BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

UNAMKUMBUKA LAWRENCE MWALUSAKO? July, 27, 2007

Filed under: Kabumbu/Soka,Michezo,Soka,Wachezaji — bongocelebrity @ 11:55 AM

Kwa mpenda soka ya Tanzania yeyote yule, hususani mnamo miaka ya themanini,jina Lawrence Mwalusako sio geni hata kidogo. Alikuwa sio tu kipenzi cha wapenda soka bali beki wa kutumainiwa wa timu zote alizowahi kuchezea, zikiwemo Waziri Mkuu Dodoma, Pan African, Yanga na timu ya taifa,Taifa Stars. Ndio maana yanapotajwa majina ya wachezaji soka nchini Tanzania waliowahi kuwika na jina la Mwalusako likakosekana,wadau wa soka,wanaoijua vyema historia ya soka la Tanzania,watakuambia wazi,something is missing.

 

Lawrence Mwalusako ni wa sita kutoka kushoto waliosimama.

Waliosimama kutoka kushoto: Marehemu Daktari wa timu Peter Manyika,Meneja John Manongi,Abeid Mziba “Tekero”,Athumani China,Yusuf Ismail Bana,Lawrence Mwalusako,Said Mrisho,Edgar Fongo,Isihaka Hasan,Golikipa Joseph Fungo,Kocha Mwinda Ramadhan.

Waliochuchumaa kutoka kushoto: Marehemu Lucias Mwanga,Rashid Idd Chama,Moshi Majungu,Allan Shomari,Ali Mchumila,Freddy Ferix Minziro,Abubakar Salum “Sure Boy”

Picha hii ilipigwa Mwaka 1987 uwanja wa taifa wakati wa mechi ya premier kati ya Yanga na Maji Maji.

Safari ya Mwalusako katika medani ya soka inaanzia kule Kyela mkoani Mbeya alipozaliwa mnamo mwaka 1960.Tulipofanya naye mahojiano hivi karibuni,Mwalusako ameongelea mambo mengi yakiwemo mtazamo wake wa soka la bongo hivi sasa,washambuliaji aliokuwa anawaheshimu,ushauri kwa wanasoka chipukizi nk.Pia anagusia jinsi “juju” ilivyo katika timu kubwa na pengine hata zile ndogo. Fuatana nasi katika mahojiano haya ambayo hata yeye mwenyewe anakiri,hajawahi kufanya na chombo chochote cha habari duniani akiwa kama mchezaji na hata baada ya kustaafu. Hivi sasa yeye ni Corporate Affairs Manager wa kampuni ya Sumaia Group Tanzania.Anaishi Dar-es-salaam.

BC: Unaweza kukumbuka wakati ulipokuwa mdogo ni nani alikuvutia katika mchezo wa soka? Kulikuwa na mtu yeyote maalumu ambaye ulimuona kama role model wako katika soka?

LM: Mimi nimekuwa mpenzi wa timu ya Yanga tangu mdogo. Hivyo basi nilikuwa navutiwa sana na wachezaji wote wa Yanga hasa Maulid Dilunga na Sunday Manara. Kwa upande wa timu ya Simba, nilikuwa navutiwa sana na uchezaji wa Haidari Abeid na marehemu Willy Mwaijibe. Willy Mwaijibe alikuwa ni home boy wangu na akija likizo nyumbani nilikuwa nabahatika kuwa naye kwani tulikuwa tunatoka kitongoji kimoja. Willy alikuwa ni role model kwangu kwani alikuwa anatoa demonstration ya uchezaji mpira katika kiwango cha kimataifa. Alinifanya niupende mpira sana kwa sababu wakati huo yeye alikuwa anasoma secondary school huku akichezea Simba Sports club. Ila hakuweza kunishawishi nibadilike kuwa mpenzi wa timu ya Simba.

BC: Je wazazi wako waliyachukulia vipi mapenzi yako ya kucheza soka?

LM: Wazazi wangu walipenda sana niwe na soma hasa mama yangu.Alikuwa ananikataza kucheza mpira wakati niko shule ya msingi. Hata hivyo kwa sababu alijua kuwa nafanya vizuri shuleni aliniruhusu kucheza chandimu baada ya masomo hapo kijijini kwetu. Sikuweza kuchezea timu ya shule ya wakati nasoma primary school kwa sababu nilikuwa mdogo sana pamoja na kwamba wengi walitabiria kuwa nitakuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu nikikua.

BC: Mbali na soka uliwahi kucheza aina zingine za michezo? Kama ndio ikawaje basi ubobee zaidi kwenye soka?

