanyika mapinduzi aliyoyaelezea Okello kwenye kitabu chake. Nilifika Zanzibar mara baada ya kumaliza kidato cha nne. Na nilikuwapo kwenye sherehe za mapinduzi Januari 12, 1989. Yote hii inaonyesha kwa namna moja au nyingine jinsi vitabu vinavyoweza kutujenga kama wanadamu.

Kuhusu picha nakumbuka pale Karume Stadium nilipenda sana kukaa nyuma ya goli na karibu kabisa na wapiga picha. Namkumbuka sana mpiga picha wa Daily News, Ernest Millinga. Nilifuatilia kazi zake uwanjani na hata magazetini. Siku moja baada ya mechi nilitafuta Daily News na kuangalia picha alizopiga Millinga. Zilinifanya nitake kujua pia maelezo ya picha hizo. Kwa namna moja au nyingine zilinisaidia kujifunza lugha ya Kiingereza.

Maggid alipoitembelea Zanzibar enzi hizo.Unakumbuka hizo gari zilikuwa zinaitwaje?

BC: Katika pekua pekua zetu kukuhusu tumegundua kwamba ulianza kuandika siku nyingi sana,tangu ukiwa shuleni Tambaza.Kwa msingi huo utakuwa ukifuatilia kwa karibu masuala ya maendeleo ya habari duniani na zaidi nchini Tanzania.Leo hii ukiangalia nyuma,unadhani pamekuwepo mabadiliko gani ya msingi tokea miaka ile ulipoanza kuandika mpaka hivi leo? Hapa nazungumzia mabadiliko kwako wewe binafsi na kwenye uandishi kwa ujumla.

MJENGWA: Ni kweli kuwa nimeanza kuandika tangu nikiwa Kidato cha Pili pale Tambaza. Lakini naweza kusema nimeanza kuandika tangu nikiwa shule ya msingi. Nakumbuka nilipenda sana pale mwalimu wa Kiswahili alipotupa kazi ya kutunga sentesi. Tukiambiwa tutunge sentesi tano mimi nilitunga kumi na tano!

Hata hivyo, Tambaza ndipo hasa nilipoanzia uandishi wa kuonekana na wengine. Mathalan, nilianzisha ‘ kijigazeti’ changu. Niliandika kwa mkono juu ya mambo yanayotokea kwenye jamii yetu ya Tambaza, iwe michezoni au hata yanayotokea wakati wa kugawa chakula na matunda jikoni na darasani. Nilivutiwa zaidi na kutiwa moyo nilipoona si wanafunzi wenzangu tu wanaosoma maandishi yangu, bali hata walimu walisoma pia. Sikupata kumwona Mkuu wa Shule, Mzee Kalumuna akisoma maandishi yangu yale, lakini, Second Master wetu Mwaipopo alikuwa mmoja wa wasomaji wangu wakubwa.

Hata hili la kuandika kwa namna fulani linatokana na mazingira niliyokulia. Naamini uandishi unatokana na kusoma. Mama yangu alikuwa akifanya kazi Idara ya kupiga Chapa ya Serikali ( Government Press). Aliitambua mapema kiu yangu ya maandishi na kupenda kusoma na hata picha. Akitoka kazini alikuja na machapisho mbali mbali ya Kiserikali. Na hapa, kwa mara kwanza nabainisha, kuwa mama yangu aliniruhusu kusoma vitabu vya bajeti za Wizara za Serikali hata kabla ya wabunge hawajavitia machoni! Mama alikuja na kopi nyumbani akijua kuwa nilipenda sana kusoma, kudadisi na kufuatilia mambo. Ziada katika hilo ni kuwa niliweza pia kupata kopi ya gazeti maalum la serikali. ( Government gazette). Mara nyingi humo ziliandikwa habari za ndani ya Serikali kama vile uhamisho wa watumishi na mengineyo.

Wakati mwingine mama alirudi nyumbani na sahani ( plates) zenye picha mbali mbali zilizochapwa kwenye vitabu na mabango ya Serikali. Nilipenda sana kuziangalia kwa karibu picha zile. Hakika haya ya vitabu na picha yalinifanya nianze darasa la kwanza nikiwa najua kusoma na kuandika. Shida yangu ilikuwa siangalii vituo wakati nasoma ‘ Juma na Roza’!

