BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

“VIJANA WAJITOLEE,WAWE WAVUMILIVU NA WAAMINIFU”-NYIRENDA December, 9, 2008

Filed under: African Pride,Serikali/Uongozi,Sikukuu,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 12:44 AM

nyirendabcMiaka 47 iliyopita,katika tarehe inayofanana na leo,Tanganyika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni mwingereza.Nchi ilizizima kwa nderemo na vifijo huku kila mtu akiwa amejawa na matumaini yaliyotokana na kujikomboa kutoka katika mikono ya mkoloni.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndio alikuwa kiranja mkuu wa mchakato wa uhuru.Lakini kama tujuavyo,Nyerere hakuwa peke yake.Wapo mashujaa wengi waliochangia kupatikana kwa uhuru.Hatuna budi kuwaenzi viongozi na mashujaa hao daima.

Kwa upande mwingine wapo mashujaa ambao mbali na kuchangia katika harakati za kuutafuta uhuru, kwa njia moja ama nyingine,wao walikwenda hatua moja mbele na kuhakikisha kwamba uhuru unapatikana na alama mbalimbali za kuuthibitisha uhuru,kwa faida ya vizazi vilivyokuwepo wakati huo na vya mbeleni,zinasimikwa pia.

Miongoni mwa watu hao,hakuna ubishi kwamba jina la Major Alexander Gwebe Nyirenda, ni jina ambalo linakumbukwa na litaendelea kukumbukwa kutokana na mchango wake hususani wakati wa sherehe za uhuru.Nyirenda ndiye aliyeipandisha bendera ya uhuru kileleni katika Mlima Kilimanjaro na kuuwasha mwenge wa uhuru ili umulike mipaka yote ya Tanganyika.

Tulipata fursa ya kufanya mahojiano na Major Nyirenda ambaye bila kusita alikuwa mwepesi wa kutueleza historia ya maisha yake na zaidi juu ya utumishi wake jeshini na kumbukumbu yake kuhusiana na siku ile ambayo tunaidhimisha leo hii.Mahojiano yetu yalikuwa kama ifuatavyo;

BC: Major Nyirenda, kwa faida ya wasomaji wa mahojiano haya,unaweza kutuambia kwa kifupi historia ya maisha yako? Ulizaliwa lini,wapi,ukasomea wapi nk?

NYIRENDA: Mimi nilizaliwa tarehe 2 Februari 1936, Kasonga (Nyasaland) Malawi. Wazazi wangu,Mama na Baba,walitoka Malawi. Baba yangu alikuwa anafanya kazi katika Wizara ya Afya kama Mganga wa Afya (Medical Assistant). Tulizaliwa watoto wanne. Wanaume wawili na wanawake wawili. Mimi nilizaliwa mwisho-Kitinda Mimba.

Nilizaliwa Malawi kwa sababu Baba alipata likizo ya miezi mitatu toka kazini. Alipopata likizo hii kwenda Malawi, Mama alikuwa mjamzito wa miezi saba. Ndio maana mimi nikazaliwa Malawi. Lakini marehemu kaka yangu na marehemu dada zangu wote walizaliwa Tanganyika.

Nilianza kusoma shule darasa la kwanza shule ya Mchikichini,Dar-es-salaam. Niliendelea na elimu ya msingi Iringa katika shule ya msingi Mlandege na baadaye nikaendelea na masomo ya sekondari Malangali Secondary School huko Iringa. Kutoka Malangali Secondary School niliendelea kusoma darasa la kumi na moja na kumi na mbili mkoani Tabora katika shule ya Wavulana Tabora(Boys) Secondary School na kupata Cambridge School Certificate mwaka 1957.

Kabla ya kufanya mtihani wa darasa la kumi na mbili (12) walikuja pale Tabora School maofisa wa kijeshi( wazungu) wakiwa katika harakati ya kutafuta watu ili waingie katika jeshi la wakati huo yaani Kings African Rifles(KAR) kama maofisa kwani wakati huo hakukuwa na ofisa Mtanzania katika jeshi la KAR.

BC: Unakumbuka nini hasa kuhusu maisha yako ya utotoni? Ulikuwa na ndoto au nia moja kwa moja ya kuwa mwanajeshi siku za mbeleni? Kama jibu ni hapana, ulikuwa unataka kuwa nani?

