BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

HAPPY NEW YEAR! December, 31, 2008

Filed under: Editorial,Sikukuu — bongocelebrity @ 11:21 AM

header1

Hatimaye siku 365 za mwaka 2008 zimefikia ukingoni.Ninavyoandika ujumbe huu tayari kuna sehemu mbalimbali za dunia ambapo tayari sekunde za mwisho za mwaka huu zimeshahesabiwa na tayari takwimu mpya zimeshaandikwa.Kwa maana hiyo leo ni mwaka mpya. Kwa heri mwaka 2008 karibu mwaka 2009.Kwa wengi leo huwa ni siku nzuri kwa maazimio mapya ndani ya matumaini mapya.Kwa jinsi hali ya uchumi duniani ilivyoishia mwaka tunaoupa kisogo,basi sio ajabu kwamba malengo ya wengi ni kulinda zaidi mifuko yetu kwa kuwa makini zaidi na matumizi hesabu za mapato na matumizi na pia kulinda zaidi kazi zinazotuingizia kipato.Nakutakia kila la kheri katika hilo.

Bila kujali hali ya kiafya,kiuchumi,kisiasa wala kijamii, ukweli kwamba mwaka mpya umewadia huku wewe na sisi sote hapa BC tukiwa hai, ni jambo la kufurahia na kumshukuru Muumba.Ukivuka mwaka unakuwa umeandika historia mpya katika maisha yako. Vitabu vya kumbukumbu vitaandika kwamba uliuona mwaka 2009! Ni jambo la kumshukuru muumba kwani ni wazi wapo wengi sana waliotamani kuuona mwaka huu na wasifanikiwe.Kama huamini, fikiria kidogo tu ni watu wangapi ambao umehudhuria mazishi yao au kusikia habari juu ya misiba yao?Unaona? Hatuna budi kumshukuru Mungu.

Wakati huu tunapoingia mwaka mpya wa 2009,tungependa kwanza kukutakia kila la kheri wewe msomaji,mtembeleaji au mchangiaji wetu.Mwenyezi Mungu akuongoze na kukubariki katika kila jambo utakalolifanya ndani ya mwaka huu wa 2009.Kama mwaka 2008 haukuwa wenye mafanikio kwako au haukutimiza malengo yako,usikate tama.Fungua ukurasa mpya huku ukiwa na fikra chanya zaidi na utaona mabadiliko.

Tungependa pia kukupa shukrani zetu za pekee kwa kuwa mtembeleaji,msomaji au mchangiaji mzuri wa BC.Kama kuna mafanikio yoyote ambayo tumeyapata tangu kuanzishwa kwa blog/site hii,ni wazi kabisa kwamba mafanikio hayo yametokana na mchango wako wewe msomaji,mtembeleaji na mchangiaji wetu.

Shukrani nyingi ziwaendee celebrities mbalimbali ambao bila maringo,kinyongo wala ngendembwe walikubali aidha kufanya nasi mahojiano au kutokuwa na kinyongo nasi pale tulipoweka picha zao na kukaribisha mvua ya maoni kutoka kwa wasomaji huku wengine wakiwa chanya na wengine hasi.Celebrities kama hao wanakuwa wametambua vyema nafasi au mchango wao katika jamii.Wametambua pia kwamba haiwezekani kuwa bondia ulingoni halafu ukawa unaogopa ngumi za uso.Tunawashukuru na kuwaomba tuendelee kushirikiana.

Shukrani za pekee ziwafikie bloggers wenzetu mbalimbali,vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Tanzania,wapiga picha mbalimbali na wengineo wote ambao wanaendelea kushirikiana nasi katika jukumu hili zito la habari na mawasiliano.Asanteni sana.Bila ninyi,haiwezekani.BC inathamini sana mchango wenu.

Kama binadamu inawezekana kabisa kuna wakati tunatokea kutoelewana au hata kukwazana.Bila shaka hata sisi hapa BC inawezekana kuna wakati tulikukwaza.Yawezekana hatukuweka maoni yako kwa sababu moja au nyingine,yawezekana tulichelewa kuruhusu maoni yako yaonekane,yawezekana wewe ni celebrity na tuliruhusu maoni ambayo kimsingi uliona kama umetusiwa nk.Mifano ipo mingi.Lakini kwa wote hao,tunaomba samahani.Yote hayo ni katika kujitahidi kuitenda vyema kazi yetu.

Tunapouanza mwaka mpya wa 2009,tunakusihi uendele kututembelea,kuchangia,kutukosoa tunapokosea na pia kumwambia mwenzako kuhusu uwanja huu ili naye asipitwe na yanayojiri.Tunakutakia kila la kheri.HAPPY NEW YEAR 2009.