Halafu linakuja suala la kupenda masuala ya siasa. Bila shaka, kwa namna moja au nyingine limechangiwa na hayo niliyoyaeleza hapo juu. Lakini pia pale Ilala tuliishi karibu kabisa na barabara kuu ya Uhuru na viwanja vya jangwani. Utotoni nilibahatika kuwaona viongozi wengi maarufu kutoka nje ya nchi wakipita barabara hiyo. Nakumbuka kuwaona viongozi maarufu kama vile Fidel Castro, Kaunda, Chu En Lai, Indira Gadhi ( Gandhi alipita Pugu Road ) na wengine wengi. Viwanja vya jangwani nilikwenda mara kadhaa kusikiliza mikutano ya kisiasa.

Kubwa kabisa la kisiasa nililopata kushuhudia katika maisha yangu ni kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi. Siku ile ya tarehe 5 Februari, 1977 nilikuwapo pale Ilala Bomani. Barabara ya Uhuru ilifungwa kwa magari. Kwaya ya Mzee Makongoro ilitumbuiza. Kulikuwa na gwaride la chipukizi na ngoma za asili. Ilikuwa ni shangwe na shamramshamra kila mahali. Tuliokuwa watoto wakati huo tuliingiwa na matumaini ya maisha bora ya baadae chini ya Chama kipya cha Mapinduzi. Iliimbwa; ” Chama Mapinduzi ee, Endeleza Kazi Ya Afro Na TANU!”

Miaka 30 imepita tangu kulishuhudia tukio lile kubwa maishani mwangu, ndio maana, siku zote najihisi ninayo ya kuandika kuhusu masuala ya siasa na kijamii, kwani, sikushuhudia tu kuzaliwa kwa CCM, bali tangu nikiwa na miaka saba nimekuwa nikifuatilia masuala ya kisiasa na kijamii katika nchi yetu bila kujihusisha na chama chochote cha siasa kwa maana ya kuwa mwanachama au mshabiki wa chama cha siasa.

BC: Umekuwa mwandishi kwenye magazeti kwa muda mrefu sasa.Ingawa hivi sasa huandikii tena gazeti la Rai ambalo ulikuwa unaliandikia kwa muda mrefu,kuna watu ambao bado wanakutambua kama “Maggid Mjengwa wa Rai”.Kwa maana hiyo nadhani sio vibaya kama tutakuuliza kidogo kuhusu Rai.Ni kwanini uliamua kupumzika kuandikia Rai? Unadhani ulijifunza mambo gani ya msingi wakati wa uandishi wako kwenye gazeti la Rai?

MJENGWA: Ah! ‘ Maggid wa Rai’. Sasa ni ‘ Maggid wa Raia Mwema!’ Ndio, nilianza kuandikia Rai Agosti 8, 2004. Nakumbuka Agosti 4, 2004 nilikwenda Sinza Kijiweni kuwasalimia kaka zangu akina Bwire, Mbwambo, Salva na jamaa wengine. Sikuwa na mawazo ya kuandikia Rai, maana nilikuwa na safu yangu ya ‘ Gumzo la Ijumaa’ kwenye gazeti la Majira. Mtu wa kwanza kukutana nae kabla sijaingia ndani alikuwa Salva Rweyemamu. Baada ya kumuamkia akaniambia; ” Tena Maggid imekuwa vizuri umekuja, njoo utuandikie kwenye Rai”. Nilishtuka kidogo, lakini nikaiona hiyo ni changamoto mpya.

” Why not?” Nikamjibu. Kisha akanichukua na kunikabidhi kwa Bwire. Tangu hapo ikawa kama ilivyokuwa. Lakini, katika muda wote wa kuandikia Rai sikuwahi kushinikizwa kwa namna yoyote ile kuandika kile ambacho wengine walitaka niandike. Nimejisikia huru kuandika fikra zangu. Rai ilinisaidia kutengeneza jukwaa na kuwafikia watu wengi zaidi ambao nisingeweza kuwafikia. Nitakuwa ni mwizi wa fadhila nisipowashukuru wale wote waliofanikisha hili na hususan Salva Rweyemamu aliyeuona uwezo wangu na kunipa changamoto. Huyu Salva Rweyemamu ni mmoja wa watu ninaowaheshimu sana hata kama kuna ambayo huwa hatukubaliani. Ana uwezo wa kutambua vipaji na fursa zilizopo kwa wengine na namna ya kuzitumia vema. Ni Salva Rweyemamu, wakati akiwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mtanzania aliyenikaribisha ofisini kwake, pale Mtaa Mkwepu, si mara moja, na kunishauri mawili matatu katika fani hii ya uandishi ili niwe bora zaidi. Ni Salva Rweyemamu, Mhariri wa kwanza kabisa kunitumia faksi nikiwa Sweden mwaka 1995. Alifanya hivyo hata kabla ya kunitia machoni. Alinitumia faksi kunishukuru kwa kuchagua kuliandikia gazeti la Mtanzania.