NYIRENDA: Nikiwa bado mtoto mdogo sikuwa na ujuzi wowote uliohusiana na majeshi. Ingawa baba yangu mdogo (Kelvin Gwebe Nyirenda) alipigana vita ya ulimwengu ya pili (1939-1945) Burma, mimi sikuichukulia hii kama ni kitu cha maana.Matarajio yangu ilikuwa ni kuwa daktari kuzidi alivyokuwa baba yangu.

Maisha yamejaa mabadiliko.Baada ya kuwasiliana na maofisa wa jeshi waliotutembelea shuleni na mimi binafsi kuzungumza na Mwalimu wetu mkuu(Headmaster),Mr.Crabbe, niliingiwa na kishawishi cha kuingia jeshini.Nikajiandikisha.

BC: Unatoka kwenye familia ya watoto wangapi? Au kwa maana nyingine unao dada na kaka wangapi?

NYIRENDA: Tulizaliwa watoto wanne.Kaka alikuwa wa kwanza (Robert Gwebe Nyirenda),Dada wawili (Myra na Katirina Gwebe Nyirenda) na mimi wa mwisho.

BC: Ulijiunga lini rasmi na Jeshi la Wananchi la Tanzania? Nini kilikusukuma au kilichangia uamuzi wako wa kujiunga na jeshi?

NYIRENDA: Nilijiunga na jeshi mwaka 1960 mara tu baada ya kuhitimu mafunzo ya Royal Military Academy Sandhurst. Kama nilivyojibu hapo juu-Niliingiwa na kishawishi baada ya Headmaster wetu Mr.Crabbe kuniongoza

BC: Je kuna mtu yeyote jeshini ambaye ulikuwa unamuona kama role model wako?Kwanini?

NYIRENDA: Hapana sikuwahi kupata hatima kama hiyo kwani mimi ndie niliyekuwa wa kwanza ofisa mtanzania.Niliwakuta wazee watanzania wenye hekima lakini hawakuwa maofisa.

BC: Hivi sasa unajishughulisha na nini baada ya kustaafu kutoka jeshini?

NYIRENDA: Hivi sasa nikiwa mtu mstaafu,mzee,najishughulisha na kazi za kibinafsi nikisaidiwa na watoto wangu wawili wa kiume.

BC: Tukio moja kubwa sana ambalo daima utakumbukwa kwalo ni lile la kuipandisha bendera ya Tanganyika (sasa Tanzania) katika mlima Kilimanjaro mnamo tarehe 9 December 1961. Sasa,hivi leo unapoikumbuka siku ile, unajisikiaje? Ulikuwa na cheo gani jeshini wakati huo?

NYIRENDA: Tukio hilo ni kwa manufaa ya wananchi watanzania.Motto ya Sandhurst Military Academy ilikuwa ni “SERVE TO LEAD”. Na hii inamaanisha kwamba kiongozi mwema ni mfanyakazi (mtendaji) mwema. “A good leader is a good servant”. Na haya yote ndiyo yale Hayati Mwalimu Nyerere aliyazungumza kufuatana na kitendo cha kuweka tochi juu ya Mlima Kilimanjaro.Najisikia faraja kila mara ninapokumbuka tukio lile.

BC: Unaweza kutuambia ni watu wangapi mlipanda mlima Kilimanjaro siku ile? Unaweza kututajia majina ya wenzako mliopanda nao?

NYIRENDA: Tulikuwa kama watu kumi na moja wakiwemo wapiga picha na watangazaji wa radio.Kwa bahati mbaya hivi sasa sina majina kwani mimi sikuchukua orodha kamili (makosa yangu) ya watu tuliokuwa pamoja siku ile.

BC: Iliwachukua siku ngapi kukifikia kilele cha mlima Kilimanjaro ambacho hivi leo kinajulikana kama Uhuru Peak?

NYIRENDA: Kutoka Dar-es-salaam kwenda Kilimanjaro kutimiza shughuli ya Mwenge mpaka kurudi Dar-es-salaam tulichukua siku kumi na sita. Hii ni kwa sababu ya mazoezi ya kupanda mlima na maandalizi mengine.Siku ya mwisho tulitoka chini ya mlima kama saa kumi na mbili jioni na tulifika kileleni saa tano ya usiku na kuanza kujitayarisha kuweka Mwenge huku tukishirikiana na Dar-es-salaam kwa njia ya radio.