LM : Soka ni mchezo unaopendwa sana hapa duniani. Hata vijijini utaona vijana wengi wanajishughulisha na mchezo wa mpira wa miguu kuliko michezo mingine yoyote. Katika ujana wangu nilibahatika kuupenda mpira kwa sababu kaka zangu wengi wa kijijini walikuwa wanacheza mpira katika kiwango kikubwa sana. Kuna baadhi ya wachezaji wengine wa kijijini walifanikiwa kuchezea timu kubwa kama vile Marehemu Yusufu Ambewne (CDA) na Marehemu Awidson Mwafongo (Maji Maji) ukiachia mbali mrehemu Willy Mwaijibe. Mpira wa miguu huwakutanisha watu pamoja na hujenga mahusiano mazuri miongoni mwa wachezaji.

 

Lawrence Mwalusako alivyo hivi sasa.

BC : Mchezo wa soka katika bara la Afrika ikiwemo Tanzania huwa imetawaliwa sana na imani za kishirikina.Unaweza kutuambia kidogo ni kwanini na ilikuwaje enzi zako ulipokuwa unachezea vilabu vikubwa kama Pan Afrika na Yanga?Kuna tukio lolote la “juju” unalolikumbuka?

LM : Katika nchi nyingi zinazoendea hapa duniani utaona kuwa watu wake wanatawaliwa na imani za kishirikina tangu enzi na enzi. Sio tu kwenye maswala ya michezo, ni katika masuala yote ya kijamii. Hizo imani zimejengeka ndani ya mioyo ya kila jamii. Hata kwenye michezo, watu wamejenga imani za kishirikina. Timu nyingi za Tanzania huwa zinaamini kuwa pamoja na kuwa na wachezaji wazuri, ushindi wa timu hauwezi kupatikana bila juju kuwepo.Pan Africa na Yanga ni timu ambazo nimezichezea na ni timu ambazo zina imani na juju kuwa ni mojawapo ya nguzo ya ushindi. Kwa sababu mchezaji ni mwajiriwa katika timu hizo analazimika kufuata kanuni na taratibu za uendeshaji mpira kwenye klabu. Hata hivyo kitu cha msingi katika kuleta ushindi kwenye timu ni kuwa na wachezaji wazuri wenye kufuata maadili ya mchezo wa mpira wa miguu na kufanya mazoezi ya nguvu. Sijawahi kuona viongozi wa timu hizi wakiwaamuru wachezaji kukaa bila kufanya mazoezi ya nguvu huku wakitegemea juju kupata ushindi. Mechi kati ya Yanga na Simba hutawaliwa sana na imani za ushirikina kiasi cha watu kushinda makaburini na kusoma dua siku nzima kabla ya mechi. Kuna kipindi hata wachezaji hawapati nafasi ya kulala usingizi kwani usiku kucha mnaamshwa na kila aina ya watu wakidai tunakuja kusoma dua.

BC : Kabla ya kuingia uwanjani katika mechi kubwa kwa mfano kati ya Simba na Yanga ulikuwa unajiandaa vipi kisaikolojia huku ukijua fika jinsi mashabiki wa timu yako wanavyoutamani ushindi?

LM : Kwa kweli unavyozungumzia upenzi wa mpira Tanzania ni katika mechi ya Simba na Yanga. Wachezaji wa timu zote mbili huwa wanakuwa kwenye tension ya hali ya juu kiasi cha kushindwa hata kula kabla ya mechi. Kwa upande wangu kwenye mechi kama hiyo nilikuwa namuomba mungu ili niweze kucheza vizuri na kisaikolojia nilikuwa najiweka sawa kwani nilikuwa najiandaa wiki moja kuanzia mazoezini mpaka siku ya mechi. Ni mechi ambazo zilikuwa zinanifanya nionekane mchezaji mzuri kwani nilikuwa nacheza ili niwape wanachama na wapenzi wa Yanga kile kitu walichokuwa wanatarajia yaani ushindi. Unapokuwa mchezaji mzuri wa timu hizi mbili unapata marafiki wengi wapenda mpira bila kujali itikadi zao za Simba na Yanga. Nimebahatika kuwa na marafiki wengi na mpaka sasa wananikumbuka kuwa nilikuwa mchezaji mzuri wa kiwango cha kimataifa. Mimi mwenyewe sikuwa sijielewi kama mchezaji mzuri ila tu kwa sifa wanazonipa sasa hivi baada ya kuacha kucheza mprira.

LM :Ni tukio gani kubwa katika maisha yako ya uanasoka au unamichezo ambalo hutokaa ulisahau kamwe?