Tangu 2004 nimeliandikia Rai hadi mwaka jana kunako mwezi Septemba. Naam. Ilifika mahali mazingira na upepo wa kiuandishi ulinilazimisha nimwandikie Mhariri wa Rai, kaka yangu Muhingo Rweyemamu kumshukuru na kumjulisha kuwa nimeamua kujipumzisha na kuwapisha wengine. Nilikaa kijiweni kwa zaidi ya mwezi mmoja bila kuandika makala za magazetini. Nilibaki kuwa msomaji kama wengine. Hatimaye nikapokea simu ya John Bwire akiniomba rasmi nijiunge na jarida jipya la Raia Mwema. Sikusita kuchukua changamoto hiyo.

BC: Katika historia yako ya uandishi wa habari na makala magazetini,ilishawahi kukutokea ukaandika jambo ambalo baadaye ulipokaa na kutafakari upya ulitamani siku zirudi nyuma na jambo lile lisiwemo tena magazetini?Kama ndio ilikuwaje na ilikupa fundisho gani?

MJENGWA: Hakika hilo kwa bahati nzuri halijanitokea.

BC: Tukiwa bado kwenye suala hilo hilo la ukuaji wa nyanja za habari na mawasiliano nchini Tanzania.Unaliongeleaje suala zima la uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania?

MJENGWA: Ni swali gumu na zuri. Katika nchi yetu bado hatuna uhuru wa vyombo vya habari nikimaanisha uhuru wa kiuchumi. Tuna vyombo vya habari na wanahabari tegemezi. Hakuna ruzuku ya Serikali kwa vyombo vya habari vya binafsi. Hili linapelekea kushuka kwa viwango vya wanahabari na habari zenyewe.

Leo tuna mwanahabari anayetegemea lifti ya Mkuu wa Wilaya ili afike kwenye ziara ya DC. Hata hela ya kutuma faksi itoke kwa huyo huyo DC! Sasa unategemea mwandishi huyu ataandika jinsi wakazi wa eneo fulani walivyomweka kiti moto DC! Anajihatarishia kushushwa njiani kwenye ziara inayofuata ya DC! Hakika hilo ni swali gumu na zuri lenye kuhitaji makala nzima kuelezea.

BC: Sasa tuongelee blog yako ambayo siku za hivi karibuni imezidi kujipatia umaarufu. Katika mahojiano uliyofanya na jamaa wa Global Voices hivi karibuni ulikaririwa ukisema kwamba ulitaka upate mahali kama “kijiji” hivi ambapo watu wanaokosa pa kusemea wapate jinsi ya kufanya hivyo.Mbali na hilo,ni mambo gani matatu ambayo uliyatarajia na yepi matatu ambayo hukuyatarajia ulipokuwa unaanzisha blog hiyo?

MJENGWA: Nilitarajia blogu iwe ni ‘ jukwaa la maarifa’, mahali pa watu kukutana na kufahamiana, mahali pa burudani kupitia picha na mengineyo ili watu waweze kucheka na kutafakari. Binafsi napenda sana utani. Na wakati mwingine natumia blogu na picha kama kufanya utani huo. Si jambo rahisi sana kutaniana kwa njia ya blogu. Hutokea baadhi hawanielewi kama natania. Hata picha nyingine na maelezo huweka kwa makusudi mazima ya kuchokoza mjadala. Naona wajibu wangu ni kama wa mwalimu darasani, si kufundisha, bali kuandaa mazingira ya wanafunzi kujadili na kutoa maarifa waliyo nayo.

Sikutarajia; lingekuwa jukwaa kubwa hivi kwa muda mfupi, kuwa lingetoa fursa kwa wengine na hata kwangu mwenyewe kuwa na mahali pa kupata habari moto moto na kuwa jukwaa la kujieleza kwa uhuru na kupata maarifa mapya. Tatu, sikutarajia kuwa watu wengi hivi, ndani na nje ya nchi wangetumia blogu kama vile wanavyotumia magazeti katika kupata habari.