Tuliwasha mwenge Mlimani dakika ile ile ambayo wenzetu wa Dar-es-salaam walipopandisha bendera yetu ya uhuru wa Tanganyika.

BC: Nani alikua mpiga picha wenu? Au kwa maana nyingine nani alipiga picha ile maarufu ya kumbukumbu?

NYIRENDA: Kulikuwa na wapiga picha kadhaa kutoka serikalini.Kwa bahati sikumbuki majina yao na kwa uhakika kabisa kwamba ni yupi alipiga ile picha.Sasa umenipa harakati ya kuwatafuta au kupata majina yao kamili.

BC: Mlifanya maandalizi gani rasmi kabla ya kwanza kuelekea Moshi na kisha kupanda mlima Kilimanjaro?

NYIRENDA: Hatukuwa na maandalizi rasmi sana zaidi ya maandalizi ya kawaida ya kijeshi.Tulipata misaada mbalimbali tukiwa katika safari ya kwenda kuuweka mwenge kileleni.

nyirenda-4

Ni wakati wa furaha.Tanganyika iko huru.

BC: Baada ya kurejea jijini Dar-es-salaam (natumaini mlirejea Dar-es-salaam kwa sababu ndipo yalipokuwa makao makuu ya nchi wakati huo) mlikutana na Mwalimu Nyerere au kiongozi yeyote wa kitaifa? Ilikuwaje?

NYIRENDA: Ni kweli.Baada ya kukamilisha shughuli ile huku nchi ikiwa bado inasheherekea uhuru, tulirejea Dar-es-salaam. Tulipokelewa vizuri sana na ndio tulikutana na Mwalimu Nyerere na mume wa Malikia wa Uingereza (Duke of Edinburgh) ambaye alikuwa amekuja nchini mahsusi kwa ajili ya sherehe hizo za uhuru.

BC: Ni jambo gani unalolikumbuka zaidi kuhusiana na uongozi wa Hayati baba wa Taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere?

NYIRENDA: Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa mtu ambaye alijitolea kuwa mtumishi wa dhati. Alitufundisha sisi kuwa “sisi” na sio “mimi”.Alitufundisha umoja-tuwe pamoja bila kutengana.

BC: Unaweza kuyaongelea namna gani matumaini mliyokuwa nayo tarehe ile ya 9 December 1961 ukilinganisha na matumaini waliyonayo vijana wa kitanzania hivi leo?

NYIRENDA: Vijana wa leo walizaliwa na kukua katika Tanzania huru.Kwa hiyo mawazo na matarajio yao ni yale ambayo serikali ya uhuru iliahidi kutekeleza. Ni vigumu kukumbuka na sidhani kama mimi nilikuwa na matumaini dhati wakati wa uhuru kwani uhuru ulikuja kama mgeni nisiyemtarajia.

nyirenda-5

BC: Unatoa ushauri gani kwa vijana hivi leo kuhusu suala zima la kuchangia maendeleo ya nchi yao?(Tanzania)

NYIRENDA: Vijana wawe watendaji, wajitolee na wawe wavumilivu na waaminifu.

BC: Asante sana kwa muda wako.

NYIRENDA: Asante na wewe Jeff kwa kunikumbuka.

BC inawatakieni nyote sherehe njema za uhuru.Tukumbuke Uhuru unakwenda sambamba na uwajibikaji.Pia tunaomba radhi kwa kutokuwa na picha za Nyirenda za hivi karibuni au alivyo hivi sasa.Hiyo ni kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu.Zikipatikana tutaziweka.Asanteni

Kwa msaada zaidi wa historia ya taifa letu,bonyeza hapa.


Advertisements
 

20 Responses to ““VIJANA WAJITOLEE,WAWE WAVUMILIVU NA WAAMINIFU”-NYIRENDA”

 1. BLACKMANNEN Says:

  Hongera sana Watanzania wenzangu, kwa kutimiza miaka 47 ya Uhuru wa Tanganyika. Uhuru ni kitu muhimu sana kwa binadamu yeyote duniani. Uhuru huo ndiyo unaotufanya tuweze kutoa maoni yetu hapa.

