BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

MANENO MANENO-DDC MLIMANI PARK February, 12, 2009

Filed under: Burudani,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 9:44 PM

sikinde

Katika medani ya soka nchini Tanzania,inaaminika kwamba kama wewe sio mshabiki wa Yanga(Watoto wa Jangwani) basi ni mshabiki wa Simba(Wekundu wa Msimbazi).Hivyo ndivyo ambavyo imekuwa tangu enzi na enzi.

Kwa upande wa muziki wa dansi,inaaminika kabisa kwamba kama wewe sio mnazi wa Sikinde basi ni wa Msondo.Utashi na ushindani uliopo katika muziki wa dansi ni sawa kabisa na ule uliokuwepo katika soka la bongo.

Haishangazi basi kusikia kwamba uvumi ulipoenea jijini Dar-es-salaam mapema wiki hii kwamba DDC Mlimani Park Orchestra imesambaratika,habari hiyo haikuwa nzuri hata kidogo kwa mashabiki wa muziki nchini Tanzania achilia mbali wanazi wa Sikinde.Hakuna ambaye alitaka kuamini kwamba inawezekana ikawepo Msondo bila Sikinde.

Lakini sio kweli kwamba Sikinde ndio imefikia tamati.Kilichotokea ni kwamba kumekuwepo hali ya kutoelewana katika mambo fulani fulani baina ya uongozi wa DDC(Shirika la Maendeleo la Dar-es-salaam) ambao ndio walikuwa wamiliki wa bendi hiyo na hivyo kuitwa “DDC Mlimani Park Orchestra).Matokeo yake ni kwamba bendi hiyo,kuanzia tarehe 1 Machi mwaka huu itaanza kujiendesha yenyewe bila usimamizi wala udhamini wa DDC.Na kuanzia hapo watajulikana kama Mlimani Park Orchestra. Kwa hiyo mashabiki wa muziki wa dansi,Sikinde bado ipo!

Naam baada ya ufafanuzi huo,leo ni mwanzo wa weekend.Hapa kwetu BC ni kama jadi.Ni wakati wa zilipendwa.Wiki hii kwa upande wangu binafsi imekuwa ngumu kidogo.Imekuwa na maudhi ya haja.Si unajua inavyokuwa pale unapomthamini mtu na kujaribu kumtendea kila aina ya wema unaoweza lakini yeye akakuona kama kinyesi tu?Inaudhi eenh?Basi hali hiyo ndiyo iliyonikumba.Ni vurumai za maisha ambazo kwa kweli huwa natamani zingekuwa na suluhisho la kudumu!

Bahati nzuri ni kwamba zipo nyimbo kama hii ya leo ya Maneno Maneno kutoka kwao wana Sikinde,ambayo inaweza kusaidia pindi joto la nyikani linapojiri.Hakuna haja ya maneno.Inafikia mahala lazima utulie na kumuachia Mola.Usikilize wimbo huu kwa makini lakini wakati huo huo usisahau “kujirusha”.Kibao hiki kitabakia kuwa mojawapo ya kumbukumbu nzuri za Sikinde wakiwa kama DDC Mlimani Park Orchestra.Tunawatakia kila la kheri katika safari yao mpya kama Mlimani Park Orchestra.Tunaamini kwamba Sikinde will always be Sikinde.Ciao


Picha ni kundi zima la wanamuziki wa Mlimani Park Orchestra kabla ya kuanza kwa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar mapema wiki hii.Picha na John Bukuku.


Advertisements
 

MASIMANGO-MBARAKA MWINSHEHE February, 5, 2009

Filed under: Burudani,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 9:32 PM

masimangoNahisi ni kama juzi tu tulikuwa tunaongelea sikukuu za xmas na kisha mwaka mpya.Ile kutahamaki,mwezi wa kwanza ulishaisha na wa pili ndio unaelekea katikati.Ukizingatia kwamba huu ni mwezi mfupi kuliko yote,utagundua kwamba siku zaenda yakhe!Tayari mbio za kutimiza malengo ya mwaka huu zishaanza kushika kasi.Kazi kwelikweli.