Novemba, 1996. Wafuasi wa CCM wakiandama kuingia Uwanja Wa Sokoine Mbeya kumsilikiza Rais Mstaafu Benjamin Mkapa. Maggid anasema; “Nilikuwepo uwanjani kushuhudia tukio lile. Watu hawakuwa wengi, wanafunzi wengi wa shule za Msingi waliletwa uwanjani. Wanafunzi hao wanaoonekana pichani sasa ni wapiga kura. Picha hii ni baadhi ya kazi zangu ambazo hazikuwahi kuchapishwa magazetini. Hakika, teknolojia hii ya blogu imetuwezesha baadhi yetu kupekua kwenye maktaba zetu na kukutana na kazi ambazo, huko nyuma tulizifanya kama hobby. Hakukuwa na vyombo vingi vya habari . Lakini sasa, kwa kutumia blogu tunaweza na tuna uhuru zaidi wa kuzichapa kazi hizo na wengi wakaziona.”

BC: Pamoja na kwamba uandishi wa kiraia(citizen journalism) kwa mfano kupitia blogs nk umekuwa ukiendelea kukua kwa kasi na hivyo wakati mwingine kuwa news breaker wa mwanzo kabisa,kwa upande wa Tanzania bado blogs zenye habari mpya kila siku ni chache sana.Unadhani hii inatokana na nini?Nini kifanyike ili kushawishi watu wengi zaidi waanzishe blogs zao na kuzihudumia kila siku?

MJENGWA: Nadhani hili la blogu inahusu mapenzi na nia ya mtu. Blogu inaweza kuanzishwa kwa madhumuni mbali mbali. Kuna wanaoanzisha kama photo album. Kuna wanaoanzisha wakiwa na nia ya kuihudumia kila siku, lakini muda hawana. Na kama ni blogu ya picha inabidi mtu uwe na mapenzi na picha. Hakuna jibu la jumla la nini kifanyike isipokuwa kila anayeanzisha blogu ajiulize kwanini anaanzisha blogu.

BC: Ni wanablog gani duniani,ikiwemo Tanzania, wanaokuvutia hivi sasa?Kwanini?

MJENGWA: Navutiwa na wanablogu wengi, ndani na nje ya nchi. Nikiorodhesha watakuwa wengi. Lakini kwa nyumbani kaka yangu Issa Michuzi ni mmoja wa wanaonivutia sana. Kwa Michuzi si picha tu, ni zaidi ya picha. Mara nyingi nikikutana na Michuzi hufurahia sana, maana tunaongea lugha moja ( lugha ya picha) Tunavaa miwani sawa ya ‘macho ya picha’ ( Ingawa Michuzi yake ni 2.5 na miye 1.5!)

Vinginevyo kazi kama za kwako Jeff na hata Haki Ngowi zinanifurahisha sana. Kwamba ubunifu wenu umewafanya muwe karibu sana na jamii yenu pamoja na tofauti ya maelfu ya maili kutoka ilipo jamii yenu. Kuna vijana wengine wanaoibukia na kufanya kazi ya kusifika, mfano ni kijana Bob Sankofa. Navutiwa na ubunifu na kazi zake. Halafu tuna vijana nje ya nchi, baadhi nimekutana nao nilipobahatika kutembelea ughaibuni. Nao wanafanya kazi ya nzuri kupitia majukwaa kama haya ya blogu na hata nje ya blogu. Tuwatambue na tuwape moyo kwa kazi zao.

Maggid(kulia) akiwa na Issa Michuzi ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.Wote ni wapenzi wa Michezo na wote ni bloggers.Raha ilioje.Maggid ni Simba wa kutupwa.Michuzi je?

BC: Kwa sababu blog yako ni ya picha tungependa kukuuliza swali hili.Mpaka hivi leo ni picha gani ambayo uliipiga na kuitumia kwenye blog yako ambayo kila mara inakurudia mawazoni?Kwanini?

MJENGWA: Swali zuri, kuna picha mbili, moja niliipiga Morogoro. Mwenyeji wangu yule alinikaribisha vema nyumbani kwake. Nilisikitika sana pale aliponielezea matatizo ya wadudu wanaoharibu maharage yake shambani. Ilifika mahali aliwakusanya na kuwachoma moto akiamini kuwa harufu yake itawafukuza wadudu wengine. Ilisikitisha kwa vile aliko mwanakijiji yule ni mwendo wa saa moja tu kwa gari hadi kilipo Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine. Unajiuliza, wataalam wetu wa kilimo wanafanya nini kumsaidia mkulima kama huyu?