Tukio ninalolikumbuka katika maisha yangu ya uanamichezo ni wakati wa mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati. Mpambano wa fainali kati ya Yanga na EL Merek ya Sudani mwaka 1986. Mechi hiyo tulifungwa kwa mikwaju ya penati. Mchezo ulichezwa dakika 130 na matokeo ya uwanjani yalikuwa sale ya mbili kwa mbili. Hiyo mechi naikumbuka kwani mpaka dakika 86 tulikuwa tumefungwa magoli mawili na washabiki wa soka walikuwa wamekata tamaa wakielekea kutoka nje ya uwanja huku wakisema Yanga wamefungwa.Mimi niliongea na golikipa wetu Joseph Fungo kuwa sasa muda umeishaisha nianzie mpira kwangu nijaribu kupita ili niongeze mashambulizi. Joseph alinisikia na nikaongea na Abubakar Salum na Abeid Mziba kuwa wawe tayari kupata krosi kutoka kwangu. Bahati nilivyoanza kuoverlap nikapiga krosi na Abubakari kafunga goli la kwanza. Zikiwa zimebaki sekunde nikaoverlap tena na wakati naenda golini kufunga mwenyewe beki wa El merek akanichezea rafu karibu kabisa na goli. Athumani Chama alipiga mpira ambao ulitua kwenye kichwa cha Abubakari na kufunga goli la kusawazisha na kuwa draw. Washabiki waliokuwa wametoka ikabidi waanze kupanda mabasi ya kurudi kiwanjani kushuhudia dakika 30 za nyongeza . Mshindi aliamuliwa kwa kupigiana matuta. Yanga tulipata penati 3 na El merek wakifunga penati 4 na kuwa mabingwa. Hii mechi ilinipandisha chati sana na mpaka sasa hivi watu wanikumbuka kwa jinsi nilivyojituma na kusababisha kurudisha magoli kwa muda wa dakika 4 tu.

BC :Kumekuwepo na dhana kwamba mpira wa Tanzania ni kama kupoteza muda tu.Wanaosema hivyo wanadai hakuna mafanikio makubwa yanayotokana na uanasoka nchini Tanzania.Unasemaje kuhusu dhana hiyo? Kwa maoni yako binafsi, ni kweli au uongo?

LM : Hiyo ni dhana potofu.Unajua bwana Jeff, watanzania wengi wanapenda sana mtelemko. Nikimaanisha kuwa wanataka ushindi wa timu zetu bila kujua kuwa mpira wa kisasa lazima uwekeze na bila kuwekeza usitegemee kupata mafanikio. Kila shughuli afanyayo binadamu inahitaji uwe na malengo. Ukishapanga malengo yako ndipo unaweza kujiuliza je hayo malengo nitayafikia vipi. Kwenye maendeleo ya mpira wa kitanzania tunakuwa tunakosa malengo hata kama tuna malengo hatujui jinsi gani au njia zipi zitumike kufikia malengo. Viongozi wengi wanaingia madarakani wakiwa na malengo yao binafsi bila kujali malengo ya klabu. Mimi nasema kuwa watanzania tukidhamiria kuinua kiwango cha soka tunaweza kwani tuna vijana wengi wenye vipaji vya kucheza mpira lakini kwa sababu hatuna mikakati endelevu ya kuinua kiwango cha mpira wa miguu ndio maana watu wanasema mpira wa Tanzania ni upotezaji muda tu. Lakini kwa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, imeonyesha mategemeo mazuri ya kujaribu kuinua kiwango cha mpira Tanzania. Mimi binafsi napenda kumpongeza Raisi wetu na serikali yake kwa moyo na mapenzi yao ya kuendeleza soka letu. Mimi nina uhakika baada ya kumalizika awamu hii ya nne tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye medani ya soka barani Afrika na duniani kote. Vijana wengi miaka ya nyuma walikatishwa tamaa na migogoro kwenye michezo hasa kwenye ngazi ya kitaifa ya uongozi wa soka. Hata serikali ikabidi isijishughulishe kutoa msukumo wa kuendeleza soka nchini. Na napenda kutoa pongeza kwa viongozi wetu wa TFF wakiongozwa na Raisi Leodgar Tenga Chilla kwa uongozi wao thabiti wa kuendeleza soka nchini.

BC : Mchezo wa soka nchini Tanzania siku hizi umepoteza msisimko uliokuwapo siku za nyuma. Ushabiki wa kufa mtu baina ya Yanga na Simba kwa mfano siku hizi ni kama haupo. Unadhani nini kimesababisha kupotea kwa ule msisimko na nini kifanyike ili turejee kule tulikotoka?