 

SIKUKUU ILIKUWAJE? December, 30, 2008

Filed under: Burudani,Sikukuu,Swali kwa Jamii,Zilipendwa — bongocelebrity @ 11:54 AM

comedi-orijinobc

Naam!Xmas kwa mwaka 2008 ndio imeshaisha.Kwa bahati mbaya siku kama hizi huwa hazirudi tena.Ilivyokuwa Xmas mwaka huu sivyo itakavyokuwa mwaka ujao na mingine itakayofuata.Ulipokuwa mwaka huu si ajabu hutokuwepo mwakani.Ndio maana huwa tunasisitiza kwamba Make The Most Use of It when/whenever you can(nimetia kizungu hapo kuonyesha msisitizo).

Najua wengi wenu bado mpo kwenye hali ya sikukuu.Wengine nasikia bado wanatibu mning’inio wa ziada(hangover).Kwa wengine huu ni wakati wa kutafakari jinsi matumizi yalivyokwenda.Ni wakati wa kukagua risiti huku macho yakiwa yamekutoka na simanzi likiwa limetanda usoni.Usijali,ndio maisha.Si ushasikia ule msemo usemao Ponda Mali kwani Kufa Kwaja?Sasa?

Lazima pia nikiri kwamba hata sisi wenyewe tupo kwenye holiday mood bado.Ndio maana mwendo kidogo unakuwa taratibu ingawa sio kama wa kinyonga.Bahati nzuri hatubadiliki rangi pia.Tunajongea huku tukiandaa mambo makubwa zaidi kwa ajili ya mwaka ujao ambao kimsingi tunataka uwe mwaka wa BC!

Sikukuu ilikuwaje?Uliserebukia wapi?Mambo yalikwendaje?Tungependa kusikia kutoka kwako msomaji.Wakati unatafakari jinsi sikukuu ilivyokwenda,hatungependa kukuacha hivi hivi.Burudika na wimbo Ndoa Fungo la Imani kutoka kwa Bima Lee.Pata burudani


Tumeshindwa kupata maelezo au caption ya hiyo picha.Unaweza kutusaidia?

 

HONGERA MWL.ARNOLD CHIWALA

Filed under: African Pride,Watanzania Kimataifa — bongocelebrity @ 11:30 AM

chiwala1bc

Wapo watanzania ambao pengine hawajulikani sana miongoni mwetu ingawa mambo wanayoyafanya ni makubwa na ambayo huiletea nchi yetu sifa na heshima kubwa achilia mbali kuitangaza kwa mapana na marefu.

Ni jukumu letu kuwatambulisha kwa jamii pana zaidi na pia kuwapa shukrani kwa mchango wao katika jamii.Ukiangalia sana,kimsingi,watu hao ndio celebrity wa kweli.

Leo tunapenda kumpongeza Arnold Chiwala,mwanamuziki/mwalimu wa Kitanzania anayechukua Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Cha Muziki Cha Sibelius (Sibelius Academy).Hivi karibuni Arnold ametunukiwa Tuzo ya Dhahabu ya muziki wa Ala ya Kantele 2008. Kantele ni ala ya kiasili ya Finland. Tuzo hii hutolewa kila mwaka na Wizara ya Utamaduni ya Finland kwa mwanamuziki bora ambaye amechangia katika utunzi(composition) na uendelezaji (promotion) wa ala ya Kantele ndani na nje ya Finland.

chiwalabc

Arnold Chiwalala ni muhitimu na mwalimu kutokea Chuo cha Sanaa Bagamoyo. Vile vile ni mwanamuziki, mtunzi, muandishi wa nyimbo na mbunifu wa miondoko (choreographer).

Kazi za Mwalimu Chiwalala zinatambulika kimataifa ambapo ameshiriki katika warsha, matamasha na makongamano sehemu mbali mbali ulimwenguni ikiwemo Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Msumbiji, Uingereza, Ujerumani, Marekani, Urusi, Norway, Denmark,Sweden,Finland, Estonia na Yugoslavia.

Hongera sana Arnold.Tunakutakia kazi njema na tafadhali endelea kuwa balozi mzuri wa Tanzania.

Pichani juu katikati ni Mwalimu Arnold baada ya kukabidhiwa tuzo.Wengine ni wakufunzi wa chuo anachosoma Arnold.

 

TUNAWATAKIA KHERI YA SIKUKUU December, 23, 2008

Filed under: Sikukuu,Watu na Matukio — bongocelebrity @ 1:46 PM

happy-holidays-glitter

Sikukuu imewadia.Ni wakati mwingine wa kusheherekea Sikukuu ya Xmas na wakati huo huo kuanza makaribisho ya mwaka mpya,2009.Kama ilivyo jadi ya enzi na enzi,huu ni wakati wa kukumbukana,kutembeleana,kujuliana hali,kutakiana kheri,kujumuika pamoja,kula na kunywa kwa furaha,amani na upendo.Kwa wengine ni wakati muhimu wa kupeana zawadi.Kwa ujumla ni wakati wa kufurahi!