Picha nyingine ni wakati nilipotembelea vijji viwili vya kandokando ya ziwa Nyasa. Moja ya kijiji hicho ni Ikolo. Ni kijiji kisichofikika kwa barabara. Wakati napanda mtumbwi kuelekea huko niliona hatari iliyopo, kwamba fikiri kama nahodha wangu atapatwa na kifafa au mshtuko wa moyo. Tulikuwa wawili tu kwenye mtumbwi. Katika hali hiyo nisingeweza kuungoza mtumbwi, nami ningezama katikati ya ziwa.

Lakini pamoja na fikra hizo niliona umuhimu wa kufika huko. Ni wajibu wangu kujaribu kuwafikia wasiofikika kirahisi. Nifanye hivyo ili sauti zao nao zisikike. Baada ya saa mbili ziwani nilifika Ikolo. Nilipokewa vizuri. Nilikwenda na jarida la FEMA. Niliona jinsi vijana wa mahali pale walivyoligombania jarida lile. Vijana wale walikuwa na kiu kubwa ya kusoma. Ikolo hakuna magazeti wala majarida.

Nikiwa Ikolo, na katika mazingira yale, nilijiwa na fikra za kuanzisha kampuni itakayohusika zaidi na machapisho ya majarida na vitabu. Ndipo wazo la kuanza na jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani lilipoibuka. Haikupita miezi mingi, nikasajili kampuni kwa jina la Ikolo Investiment Co. Ltd. Mimi ni Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo. Kwa miezi minne sasa kampuni hiyo inazalisha jarida la Gozi Spoti; jarida la michezo, sanaa, maisha na burudani linalotoka kila Jumatano. Gozi Spoti linafika hadi Ikolo na vijiji vya jirani kupitia mawakala wetu. Huko zinakwenda nakala kadhaa za bure kwa vijana wa Ikolo. Ikolo Investiment Co. Ltd pia imechapisha kitabu kuhusu maisha ya Barack Obama; alikotoka, aliko na anakokwenda. Machapisho zaidi yanatarajiwa kutolewa. Yote haya ni katika kujaribu kukata kiu ya kusoma kwa wananchi, lakini pia kuchangia katika kuwajengea Watanzania kiu ya kupenda kusoma. Mimi niliandaliwa mazingira ya kupata kiu ya kupenda kusoma. Nimesomeshwa na kufika hapa nilipo kwa gharama za wakulima na wafanyakazi walipa kodi wa nchi hii. Naliona ni jukumu langu na nina deni la kulipa kwa nchi yangu. Deni ni kubwa na sitalimaliza, lakini kushiriki kazi ya kuchapisha majarida na vitabu na kuwafikishia Watanzania hata walio vijijini kwa bei nafuu ni namna ya kupunguza deni hilo, ni wajibu wetu sote.

Hali halisi ya maisha ya mkulima wa Tanzania.Je tutafika kweli?

BC: Blog yako imejipatia umaarufu kwa sababu moja kuu;inaonyesha hali halisi ya mtanzania wa kawaida. Tangu uanze kufanya hivyo umekuwa ukitembelea vijiji na vijiji ambapo umekuwa ukikutana na watanzania wenyeji wa huko vijijini ambao bila kusita tunaweza kusema hali zao ni duni.Ukiongea nao wanakupa ujumbe gani wa msingi kuhusu hali zao?Nini unadhani kinatakiwa kufanyika ili kubadili hali zao?

MJENGWA: Nimejitahidi kuifanya blogu yangu kuwa sauti kwa wasio na sauti. Kwamba ilenge kwenye kuelezea maisha ya kila siku ya Mtanzania wa kawaida. Ionyeshe mafanikio na changamoto zinazomkabili Mtanzania huyo. Kazi yangu imenipa fursa ya kutembelea vijiji vingi vya nchi yetu. Huko nimekutana na kuongea na Watanzania wa kada mbalimbali. Wanavijiji wengi wa nchi hii wanayajua matatizo yao na namna ya kukabiliana nayo. Wanachokosa ni nyenzo. Moja ya nyenzo hizo ni elimu. Cha kwanza wanachohitaji ni elimu, elimu, elimu. Na hapa sina maana ya elimu ya kuingia darasani tu, bali elimu kwa maana ya kusaidiwa kupata maarifa mbalimbali ya kukabiliana na matatizo yao ikiwamo kujua haki na wajibu wao.

