BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

HAPPY VALENTINE’S DAY February, 14, 2009

Filed under: Sikukuu — bongocelebrity @ 10:03 AM

valentino

Leo ni siku ya wapendanao duniani au maarufu kama Valentine’s Day.Ni sikukuu ambayo zamani ilikuwa ya “kimagharibi” zaidi kabla ya kuenea ulimwenguni kote.Sina mengi sana zaidi ya kuwaambieni wasomaji na watembeleaji wote wa BC kwamba tunawapenda na tunawatakia sikukuu njema.Enjoy!

 

HAPPY NEW YEAR! December, 31, 2008

Filed under: Editorial,Sikukuu — bongocelebrity @ 11:21 AM

header1

Hatimaye siku 365 za mwaka 2008 zimefikia ukingoni.Ninavyoandika ujumbe huu tayari kuna sehemu mbalimbali za dunia ambapo tayari sekunde za mwisho za mwaka huu zimeshahesabiwa na tayari takwimu mpya zimeshaandikwa.Kwa maana hiyo leo ni mwaka mpya. Kwa heri mwaka 2008 karibu mwaka 2009.Kwa wengi leo huwa ni siku nzuri kwa maazimio mapya ndani ya matumaini mapya.Kwa jinsi hali ya uchumi duniani ilivyoishia mwaka tunaoupa kisogo,basi sio ajabu kwamba malengo ya wengi ni kulinda zaidi mifuko yetu kwa kuwa makini zaidi na matumizi hesabu za mapato na matumizi na pia kulinda zaidi kazi zinazotuingizia kipato.Nakutakia kila la kheri katika hilo.

Bila kujali hali ya kiafya,kiuchumi,kisiasa wala kijamii, ukweli kwamba mwaka mpya umewadia huku wewe na sisi sote hapa BC tukiwa hai, ni jambo la kufurahia na kumshukuru Muumba.Ukivuka mwaka unakuwa umeandika historia mpya katika maisha yako. Vitabu vya kumbukumbu vitaandika kwamba uliuona mwaka 2009! Ni jambo la kumshukuru muumba kwani ni wazi wapo wengi sana waliotamani kuuona mwaka huu na wasifanikiwe.Kama huamini, fikiria kidogo tu ni watu wangapi ambao umehudhuria mazishi yao au kusikia habari juu ya misiba yao?Unaona? Hatuna budi kumshukuru Mungu.

Wakati huu tunapoingia mwaka mpya wa 2009,tungependa kwanza kukutakia kila la kheri wewe msomaji,mtembeleaji au mchangiaji wetu.Mwenyezi Mungu akuongoze na kukubariki katika kila jambo utakalolifanya ndani ya mwaka huu wa 2009.Kama mwaka 2008 haukuwa wenye mafanikio kwako au haukutimiza malengo yako,usikate tama.Fungua ukurasa mpya huku ukiwa na fikra chanya zaidi na utaona mabadiliko.

Tungependa pia kukupa shukrani zetu za pekee kwa kuwa mtembeleaji,msomaji au mchangiaji mzuri wa BC.Kama kuna mafanikio yoyote ambayo tumeyapata tangu kuanzishwa kwa blog/site hii,ni wazi kabisa kwamba mafanikio hayo yametokana na mchango wako wewe msomaji,mtembeleaji na mchangiaji wetu.

Shukrani nyingi ziwaendee celebrities mbalimbali ambao bila maringo,kinyongo wala ngendembwe walikubali aidha kufanya nasi mahojiano au kutokuwa na kinyongo nasi pale tulipoweka picha zao na kukaribisha mvua ya maoni kutoka kwa wasomaji huku wengine wakiwa chanya na wengine hasi.Celebrities kama hao wanakuwa wametambua vyema nafasi au mchango wao katika jamii.Wametambua pia kwamba haiwezekani kuwa bondia ulingoni halafu ukawa unaogopa ngumi za uso.Tunawashukuru na kuwaomba tuendelee kushirikiana.

Shukrani za pekee ziwafikie bloggers wenzetu mbalimbali,vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya Tanzania,wapiga picha mbalimbali na wengineo wote ambao wanaendelea kushirikiana nasi katika jukumu hili zito la habari na mawasiliano.Asanteni sana.Bila ninyi,haiwezekani.BC inathamini sana mchango wenu.

Kama binadamu inawezekana kabisa kuna wakati tunatokea kutoelewana au hata kukwazana.Bila shaka hata sisi hapa BC inawezekana kuna wakati tulikukwaza.Yawezekana hatukuweka maoni yako kwa sababu moja au nyingine,yawezekana tulichelewa kuruhusu maoni yako yaonekane,yawezekana wewe ni celebrity na tuliruhusu maoni ambayo kimsingi uliona kama umetusiwa nk.Mifano ipo mingi.Lakini kwa wote hao,tunaomba samahani.Yote hayo ni katika kujitahidi kuitenda vyema kazi yetu.