LM : Ushabiki wa zamani kweli umepotea na mimi nakubaliana kabisa. Kwa mtazamo wangu kuna sababu kuu tatu.

Migogoro ndani ya klabu hizi umesababisha wapenzi wengi wakate tamaa kwani maandalizi ya timu yanakuwa hafifu na hata kama yapo utaona kundi moja halitaki timu ishinde eti inaongozwa na wapinzani. Zamani wanachama wote wakati wa maandalizi ya mechi walikuwa kitu kimoja na dhamira yao ni kushinda.

Mpira wa Tanzania umegeuka kuwa biashara. Kuna watu ambao wanakuwa na hela zao na kutoa hongo kwa wachezaji ili timu yake ishinde abaki madarakani. Wachezaji nao sio rahisi kuziacha pesa ambazo anajua hawezi kuzipata hata timu yake ikishinda hivyo matokeo yake wachezaji waliopewa pesa hucheza chini ya kiwango na kuashiria timu ifungwe. Wanachama huwa wanakuwa wepesi kubaini kasoro hizo na kuanza kukata tamaa.

-Kiwango cha wachezaji nacho kupungua ni moja ya sababu ya kutokuwa na ushabiki wa watani wa jadi. Zamani mechi ya Simba na Yanga ilikuwa ni gumzo la wiki nzima kwa kuweza kutambiana magoli na umahiri wa wachezaji wao. Wanachama walikuwa wanaona faraja sana kuwaongelea wachezaji wao mahiri kwenye vigenge vya starehe kama vile bar na kwenye migahawa ya vinywaji mbalimbali. Na wachezaji tulikuwa tunajituma ili uweze kupata washabiki wengi watakao kupenda kwa sababu ya uchezaji mzuri.

BC :Katika siku za karibuni mashabiki wa soka nchini Tanzania wamehamishia ushabiki wao katika ligi kuu ya soka ya nchini Uingereza. Majina ya vilabu kama Manchester,Liverpool,Chelsea,Arsenal nk ndio yanasikika zaidi. Je unadhani hili linachangia kwa njia moja au nyingine kwa timu zetu ikiwemo ile ya Taifa ,kudorora katika michezo ya kimataifa kwa kukosa support ya mashabiki wa nyumbani?

LM: Hapana. Ushabiki wa timu za nyumbani una raha yake na ushabiki wa timu za nje una raha yake pia. Nafikiri sababu nilizokutajia hapo juu ndio chanzo kikuu cha kupunguza ushabiki nyumbani. Kwa sababu ya uchezaji mbovu wa wachezaji wetu, watu wanakata tamaa na kutupia macho timu za nje. Wachezaji wetu wa siku hizi wanashidwa kutambua matakwa na matarajio ya wapeda soka nchini.

BC: Enzi zenu wachezaji mlikuwa mnacheza soka kwa mapenzi zaidi kuliko biashara au kwa hela kama ilivyo siku hizi.Je unadhani mabadiliko haya ni jambo jema au baya?Kwanini?

LM: Dunia sasa hivi inabadilika kwa kasi kubwa, hivyo basi hata watu inabidi tubadilike ili twende na wakati. Kama nilivyo kwambia kuwa mpira wa siku hizi ni biashara. Mabadiliko haya lazima yawepo kwa sababu kama binadamu hubadiliki utakuwa una “miss future”.Sisi zamani tulikuwa tunacheza mpira huku tukifanya kazi serikalini au katika mashirika ya umma. Sasa hivi vijana wanaocheza mpira ili waweze kujenga maisha yao kwa kipato wapatacho. Ni wakati mzuri kwa viongozi kutambua kuwa mpira wa mapenzi umekwisha hivi sasa unaweza ukaamua kusajili wachezaji wengi wa timu yoyote bila kujali itikadi mradi unao uwezo wa kipesa. Zamani usajili wa Simba na Yanga ulikuwa unamchunguza mchezaji kama ana asili ya itikadi ya timu.

BC:Maisha mara kwa mara huwa na nyakati za majuto kutokana na maamuzi mabaya ambayo tunayafanya kama binadamu. Kama mchezaji, unapokuwa uwanjani, ,maamuzi makini ni jambo muhimu sana.Je unakumbuka uamuzi wowote mbaya uliowahi kuufanya ambao ulipelekea timu yako kushindwa? Ilikuwaje?