BC: Unadhani tekinolojia mpya kama hizi za blogs zinaweza kuwa na mchango gani katika maendeleo ya kijamii na kwa mfano kubadilisha hali za kimaisha za watanzania hususani waliopo vijijini ukizingatia kwamba tekinolojia hizi ni za mtandaoni jambo ambalo bado ni geni sana vijijini?

MJENGWA: Ni kweli, kuwa teknolojia hii bado mpya sana sio tu vijijini bali hata katika sehemu nyingi za mijini. Bado ni asilimia ndogo sana ya Watanzania wanaopata taarifa kupitia teknolojia hii. Iko haja ya kutafuta namna ya kuhamisha baadhi ya taarifa muhimu zinazopatikana katika mtandao zitoke pia katika magazeti na hata redio.

Maggid,he often goes where our leaders don’t bother to go!

BC: Maggid unajulikana kuwa mpenzi wa michezo hususani soka.Pia tunafahamu kwamba wewe ni shabiki mkubwa wa Simba Sports Club au wana Msimbazi.Sasa kama ujuavyo siku hizi watanzania wengi wana ushabiki wa timu za Uingereza.Kwa upande wako unaishabikia timu gani kule?

MJENGWA: Mimi ni mpenzi wa Wekundu wa Msimbazi kwa maana ya Simba tangu nikiwa na miaka sita. Lakini zaidi ni mpenzi wa michezo kwa ujumla. Naamini katika fair play. Ndio maana kuna wakati hata Simba wenzangu hawanielewi pale ninapoandika fikra zangu zenye kuwatetea watani zetu wa jadi.

Nakumbuka kuna wakati niliandika makala kuishutumu Simba kwa kumfungia Athuman Idd na kupelekea mchezaji huyo kushindwa kuchezea Yanga, timu aliyotaka kuchezea. Katika makala hiyo niliandika kuwa mimi ni mpenzi wa Simba lakini nilikuwa na fikra tofauti katika suala la Athuman Idd. Basi, siku hiyo nilipigiwa simu nyingi na baadhi ya wapenzi wa Simba wenye hasira. Kuna walionitukana pia, mmoja aliniambia; ” Acha upumbavu wewe, huwezi kuwa Simba bali ni kondoo unayejifanya simba!”

Hata juzi hapa niliandika kupitia blogu yangu kuwataka Simba wenzangu tuwapiganie watani zetu Yanga wafutiwe adhabu yao ya kufungiwa au kupunguzwa kwa adhabu hiyo. Na laiti makala ile ingechapwa gazetini, naamini kuna Simba ambao wangenipigia simu kunitukana. Nafuatilia pia kandanda ya England, huko naipenda sana Man United.

BC: Mbali na uandishi na pia pia blog,unajishughulisha na nini?

MJENGWA: Tangu mwaka 2004 nimekuwa mwajiriwa wa Shirika la Forum Syd lenye Makao yake Makuu Sweden. Mbali ya majukumu mengine nimekuwa nikifanya kazi ya kiushauri na hata kupanga na kuratibu semina za mafunzo kwa walimu wa Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania. Mkataba wangu umemalizika Julai mwaka huu. Hata hivyo, mwajiri wangu ameniongezea miezi mitano zaidi, namaliza Desemba mwaka huu. Baada ya hapo nitatafuta kibarua mahali kwingine, kama mambo yatakuwa magumu nina kijishamba changu Bagamoyo, nitakwenda huko kulima mananasi. Usisahau nina ujuzi kidogo wa kuvua samaki, nitaishi tu!

Mvuvi Maggid Mjengwa!

BC: Unapenda kujishughulisha na nini baada ya kazi zako?

MJENGWA: Napenda kusoma vitabu na kuandika. Napenda kujumuika na marafiki na kuongea. Napenda kupika vyakula. Napenda michezo. Hutokea nikachukua muda wangu kuangalia soka uwanjani au kwenye tv. Napenda kusikiliza muziki na kudansi pia. Nacheza pia mpira wa meza ( table tennis). Lakini juu ya yote mimi ni mtu wa kawaida tu ninayefanya mambo mengine ambayo wengine watasema ni ya kijinga. Ni binadamu ambaye kamwe siwezi kukamilika. Najifunza kila siku. Napokea shutuma na lawama kama sehemu ya kujifunza katika maisha.