Tunapouanza mwaka mpya wa 2009,tunakusihi uendele kututembelea,kuchangia,kutukosoa tunapokosea na pia kumwambia mwenzako kuhusu uwanja huu ili naye asipitwe na yanayojiri.Tunakutakia kila la kheri.HAPPY NEW YEAR 2009.

 

SIKUKUU ILIKUWAJE? December, 30, 2008

Filed under: Burudani,Sikukuu,Swali kwa Jamii,Zilipendwa — bongocelebrity @ 11:54 AM

comedi-orijinobc

Naam!Xmas kwa mwaka 2008 ndio imeshaisha.Kwa bahati mbaya siku kama hizi huwa hazirudi tena.Ilivyokuwa Xmas mwaka huu sivyo itakavyokuwa mwaka ujao na mingine itakayofuata.Ulipokuwa mwaka huu si ajabu hutokuwepo mwakani.Ndio maana huwa tunasisitiza kwamba Make The Most Use of It when/whenever you can(nimetia kizungu hapo kuonyesha msisitizo).

Najua wengi wenu bado mpo kwenye hali ya sikukuu.Wengine nasikia bado wanatibu mning’inio wa ziada(hangover).Kwa wengine huu ni wakati wa kutafakari jinsi matumizi yalivyokwenda.Ni wakati wa kukagua risiti huku macho yakiwa yamekutoka na simanzi likiwa limetanda usoni.Usijali,ndio maisha.Si ushasikia ule msemo usemao Ponda Mali kwani Kufa Kwaja?Sasa?

Lazima pia nikiri kwamba hata sisi wenyewe tupo kwenye holiday mood bado.Ndio maana mwendo kidogo unakuwa taratibu ingawa sio kama wa kinyonga.Bahati nzuri hatubadiliki rangi pia.Tunajongea huku tukiandaa mambo makubwa zaidi kwa ajili ya mwaka ujao ambao kimsingi tunataka uwe mwaka wa BC!

Sikukuu ilikuwaje?Uliserebukia wapi?Mambo yalikwendaje?Tungependa kusikia kutoka kwako msomaji.Wakati unatafakari jinsi sikukuu ilivyokwenda,hatungependa kukuacha hivi hivi.Burudika na wimbo Ndoa Fungo la Imani kutoka kwa Bima Lee.Pata burudani


Tumeshindwa kupata maelezo au caption ya hiyo picha.Unaweza kutusaidia?

 

TUNAWATAKIA KHERI YA SIKUKUU December, 23, 2008

Filed under: Sikukuu,Watu na Matukio — bongocelebrity @ 1:46 PM

happy-holidays-glitter

Sikukuu imewadia.Ni wakati mwingine wa kusheherekea Sikukuu ya Xmas na wakati huo huo kuanza makaribisho ya mwaka mpya,2009.Kama ilivyo jadi ya enzi na enzi,huu ni wakati wa kukumbukana,kutembeleana,kujuliana hali,kutakiana kheri,kujumuika pamoja,kula na kunywa kwa furaha,amani na upendo.Kwa wengine ni wakati muhimu wa kupeana zawadi.Kwa ujumla ni wakati wa kufurahi!

Ni kwa kuzingatia hayo yote yaliyotajwa hapo juu ambapo tunakukaribisha wewe msomaji,mchangiaji au mtembeleaji wa BC,kutumia nafasi hii kuwatumia ndugu,jamaa na marafiki zako,popote pale walipo,Kheri ya Sikukuu ya Xmas kwa mwaka huu wa 2008.Unaweza kufanya hivyo kwa kuandika salamu na majina yao hapo kwenye sehemu ya maoni au kututumia picha au chochote kile ambacho ungependa ili kusindikiza salamu zako.Tumia anuani pepe (bongocelebrity at gmail dot com)Ukituma picha tutaiweka kwenye post hii hii.Jisikie huru.

Kutoka kwetu: Tunatoa shukrani nyingi na za dhati kwa jinsi ambavyo umekuwa nasi kwa wakati wote huu.Tunapenda kuchukua nafasi hii kukutakia wewe,ndugu,jamaa na marafiki zako KHERI YA SIKUUKUU YA XMAS na maandalizi mema ya MWAKA MPYA 2009.Tunatumaini itakuwa sikukuu ya kukumbukwa na iliyojaa furaha na mafanikio tele.Amani itawale.