LM: Mimi wakati wa uchezaji wangu nilikuwa najitahidi sana kufuata maadili ya uchezaji kama vile kufanya mazoezi ya nguvu na kuwa na nidhamu ya kimpira. Na ndio maana nilibahatika kupendwa na wachezaji wengi na wapenda soka Tanzania na kubahatika kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora 1987. Kufungwa kwa timu yangu ilikuwa ni moja ya matokeo ya michezo kwa ujumla. Ila mimi mwenyewe sipendi kufungwa hata kwenye mazoezi ya kawaida kwani huwa mara nyingi nakuwa na imani wa ushindi muda wote.

BC: Kwa miaka yote uliyocheza soka umefundishwa na makocha mbalimbali.Ni kocha gani unayemkumbuka zaidi?Kwanini?

LM: Nimechezea timu nyingi na nimefundishwa na makocha wengi. Kocha ninayemkumbuka sana ni Kilambo mchezajiwa zamani wa Yanga na Pan Africa. Wakati najiunga na Pan kutoka Waziri Mkuu, Kilambo ndiye alikuwa ni kocha wetu.Namkumbuka kwa sababu ndiye alikuwa ananipa moyo wa kufanya mazoezi ya nguvu na kuniambia kuwa wewe utakuwa mchezaji nzuri sana kwani unasifa zote za uchezaji mzuri wa mpira wa miguu. Wakati huo PAN Africa ilikuwa na mabeki wazuri sana kama vile Carlos Mwinyinkuu, Mohamed Mkweche, Kassim Matitu, Rashid idd Chama, Adolf Rishard,John Faya,Jafari Abdulhaman, Jella Mtagwa (alikuwa ameumia goti) na Sir Leodgar Tenga( Alikuwa anasoma UDSM Masters of Business Administration hiyo muda miwingi alikuwa masomoni na yeye alipata matatizo ya goti).Ilikuwa ni vigumu mchezaji kutoka mikoani na huna jina kupata namba timu ya Pan Africa. Lakini mimi kwa umahiri wangu niliweza kupata namba ya kudumu na kuwa mchezaji tegemeo. Kocha mwingine ninayemkumbuka ni Mheshimiwa Joel Bendera ambaye wakati huo alikuwa ni kocha wa timu ya taifa(Taifa Stars). Ni kocha ninayemkumbuka kwa sababu alivyoniita kuwa mmoja wa wachezaji wa timu ya taifa aliniambia kuwa wewe ni mchezaji mzuri sana kinachotakiwa ni bidii ya mazoezi na nidhamu ukiwa mpirani na nje ya mpira. Alibahatika kunifundisha hata kwenye timu ya Yanga wakati tukikabiliwa na mechi za kimataifa na kwa kweli Mheshimiwa Bendera alikuwa anapenda sana uchezaji wangu. Alidiriki kunitolea mfano kwa wachezaji wa timu ya taifa tuwapo mazoezini kuwa mimi ni role model nzuri ya kuigwa na wachezaji wengine kitu ambacho ni nadra kwa kocha kukisema kwa wachezaji.

BC: Unatoa ushauri gani kwa vijana wanaochipukia hivi sasa katika ulimwengu wa soka?

LM: Mimi ushauri wangu kwa vijana chipukuzi katika ulimwengu wa soka ni kuwa na nidhamu na kupenda kufanya mazoezi ya nguvu ili wawe ni wachezaji wa kimataifa. Wasifikirie kuchezea Yanga na Simba tu.

BC:Tatizo moja ambalo wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa wakisakamwa nalo ni ukosefu wa elimu kiasi kwamba watu wengine wanadai ndio maana wanakuwa wagumu kufundishika(coached).Wewe umekuwa mchezaji na pia msomi mahiri.Nini siri yako na unatoa ushauri gani kwa wachezaji wa leo?

LM: Mchezo wa mpira ni kipaji anachozaliwa nacho mtu. Anaweza akawa hajasoma lakini akawa ni mchezaji mzuri wa mpira wa miguu. Elimu inasaidia kuwa na nidhamu ambayo ni moja ya kigezo cha kuwa mchezaji mzuri.Kama unakuwa na timu yenye wasomi wengi kuna uwezekano mkubwa kuwa na mjumuiko wa kuwa na wachezaji wazuri na timu nzuri ya ushindani. Ukiwa na timu ya wachezaji wengi wasiosoma kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na timu isiyo ya ushindi. Pamoja na kwamba mpira ni kipaji lakini kwenye ufundishaji wa timu mara nyingi makocha wanatumia sana “scientific approach” na mpira duniani kote unafundishwa kisayansi. Mara nyingi mtu msomi anatoa maamuzi ambayo yananufaisha jamii na kujenga umoja. Mtu asiyesoma maamuzi yake ni ya majaribio sio maamuzi ya uhakika. Mimi ushauri wangu nasisitiza kuwa na wachezaji wenye elimu nzuri ili wawe mfano nzuri katika maamuzi yao kwa wachezaji wachache wasiokuwa na elimu.