BC: Shukrani sana Maggid.Nakutakia kila la kheri katika kazi zako.Endelea kuelimisha jamii.


Advertisements
 

16 Responses to “ANA KWA ANA NA “MWENYEKITI” MAGGID MJENGWA.”

 1. kitoto Says:

  Ahsante BC kwa kutuletea habari za tusiomjua sana kaka Maggid. Ukweli huyu bwana ni tofauti na kaleta upya fulani katika suala la habari na fasihi hii ya Blogu. Nani angejua kuna Iringa kama si Maggid? Iringa tuliyoizoe ni tu ile historia ya Mkwawa na vita vyake dhidi ya Wajerumani …karne iliyopita ya juzi….JUZI!!!
  Nani angejua habari za vijijini kama si mchango wake ndugu Mjengwa, mwanakalamu wa matope, ushamba, kilimo, ardhi, vumbi, majani, mito na vilima? Nafikiri wengi (nikiwemo miye mwenyewe) husahau kuwa watu wanaoilisha dunia yetu ni wakulima. Kwamba asilimia kubwa ya wananchi wa Bongo yetu ni watu wa vijijini. Kwamba miji ni ghala na vurugu mechi tu. Mchango wa uandishi wake ni muhimu sana…

 2. Bablee Says:

  Hongera kaka Mjengwa kwa maelezo mazuri, zaidi ya yote umenidhihirishia kwamba wewe ni mwanasiasa! Ni kawaida ya wana siasa kama wewe kutokujibu maswali wanayoulizwa, badala yake hutoa hadithi ndeefu, mpaka muulizaji husahau kauliza nini!

  BC kakuuliza, nanuku
  “…Leo hii ukiangalia nyuma,unadhani pamekuwepo mabadiliko gani ya msingi tokea miaka ile ulipoanza kuandika mpaka hivi leo? Hapa nazungumzia mabadiliko kwako wewe binafsi na kwenye uandishi kwa ujumla”

  Lakini wewe hukumpa jawabau sahihi badala yake umeanza kutoa hadithi ya ujio wa viongozi wa nje akina Fidel castro…!

  Jitahidini kutoa majibu kwa swali husika !

 3. Mumbala Says:

  Yote umeelezea yaani Mjengwa huna mke wala mtoto? Vibaya hivyo kumsahau mwenzio kiasi hicho, Kweli wanaume tu wabinafsi.

 4. Yanolyno Says:

  Yaaan kaka Majidi Dunia ni kama kule kijijini kwetu nilongea nawe siku ya pili mala uko bongo safi sana ongera kwa nyuzi bin nyuzi zako
  salam wote wana kijiji na wapenzi wa Gozi sport

 5. Edwin Ndaki Says:

  BC nimependa sana mahojiano uliyofanya na mwenyekiti.

  Hakika ni changamoto.Kikubwa nilichojifunza kutokana na mazungumzo hayo..Ukiwa na nia na malengo yote yanawezekana.

  Ila BC ulimuuliza Maggid mwanahabari gani aliyemvutia au kumvutia ,lakini kwa namna moja au nyingine Mwenyekiti hakujibu hilo swali na wewe ukasahau kuwa ulimuuliza hivyo mpaka tuna rudi ‘pugu rodi’ jibu lilikuwa halijatolewa..

  Ila pongezi hakika blog ya Maggid Mjengwa naweza ni moja ya blog ambayo inajitahidi sana kuinua sauti zetu tusio na majukwaa na pia kutuletea picha ya upande wa pili wa “bongo tambarare”

  Maana hata viongozi wengine hajui ugumu unaotukabiri sisi kima cha chini ndio maana wanatupuuza na kutubeza.

  kila la kheri Mwenyekiti..tupo pamoja.

  Tutafika tu.

 6. WTUGURU Says:

  HONGERA SANA KAKA MJENGWA, ILA UMENIKUMBUSHA MBALALI SANA NIMEPENDA SANA ULIVYOJIBU MASWALI, HAPO KWELI KICHWA KIPO, MIMI NINGEKUSHAURI UJARIBU KUGOMBEA UBUNGE MWAKA 2010 WEWE NDIE UNAWAFAA WANANCHI UNAJUA SHIDA ZAO NA UNAWEZA KUWA CHANGAMOTO KUBWA KATIKA SIASA.NI MTAZAMO WANGU TU KWA JINSI NIMEKUA NIKIFUATILIA BLOGU YAKO NA MATUKIO YAKE.