  Mtu pekee ambaye ndiye aliyetuletea “UHURU” huu ni Baba Wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere (R.I.P.). Kama mtakumbuka Mwalimu Nyerere, miaka ya kuutafuta Uhuru huu, aliamua kuacha kazi yake ya Ualimu ili aendeleze Mapambano ya kuutafuta Uhuru huu.

  Watanzania wenzangu, katika kumwenzi Mwalimu Nyerere, ni jukumu letu wote, wake kwa waume, kuulinda na kuuboresha Uhuru huu, kwa kushirikiana katika ujenzi wa nchi ya Tanzania, bila kujali utofauti wa itikadi zetu kisiasa na ukabila.

  Tuulinde Mwungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Tusikubali kugawanywa na watu wenye nia mbaya na nchi yetu ya Tanzania.

  Mengi nawaachia wenzangu nao wachangie. Majita, Gervas, binti-mzuri, Pearl, Mattylda, Frateline, halima, any,Mama wa kichagga na wengine – mpooooooooo????????????

  It’s Great To Be Black=Blackmannen

 2. Mattylda Says:

  Asante BC, mahojiano mazuri nimempenda huyu baba anaonekana mstarabu fulani hv!
  Ila ukipata picha zake za sasa pls tumuvuzishie hapa tumuone alivyo, nahisi kama kashazeeka kiaina!
  All the best Nyirenda, uishi maisha mengi!

 3. Lalola Says:

  Mungu ibariki Tanzania na watu wake. Mungu ibariki Afrika. Thiiiiii utadhani naimba wimbo wa taifa vile, tehe tehe tehe.

  Watanzania tudumishe uhuru wetu na tumuombe Mwenyezi Mungu atuepushe na balaa lolote la dunia.

 4. Dinah Says:

  Nimefurahi kusoma mahojiano ya mzee huyu muhimu sana kwenye historia ya taifa letu.

  Kujitolea ni ngumu wakati tumboni hakuna kitu. Hilo moja.
  Uwaminifu nayo ngumu kwa vile rushwa imeota mizizi yaani iko kwenye sytem….pili.

  Tumevumilia wee na leo ni mwaka wa 47 hatujaona,Hivi sasa tungekuwa na angalau 4 ways barabara, kila kijiji kungekuwa na umeme, watu wote wangemudu kwenda shule, kazi zingekuwa nyingi na za kuchagua kama Serikali ingetujali na ku-creat jobs na pia kuzifanya kazi hizo kuwa valued in terms of malipo n.k

  Mimi nimejichokea honestly……tatu. 🙂

 5. hilly Says:

  Huwa sisomagi mahojiano marefu kama haya,Ila leo nimeguswa na historia ya nyirenda maana napata picha halisi ya Tanganyika enzi hizo.Big up Man!!

 6. hombiz Says:

  Asante mzee A.G. Nyirenda kwa mchango wako wa hali na mali ktk uhuru wa Tanganyika. Natumaini maradhi ya koo yaliyokuwa yakikusumbua kwa muda mrefu, yalishaponywa huko India ulipokwenda kwa matibabu. Nakuombea afya njema. Happy Uhuru Day and many many many more to come 4 U

  Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwakumbuka wazalendo wengi waliosaidiana na Hayati Mwalimu Nyerere ktk kupigania na hatimaye kuikomboa Tanganyika dhidi ya utawala wa ukoloni wa waingereza. Hayati mwalimu Nyerere asingeweza hata kidogo kuifanya kazi hiyo yeye peke yake. Kwa kuwa wazalendo waliotoa mchango ni wengi saaaana, wacha leo niwataje hawa wachache wafuatao:

  -Mzalendo Abduwahid Sykes(Mwalimu alichukua uongozi wa TAA baada ya kumshinda Mzee Sykes,(mtoto wa mjini wa wakati huo) kwa kura chache sana, kwenye uchaguzi).
  -Pia tukumbuke kuwa mzee Dossa Aziz, (Mwenye kadi # 4 ya TANU)alimsaidia sana mwalimu Nyerere na TANU kifedha katika kutafuta uhuru wa Tanganyika. Zaidi ya hapo, mzee Dossa alikipa chama cha TANU gari yake ya kwanza kabisa aina ya Land Rover. Gari lile ndilo lililotumika kumzungusha mwalimu Nyerere nchi nzima wakati wa kuitangaza TANU kwa wananchi.
  -Pia, Erika Fiah na Ramadhani Mashado(ni wazalendo wa mwanzo kufungua magazeti ambayo yalikuwa sauti ya waafrika. Fiah alikuwa mmoja wa wanasiasa wa mwanzo kabisa wa mrengo wa kushoto na uandishi wake katika gazeti lake Kwetu alilolianzisha yeye mwaka 1937, ulipambana vikali kimaandishi dhidi ya ukoloni.
  Tukumbuke kuwa gazeti la kwanza kumpa Mwalimu sauti na kueneza sera za TANU lilikuwa Zuhra mhariri akiwa Plantan Makala za Fiah katika gazeti lake la Kwetu ingawa zimeandikwa zaidi ya nusu karne sasa bado zina msisimko kwa msomaji kama vile kaziandika jana.
  -Mzee Yusuph Olotu a.k.a Yusufu Ngozi toka Moshi alifanya jitihada kubwa sana kukipa chama cha TANU ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa kura 3 huko Moshi. Vile vile kuna kina wazee: Dr. Michael Lugazia, Dr. Joseph Mutahangarwa, Dr. Vedasto Kyaruzi, Mzee Paul Bomani, Mzee Lupia, Mzee Mwapachu,Mzee R.M. Kawawa, Ali Ponda, Hassan Suleiman, Ramadhani Singo, Dosa Aziz, Bibi Titi , na wengine wengi.

  Uongozi wa BC, ombi langu kwenu ni kutuletea wazalendo wengine, “mbali na Hayati mwalimu Nyerere”, ili nao tuwajue na kuchangia mambo mazuri waliyoyafanya ktk historia ya kupigania uhuru wa -the then Tanganyika.

  MWENYEZI MUNGU NAOMBA UWAREHEMU WAZALENDO WALIOTUTANGULIA WAPUMZIKE KWA AMANI. NA WALE WALE AMBAO WAKO HAI, WAJALIE AFYA NJEMA.
  PEACE!

 7. hombiz Says:

  You are welcome-Bongocelebrity (comment # 7)!
  Asante kushukuru

 8. shoogap Says:

  Nimefurahi sana kusoma mahojiano na Nyirenda, nimejifunza mambo mengi sana.

  Ni vyema watu wote waliochangia historia waenziwe na kuheshimiwa.

  Historia kama hizi ziandikwe na kurithishwa kwa kizazi cha sasa. mfano katika vitabu vya sshule kuwepo na hadithi za kuelezea harakati za uhuru na matukio mengine ya kihistoria kuhusu nchi yetu.

  TUFIKIRIE KWA UPYA JINSI GANI UHURU HUO UMETUSAIDIA NA KUNA MAPUNGUFU WAPI. TUELEKEZE NGUVU ZETU KATIKA UKOMBOZI WA KIUCHUMI SASA NA SIO HUU WA KISIASA TU, INGAWA NAO NI MUHIMU.

 9. anony Says:

  basi mtuwekee picha ya huyu mzee nyarenda ya sasa hivi tuone alivyobadilika. God bless wabongo

 10. BLACKMANNEN Says:

  Kwako Hombiz,

  Kwa kile ulichoandika hapa, nakuunga mkono na kukupongeza 100%. Maoni +ve, juu ya nchi yetu Tanzania, ndiyo ninayokuwa nikiwaomba tujikite kuyaandika. Sio kusifia vya wenzetu katika nchi tulizolowea.

  Mabaya ya Tanzania, pia ni muhimu kuyaandika. Hii ni katika kuonyesha “rangi nyeusi na nyeupe”, katika kuchambua hali ya kisiasa na maendeleo ya Tanzania katika safari yetu ndefu, na ngumu ya kulisukuma “Gurudumu letu la Maendeleo” Tanzania.

  Lakini pia ieleweke kuwa, kila tunachokiandika hapa, kinasomwa na watu wa aina nyingi. Watu wa Mataifa mengine, wanasoma, wakitaka kutuelewa sisi ni nani, tunaokaa nao katika nchi zao. Au watu wa nchi zingine tunaoishi nao katika nchi hizo za kigeni, wanataka kutujua zaidi.