BC: Kwa ujumla nini mtazamo wako wa soka la Tanzania hivi sasa?

LM: Kwa sasa hivi ni jukumu la wachezaji na viongozi wa mpira wa mguu kutambua mahitaji na mategemeo ya watanzania wote wapenda mpira. Serikali imeonyesha nia yake ya kukuza kiwango cha mpira Tanzania. Makampuni binafsi yameonyesha nia ya kukuza kiwango cha mpira Tanzania. Sasa tunawaachia viongozi na wachezaji ili watimize matakwa ya watanzania. Watanzania wametambua tulikotoka kimpira na wanaelewa wapi tunakotaka kufika. Mikakati mingi inafanyika kwa kusaidiana na serikali ni jinsi gani tunaweza tukafika tunakotaka kwenda.

BC: Tukizingatia kwamba ulikuwa unachezea zaidi nafasi ya ulinzi tungependa kukuuliza swali lifuatalo;je kuna mshambuliaji yeyote nchini Tanzania aliyekuwa anakusumbua kila mkutanapo?

LM: Kipindi changu cha uchezaji kulikuwa na wachezaji washambuliaji wengi wenye vipaji kama vile Zamoyoni Mogella, Peter Tino, Madaraka Selemani, Juma Mgunda, Prof. Angello Madundo, Kitwana Selemani, Marehemu Edward Chumila na Celestine “Sikinde” Mbunga,Abdallar Buruhani, Abeid Mziba, Edgar Fongo, Makumbi Juma, Malota Soma, Said Mrisho, Said Mwamba, Omari Hussein na wengine wengi tu. Wachezaji wote hao juu ilikuwa moto wa kuotea mbali. Lakini siku hizi mabeki wengi hawana kazi ya ziada kwa sababu Tanzania sasa hivi hatuna washambuliaji wenye uwezo kama hawa.

BC: Ni mchezaji gani duniani, anayechezea klabu yoyote ile hivi sasa anayekuvutia zaidi? Kwanini?

LM: Mchezaji anayenivutia duniani ni Kaka wa AC Milani na timu ya taifa ya Brazil. Ni mchezaji mwenye kipaji cha pekee na huweza kubadilisha speed ya mchezo na ana pasi za uhakika.Pia ana uwezo binafsi wa kuisaidia timu kupata ushindi.

BC: Je hivi sasa unajishirikisha kwa njia yoyote ile na mchezo wa soka?

LM: Mimi mpira uko kwenye damu huwa mara nyingi najumuika na wachezaji wenzangu wa zamani kufanya mazoezi ya veteran players( Wachezaji waliostafu kucheza mpira wa ligi).

BC: Ni kitu gani ambacho unaki-miss zaidi ukikumbuka maisha yako dimbani?

LM: Sasa hivi nasikitika kwamba serikali imejikita kusaidia kukuza mpira wa miguu lakini kiwango cha wachezaji wa sasa sio kizuri kama enzi zetu wakati tunacheza mpira wa hiari ya moyo. Siku za hivi karibuni watanzania wamepata muamko mzuri sana wa kupenda soka. Kila nikienda kuangalia mpira huwa nawakumbuka wachezaji wenzangu niliokuwa nacheza nao na uwezo wao nikilinganisha na uwezo wa wachezaji wa sasa hivi. Nakuwa na kumbukumbu ya kukosa ufundi wa kimpira ambao ulikuwepo enzi hizo.

BC: Umeshaoa? Kama ndio una watoto? Wangapi? Kuna ambao wanafuata nyayo zako za kusakata kabumbu?

LM: Nimeoa na nina watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike. Wakiume wanapenda sana mpira na wanacheza vizuri lakini huwa nawasisitizia kusoma sana kuliko kucheza mpira.

BC: Asante sana kwa mahojiano haya. Kila la kheri katika kazi zako.

LM: Asanteni pia.

 

16 Responses to “UNAMKUMBUKA LAWRENCE MWALUSAKO?”

  1. Tahir Says:

    Eee bwana kweli bongocelebrity nimewakubali.This is great.Mimi ni simba damu lakini nitakuambia kitu kimoja,huyu beki alikuwa kisiki ile mbaya yaani.Watu kama hawa wangetumiwa vizuri,hata kwa ushauri tu soka la bongo lingefika mbali sana.I hope Tenga na wenzake watasoma mahojiano haya.Safi sana bongocelebrity,mmenikumbusha mbali sana.

