Ijumaa nyingine imewadia.Mwezi wa pili ndio unakatika hivyo.Naona kama vile mwaka huu unaenda kwa kasi sana.Wewe unaonaje? Pamoja na hayo sisi wanadamu hatutakiwi kwenda kwa haraka sana kwani mwenda pole huwa hajikwai,au sio?
Kwa ujumla ujumbe huo ndio uliomo kwenye burudani yetu ya leo.Leo tunalo jina kubwa katika muziki wa dansi nchini Tanzania.Juwata Jazz Band.Wimbo unaitwa Msafiri Kakiri ukiwa ni utunzi wake Marehemu TX Moshi William(jina halisi Shaaban Ally Mhoja Kishiwa) ambaye alitutoka mwezi Machi 2006.Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Ukisikiliza wimbo huu utakiri jambo moja muhimu sana.Utunzi wa nyimbo enzi zile ulikuwa sio lelemama.Ilikuwa ni lazima wimbo uwe na ujumbe mzito na unaoeleweka.Burudani ilikuwa inakwenda sambamba na kuelimishana haswa.Nadhani wanamuziki wa leo wanaweza kujifunza mengi kwa japo tu kusikiliza tungo za wakongwe kama TX Moshi na wengineo wengi.Asikudanganye mtu,nyimbo zenye ujumbe wa maana na unaoeleweka bado na zitaendelea kuwa na nafasi sana katika mioyo ya wapenzi wa muziki.Kwa hiyo,wanamuziki wa leo au wa kizazi kipya,jitahidini basi,au sio?
Katika wimbo huu,gitaa la solo lilipigwa na Abdi Ridhiwani(Totoo) Rhythm na Pishuu,bass guitar na Issa Ramadhani huku saxophones zikiwa chini ya usimamizi wa Mnenge,Abdi Mketema na Hagai Kauzeni.Mnaojua zaidi mtarekebisha kama kuna makosa.Kama kawaida,bonyeza player hapo chini upate burudani.Ijumaa Njema
Recent Comments