Ni mwaka mgumu.Ni mwaka ambao unanukia kila hali ya uchumi ulioyumba.Wachumi na wanasiasa wanakiri.Kama mpaka leo hujapoteza kazi yako basi unamshukuru aliye juu na huna budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili “panga” likipita basi uwe salama.Joto hili la uchumi likija kukolea na huku kwetu ambapo bajeti zetu zinakuwa sio bajeti bila wahisani,nahisi itakuwa patashika nguo kuchanika.Mola atuepushe maana bila hivyo…dah!

Ukosefu wa kazi ni chanzo cha umasikini.Ni chanzo cha manyanyaso.Ukiwa huna chako,ni rahisi sana kunyanyaswa hapa duniani.Watakupa na kisha kukusemea pembeni.Wakikuona unaelekea upande walipo,wengine wanaweza hata kutoka mbio kabisa.Watakupa majina.Utaitwa “Kikosi cha Mizinga”.Ukiingia baa utaona jinsi watu wanavyokaa kimya kama sio kwenda maliwatoni kwa dharura.Usishangae mialiko ikawa inakupita.Mkono mtupu haulambwi.

Visa kama hivyo ndivyo vilivyomfanya Mbaraka Mwinshehe aimbe wimbo wake maarufu wa Masimango.Usikilize hapo chini na kisha unipe tafakari yako.Je unadhani uamuzi wa Mbaraka wa kuondoka kwa sababu ya masimango ni sahihi?Ungekuwa wewe ungefanyaje?Je imeshawahi kukutokea?Ilikuwaje?Nakutakia wikiendi Njema.Pata Burudani.


 

DAWA YA MAPENZI-MBARAKA MWINSHEHE January, 15, 2009

Filed under: Burudani,Muziki,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 9:02 PM

mbaraka3bc12Kwanza tukuombe radhi kwamba wikiendi iliyopita hatukuweza kukuletea burudani ya wikiendi kama ilivyo kawaida yetu.Maji yalizidi unga au unga ulizidi maji.Vyovyote vile haikuwezakana!

Bila shaka umeshawahi kusikia sana habari za watu kuhangaika huku na kule kutafuta “Dawa ya Mapenzi”.Ushasikia jinsi ambavyo wakati mwingine hufikia mtu akalala kwa karumanzira kisa eti,dawa ya mapenzi.Miaka nenda miaka rudi,imani kwamba dawa ya mapenzi inaweza kupatikana kwenye kibuyu kidogo kilichowekewa ugoro,unyoya wa bata mzinga na takataka nyingine imeendelea kutawala akili za baadhi zetu.

Je kuna dawa ya mapenzi?Ipo wapi?Hayati Mbaraka Mwinshehe anatusaidia kupata jibu la swali hilo hapo juu katika wimbo wake Dawa Ya Mapenzi. Tungependa pia kusikia kutoka kwako msomaji.Je kuna uwezekano wa kupatiwa kidonge cha mapenzi kushinda kile cha upendo,heshima,ushirikiano na maelewano baina ya wawili wanaoamua kupendana?Bonyeza player hapo chini upate burudani.Raha ya wimbo huu,pandisha sauti kisha nyanyuka uucheze.Kama unaweza nenda kabatini tafuta bugaloo kama unayo na kisha achia afro.Mkononi shikilia glass bila kusahau zile san gogo machoni.Wikiendi Njema. 

PAULATA-JUWATA JAZZ BAND January, 1, 2009

Filed under: Muziki,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 8:18 PM

juwataBaada ya kula,kunywa na kuponda raha wakati wa sikukuu,sasa ni wakati wa kurudi tena kwenye mstari.Wazungu wao wanapenda kusema “back to the real world”.

Kwa kawaida mwezi wa kwanza huwa mgumu.Kila mtu bado ana hangover ya sikukuu.Mifukoni kila mtu anaugulia,mifuko ni kama imetoboka vile.Hapo ndipo utawaza kila mtu unayemdai.Utasali na kuomba siku ziende haraka mwisho wa mwezi ufike ukakinge tena ili maisha yarudi sawasawa sawia.Usipokuwa makini huu ndio ule mwezi “mwenzako” anaweza kufungasha virago na kurejea kwao.Si ushasikia kwamba kizazi hiki sio kile cha mapenzi tena?Kizazi hiki ni kile cha hapendwi mtu hapa…ni pochi tu.Ah!Jamani.

