BONGO CELEBRITY

All You Wanted To Know But Didn’t Know How and Where

DR.REMMY ONGALA October, 20, 2007

Filed under: Burudani,Muziki,Tanzania/Zanzibar,Utamaduni — bongocelebrity @ 12:04 AM

Alipozaliwa wazazi wake walimuita Ramadhani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika mkoa wa Kivu huko Democratic Republic of Congo ya leo ambayo hapo zamani kwanza iliitwa Belgian Congo kabla ya kuitwa Zaire. Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu eneo ambalo halikuwa mbali sana kutoka mpakani na Tanzania. Baba yake alikuwa ni mwanamuziki mashuhuri pia akiwa mpiga ngoma kwa kutumia mkono na pia mbira. Pindi tu alipozaliwa familia yake ilihamia Kisangani.

Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa kwake mama yake alipata ujauzito mara mbili lakini kwa bahati mbaya kila mara mtoto alifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiiage dunia pia. Bila kusita mganga wa kienyeji akampa ushauri wake. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali bali akajifungulie maporini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndio kisa cha Remmy Ongala kutokata nywele zake kwa muda mrefu sana.

Mwenyewe anasema mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kwa kuwa na manywele marefu namna ile mpaka hapo baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni,hayati Bob Marley ilipopata umaarufu nchini Zaire, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea ufahari. Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele kitu ambacho kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji pia. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndio mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Doctor Remmy Ongalla.

Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza mambo ya muziki tangia akiwa mdogo kabisa jambo lililomfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa; kwa mfano, madaktari, wanasheria,waalimu, wakulima nk, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki. Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Remmy akiwa na miaka sita tu akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia shule, Remmy ilibidi aache shule.

Ilipofika miaka ya 60, Remmy tayari alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa sio mwaka mzuri kwa Remmy kwani mama yake mzazi alifariki dunia jambo ambalo lilimuacha Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake kwani yeye sasa ndio alikuwa mkuu wa familia. Bila elimu na ujuzi mwingine wowote,alilazimika kuanza rasmi kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu kitu ambacho kilimwezesha kuwa akitumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli mbalimbali katika sehemu mbalimbali nchini Zaire akiwa na bendi yake na vijana wenzake iliyoitwa Bantu Success.

Kwa miongo kadhaa iliyofuatia Dr.Remmy Ongala alizunguka katika sehemu mbalimbali za Zaire akiambatana na kupiga na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini Zaire zikiwemo Succ s Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.

Ingawa kwa ujumla alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, mwenyewe anakiri kwamba muziki wa kutoka nchini Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia katika kupata staili ya pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele na wa Franco ulimsaidia kupata style yake ya uimbaji kama tulivyoizoea.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar-es-salaam baada ya kuitwa na mjomba wake ili aje ajiunge na bendi maarufu ya wakati huo,Orchestra Makassy, iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo, Mzee Makassy. Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha ya Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, aliandika wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama “Siku ya Kufa”, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki. Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu.

Dr.Remmy Ongala alivyo hivi sasa.

Alidumu na bendi ya Ochestra Makassy kwa kama miaka mitatu hivi kabla ya mwaka 1981 kuhamia katika bendi ya Orchestre Super Matimila iliyokuwa ndio inaanza kuchipukia miaka hiyo. Hiyo ilifuatia Mzee Makassy kuhamishia bendi yake nchini Kenya. Jina la bendi hiyo, Matimila, lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Baada ya kujiunga kwa Remmy, bendi ya Matimila ilijiongezea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Bendi hiyo kwa wakati mmoja ilikuwa na wanamuziki kama 18 hivi ingawa kati yao wanamuziki 6 mpaka 8 tu ndio waliokuwa wanalikwaa jukwaa kufanya vitu vyao. Pamoja na hayo kila mmoja alikuwa anapata japo nafasi ya kupanda jukwaani kuimba au kupiga chombo/vyombo. Wakati huo ilikuwa imeshakuwa chini ya uongozi wa Remmy Ongala ambapo pia baadaye aliiunda upya na kuibadilisha jina na kuiita Super Matimila.

Miaka iliyofuatia ilishuhudia umaarufu wa Remmy ukiongezeka hususani kutokana na mashairi ya nyimbo zake ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, siasa nk. Mkusanyiko wa mashairi yake ulijulikana kama Ubongo au akili.