Ni kwa kuzingatia hayo yote yaliyotajwa hapo juu ambapo tunakukaribisha wewe msomaji,mchangiaji au mtembeleaji wa BC,kutumia nafasi hii kuwatumia ndugu,jamaa na marafiki zako,popote pale walipo,Kheri ya Sikukuu ya Xmas kwa mwaka huu wa 2008.Unaweza kufanya hivyo kwa kuandika salamu na majina yao hapo kwenye sehemu ya maoni au kututumia picha au chochote kile ambacho ungependa ili kusindikiza salamu zako.Tumia anuani pepe (bongocelebrity at gmail dot com)Ukituma picha tutaiweka kwenye post hii hii.Jisikie huru.

Kutoka kwetu: Tunatoa shukrani nyingi na za dhati kwa jinsi ambavyo umekuwa nasi kwa wakati wote huu.Tunapenda kuchukua nafasi hii kukutakia wewe,ndugu,jamaa na marafiki zako KHERI YA SIKUUKUU YA XMAS na maandalizi mema ya MWAKA MPYA 2009.Tunatumaini itakuwa sikukuu ya kukumbukwa na iliyojaa furaha na mafanikio tele.Amani itawale.

Kwa niaba ya timu nzima ya BC-Jeff Msangi

 

PASS ME THE JOINT MR.PRESIDENT! December, 21, 2008

Filed under: African Pride — bongocelebrity @ 8:23 PM

barack

Si unamtambua?Kama mambo ya Facebook na Myspace yangekuwepo enzi za ujana wake,basi bila shaka angeweka picha hii kama utambulisho.Ama kweli Baraka anainua matumaini ya wengi.

 

MAJOR NYIRENDA HATUNAYE TENA!

Filed under: African Pride,Breaking News,Msiba — bongocelebrity @ 1:47 PM

nyirendabc1

Kwa huzuni na masikitiko makubwa tumezipokea habari za msiba wa Major Alex Gwebe Nyirenda.Huyu ndiye shujaa aliyepandisha bendera ya Tanganyika huru na Mwenge wa Uhuru kileleni Mlima Kilimanjaro usiku ule wa mkesha wa Uhuru miaka 47 iliyopita.

Marehemu Nyirenda ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kansa kwa muda sasa, amefariki jana majira ya saa moja jioni(saa za Afrika Mashariki) katika hospitali ya taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.Mapema mwaka huu Major Nyirenda alipelekwa nchini India kwa matibabu zaidi kufuatia kudhoofika kwa afya yake.

Marehemu Nyirenda anatarajiwa kuzikwa siku ya jumatano ijayo katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar-es-salaam.Msiba upo nyumbani kwake huko Mbezi Beach,Flats za National Milling karibu na njia panda ya kwenda Africana.

Ni siku chache tu zilizopita ambapo tuliweka mahojiano tuliyofanya na Major Nyirenda kuhusiana na harakati za uhuru,zoezi zima la sherehe za uhuru nk.Unaweza kuyasoma mahojiano hayo kwa kubonyeza hapa.

Katika mahojiano yale,Major Nyirenda aliongelea mambo mengi.Lakini katika mengi hayo pengine ushauri au usia aliotuachia wa kujitolea,uvumilivu na uaminifu ndio ambao hatuna budi kuufanyia kazi ipasavyo kwa minajili ya kumuenzi Major Nyirenda na pia kwa maendeleo yetu binafsi na jamii zetu.

nyirenda-3

Katika picha hii iliyopigwa mwezi wa pili (February) mwaka huu,inamuonyesha Major Nyirenda akiwa hospitali jijini Dar-es-salaam akihudumiwa na mkewe.Hii ilikuwa ni kabla serikali haijaingilia kati na kumpeleka nchini India kwa matibabu zaidi.Picha na Mpoki Bukuku.

Tunapenda kuungana na ndugu,jamaa,marafiki na watanzania wote kwa ujumla katika wakati huu mgumu wa kuondokewa na shujaa wetu,Major Alex Gwebe Nyirenda.Mungu ailaze pema roho yake milele na milele.Rest in Peace Major Nyirenda.


 

DR.JAKAYA MRISHO KIKWETE December, 19, 2008

Filed under: Serikali/Uongozi,Watu na Matukio — bongocelebrity @ 3:48 PM

jk

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya, Dk.Harris Mule akimtunuku Phd ya Heshima Rais Jakaya Kikwete wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika mjini Nairobi,Kenya leo. Phd hiyo inatokana na jitihada zake za utatuzi wa migogoro kwa nchi za Afrika hasa mgogoro wa Kenya uliozuka baada ya uchaguzi mapema mwaka huu.

Photo/Freddy Maro