Kwa niaba ya timu nzima ya BC-Jeff Msangi

 

“VIJANA WAJITOLEE,WAWE WAVUMILIVU NA WAAMINIFU”-NYIRENDA December, 9, 2008

Filed under: African Pride,Serikali/Uongozi,Sikukuu,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 12:44 AM

nyirendabcMiaka 47 iliyopita,katika tarehe inayofanana na leo,Tanganyika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni mwingereza.Nchi ilizizima kwa nderemo na vifijo huku kila mtu akiwa amejawa na matumaini yaliyotokana na kujikomboa kutoka katika mikono ya mkoloni.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndio alikuwa kiranja mkuu wa mchakato wa uhuru.Lakini kama tujuavyo,Nyerere hakuwa peke yake.Wapo mashujaa wengi waliochangia kupatikana kwa uhuru.Hatuna budi kuwaenzi viongozi na mashujaa hao daima.

Kwa upande mwingine wapo mashujaa ambao mbali na kuchangia katika harakati za kuutafuta uhuru, kwa njia moja ama nyingine,wao walikwenda hatua moja mbele na kuhakikisha kwamba uhuru unapatikana na alama mbalimbali za kuuthibitisha uhuru,kwa faida ya vizazi vilivyokuwepo wakati huo na vya mbeleni,zinasimikwa pia.

Miongoni mwa watu hao,hakuna ubishi kwamba jina la Major Alexander Gwebe Nyirenda, ni jina ambalo linakumbukwa na litaendelea kukumbukwa kutokana na mchango wake hususani wakati wa sherehe za uhuru.Nyirenda ndiye aliyeipandisha bendera ya uhuru kileleni katika Mlima Kilimanjaro na kuuwasha mwenge wa uhuru ili umulike mipaka yote ya Tanganyika.

Tulipata fursa ya kufanya mahojiano na Major Nyirenda ambaye bila kusita alikuwa mwepesi wa kutueleza historia ya maisha yake na zaidi juu ya utumishi wake jeshini na kumbukumbu yake kuhusiana na siku ile ambayo tunaidhimisha leo hii.Mahojiano yetu yalikuwa kama ifuatavyo;

BC: Major Nyirenda, kwa faida ya wasomaji wa mahojiano haya,unaweza kutuambia kwa kifupi historia ya maisha yako? Ulizaliwa lini,wapi,ukasomea wapi nk?

NYIRENDA: Mimi nilizaliwa tarehe 2 Februari 1936, Kasonga (Nyasaland) Malawi. Wazazi wangu,Mama na Baba,walitoka Malawi. Baba yangu alikuwa anafanya kazi katika Wizara ya Afya kama Mganga wa Afya (Medical Assistant). Tulizaliwa watoto wanne. Wanaume wawili na wanawake wawili. Mimi nilizaliwa mwisho-Kitinda Mimba.

Nilizaliwa Malawi kwa sababu Baba alipata likizo ya miezi mitatu toka kazini. Alipopata likizo hii kwenda Malawi, Mama alikuwa mjamzito wa miezi saba. Ndio maana mimi nikazaliwa Malawi. Lakini marehemu kaka yangu na marehemu dada zangu wote walizaliwa Tanganyika.

Nilianza kusoma shule darasa la kwanza shule ya Mchikichini,Dar-es-salaam. Niliendelea na elimu ya msingi Iringa katika shule ya msingi Mlandege na baadaye nikaendelea na masomo ya sekondari Malangali Secondary School huko Iringa. Kutoka Malangali Secondary School niliendelea kusoma darasa la kumi na moja na kumi na mbili mkoani Tabora katika shule ya Wavulana Tabora(Boys) Secondary School na kupata Cambridge School Certificate mwaka 1957.

Kabla ya kufanya mtihani wa darasa la kumi na mbili (12) walikuja pale Tabora School maofisa wa kijeshi( wazungu) wakiwa katika harakati ya kutafuta watu ili waingie katika jeshi la wakati huo yaani Kings African Rifles(KAR) kama maofisa kwani wakati huo hakukuwa na ofisa Mtanzania katika jeshi la KAR. (more…)

 

EID MUBARAK December, 7, 2008

Filed under: Sikukuu — bongocelebrity @ 7:13 PM

eid-mubarakbc

Kwa niaba ya timu nzima ya BC,napenda kuchukua fursa hii kuwatakieni nyote sikukuu njema ya Eid mahali popote pale mlipo.Amani na upendo vitawale leo,kesho na daima.Umoja wetu ndio nguvu na tegemeo letu.Mola awape uzima na afya njema milele na milele.

Jeff Msangi, December 2008


 

SIKUKUU NJEMA September, 30, 2008

Filed under: Sikukuu — bongocelebrity @ 10:43 AM

Tunawatakieni nyote sikukuu njema.

 

TUNAPOWAKUMBUKA MASHUJAA;NANI SHUJAA WAKO? July, 28, 2008

Filed under: In Memory/Kumbukumbu,Jeshi,Serikali/Uongozi,Sikukuu,Tanzania/Zanzibar — bongocelebrity @ 11:44 PM

Kila nchi ulimwenguni ina mashujaa wake.Lakini tafsiri ya shujaa katika nchi nyingi ulimwenguni ikiwemo yetu ya Tanzania,huwa ni wale waliopigana vita iwe ya msituni,nchi kavu,majini nk.Hivi juzi nchini Tanzania ilikuwa ni siku ya kumbukumbu ya mashujaa.