Mafanikio ya Remmy na kundi lake zima la Matimila hayakuishia nchini Tanzania kwani katika miaka ya mwishoni ya 80 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania na Afrika. Mwenyewe Remmy anasema zali la kuanza kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Anasema alimpa rafiki yake mmoja mzungu aliyekuwa anaondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza kaseti yenye nyimbo zao. Rafiki yake naye alipofika huko aliwapatia jamaa wa WOMAD (World of Music,Arts and Dance) shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za dunia ya tatu. Jamaa walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa mwaliko kushiriki katika maonyesho yao barani Ulaya ya mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya bendi ya Matimila ilitoa mkusanyiko wa nyimbo zao waliouita Nalilia Mwana ambamo zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki. Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kufuatia mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo ambapo walipata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa inaitwa Real World Studios. Matokeo yake ni nyimbo maarufu kama Kipenda Roho nyimbo ambayo inasemekana aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe mzungu muingereza ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa naye watoto watatu.

Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambapo walirekodi mkusanyiko wa nyimbo ulioitwa Mambo ambao ulikuwa na nyimbo kama hiyo ya Mambo (aliimba nyimbo hii kwa kiingereza pia ili kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili) na nyinginezo kama ule wa “No Money, No Life” na “One World”.

Umaarufu wake ulizidi mwaka 1990 alipotoa wimbo wa Mambo Kwa Socks ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba “hauna maadili” ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi.

Pamoja na yote hayo, miaka michache iliyopita Dr.Remmy Ongala aliamua kuachana na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Remmy akaokoka, akatubudu dhambi zake na hivi sasa anamuimbia bwana. Mpaka hivi sasa ameshatoa albamu yake ya injili aliyooiita Kwa Yesu Kuna Furaha. Mapema mwaka huu alikuwa mbioni kukamilisha albamu yake ya pili. Bado anaishi Sinza (Kwa Remmy) mahali ambapo panaitwa hivyo kwa heshima yake.

Dr.Remmy Ongala(mwenye rasta) siku alipobatizwa.Pichani yuko na waumini wenzake.

Imeandikwa kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari mtandaoni.

 

12 Responses to “DR.REMMY ONGALA”

  1. Dinah Says:

    Kila la kheri ktk kutangaza Injili kupitia sanaa ya Muziki. Ni mtu muhimu sana katka hostoria ya sanaa ya Muziki.

    Kazi musuri!

  2. Kila la kheri Dr.Remmy umeitangaza sana nchi ya Tanzania,achilia mbali kuna kipindi serikali ilitaka kukugeuzia kibao eti sio raia kisa kumsifikia kipindi kile Mrema alipokuwa serious na kazi.

    Tupo pamoja.Alleluyah …..Ameni

    Naomba kuwasilisha.

  3. Kimori Says:

    You have turned 60 and you look capable still…It is never too late to serve the Lord after all you don’t loose anything!

    Preach the Word….all of it!

  4. maya65 Says:

    ndaki unasema eti serikali ilitaka kukugeuzia kibao..je huyo remmy ni mtanzania?
    umeshasoma historia yake kuwa anatoka congo…harafu bado hujui kuwa ni mkongo!!!!
    au kwa kuwa amekaa sana hapo bongo?
    huyo jamaa ni mkongo na ataendelea kuwa mkongo!!!!

  5. hombiz Says:

    maya65 hebu acha ubwege wewe. Inabidi uende ofisi za uhamiaji ukapate dondoo juu ya sheria za uhamiaji. Dr Remi ni raia wa Tanzania hivi sasa ingawa ni kweli alizaliwa DRC. Kafuata sheria zote za uhamiaji na kutunukiwa uraia wa Tanzania baada ya kukidhi matakwa ya sheria za nchi ktk swala zima la uhamiaji. Hongela Dr Remi kwa kuitangaza tanzania na kuwa Mtanzania ingawa si wa kuzaliwa.

  6. maya65 Says:

    “kukidhi matakwa ya sheria za nchi katika suala zima la uhamiaji” hayo matakwa aliyekidhi mbona hutuambii?
    ina maana hata wewe huyajui ila unashabikia tu… na wewe ni bwege tu?
    haahaahaaaa…..

  7. Colin Says:

    Dr remmy ni shujaa na mfano wa kuigwa kwa kizazi hiki na kijacho ni msanii wa kweli sio mwanamziki,Nyimbo za remmy zinafundisha,burudisha na zingine chache baadhi ya jamii haikizikubali kwa kile walichokiita maadili.Remmy huwezi kusema mziki wa dansi umejaa uhuni na shetani,hayo ni mawazo yako binafsi ,uhuni ulikuwa unaufanya wewe sio mziki wa dansi,Bangi na Umalaya vilikuwa ni vitu vyako binafsi na sio mziki wa dansi.Ulivyoona umezidiwa na rahaa na magojwa kanisa ndo likawa kimbilio ,bado tunaufeel mziki wa dansi .