  Watu muhimu kuliko wote wanaofuatilia habari za Tanzania, na wana hamu kujielewa wao ni nani, ni watoto wa Watanzania wanaoishi nchi za nje. Watoto hawa, ili waweze kuwa na maendeleo ya kiakili na kimaisha, kisaikolojia, ni muhimu wajielewe wao ni nani, kama Watanzania. Nafasi ya kwenda Tanzania, kujionea wenyewe nchi yao, ni ndogo sana, kutoka na hali halisi ya kiuchumi kwa Wazazi wao.

  Kutokana na hali ya namna hiyo, ni jukumu letu Watanzania, watu wazima, kuwaelimisha vijana wetu, mambo mazuri na pia mabaya, yanayotokea Tanzania. Historia uliyoitoa hapa Hombiz, kwa kweli umenifurahisha sana, na ina manufaa kwa watu wote ambao walikuwa hawaijui historia ya Uhuru wetu na mashujaa wetu wa kututafutia Uhuru huu zaidi ya miaka 47 iliyopita. Hii ikiwa ni pamoja na vijana wetu wote, ndani na nje ya Tanzania.

  Vijana wetu wanaoishi na kukulia nchi za nje. Tunawatisha sana tunapoiongelea vibaya nchi yetu Tanzania. Wanakuwa na picha mbaya zaidi kuliko tunavyoizungumza sisi. Hakuna mtu mwingine atakayewaelimisha kuhusu mambo mengi tunayoyaandika hapa, wanabaki na picha mbaya kuliko nzuri kuhusu Tanzania. Wanabaki na maswali yasiyokuwa na majibu wakati wote.

  Hombiz, “dawa” niliyokuwa naitengeneza jikoni kwa ajili yako, sasa nitamnywesha ndugu yangu “Majita”, sijui ni kwanini. Lakini, na wewe nakushauri, “dozi” uliyokuwa umeitayarisha kuintasepti kombora langu, mpe “Frateline”- mwanahistoria. Ili naye atuletee historia kama hiyo uliyotuletea wewe hapa, sio yeye, anatuletea bla bla za CCM.

  Yeah!……It’s Always Great To Be Black………..Blackmannen

 11. binti-mzuri Says:

  ha ha ha..hii dawa ya migombaaaaaaaa aauu lol

 12. Paul Says:

  Kweli hii blog babu kubwaa. nimepata kusoma huyu shujaa ambaye nilikuwa nafikili atunaye tena. Asante kwa ujumbe Bwana Nyirenda, kwani tukizingatia hayo tutakuwa na mafanikio. Paul- London

 13. WABIKE Says:

  Vijana tuzingatie ujumbe. Wabike Iaty

 14. Asante kwa mahojiano mazuri!

 15. hombiz Says:

  Blackmannen,
  Asante kwa kuniunga mkono na kunipongeza 100% juu ya maoni yangu +ve juu ya nchi yetu Tanzania-ktk mada ya KUWAKUMBUKA WAZALENDO WALIOPIGANIA UHURU WA TANZANIA.
  Pia umegusia swala la kuandika mazuri na mabaya yanayojili nchini Tanzania ili kujua “rangi nyeusi na nyeupe” ktk kuchambua hali ya siasa na maendeleo ya Tanzania ktk safari yetu ndefu, na ngumu ya kulisukuma “Gurudumu letu la Maendeleo” Tanzania . Hapo nakubaliana na wewe 100% pia. Na naamini hiyo ndiyo imekuwa dhamira yangu siku zote.
  Hata hivyo, umesema haupendezwi na kusifia vya wenzetu ktk nchi tulizolowea. Kwenye hoja hii, mimi naona siwezi kukubaliana na wewe. Mimi napenda kutoa hoja zangu kimataifa zaidi. Kwa maana hiyo, napenda kuzungumzia mazuri na mabaya ya nyumbani Tanzania , na kwingineko duniani. Na nnavyofanya hivyo, najitahidi kuwa wazi bila kuficha fikra na mtazamo wangu, kulingana na uelewa wangu, juu ya swala husika. Pia, kila ninapokutana na watu wa mataifa mbalimbali, hu-share mambo mbali mbali yakiwemo ya kiuchumi, kitamaduni na kijamii kwa kuwa mkweli na muwazi juu ya jambo ninaloamini kulifahamu kiufasaha. I believe this is one of the best ways to learn from each other.
  Kwa watoto watanzania wanaoishi nchi za nje, mimi nadhani tuwafundishe juu ya nchi yao Tanzania kwa kuwaambia ukweli juu ya mabaya na mazuri bila kuficha. Na hii sio kwa watoto wa Tanzania peke yao bali hata watoto wa nchi nyingine duniani. Kwa mfano, ni muhimu sana kuwafundisha watoto kuwa kusema uongo, kutapeli na kuiba ni mambo mabaya sana yasiyokubalika ktk jamii . Hivyo basi hawapaswi kuyafanya hata kidogo maishani mwao. Wakati huo huo ni vema tufahamu, hatuwezi kuwaambia watoto wetu kuwa kufanya mambo hayo ni vibaya wakati sisi wenyewe tunayafanya kila siku. Tukumbuke kuwa watoto huiga zaidi yale ambayo wanaona wazazi wao wanayatenda kila siku na kuliko wasemayo. Samaki mkunje angali mbichi. Kama wazazi wanatabia ya kugombana kila siku, uwezekano ni mkubwa wa watoto wao kuwa na tabia mbaya mbele ya jamii. Hivyo basi mimi naamini kuwa watoto wakiona sisi wazazi, walezi (wakubwa) tunakemea maovu kama UFISADI kwa vitendo, nao watajua wazi kuwa hii ni tabia mbovu na haifai kuigwa hata kidogo na wataiogopa kama umeme wa radi. Na tunaposifia mambo mema, naamini itawapa watoto changamoto ya kujitahidi kutenda matendo mema ili jamii iwakubali kwa mazuri yao na kuwazawadia pale inapostahili na kubidi . Ni vema pia tukawahamasisha watoto kujisomea zaidi na kuwa watundu wa kutafuta maarifa ktk maktaba, internet, TV, Radio n.k. Hii itawafanya kujua kuwa unaposoma zaidi maarifa nayo yanaongezeka. Pia itawasaidia watoto kuwa wadadisi wa mambo mbali mbali yanayowazunguka ktk maisha yao ya kila siku. Let’s live through examples!

  Kwa wadau mbali mbali wanaoingia ktk wanja la BC, “kama ulivyobainisha Blackmannen”, wanakalibishwa kujionea mengi kujifunza, kuchangia, kurekebisha, kuelimisha, kukosoa hoja mbali mbali ktk kujenga sio Tanzania pekee, bali dunia nzima ambayo kwa sasa ni kama kijiji.
  Long live BC with all it`s Blog memberz
  That’s what’s up!

 16. TIANDRA Says:

  IAM PROUD OF YOU UNCLE . KEEP ON FIGHTING I HOPE YOUR OK

 17. Azania Bitoz Says:

  Hombiz,
  Thanks for acknowledging the other heroes of our struggle of indepence , which our new generation, sadly I might ,is totally unaware off. I am proud to say that as a five year old, I remember my dad hoisting me up on his shoulders in the stands of the newly built Old National Stadium, to watch the flag of Tanganyika being raised up while the Union Jack was being lowered.
  I also had the pleasure of attending school with one of Major Nirendas daughter ( Sambawayo) , She was a year ahead of me at St Josephs Convent as it was known back then and such my deepest condolences to the family

  Azania Bitoz

 18. hombiz Says:

  You are welcome, Azania Bitoz!
  Peace and Love!

 19. Chabwela Nyirenda Says:

  Asante sana BC kwa kutuletea mahojiano haya ya mzee wetu Nyirenda. Pia asante sana wachangia wote hasa Hombiz kwa kutuletea majina ya watu muhimu katika historia yetu.

  Mdau Azania Bitoz, Sambayawo uliyosoma naye pale St Josephs Convent hakuwa mtoto wa Major Nyirenda bali alikuwa mtoto wa kaka yake na Major Nyirenda aliyeitwa Robert Gwebe Nyirenda. Robert Gwebe Nyirenda ni mmoja wa watanzania wa mwanzo kabisa kuunda Tobacco Board na baadaye kuanzisha kiwanda cha Sigara. Nyirenda mkubwa naye Amefariki mwaka jana (2007) huko Afrika kusini kwa ugonjwa wa cancer na kuzikwa nchini Malawi. Sambayawo sasa ni doctor aliye specialize kwa magonjwa ya TB in one of the leading hospitals in Botswana.

  R.I.P


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s