Ndio maana wana JUWATA JAZZ BAND katika wimbo wao Paulata wanasema “Maradhi yote ugua lakini kuchacha usiombee”.Wasikilize kwa makini katika wimbo huo uliojaa mafundisho ya msingi.Pata burudani.Wikiendi Njema.Kumbuka 2009 ndio ishaanza hivyo,twende taratibu.


Burudani ya leo imeletwa kwenu kwa niaba ya changamotoyetu.blogspot.com.

 

DUNIA/KUTELEZA SIO KUANGUKA-LADY ISSA December, 18, 2008

Filed under: Muziki,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 9:17 PM

kilimanjarobc1Mambo vipi?Unajiandaa vipi kuumaliza mwaka?Unajiandaa vipi kusheherekea mas mas?Ushanunua zawadi kwa mama watoto na watoto wenyewe?Usikasirike ninapokukumbusha.Si wenyewe tumekubali kuiga utamaduni wa watu?Tukaiita siku ya mabox bila hata kuelewa chanzo cha siku yenyewe.Kumbe ni mambo ya biashara tu na wala sio ya rohoni.Leo hii usiponunua zawadi usije shangaa watoto wakikupita bila kukupa shikamoo na wala usije niuliza imekuwaje mama watoto akigoma kukupa nanihii.

Bado nakumbuka jinsi nilivyokuwa nampa wakati mgumu mama yangu wakati wa mas mas ukikaribia.Nilikuwa sisikii kitu nisiponunuliwa mokasini suruali na shati mpya.Ningeelewa vipi wakati watoto wenzangu wote nina uhakika siku ya siku wakitoka majumbani kwao wanameremeta sio tu kwa mafuta waliyojikandika usoni bali pia nguo mpya walizovaa?Tena hapo nazungumzia enzi zile za suruali za “mchelemchele” na mashati ya bahama!

Nakumbuka zile safari za “mgombani”.Si umeshawahi kusikia habari za wachaga na wapare kwenda “kuhiji” kwao kila ifikapo mwisho wa mwaka?Sijui kama siku hizi bado kasi ya kuelekea mgombani ipo kama hapo zamani.Kasi itakuwepo kweli katika enzi hizi ambapo wachache ndio wana “vijisenti” wakati wengine wanaendelea kutokomea kwenye umasikini?Mgombani kulikuwa na raha zake.Mojawapo ilikuwa ni kukutana na ndugu,jamaa na marafiki bila kusahau “vimwana” waliotoka sehemu mbalimbali za ulimwengu.Vijana wa leo kuna mambo mnayakosa walahi.Waulizeni wakubwa zenu watakupeni michapo.Ngoja niishie hapa maana sitaki kulia…where did the days go?

Leo tunaye Lady Issa kutoka pale kwa watani zetu.Tunazo nyimbo mbili.Wa kwanza ni Dunia na wa pili ni Kuteleza Sio Kuanguka.Natumaini nyimbo hizi zitakukumbusha enzi zile na pia kukupa burudani.Kama haiwezekani kumpatia mama watoto kijizawadi mkumbushe kwamba kuteleza sio kuanguka.Sema naye tu atakuelewa.Pata burudani.Wikiendi Njema.
 

JELA-FM ACADEMIA ORIGINAL December, 13, 2008

Filed under: Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 6:34 PM

ndanda-kosovoZimebakia siku chache tu tuumalize mwaka 2008.Weekend inapojongea namna hii ni kuashiria kwamba ni wakati wa kuburudika,kupumzisha akili,kutembeleana,kuhudhuria vikao vya harusi,mwali kutolewa ndani,vikao vya familia,kiti kirefu(cha kaunta),nyama choma nk.

Kwa wengine huu ndio wakati wa maandalizi ya krismas.Ni wakati wa kuwaza na kuwazua kuhusu zawadi za x-mas.Ni wakati wa kupamba miti ya x-mas.Wakati wa kuweka pamba kwenye miti eti kuashiria barafu!Ama kweli wenzetu wanatupata.Hapo sijajiuliza kuhusu mambo ya Santa Claus na jinsi ambavyo wabongo tunamshobokea bila hata kujua au kudadisi chanzo na mwisho wake.Ajabu tukiambiwa kwamba tuna kautumwa ka akili tunakuja juu ile mbaya!Hivi ni lazima kila siku tuige kila kitu wanachofanya “wa magharibi”?Wao wanaiga nini kutoka kwetu?