  8. Mwl. Ngimbudzi Fredy Says:

    Mpendwa Remmy,
    Binafsi ninakupongeza kwa kumrudia Mungu na kuamua kumtumikia yeye siku za maisha yako kwa njia ya uimbaji.
    Nakutakia baraka zake Mungu na namwomba yeye akujalie afya na nguvu ili kupitia uinjilisti wako watu wengi wamrudie. Ikimpendeza yeye upite sehemu mbalimbali nchini ili utoe ushuhuda wako kwa wengine. Pita mikoani na vijijini kaseme Mungu anakusudi nao. Imba mpaka waisikie sauti yake Mungu.
    Bwana anakupenda sana Remmy.
    Ubarikiwe sana.

  9. Mie Says:

    Mwl. Ngumbudzi Freddy unapenda kufahamu waimbaji wa injili Tanzania? karibu http://www.strictlygospel.wordpress.com
    Ubarikiwe sana

  10. hombiz Says:

    Wewe maya65 hii ni kwa ajili yako

    Uraia wa kuandikishwa, raia wa nje atapata uraia wa Tanzania wa kuandikishwa kwa kuomba kwa Waziri mwenye dhamana ya uraia na pia ombi lake liwe limekidhi masharti yote ya kisheria ambayo ni:-

    – Awe amekaa nchini mfululizo kwa kipindi kisichopungua miaka 10;

    – Awe ni mwenye manufaa kwa Taifa kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, maendeleo ya jamii au utamaduni;

    – Awe na uwezo wa kuongea kwa ufasaha lugha ya Kiswahili au ya Kingereza au lugha zote mbili;

    – Awe ni mwenye tabia njema na alipojitangaza kwenye gazeti hakutolewa pingamizi na mtu yoyote; na

    – Baada ya kupata uraia aonyeshe utii kwa nchi na nia ya kuishi nchini muda wote.
    Hayo ndio matakwa ambayo Dr.Remmy Ongala ameyatimiza na kufanikiwa kupata uraia wa Tanzania.

  11. Joji Says:

    Namwunga mkono Colin (N 7).

    Hasa zile nyimbo za zamani zitafanya Dr Remmy atakumkukwa kwa miaka mingi, au niseme daima na milele. Yeye mwenyewe aliimba : ‘Muziki sio uhuni’. Muziki wake – hasa zile nyimbo za kabla ya kuokoka kwake – ni zawadi kutoka kwa Mungu!

    Dr Remmy Ongala alikuwa nabii. Lakini kama manabii wa kweli aliimba jangwani… Nasikitika sana wimbo wake bora zaidi ‘Mambo kwa soksi’ ulipigwa marufuku na mpaka sasa haupatikani kwenye CD.

  12. Gandu Says:

    Mbona Remmy ! unatoa historia ya Uhongo?
    wakati wewe unasema umeokoka! na huku unaongopa?

    (a) umezaliwa katika kijiji cha Kindu kule Bukavu?
    upande moja wa wazaziwako ni Mmanyema na upande wa
    pili ni Mmayoke!
    Ulipozaliwa unasema ulipewa jina la Ramadhani Mtoro
    yaani mtoto alezaliwa na meno
    Kutokana na maelezo yako ya majarida mbali mbali ya siku za nyuma!
    (b) Ulipokuja Tanzania kwa mara ya kwanza kutoka kwenu
    ulikuwa (bitoz) mzuri mwenye nywele fupi katika miaka 19975
    hata picha zako za siku za nyuma zinaonyesha hivyo!

    Sasa hapa ukisema kuwa ulikuwa na nywele ndefu kwa sababu ya ushauri alipoewa mama yako kutoka kwa mganga wa kienyeji! kidigo unadanganya!

    Kuanzia miaka ya 1980s ndipo ulipoanza kuweka Rasta… na kabla yako kuna yule mpiga gitaa wakowa mwanzo Kassongo mliyekuwa naye makassy ndiye aliyeweka rasta

    Jaribu kuwa mkweli wewe sasa unamwimbia bwana…ALELUYA
    bwana Ramadhani Mtoro Ongara Karimagonga ukifika
    Kindu,Uvila na Kalemi tusalimie


Leave a comment