  2. Innocent Peter Mosha Says:

    Maojihano yamekumbusha mbali sana: enzi zile ukisikia mechi mwili unasisimuka sana: Bravo mwalusakao hata mimi ni shabiki wa yanga damu na kile kipindi chenu kweli ukisikia mechi akili inaumwa kabisa: anyway jitahidini sana na nyie kutoa ushauri wenu kwa vizazi vinavyochepukia msikae kimya angalia hawa madogo nao waseme mie nacheza kama Mwalusako, china nk.TUNAJUA UKITAKA KUSAIDIA MAJUNGU NI MENGI LAKINI KUMBUKA WE NIA YAKO NI NINI NA SONGA MBELE; bRAVO mWALUSAKO???

  3. Michael Godfrey Mngodo Says:

    Mpira ulikuwa ndio starehe ya Mtanzania. Dhana hiyo iliondolewa na wenye pesa wasio kuwa na Malengo ya maendeleo kimpira. Nikweli hivi sasa hakuna “vipaji na bidii” kama alivyosema Kaka Mwalusako.

    Mpira ulikuwa kote Mwanza, Tanga, Dodoma, Morogoro, Dar n.k.

  4. Mpira ulikuwa starehe ya Mtanzania.

  5. Habi Litaunga Says:

    Keep on giving us pro and fact files of our Tanzanian football legends so that the current generation of bongo footballers could learn about those good times that made Simba and Yanga teams known all over Africa for their prolific soccer. A big hand to Mwalusako for encouraging Tanzanian footballers to keep on playing socccer at the same time concentrating on education which is a key of life.

  6. Neema Says:

    Safi sana Bongo celebrity! nimefurahi sana nimekumbuka mbali saaaana. nakumbuka picha hizo unanunua unabandika kwenye daftari au albam za wakati ule. Enzi ile soka ilikuwa soka kweli na ligi yenye msisimko sana. Mwalusako kweli alikuwa moto wa kuotea mbali tunakukumbuka sana mchango wako naamini unahitajika sana katika kujenga soka la Tanzania

  7. rose john Says:

    Nimekukubali sana.je kati ya hao wanao huyo wa kike anapenda nini? pili mara nyingi madoctor huowa manes, je wewe mkeo pia ni mwanamichezo? na hujatwambia elimu yako sasa hivi ni kiwango gani.mwisho nakutakia kila la heri katika kazi zako na ninaishauri serikali angalau uwe meneja wa timu ya taifa.
    Ni mimi Rose john MTWARA

  8. Lawrence Mwalusako Says:

    kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wandaaji wa bongocelebrity akina Jeff aishiye Toronto Canada. kwa kweli bongocelebrity inaleta changamoto kwa watanzania wengi wanaotembelea hii tovuti kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kutoa maoni na mtazamo.Mimi mwenyewe nimefarijika sana kwa kuweza kuwa na bahati ya kuchaguliwa kama mmoja wa watu maarufu Tanzania. Pili napenda kuwapongeza wale wote waliotoa mchango na wale watakaoendelea kutoa mchango kwenye mahojiano haya kwani yote ni kwa faida ya watanzania wadau wa mpira wa miguu.
    Nachukua nafasi hii kutoa majibu kwa maswali ambayo dada Rose John ameyauliza wakati wa mchango wake.
    Mtoto wangu wa kike anapenda kusoma na yuko darasa la sita. nikimuuliza anapendelea kuwa nani anasema anataka kuwa mwanasheria.Nikimuuliza kwa nini umechagua uanasheria, anasema antaka kuwa mtetezi wa haki za wanawake. Mke wangu ni mwanamichezo lakini sikumuoa eti kwa sababu ni mwanamichezo ilitokea coincidence. Elimu yangu ni ya chuo kikuu. Nimemaliza digrii ya kwanza ya uchumi BA (economics)UDSM mwaka 1989.Nimemaliza digrii ya pili ya juu ya utawala katika maswala ya biashara MBA(marketing) chuo kikuu cha DSM mwaka 2006.Ni mategmeo yangu kuwa majibu haya yatakidhi haja yako. Lawrence mwalusako

  9. Rose john Says:

    Nashukuru kwa majibu yako kaka Lawrence.Hongera kwa yote.Nimekuwa nakusumbua kwa maswali yangu.nakupongeza sana ni nadra kuona mwanamichezo msomi.kwani hata wachezaji wa ulaya sidhani kama kunamsomi kama wewe.bado naishauri serikali iutambue mchango wako kwa taifa.nadhani wewe na tenga ndo wanamichezo wasomi kwa kiwango cha kufikia shahada ya pili hapa tanzania kwa ufahamu wangu kama kunawengine basi siwajui.pili hata huyo mwanao naona anaupeo na anatafuta future nzuri.mwendeleze.mwisho nakutakia kazi njema
    Rose

  10. Iam naomi,11yrs.Iam Mwalusako`s daughter.Thanx to sister Rose for your advice to me and my father.I promise you i will do my best to study hard so that i can be a lawyer in order to defend your right and other women and children`s right.
    thank you,
    Naomi Lawrence Mwalusako.