Kama inavyoonekana pichani,katika siku kama hiyo,huwa ni wakati wa wanasiasa kuweka pembeni tofauti zao za kisera,kiitikadi na kimtazamo na kuikumbuka siku hiyo muhimu.

Pamoja na hayo,yawezekana kabisa kwamba wewe binafsi ukawa na shujaa wako binafsi.Kwa mfano,kwangu mimi shujaa ni mama yangu,aliyenizaa na kunilea mpaka kufikia hapa nilipo.Je kwako wewe nani ni shujaa wako ukiachilia mbali “mashujaa” tuliowakumbuka juzi?

Pichani ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi,CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba (kulia) akifurahia jambo na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, walipokutana katika maadhimisho ya siku ya mashujaa iliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam juzi.

 

HAPPY FATHER’S DAY June, 15, 2008

Filed under: Burudani,Maisha,Sikukuu,Zilipendwa — bongocelebrity @ 10:52 AM

Leo ni siku ya kina baba.Kwa kutumia ile lugha ya malikia,tunaweza kusema Today is Father’s Day! Ni siku maalumu ya kumkumbuka baba yako,awe hai au awe alishaaga dunia. Ni siku ya kukumbushana upendo,amani na kutakiana mafanikio mema baina yako na mzazi wako.Kama kumetokea kutokuelewana kati yenu,basi siku hii inaweza tumika kama fursa nzuri ya kurekebisha mambo.

Bila shaka tunakubaliana kwamba kama ilivyo kwa mama,bila baba hakuna mtoto.Kwa maana hiyo mchango wa baba na mama katika malezi ni jambo muhimu.Kinachohitajika ni kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Kuisindikiza siku hii,sikiliza kwa makini Wosia huu mzito kutoka kwa Baba kwa kubonyeza player hapo chini.Kisha zingatia yasemwayo katika wimbo huo.Happy Father’s Day.

 

HAPPY MOTHER’S DAY TO OUR SWEET MOTHERS. May, 11, 2008

Filed under: African Pride,Familia,Sikukuu,Uncategorized,Wanawake na Watoto — bongocelebrity @ 12:03 AM

Katika nchi nyingi za magharibi,leo ni Mother’s Day au kwa maneno mengine Siku ya Mama.Leo ni siku maalumu ya kumkumbuka,kuutambua na kuuthamini rasmi mchango wa mama yako katika maisha yako.Huu ni utamaduni wa kimagharibi ambao unazidi kuenea kwa kasi ulimwenguni kote zikiwemo pia nchi zetu za kiafrika.Sasa hii sio kumaanisha kwamba katika siku zingine usimkumbuke,usiutambue wala usiuheshimu rasmi mchango wa mama yako.La Hasha!Kila siku,kwa walio wengi, ni siku ya mama. Kwetu sisi waafrika ndio kabisaa.Ndio maana kuna ule usemi kwetu wa Nani Kama Mama?

Itumie siku ya leo kumkumbuka mama yako.Kama kwa bahati mbaya alishaiaga dunia,basi chukua muda maalumu kumkumbuka,kumuombea na muhimu zaidi kumuenzi.Kama upo karibu na mama yako,basi mkumbatie na umkumbushe kwamba unampenda na unamtakia kila la kheri katika maisha.

Ni muhimu pia kukumbuka kwamba, kama binadamu,huwa inatokea wakati mwingine tukakosa kuelewana.Ndio.Huwa inaweza kutokea tukakosa kuelewana hata na mama zetu! Kama hali ipo namna hiyo katika maisha yako,itumie siku hii kusameheana na kuweka mambo sawa na mzazi wako.Jinsi moja nzuri ya kuweza kusamehe ni kujiuliza swali;Je kuna ulazima au manufaa yoyote ninayoyapata kutokana na kutokuelewana huku? Usiwe mgumu wa kusamehe ili nawe upate kusamehewa.Sote tunakosea katika maisha.Kama leo basi ni kesho.Usisite kutenda lililo jema leo.

Katika kuisindikiza siku hii,tumekuchagulia wimbo maalumu kutoka kwa mwanamuziki mkongwe wa nchini Nigeria, Prince Nicco Mbagga.Wimbo unaitwa Sweet Mother. Huu ni wimbo maalumu kwa kina mama wote.Kinamama,tunawapenda na tunawathamini.Bila ninyi dunia si dunia.Bonyeza player hapo chini upate burudani,sikiliza ujumbe uliomo ndani ya wimbo.Happy Mother’s Day!