Anyway,ngoja niyaache hayo kwa sababu kadri ninavyozidi kujiuliza ndivyo ninavyoshindwa kujizuia kumkumbuka rafiki yangu Ampeninimungu aliyewahi kunionya kuhusu madhara ujinga.Leo ni Ijumaa,ni siku ya kuburudika.Ndio jadi yetu hapa BC.

Wiki hii Rais ametangaza msamaha kwa wafungwa 4,306.Miongoni mwao ni mwanamuziki TID.Msamaha huo ndio ulionifanya nikumbuke wimbo kutoka kwa FM Academia(Wajela jela Gwa) au The Dream Team.Enzi zilee za kina Ndanda Kosovo(pichani).Wimbo ni Jela.Wasikilize hapo chini.Wanasema jela…jela…jela ni mbaya.Wikiendi njema.


Burudani ya leo imewezeshwa na DJ Dennis ambaye huwa kila jumamosi anavurumisha midundo pale Bongo Radio

 

SEYA-NGUZA VIKING November, 27, 2008

Filed under: Burudani,Muziki,Weekend Special,Zilipendwa — bongocelebrity @ 9:45 PM

seyaMwaka 2008 upo mbioni kuelekea ukingoni mwake.Zimebaki wiki kadhaa tu kabla hatujaona zile fataki hewani na kusikia ving’ora vikitusindikiza kuumalizia mwaka.Kwa vyovyote vile mwaka 2008 utaenda na historia kadhaa zenyewe kuvutia kwa wengine na kutia simanzi kwa wengine.Ndio maisha.Ni mwaka ambao hakuna atakayeweza kamwe kusahau kwamba mtu mweusi wa kwanza amechaguliwa kuliongoza taifa kubwa la Marekani.

Lakini nchini kwetu pia ni mwaka ambao tunaweza kusema tumeshuhudia mengi ambayo siku za nyuma yalionekana kuwa hayawezekani.Tumeona viongozi kadhaa wakijiuzulu nyadhifa zao.Tumeshuhudia wengine wakipandishwa kwenye karandiga.Tumeona wazee wengine wakipandwa na pressure kwa sababu wanajua walishaharibu na hawana uhakika na kesho.Nadhani tunakubaliana kabisa kwamba miaka kadhaa ya nyuma,ilikuwa ni kama ndoto kusikia kiongozi akitangaza kujiuzulu.Mifano ya waliowahi kujiuzulu ilikuwa ni michache sana.

Najua kuna ambao mnasema yote hii ni “changa la macho” na kwamba kinachofanyika ni mchezo wa aina yake wenye wingu zito la kisiasa.Inawezekana kabisa(hakuna lisilowezekana katika dunia hii).Lakini pamoja na yote hayo,tofauti na siku za nyuma,hata kile kitendo tu cha kuwaona waheshimiwa wakitokwa na jasho kwa sababu hawamo ndani ya yale “mashangingi” yao na badala yake wamekalia yale yale mabenchi ambayo hawakuwahi kuona umuhimu wa kuyakarabati kwa sababu “hayakuwahusu” na huku wakiwa wameegemea zile kuta ambazo hela yake ya rangi waliipeleka kusipotakiwa,ni vitu ambavyo vinaufanya mwaka 2008 uwe na lake katika historia.Bado tunasubiri kuona jinsi “changa la macho” litakavyopelekwa.Tupo na tunatizama kwa makini.Anayedhani tumelala anajidanganya.

Ni wikiendi tena.Ni wakati wa kujikumbusha zile tulizowahi kuzipenda kama ilivyo jadi yetu hapa BC.Kwa sababu wiki hii tumeshuhudia kiasi kuhusu niliyoyaongelea hapo juu,basi sio vibaya kama tukiwakumbuka Nguza Viking na mwanae Papii Kocha ambao wapo gerezani ambako ndiko tunapotarajia “waheshimiwa” watakuwa wamehifadhiwa.Wimbo unaitwa Seya.Pata burudani,wikiendi njema.