Miaka 47 iliyopita,katika tarehe inayofanana na leo,Tanganyika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni mwingereza.Nchi ilizizima kwa nderemo na vifijo huku kila mtu akiwa amejawa na matumaini yaliyotokana na kujikomboa kutoka katika mikono ya mkoloni.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndio alikuwa kiranja mkuu wa mchakato wa uhuru.Lakini kama tujuavyo,Nyerere hakuwa peke yake.Wapo mashujaa wengi waliochangia kupatikana kwa uhuru.Hatuna budi kuwaenzi viongozi na mashujaa hao daima.
Kwa upande mwingine wapo mashujaa ambao mbali na kuchangia katika harakati za kuutafuta uhuru, kwa njia moja ama nyingine,wao walikwenda hatua moja mbele na kuhakikisha kwamba uhuru unapatikana na alama mbalimbali za kuuthibitisha uhuru,kwa faida ya vizazi vilivyokuwepo wakati huo na vya mbeleni,zinasimikwa pia.
Miongoni mwa watu hao,hakuna ubishi kwamba jina la Major Alexander Gwebe Nyirenda, ni jina ambalo linakumbukwa na litaendelea kukumbukwa kutokana na mchango wake hususani wakati wa sherehe za uhuru.Nyirenda ndiye aliyeipandisha bendera ya uhuru kileleni katika Mlima Kilimanjaro na kuuwasha mwenge wa uhuru ili umulike mipaka yote ya Tanganyika.
Tulipata fursa ya kufanya mahojiano na Major Nyirenda ambaye bila kusita alikuwa mwepesi wa kutueleza historia ya maisha yake na zaidi juu ya utumishi wake jeshini na kumbukumbu yake kuhusiana na siku ile ambayo tunaidhimisha leo hii.Mahojiano yetu yalikuwa kama ifuatavyo;
BC: Major Nyirenda, kwa faida ya wasomaji wa mahojiano haya,unaweza kutuambia kwa kifupi historia ya maisha yako? Ulizaliwa lini,wapi,ukasomea wapi nk?
NYIRENDA: Mimi nilizaliwa tarehe 2 Februari 1936, Kasonga (Nyasaland) Malawi. Wazazi wangu,Mama na Baba,walitoka Malawi. Baba yangu alikuwa anafanya kazi katika Wizara ya Afya kama Mganga wa Afya (Medical Assistant). Tulizaliwa watoto wanne. Wanaume wawili na wanawake wawili. Mimi nilizaliwa mwisho-Kitinda Mimba.
Nilizaliwa Malawi kwa sababu Baba alipata likizo ya miezi mitatu toka kazini. Alipopata likizo hii kwenda Malawi, Mama alikuwa mjamzito wa miezi saba. Ndio maana mimi nikazaliwa Malawi. Lakini marehemu kaka yangu na marehemu dada zangu wote walizaliwa Tanganyika.
Nilianza kusoma shule darasa la kwanza shule ya Mchikichini,Dar-es-salaam. Niliendelea na elimu ya msingi Iringa katika shule ya msingi Mlandege na baadaye nikaendelea na masomo ya sekondari Malangali Secondary School huko Iringa. Kutoka Malangali Secondary School niliendelea kusoma darasa la kumi na moja na kumi na mbili mkoani Tabora katika shule ya Wavulana Tabora(Boys) Secondary School na kupata Cambridge School Certificate mwaka 1957.
Kabla ya kufanya mtihani wa darasa la kumi na mbili (12) walikuja pale Tabora School maofisa wa kijeshi( wazungu) wakiwa katika harakati ya kutafuta watu ili waingie katika jeshi la wakati huo yaani Kings African Rifles(KAR) kama maofisa kwani wakati huo hakukuwa na ofisa Mtanzania katika jeshi la KAR. (more…)
Recent Comments