  11. Msanii Says:

    Nilikuwa hata sijafikisha miaka 8 mwaka 1987 lakini nakumbuka vizuri majina hayo ya wachezaji mahiri wa enzi hizo: China, Minziro, Chama, Mziba, and ofcourse the one and only “Sure Boy.” Sijui kama Tanzania itaendelea kutoa vipaji kama hivyo tulivyoshuhudia miaka ya themanini.

  12. mungi Says:

    mimi ni mpenzi wa yanga damu kabisa mtu kama mwalusako nadhani alikuwa ni pekee yanga ambaye ni mwanafunzi chuo kikuu.
    Lakini mtu ambaye amenivutia sana miaka ya 80 ni abubakar salum sure boy na nilikuwa nimepangawa zaidi siku ya mechi na elmeric ya sudan kwani alisawazisha bao dakika ya 91
    nawatakia kila la kheri wachezaji wetu

  13. Ed (USA) Says:

    Mimi kipindi ambacho Mwalusako unawika nilikuwa mwanafunzi primary na secondary nikishabikia simba. Nilikuwa nakushabikia Mwalusako ulipokuwa akichezea taifa stars. Ni kweli wakati ule simba na yanga ilikuwa moto sana. Ninajiuliza mara nyingi, iwapo kiwango cha mpira wakati huo kilikuwa juu, mbona hatukufanikiwa kufika mbali kimataifa?

    Hakuna wakati ulikuwa unanikosesha raha kama timu zetu wakati ule zinapofikia kupangiwa na timu za misri. Nafikiri hata wachezaji walikuwa wanaathirika kisaikolojia. Tunaweza kujitahidi tukicheza nyumbani lakini kwao ilikuwa balaa.

    Kitu kingine ningependa kujua wakati ule akina mwalusako mnacheza je, waamuzi walikuwa wanasimamia vipi mpira wa mabavu? Mazingira yalikuwa yananizuia kwenda mpirani kushuhudia, lakini nilikuwa msikilizaji mzuri wa redio Tanzania na kusoma magazeti. Nakumbuka yanga walikuwa wanampa kazi ya ziada Athuman Chama kumzuia Zamoyoni Mogela. Sijui kama uchezaji ule bwana Mwalusako una nafasi katika soka la leo?

    Nakupongeza sana Mwalusako jinsi ulivyokuwa hodari uwanjani bila kuaffect maendeleo yako shuleni.

  14. DIDA MOSHI Says:

    Mi ni mtoto wa Moshi Majungu, in my 20s, Naishi Lewisham, South London. Nimefurahi sana kupata kumbukumbu za back in the days, za baba yangu, ktk picha hii nae alikuwa in his 20s, ama kweli siku zinakwenda!! naona alikuwa chekibob,kama kina “BECKS”. Baba alikuwa mchezaji mzuri saaana!!! { i think some people will agree with me on that one} Thank you so much for the photo, umenikumbusha saana na lots of memories. GOD BLESS YOU ON EVERYTHING and keep on representing OUR BEATIFUL country TANZANIA.

  15. John Mlay Says:

    Namkumbuka vizuri Lawrence zamani za Pugu high school(Mwakanga), ukiwa nae na Madundo(now Prof. Madundo) kikosi kimekamilika.

  16. abdallah a. mabina Says:

    Nakumbuka siku nyingi nikiwa mdogo darasa 4. nashikwa mkono kweda uwanja wa taifa kuangalia mechi, nanilikua napenda kukaa nyuma ya goli na marafiki zangu augustino francis, A,milanzi, Ambaye baba yake sasa ndio raisi wa timu
    ya mzizima inayoshiliki ligi ya TFF ngazi ya mkoa, nami nikiwa katibu wa young boys inayoshiliki ligi hiyo pia… pia historia inanikumbusha marehemu baba yangu mdogo Elias robart, aliyechezea kagera,simba, mavumbi omary, godfrey mwiga nawengine wengi.. nawaasa chipukizi wasasa mpira ni..nidham,kujituma,kujifunza,uvumilivu,chakula,mazoezi,mapumziko.


Leave a reply to Tahir Cancel reply