  NIMESEMA UMENIKUMBUSHA MBALI SANA KWA JUMA NA ROZA!!!! DAMAS NA LUCY, LUCY AKAWA ANALIA HAKUWA NA MWANA SESERE , ROSE AKAMUULIZA UNALIA NINI LUCY? LUCY AKAJIBU ANAMLILIA MWANASESERE, ROSE AKASEMA CHUKUA LUCY RAFIKI NI BORA ZAIDI KULIKO MWANASESERE, HAKIKA KILIKUA NI KITABU KIZURI SANA KILIVUTIA SANA KUKISOMA KWELI TULIKIPENDA, BAHATI MBAYA SIKU HIZI HAWASOMI TENA VITABU KAMA HIVYO.

  UJUMBE KWA BC MBONA UMESAHAU KUMUULIZA KAMA AMEOA AU ANAMCHUMBA AU ANISHI NA MTU KAMA PATNER? JE ANA MTOTO AU WATOTO? PLEASE!

 7. binti-mzuri Says:

  nice. kwakweli nilikua simfahamu,lakini nimefurahia mahojiano. goodluck in your future

 8. Mickey Jones Amos-Denmark Says:

  From the “street level” down the lanes of Kinondoni-Biafra to an amazing & extraodinary local news digger of all time……

  Your utmost photos in our village blog and the way you write is outstanding, no doubt you are a creator of the past & future !!

  Its high time now for challenges…write a book…for our new generation to follow your foot steps …

  mickey@mail-online.dk
  Copenhagen

 9. the ma-juuz Says:

  Kusema kweli bwana Maggid Mjengwa mimi naipa blog yako “tano”. Ninavutiwa sana na picha na habari mbali mbali ktk kijiji chako mzee wa Ikolo. Ninapoperuzi kwenye kijiji chako, huwa najisikia kama niko ndani ya “BONGO”. Hongera sana mzee! Endelea kuhawirisha maarifa kwa njia hii ya blog na magazeti.
  Kila la kheri ktk mipango yako ya maisha. Nikirudi BONGO naomba nitaomba unipeleke Ikolo na mimi nikatembee. Au vipi!?

 10. Matty Says:

  Hongera Kaka unatakiwa ugombee hata ubunge tutakuchagua kaka!ila kuoa bado upo upo kwanza nadhani!

 11. shafii Says:

  Huyu ni Legend wangu wa 2 katika fani ya habari hapa Tanzania baada ya Mike Mhagama.Tofauti yao Mike kaitoa mbali bongo flava wakati Maggid Kafanya tuweze kujua kinachoendelea nyumbani kwa kutumia picha bila kujisumbua kusoma maelezo yenyewe.

  By the way inawezekana majina yenu yamechangia mafanikio yenu… wote ni M-M, Maggid Mwendwa na Mike Mhagama.

  Keep it up brother!

 12. Ignorant Says:

  Maelezo mazuri kutoka kwa mwenyekiti. Hata hivyo nina mawazo tofauti kidogo kuhusu uwezo wake wa kutathmini mchezo wa Simba na Cosmos akiwa na umri wa miaka 6. Pengine mwenyekiti ni moja ya watu genius, lakini nasita kuamini kua aliweza kutambua timu gani imecheza vizuri akiwa na umri huo na kama sio kutambua timu gani imeshinda.

 13. Ignorant Says:

  Sorry wadau… ninamaanisha Cosmo na wala si Cosmos

 14. jingo Says:

  ondoa filter kwy blog yako…inazuia watu kukutembelea na kutoa maoni….tafuta njia nzuri zaidi ya kufilter maoni machafu na matusi………………….

 15. ibrahim Says:

  ama kwa hakika nimefurahi kwa jinsi ulivyofanya mahojiano na bongo celebrity, majibu pekee yanajengwa taswira ya wewe ulivyo na mimi ni mmoja wa mashabiki wako ambao kila kukicha nataka niige mfano wako kaka big up

 16. Mswahilina Says:

  Mambo yake ninayapenda. Lakini mshaurini awe anachana hizo nywele. Au aoe mke mwingine ili awe anamchana nywele.


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s